MKUTANO WA WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA, DKT. STERGOMENA LAWRENCE TAX NA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU MAFANIKIO YA MIAKA 60 YA MUUNGANO, LEO APRILI 3, 2024 JIJINI DODOMA


Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ni miongoni mwa wizara zinazotekeleza masuala ya muungano. Dira ya Wizara ni “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye amani na usalama” na Dhima yake ni “kulinda mamlaka, mipaka ya nchi na maslahi ya Taifa kwa kutekeleza Sera ya Ulinzi wa Taifa katika kudumisha amani na usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”.

# Majukumu ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ni kuandaa Sera ya Taifa ya Ulinzi na kusimamia utekelezaji wake; kulijengea uwezo wa kimedani Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kulipatia vifaa na zana bora; kuwezesha mafunzo na mazoezi; kuboresha mazingira ya kufanyia kazi, makazi na kuimarisha upatikanaji wa huduma stahiki na mahitaji ya msingi kwa wanajeshi na watumishi wa Umma; kuwapa vijana wa kitanzania mafunzo ya awali ya kijeshi na stadi za kazi ili kuwajengea ukakamavu, uzalendo, umoja wa kitaifa na uwezo wa kujitegemea; kuendeleza tafiti na uhawilishaji wa teknolojia kwa ajili ya kuzalisha bidhaa na huduma kwa matumizi ya kijeshi na kiraia; kuendelea kutoa mafunzo ya jeshi la akiba katika mikoa yote; kuimarisha ushirikiano kimataifa, kikanda na baina ya Tanzania na nchi nyingine katika nyanja za kijeshi na kiulinzi; na kushirikiana na Mamlaka za Kiraia katika kutoa misaada ya kibinadamu na uokoaji.

# Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inajumuisha Wizara, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), na Mashirika ya NYUMBU, MZINGA na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT).

MAFANIKIO YA WIZARA KWENYE MIAKA 60 YA MUUNGANO

# Tunapoadhimisha miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wizara ya Ulinzi na JKT inayo kila sababu ya kujivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika awamu zote sita (6) za uongozi. Awamu ya kwanza ilijenga nchi, umoja wa kitaifa, iliunda Jeshi, iliandaa vijana kwa ulinzi wa nchi yao ambao walimshinda Nduli  Iddi Amin Dadaa, mafanikio haya yameendelezwa na awamu zilizofuata zote.

# Katika kulinda mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uhuru, na usalama wa nchi, wizara kupitia JWTZ imechangia katika kujenga uchumi imara ambapo wananchi hujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali bila hofu. Aidha, Serikali kupitia Wizara imeendelea kutekeleza, na kuliimarisha Jeshi kwa kulipatia zana na vifaa bora na vya kisasa, rasilimali watu, na nyenzo za kufanyia mazoezi ili kuwa imara wakati wote.

# Ili kuliimarisha Jeshi, Serikali kupitia Wizara imeendelea kuboresha maslahi kwa Wanajeshi na Watumishi wa Umma kadri uwezo wa kifedha unavyoruhusu, kwa kuwapatia makazi bora kwa kuwajengea nyumba, pamoja na stahili mbalimbali, kupandisha vyeo kulingana na sifa, vigezo na taratibu.

# Hadi sasa Serikali imejenga nyumba za makazi katika kambi mbalimbali za Jeshi kwenye mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Kagera, Kigoma, Morogoro, Mwanza, Pemba, Pwani, Rukwa, Tabora, na Tanga. Aidha, ujenzi wa nyumba hizo, kwa kiasi kikubwa umepunguza uhaba wa nyumba pamoja na changamoto zitokanazo na wanajeshi kuishi uraiani.

# Mchango mwingine mkubwa wa Jeshi la Ulinzi la wananchi wa Tanzania katika miaka 60 ya Muungano, ni ulinzi madhubuti wa mipaka yetu, uhuru, na katiba. Nchi imeendelea kuwa imara na yenye amani katika awamu zote.

# Mafanikio mengine ni ushiriki wa Wizara kupitia Taasisi zake, hususan JWTZ katika kukabiliana na majanga au maafa mbalimbali pale yanapotokea. Katika kutekeleza jukumu hilo, JWTZ imeendelea kushiriki kikamilifu katika kutoa misaada ya uokoaji na ile ya kibinadamu kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.

# Wizara kupitia JWTZ imeendelea kushirikiana na mamlaka za kiraia katika miradi ya kimkakati. Baadhi ya maeneo ambayo JWTZ imeshirikiana na mamlaka za kiraia ni pamoja na kushiriki katika kuboresha huduma katika taasisi za serikali; kushiriki katika ulinzi wa miradi na maeneo ya kimkakati kwa nchi ikiwemo katika migodi mbalimbali, ulinzi wa miundombinu kama reli, ikiwa ni pamoja na reli ya kisasa Standard Gauge Railway (SGR), Mradi wa Bwawa la kufua Umeme wa Maji la Julius Nyerere (Julius Nyerere Hydro Power Project - JNHPP); ulinzi katika mamlaka ya usimamizi wa bandari Tanzania (TPA), kampuni ya simu (TTCL), na maeneo ya viwanja vya ndege.

# Wizara imefanikia pia kwenye utoaji wa huduma za afya na tiba kupitia hospitali za jeshi za kanda ambazo ni Lugalo Dar es Salaam, MH Mwanza, Bububu Zanzibar, Mirambo Tabora, MH Arusha, MH Mbeya ambazo hutoa huduma kwa wanajeshi, wananchi waishio maeneo yaliyo jirani na kambi za jeshi na katika hospitali nyingine. Kwa upande wa huduma za tiba, takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wanaopata huduma katika hospitali za Jeshi ni raia wasiyo wanajeshi.

# Ujenzi wa makao makuu ya Ulinzi wa Taifa eneo la Kikombo jijini Dodoma. Ujenzi huu unatekelezwa na wataalam wa ndani ya nchi, kwa gharama ya Serikali. Hili ni suala muhimu na ni mafanikio ya kujivunia, kwani ni ishara ya uimara wa Taifa letu.

# Mafanikio mengine ni kutungwa kwa Sheria ya JKT Na. 16 ya mwaka 1964 (The National Service Act No. 16 of 1964) ambayo iliwezesha kuanzishwa kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Sheria hiyo imefanyiwa marekebisho mbalimbali hadi mabadiliko ya mwaka 2002. Sheria hiyo imewezesha kuandikishwa vijana wa kujitolea, na kwa mujibu wa sheria.

# JKT limeendelea kufanya kazi kubwa na nzuri ya kuzalisha mali, kuwapa vijana wa kitanzania mafunzo ya awali ya kijeshi na stadi za kazi, ili kuwajengea ukakamavu, uzalendo, umoja wa kitaifa, na uwezo wa kujitegemea. Aidha, JKT pamekuwa ni mahali pekee nchini ambapo vijana wa makabila yote, dini zote wanapokutana, kuishi pamoja na kufanya mafunzo na kazi kama ndugu wa familia moja, na hivyo kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa.

# JKT limeendelea kutoa mafunzo maalum kwa makundi mbalimbali ikiwamo ya viongozi wa serikali, wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, watumishi wa serikali, ili kuwajengea maadili mema, ukakamavu na moyo wa uzalendo.

# Pamoja na JKT kutekeleza jukumu lake la msingi la kuwalea vijana, uzalishaji mali na ulinzi wa Taifa, kuliundwa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT) mnamo tarehe 01 Julai, 1981 kwa sheria ya uanzishwaji wa mashirika ya kibiashara katika taasisi za umma. Lengo kuu la kuanzishwa kwake ni kufanya biashara na kuzalisha faida, ili kuchangia gharama za uendeshaji wa shughuli za JKT, pamoja na kujenga uchumi wa Taifa.

# JKT kupitia SUMAJKT imeendelea kutekeleza shughuli mbalimbali za uzalishaji mali na huduma kupitia sekta za ujenzi, uhandisi na ushauri, kilimo, mifugo na uvuvi, viwanda, na huduma na biashara. Aidha, shirika hili limeshughulika na miradi ya kimkakati kama ujenzi wa Ikulu Chamwino, na taasisi nyingine nyeti kwa taifa letu.

# Vilevile JKT kupitia SUMAJKT imekuwa ikichangia katika pato la taifa kupitia uzalishaji mali na kulipa kodi stahiki kupitia kampuni zake tanzu na miradi mbalimbali. Shirika limefanikiwa pia kuongeza ajira zilizo rasmi na zisizo rasmi takribani 36,479 (29,758 ajira rasmi, na 6720 ajira zisizo rasmi) kwa vijana wa kitanzania kupitia kampuni zake tanzu, viwanda, na miradi mbalimbali.

# Kuanzishwa kwa mafunzo ya Jeshi la Akiba. Wizara kupitia JWTZ imeendelea kutoa mafunzo ya jeshi la akiba kwa vijana katika mikoa yote ya Tanzania bara. Jeshi hili la Akiba limekuwa na mchango mkubwa katika kuwajengea wananchi uzalendo na kuwapatia ujuzi wa kulinda maeneo mbalimbali muhimu, na hivyo kujenga mshikamano wa kitaifa. Jeshi hili limeshiriki pia katika shughuli za majanga.

# Katika miaka 60 ya Muungano, Wizara ya Ulinzi na JKT kupitia taasisi zake imeendelea kufanya na kuendeleza tafiti na uhawilishaji wa teknolojia kwa ajili ya kuzalisha bidhaa na huduma kwa matumizi ya kijeshi na kiraia. Serikali imeweza kuanzisha viwanda vya kijeshi likiwemo shirika la Tanzania Automotive Technology Centre (TATC) maarufu kama NYUMBU, pamoja na Shirika la MZINGA.

# Serikali kupitia wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, imeendelea kushirikiana na taasisi za kimataifa na kikanda, na nchi rafiki kutekeleza diplomasia ya ulinzi.

# Tunapoadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanzania, serikali kupitia wizara ya Ulinzi na JKT, imeendeleza pia kudumisha uhusiano na mataifa mbalimbali duniani, kupitia mafunzo na mazoezi ya kijeshi, misaada ya kitaalam, vifaa, zana na mitambo, ubadilishanaji wa wataalam, ubadilishanaji taarifa za uhalifu unaovuka mipaka, shughuli za ulinzi wa amani, mapambano dhidi ya ugaidi, uharamia baharini, uvuvi haramu, na usafirishaji haramu wa binadamu, ushirikiano huu, umesaidia kujenga mahusiano mazuri na nchi husika na kuongeza wigo wa mahusiano ya kijeshi na kutekeleza kwa vitendo makubaliano mbalimbali ya ulinzi wa amani.

# Kimataifa na kikanda, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia JWTZ inashiriki katika operesheni mbalimbali za Umoja wa mataifa kwa kutoa vikosi vya kulinda Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Afrika ya Kati, Sudan Kusini, na Lebanon.

# Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia JWTZ pia inashiriki katika operesheni za kuleta amani nchini Msumbiji kupitia Misheni ya SADC (SADC Mission in Mozambique - SAMIM) iliyopo chini ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), na Misheni ya kuleta amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (SAMIDRC) iliyopo chini ya SADC. Aidha JWTZ limeendelea kutoa maafisa wanadhimu wakuu katika misheni za Umoja wa Mataifa na misheni za Kikanda.

# Kwa upande wa michezo, Wizara pia katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano imefanya vizuri sana ambapo timu za majeshi yaliyo chini ya wizara ya Ulinzi na JKT zimefanikiwa, ikiwemo timu ya mashujaa FC iliyopo Kigoma iliyofanikiwa kupanda ligi kuu Tanzania Bara kuungana na timu ya JKT Tanzania. Pia timu ya wanawake ya mpira wa miguu ya JKT Queens nayo imeendelea kufanya vizuri katika michezo ya ligi kuu ya wanawake na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa CECAFA kwa mwaka 2022/2023 iliyowapa tiketi ya kushiriki michuano ya klabu bingwa Afrika kwa wanawake nchini Ivory Coast.

# Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inawashukuru viongozi wa awamu zote sita kwa kuiwezesha kutekeleza majukumu yake, na kipekee katika kuujenga na kuuimarisha muungano. Wizara inatoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu kwa kutoa uzito wa kipekee kwa wizara na taasisi zake, hususan kuliboresha na kuliimarisha jeshi, kuimarisha viwanda vya jeshi, na kuimarisha diplomasia ya ulinzi.

Imeandaliowa na Idara ya Habari – Maelezo


Katibu Mkuu wa Wizara hiyo , Mnadhimu Mkuu na Mkuu wa Jeshi la Kujega Taifa (JKT) wakiwa katika mkutano huo



Wanahabari wakiwa katika mkutano huo

Wanahabari wa TBC wakiwajibika

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari MAELEZO, Zamaradi kawawa, akizungumza baada ya kumalizika kwa kutano huo
Waziri huyo na maofisa wa Wizara yake wakimsikiliza Zamaradi kwa makini
Zamaradi ,akiagana na Waziri Tax baada ya kumalizika mkutano
Zamaradi Kawawa, akiagana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo
Waziri akitoka katika kutano huo na maofisa wake baada ya kumalizika
 

Comments

Popular posts from this blog

AMANI YETU TUILINDE NAIBU WAZIRI CHANDE AZUNGUMZA KATIKA IJITIMAI JIJINI DODOMA

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?

UNAMKUMBUKA AMINA CHIFUPA WA MPAKANJIAA.