CHAMA CHA WALIMU TANZANIA-CWT IDARA YA WALIMU WENYE ULEMAVU. CHAMPONGEZA SPIKA DKT. TULIA

Spika Dkt. Tulia Ackson, akisalimiana na Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania Mwalimu Japhet Maganga, baada ya kuwasili katika ukumbi wa Pius Msekwa kwa ajili ya hafla ya kupongezwa leo jijini Dodoma.



Katibu Mkuu Maganga, akimkalibisha Spika Dkt. Tulia kuzungumza na wajumbe wake Kulia ni Ulumbi Shani Mwenyekiti wa Idara ya walimu wenye ulemavu CWT Makao Makuu,
Spika Dkt. Tulia Ackson, akizungumza na viongozi hao

Spika Dkt. Tulia akipiga picha na wageni wake pamoja na ujumbe wao pamoja na Wenyeviti wa kamati za Kudumu za bunge waliohudhulia hafla hiyo

Spika, akiagana na wageni wake baada ya kumalizika hafla hiyo


 RISALA  YA KUKUPONGEZA SPIKA WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA RAIS WA UMOJA WA MABUNGE DUNIANI MH DK TULIA AKSON MWANSASU.                                                                                                              
Mheshimiwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Katibu Mheshimiwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Wenyeviti  wa kamati za kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mlioko hapa,
Waheshimiwa  Wabunge wenye Ulemavu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Wafanyakazi kutoka ofisi  ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mliopo hapa,
Komred Ulumbi Shani Mwenyekiti wa idara ya walimu wenye ulemavu CWT,
Komred Katibu Mkuu Chama cha Walimu Tanzania,
Mkurugenzi Idara ya watu wenye ulemavu Ofisi ya Waziri Mkuu kazi, ajira, vijana na watu wenye Ulemavu,
Mkurugenzi Msaidizi wa elimu Maalum Ofisi ya Rais TAMISEMI
Wakurugenzi  wa mashirika ya Kitaifa na Kimataifa mliopo hapa,
Wawakilishi wakazi wa Mashirika ya kimataifa mliopo hapa,
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania,
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya watu  wenye ulemavu Tanzania,
Mshauri wa Elimu jumuishi na Elimu Maalum kutoka Mkoa wa Pwani.
Makomred Wawakilishi wa walimu wenye ulemavu toka mikoa 26 ya Tanzania Bara.
Makomred Makatibu  CWT wenye ulemavu.
Makomred watumishi wa Chama Cha Walimu Tanzania Makao Makuu ,
Wasindikizaji wetu Pamoja wana Habari
Mabibi na Mbwana Itifaki imezingatiwa.
Nawasalimu kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mshikamano daima na ndio mkombozi wetu,
Walimu nguvu moja sauti moja.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi;
Awali ya yote tunapenda kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia kukutana hapa tukiwa wazima wa afya.
Kipekee kabisa tunapenda kukushukuru wewe Mh.  Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa mabunge duniani  kwa kukubali ombi letu kuwa wageni wako katika hafla hii ya kukupongeza.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi;
Idara ya walimu wenye ulemavu  makao makuu kwa niaba ya Chama cha Walimu Tanzania tunayo heshima kubwa kuwasilisha kwako salamu za dhati za pongezi kwako kwa ushindi wa kishindo ulioupata katika uchaguzi wa kumpata Rais wa Mabunge duniani, hongera sana kwa kuliwakilisha taifa letu kimataifa kushika nafasi hiyo adhimu duniani. Miongoni mwa sababu zilizopelekea sisi  kuamua   kukupongeza ni Pamoja na;-
i.    Ni mwanamke wa kwanza kutoka katika bara la Afrika kushika nafasi hiyo. Na kama nchi yetu tunajivunia kwa kupata nafasi hiyo inayoonesha utekelezaji wa azimio la Mkutano mkuu wa wanawake Beljing.
ii.    Kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi mahiri wa   Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mheshimiwa Dk Samia Suluhu Hassani ambaye amefanikisha jambo hili limaloliletea taifa letu heshima kubwa.
iii.    CWT kupitia idara ya walimu wenye Ulemevu tunaamini kuwa  nafasi uliyoipata ni kubwa na itasaidia kuiwakilisha nchi yetu katika diplomasia ya kimataifa katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii. Kwani ni kwa mara ya kwanza nchi yetu inapata nafasi hiyo adhimu duniani ya kutoa Rais wa umoja wa mabunge duniani.
iv.    Mheshimiwa Dk. Tulia Akson Mwansasu Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa mabunge duniani  mara zote umekuwa mtetezi wa walimu na Chama cha Walimu Tanzania. Miongoni mwa mengi uliyoyafanya na unayoendelea kuyafanya tumeshuhudia katika siku za hivi karibuni ni pamoja na kuikumbusha serikali inapochukua nafasi ya kushughulikia masuala ya watumishi wa umma wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali kuhukumiwa bila ya kuwapa nafasi ya kusikilizwa rejea walimu wakuu wawili kutoka halmashauri ya Tunduma mkoani Songwe mwaka 2023.  Umekuwa  ukiwakumbusha wafanyakazi walioko  kwenye idara moja inapotokea mgogoro kuna vyama vya wafanyakazi zaidi ya kimoja katika  idara hiyo kuzingatia takwa la kisheria kuhusu ada ya uwakala kwa chama chenye sifa. Hasa masuala ya vyama vya wafanyakazi. Kwani ni takwa la kisheria na nchi yetu mara zote inaongozwa kwa mujibu wa sheria.
v.    Umekuwa  ukitoa michango mikubwa katika sekta ya elimu yenye lengo la kuhamasisha ufaulu kwa wanafunzi wakiwemo wenye ulemavu na kutoa motisha kwa shule , wanafunzi na  walimu. Idara ya walimu wenye Ulemavu inakuomba uendelee na moyo huu na watanzania wapenda maendeleo wajifunze kwa mifano hai kutoka kwako.
vi.    Pamoja na utetezi wako  kwa watumishi wa Umma hususani walimu, Mh. Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa mabunge duniani   Dk Tulia Akson Mwansasu umekuwa ukiendeleza michezo kwa walimu kwa kushirikiana na Chama cha Walimu Tanzania kwa kuandaa mashindano ya michezo ijulikanayo kama Tulia Marathon hususani katika jimbo Mbeya Mjini.  Hata hivyo tunakuomba michezo pia iwaguse na walimu na wanafunzi  wenye ulemavu. Kwani michezo ni ajira, michezo ni furaha,michezo  ni sehemu ya tiba kwa Watoto wenye Ulemavu.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi;
Pamoja na mambo mazuri yanayofanywa na serikali ya awamu ya sita katika Nyanja mbalimbali za maendeleo bado tunakuomba utusaidie kuishauri serikali mambo yafuatayo;-
i.    Iharakishe  maboresho  ya Sera ya Taifa ya huduma na maendeleo ya Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2004 na marekebisho machache ya Sheria namba 9 ya mwaka 2010 ili iweze kuwanufaisha watu wenye Ulemavu wakiwemo walimu wenye ulemavu.
ii.    Itoe kipaumbele kwa walimu wenye Ulemavu kuwapatia mafunzo ya Mtaala Mpya ili waweze kutekeleza majukumu yao pasipo vikwazo sambamba na wenzao wasio na ulemavu.
iii.    Kunapotolewa vitabu vya mataala Mpya viendane sambamba na vya nukta nundu ili kuwasaidia walimu na wanafunzi wenye ulemavu kusoma na kufundisha bila utegemezi.
iv.    Sisi walimu wenye Ulemavu tunatambua nafasi ya mhimili muhimu wa Bunge unaouongoza katika utungaji wa sheria kwa hiyo tunakuomba kuwasisistiza waajiri kusoma sheria zinazoongoza vyama vya wafanyakazi kupunguza migogoro mahali pa kazi.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Mwisho, tunapenda kutumia fursa hii kwa kuthamini mchango wako Idara ya walimu wenye Ulemavu inakuomba kwa heshima na taathima Mh  Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa mabunge duniani  Dk Tulia Akson Mwansasu ikikupendeza walimu wenye ulemavu nchini wanakuomba uwe mlezi wao.

Mshikamano daima na ndio ukombozi wetu.
IMEANDALIWA NA IDARA YA WALIMU WENYE ULEMAVU .
IMESOMWA NA MKUU WA IDARA YA WALIMU WENYE ULEMAVU.
MWL ROBERT BUNDALA KATUBA.





Comments

Popular posts from this blog

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?

AMANI YETU TUILINDE NAIBU WAZIRI CHANDE AZUNGUMZA KATIKA IJITIMAI JIJINI DODOMA

UNAMKUMBUKA AMINA CHIFUPA WA MPAKANJIAA.