RAIS SAMIA AZINDUA USAFIRISHAJI WA MIZIGO KWA TRENI YA UMEME YA SGR

 


Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akioepelusha bendera ikiwa ni ishara ya kuzindua usafirishaji wa mizigo kwa kutumia usafiri wa Treni ya umeme ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma eneo la Kwala Marshalling Yard mkoani Pwani, leo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akivuta kitambaa kuashiria uwekaji wa jiwe la msingi Kongani ya Viwanda ya Kwala (Kwala Industrial Park) iliyopo Kwala, Kibaha vijijini mkoani Pwani tarehe 31 Julai, 2025. Lengo kuu la Kongani ya viwanda ni kujenga viwanda 2000 na kwasasa kuna viwanda 12 katika eneo lenye ekari 2500.

  

Aliyosema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan

#Uzinduzi wa safari za mizigo kwa kutumia reli ya kisasa ya SGR ni ushahidi kuwa Tanzania imeamua kwa dhati kuimarisha mfumo wa usafirishaji wa mizigo kuanzia kwenye barabara, usafiri wa anga, maji na reli.

#Reli ya SGR kutoka bandari ya Dar es Salaam hadi Dodoma, ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kupunguza gharama za usafirishaji, uchakavu wa barabara na kulinda mazingira.

#Mzigo kutoka bandari ya Dar es Salaam unaweza kufika Kwala ndani ya dakika 45 hadi saa 1 na unaweza kufika Dodoma ndani ya masaa manne hadi matano. Haya ni maboresho makubwa yatakayopunguza muda unaotumiwa na magari ya mizigo ambayo ni wastani wa masaa 30 hadi 35 kwenda  Kwala na kukamilisha taratibu za kuingia na kutoka bandarini.

#Mradi huu unatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa malori katikati ya jiji la Dar es Salaam, kuongeza ufanisi wa bandari na kupunguza muda wa ushushaji na usafirishaji wa mizigo.

#Safari za mizigo kupitia reli ya kisasa, zitapunguza gharama za uchukuzi, zitachochea shughuli za kiuchumi na kuongeza ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam.

#Serikali imewekeza takribani shilingi bilioni 330.2 kwa ajili ya ununuzi wa mabehewa 1,430 ya mizigo ya SGR ili kuimarisha usafiri na usafirishaji wa mizigo.

#Shughuli hizi ni za kibiashara, hivyo nasisitiza vitengo vya biashara na mauzo viboreshwe kwa kuweka watu weledi na wenye ubunifu kwenye masuala ya biashara. Shirikianeni na wazalishaji wakubwa wa bidhaa mbalimbali ndani na nje ya nchi ili kubeba mizigo mingi zaidi.

#Ni vyema TRC mkashirikiana na TAZARA kama watoa huduma binafsi ili kufikia mtandao mkubwa zaidi wa mizigo, vile vile, endeleeni kuhamasisha wadau wa sekta binafsi wa ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa hii ya miundombinu ya reli kwa ajili ya kusafirisha abiria na mizigo kwa kununua vichwa vya treni na mabehewa yao wenyewe ili kuhakikisha reli inatumika kikamilifu.

#Kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya bandari ya Dar es Salaam kwa wastani wa asilimia 25 hadi 30 kwa mwaka, kiasi cha shehena kimeongezeka kutoka tani milioni 23.69 mwaka 2023 hadi tani milioni 27.76 mwaka 2024. Vile vile idadi ya meli zinazohudumiwa zimepanda kutoka 1,860 mwaka 2023 hadi 1,990 mwaka 2024.

#Ongezeko hilo limesababisha msongamano mkubwa katika barabara za jiji la Dar es Salaam na mrundikano wa makasha bandarini na katika bandari kavu nyingine jijini humo ambao unaathiri ufanisi na ushindani wa bandari ndiyo maana serikali imeamua kufanya uwekezaji mkubwa  katika eneo la Kwala.

#Ushughulikiaji wa shehena za mizigo, umehamishiwa hapa Kwala kwenye eneo kubwa zaidi, kituo hiki kitapunguza msongamano katika bandari ya Dar es Salaam, kitaongeza wigo na kuboresha huduma za bandari na kuongeza ufanisi.

#Kwa wateja wa bandari, Kwala itawarahisishia huduma zote za upokeaji na usafirishaji mizigo na kuepusha gharama zilizokuwa zinasababishwa na ucheleweshwaji wa mizigo.Mizigo inayoshushwa bandarini itahifadhiwa, kuchakatwa na kusambazwa bila usumbufu.

#Bandari kavu ya Kwala itatoa fursa kwa wafanyabiashara kutoka nchi jirani kufanya biashara kwa ufanisi zaidi kupitia lango la Dar es Salaam.

#Kituo hiki kina kongani ya kisasa ya TRC inayojumuisha sehemu ya maandalizi ya safari za treni ya mizigo na abiria. Kongani hiyo ina mtandao wa reli wa KM 35 na njia 21 mtandao wa kisasa, miundombinu ya namna hii ni ya kipee barani Afrika.

#Katika mipango yetu ya baadae, tutaunganisha bandari kavu ya Kwala na bandari ya Bagamoyo pamoja na bandari ya Tanga. Kwa sasa tuko katika hatua za awali kuelekea ujenzi wa gati kubwa ya kisasa Bagamoyo yenye uwezo wa kuhudumia meli kubwa zenye uwezo wa kubeba makasha 24,000 sawa na tani 600,000 kwa wakari mmoja.

#Hatuwezi kujitegemea kiuchumi bila kuwa na uwekezaji imara wa viwanda, uwepo wa kongani hii kutairahisishia serikali kutoa huduma zote muhimu.

#Miradi hii italeta mapinduzi makubwa ya biashara katika ukanda huu kupitia ushoroba wa kati, natoa rai kwa nchi za ukanda huo kuendeleza ushirikiano kuhakikisha tunashabiiana kwa kuwa na miundombinu ya kisasa.

#Naitaka Wizara husika na taasisi zote zinazotoa huduma katika bandari ya Dar es Salaam kuhamishia huduma zote za kibandari katika bandari kavu ya Kwala ifikapo Agosti 4, 2025 ili nayo ianze kutumika.

#Ili kupunguza msongamano wa malori unatokana na shughuli za bandari, naelekeza Wizara ya Uchukuzi kukaa na wadau wote husika ili kuja na mkakati kabambe wa kuondoa msongamano.

#Nazitaka Serikali za mikoa na halmashauri kutenga maeneo ya uwekezaji na kusimamia vizuri upangaji wa ardhi na miundombinu rafiki. Aidha, Wizara husika ihakikishe kongani ya viwanda inaunganishwa na mifumo yote ya usafirishaji. 

Aliyosema Rais Mstaafu, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete

#Nakupongeza Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri unayoendelea kuifanya kwa maendeleo ya nchi yetu, uzinduzi wa miradi hii ya leo ni ushahidi mwingine wa kazi hizo.

#Tunakushukuru Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa miradi hii kwani Kwala sasa imekuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo kwa Mji wa Chalinze na maeneo ya jirani.

Aliyosema Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa.
 
#Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya Sekta ya Uchukuzi ambapo katika mwaka wa fedha 2025/26, imetenga shilingi Trilioni 2.62 kwa ajili miradi mbalimbali ambapo kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 1.51 ni kwa ajili ya ajili ujenzi wa miundombinu ya reli.

#Leo tunashuhudia uzinduzi wa safari za treni ya mizigo (SGR) kati ya Dar es Salaam na Dodoma pamoja na upokeaji wa mabehewa mapya ya mizigo 50 kati ya mabehewa 100 yaliyonunuliwa na Serikali kwa ajili ya treni ya mizigo ya njia ya reli ya kawaida (MGR) na mabehewa 20 yaliyokarabatiwa na Wakala wa Uwezeshaji wa Usafirishaji wa ushoroba wa Kati.

#Sababu mojawapo ya ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala ni eneo la Ruvu kuwa karibu na miundombinu ya barabara kuu inayounganisha nchi jirani zinazotumia Bandari ya DSM na reli kwa ajili ya kusafirisha mizigo yao kutoka Tanzania, hivyo eneo hili lilionekana litaweza kuunganishwa kiurahisi na barabara ya Chalinze  Dar es Salaam Express Highway.

#Sababu nyingine ni uwezo mdogo wa Bandari Kavu (ICDs) zilizokuwepo nchini ambapo katika Jiji la Dar es Salaam kulikuwa na jumla ya Bandari Kavu (ICDs) 11 zenye uwezo wa kuhifadhi makasha 24,300 tu kwa wakati mmoja na Bandari Kavu (ICDs) za CFS 9 zenye uwezo wa kuhifahi magari 19,100 tu kwa wakati mmoja ambazo zilionekana kutokidhi mahitaji makubwa kwa wakati huo na baadae.

#Bandari kavu ya Kwala ambayo inatarajiwa kuhudumia shehena ya makasha yanayokwenda nchi jirani, itakuwa na uwezo wa kuhudumia makasha 823 kwa siku, hivyo kuifanya bandari hiyo kuhudumia hadi makasha 300,395 kwa mwaka sawa na asilimia 30 ya makasha yote yanayohudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa.

#Bandari Kavu ya Kwala itaongeza uwezo wa usafirishaji wa mizigo, kupunguza gharama na kuimarisha ushindani wa bandari zetu; itaongezeka ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja na hivyo kuchangia ongezeko la pato la Taifa.  

#TRC itaongeza treni ya mabehewa 30 kwa lengo la kubeba mizigo ya tani 210,000 mpaka itakapofikia kiwango cha juu kilichosanifiwa.

Aliyosema Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo

#Eneo la Kongani ya Viwanda ni eneo muhimu kwa ajili ya kujenga uchumi, lina ukubwa wa jumla ya hekari 2,500 na kazi kwa awamu ya kwanza imeanza katika hekari 500.

#Mradi huu una thamani ya Dola za Kimarekani bilioni tatu ambapo zaidi ya viwanda 200 vinatarajiwa kujengwa katika eneo hilo na vitakapokamilika, vitatoa ajira za moja kwa moja zitakuwa 50,000 na zisizo za moja wka moja ni 2
150,000.

#Kwa sasa Kongani hiyo ina jumla ya viwanda 12 ambapo kati yake, viwanda 07 vimeanza kufanya kazi na viwanda 05 vipo katika hatua mbalimbali za ujenzi.

Aliyosema Waziri wa Miundombinu wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Dieudonne Dukundane.

#Nchi ya Burundi imeshaanza ujenzi wa ukuta katika eneo lililopo bandari kavu ya Kwala na kuifanya nchi hiyo kuwa ya kwanza kwa nchi zinazopakana na Tanzania kuanza ujenzi katika bandari hiyo.

#Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa katika bara la Afrika katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi, uboreshaji na upanuzi wa bandari pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa ambao umeisababisha Tanzania kuwa nchi ya baraka katika ukanda huu.

#Nchi ya Burundi na Tanzania zinajitayarisha kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa SGR kutoka Uvinza hadi Msongati, pia ziko tayari kuunganisha reli hiyo kwenda nchini Kongo. Utekelezaji huu utazifanya nchi hizo kuwa mfano katika Afrika ulimwenguni kwa kuhakikisha kuwa ujenzi wa SGR unatimia.

Aliyosema Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge

#Katika Mkoa wa Pwani, viwanda vimeongezeka kutoka 1,387 (2020) hadi 1,681(2025) ambayo ni sawa na ongezeko la viwanda 244.

#Ndani ya Serikali ya Awamu ya Sita, viwanda vikubwa vimeongezeka kutoka 59 (2020) hadi 156 (2025) sawa na ongezeko la viwanda 97, viwanda vya kati vimeongezeka kutoka 109 (2020) hadi 180 (2025) sawa na ongezeko la viwanda 71. 

#Mkoa wa Pwani kupitia sekta ya viwanda umeweza kutoa ajira za kudumu kwa Watanzania 21,149 na ajira ambazo sio za kudumu zaidi ya 60,000.


IMEANDALIWA NA IDARA YA HABARI - MAELEZO.  Wananchi Wa  Kwala  wakimsikiliza Rais kwenye mkutano wa hadhara  baada ya kuzindua Bandari kavu ya Kwala, Kibaha vijijini mkoani Pwani leo.

Comments

Popular posts from this blog

KADA MGEJA AHUDHURIA MAZIKO YA MAMA MZAZI WA MWANDISHI MWANDAMIZI WA HABARI KAHAMA

UNAMKUMBUKA AMINA CHIFUPA WA MPAKANJIAA.

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?