NENDENI MKAMALIZE MIGOGORO YA ARDHI NA SIGTAKI KUSIKIA VISHOKA WA ARDHI-DKT.KIJAZI

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt. Allan Kijazi,  akihutubia Kikao kazi cha Idara ya Menejimenti na Maendeleo ya Ardhi kilichofanyika jijini Dodoma jana na kuhudhuliwa na wakurugenzi wote wa Idara, Makamishna wa Ardhi nchi nzima.
Makamishina wa Ardhi na Wakurugenzi wa vitengo mbalimbali vya Ardhi wakimsikiliza katibu Mkuu wa Wizra hiyo,Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Allan Kijazi



 
HOTUBA YA KATIBU MKUU, WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI KATIKA KIKAO KAZI CHA IDARA YA MENEJIMENTI NA MAENDELEO YA ARDHI KITAKACHOFANYIKA KATIKA UKUMBI WA TUME YA UCHAGUZI JIJINI DODOMA

TAREHE 02 OKTOBA, 2022

 

Kamishna wa Ardhi,

Wakurugenzi wa Idara na Vitengo,

Makamishna wa Ardhi Wasaidizi,

Ndugu Watumishi wa Idara ya Menejimenti na Maendeleo ya Ardhi,

Mabibi na Mabwana,

“Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania…”

Awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana mahali hapa katika kikao hiki muhimu ambapo tutajadili masuala mbalimbali kuhusu utawala wa ardhi ikiwemo changamoto zinazoikabili sekta ya ardhi na ufumbuzi wa changamoto hizo.

Pili, nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kusafiri na kufika salama kwa ajili ya kikao hiki muhimu.

Ndugu Watumishi; Tumekutana leo ikiwa ni utekelezaji wa utaratibu niliojiwekea wa kukutana na wataalam wa Idara zinazounda Wizara ya Ardhi. Malengo ya kikao kazi hiki, pamoja na masuala mengine ni kukumbusha majukumu yetu, kuibua changamoto zilizopo na kuweka utaratibu utakaowezesha utekelezaji wa malengo ya Wizara ya Ardhi hususan katika ukusanyaji wa maduhuli ya ardhi na kuweka mifumo itakayorahisisha utoaji huduma kwa wananchi kwenye  ushughulikiaji wa kero/malalamiko ya ardhi kwa wananchi, uharakishaji wa uandaaji na ukamilishaji wa hatimilki kwa kwa kila ombi linalopokelewa na utendaji kazi wenye weledi na ufanisi.Ndugu watumishi; Idara ya Menejimenti na Maendeleo ya Ardhi kwa kushirikiana na Wataalam wengine imepewa jukumu muhimu la kusimamia utawala wa ardhi kwa kuzingatia Sera na Sheria za Ardhi. Uzito wa jukumu hili unatokana na ukweli kuwa ardhi ni rasilimali muhimu sana kwa ustawi wa maendeleo ya uchumi wa Taifa na jamii kwa ujumla. Aidha, ni rasilimali ambayo ni mhimili wa uzalishaji wa sekta nyingine zote. Hivyo, jukumu tulilopewa la usimamizi linapaswa kupewa umuhimu na uzito wa kutosha.

Ndugu Watumishi; Ninyi kama watalaam wa masuala ya usimamizi wa ardhi ni muhimu kufahamu kuwa mmepewa jukumu la kuanzisha na kusimamia taratibu za kuthamini,kupanga, kupima, kumilikisha na kusajili ardhi, kusimamia masharti ya umiliki wa ardhi kwa milki zote zilizopo kwenye maeneo yenu, kusimamia makusanyo ya maduhuli ya Serikali yatokanayo na sekta ya ardhi pamoja na kushughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi inayojitokeza.

Ndugu Watumishi; Kwa uzito wa majukumu haya mnapaswa mujiulize je mnayatekeleza majukumu hayo ipasavyo? Au tumekuwa hatuyatekelezi mpaka tukumbushwe na viongozi wetu? Je, tumejiwekea malengo yetu sisi wenyewe katika kutekeleza majukumu hayo katika ofisi zetu, idara zetu, wilaya au mikoa wetu? Au tumekuwa tukifanya kazi kwa mazoea? Je, tumejiwekea ratiba za kutatua kero na malalamiko ya wananchi yanayojitokeza katika maeneo yetu?

Mnatakiwa kutambua kuwa majukumu mnayotekeleza siyo hisani bali ni wajibu wenu na mnapaswa kuyafanya  kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu ili kufikia malengo tuliojiwekea na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Ndugu Watumishi; Suala la ulazima wa kutumia Mifumo ya kielktroniki si la kujadiliana tena katika Ulimwengu wa sasa. Katika majukumu yenu mnapaswa kuhakikisha kuwa kumbukumbu zote za viwanja na mashamba zinaingizwa katika mifumo ya TEHAMA iliyopo(ILMIS na Molis V3). maana inarahisisha utoaji huduma na kuleta ufanisi ikiwemo kupunguza migogoro isiyo ya lazima. Nayasema haya kwani hadi sasa baadhi yenu hamjakamilisha zoezi la kuingiza kumbukumbu za ardhi kwenye mifumo hali inayosababisha kupotea kwa baadhi ya kumbukumbu na kuikosesha Serikali mapato yatokanayo na sekta ya ardhi. Hivyo naelekeza kuwa hadi kufikia tarehe 30 Novemba, 2022 majalada yote yawe yameingizwa kwenye mfumo.

Ndugu Watumishi; Usalama wa miliki unaendana na upatikanaji wa hatimilki kwa wakati.  Wizara imekuwa ikipokea malalamiko ya ucheleweshaji wa utoaji wa hati katika ofisi zenu. Hivi karibuni niliamua kutoa maelekezo ya kuhakikisha malalamiko yote ya wananchi yanayotokana na ucheleweshaji wa hati yanapatiwe ufumbuzi ndani ya mwezi mmoja. Aidha, nilielekeza muanzishe utaratibu wa kutoa huduma jumuishi za utoaji hati (One Stop Office) kwa lengo la kurahisisha upatikanaji hati kwa wananchi.

Natambua tayari kila Mkoa umeanzisha utaratibu huu ambao nimeelekza uwe wa kudumu. Napenda mtambue kuwa utekelezaji wa agizo hili  utatumika kama kipimo cha utendaji kazi wenu katika maeneo yenu ya kazi.

Aidha, naelekeza mhakikishe mnatoa elimu ya ardhi, taratibu na huduma mbalimbali za ardhi mnazozitoa ili kuwezesha wananchi kuwa na elimu ya ardhi itakayowasaidia kuepukana na malalamiko yasiyokuwa ya lazima yanayotokana na uelewa hafifu wa taratibu mbalimbali za ardhi.

Ndugu Watumishi; Zoezi la usimamizi wa miradi ya Kupanga, kupima na kumilikisha ardhi nchini lipo chini yenu Makamishna na Maafisa ardhi.  Taarifa zilizopo hadi sasa ni Halmashauri chache zilizoweza kukamilisha urejeshaji wa fedha hadi sasa, aidha, zipo Halmashauri ambazo hazijaanza kabisa kutekeleza mradi huo.

Ninaelekeza mkafuatilie na kuwasilisha taarifa ya kina ya utekelezaji wa mradi huo katika maeneo yenu pamoja na hatua mlizozichukua kukabiliana na changamoto zilizojitokeza. Taarifa hii iwasilishwe kwangu ndani ya muda wa wiki mmoja kuanzia tarehe ya kikao hiki. Aidha, ni muhimu mkakumbuka kuwa fedha zilizotolewa ni mkopo toka Serikalini na tunawajibika kuzirudisha kama tulivyoingia kwenye makubaliano. 

Ndugu Watumishi; Ukusanyaji wa Maduhuli yatokanayo na sekta za Ardhi ni mojawapo ya jukumu la msingi la Wizara. Katika mwaka wa fedha 2022/23 Wizara inatakiwa kukukusanya shilingi bilioni 250.1. Lengo hili litafikiwa ikiwa kila mmoja wetu atatekeleza ipasavyo majukumu yake katika nafasi yake pamoja na kutekeleza mikakati mbalimbali tuliojiwekea ikiwemo kuhuisha na kutunza kumbukumbu za wamiliki wa ardhi katika mfumo wa kielektroniki ili kurahisisha utumaji wa ankara; imarishaji wa miundombinu ya TEHAMA; kutoa elimu ya mlipa kodi; kuandaa na kuhuisha viwango vya ukadiriaji kodi; na kuhamasisha sekta binafsi kupanga na kupima maeneo mapya ili kuongeza wigo wa makusanyo.

Ndugu Watumishi; Mbali na lengo hilo, tunatambua sekta ya ardhi pamoja na mambo mengine, imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo migogoro ya ardhi. Katika kutatua changamoto hiyo, Wizara ya Ardhi imeweka mikakati mbalimbali ya kukabiliana na changamoto hiyo. Moja ya mikakati hiyo ni pamoja na kuanzisha madawati ya migogoro ya ardhi, kliniki za utatuzi wa migogoro ya ardhi, register za migogoro ya ardhi, kuanzisha kituo cha Mawasiliano kwa wateja (Contact Centre) kwa ajili ya kupokea na kuhakikisha kero na changamoto hizo zinatafutiwa ufumbuzi, kuunda Kamati mbalimbali za kutatua kero na malalamiko ya wananchi.

 Mfano wa Kamati hizo ni Kamati niliyoiunda tarehe 25 Julai, 2022 kwa ajili ya kupokea na kusikiliza kero/malalamiko ya ardhi ya wananchi na kuyapatia ufumbuzi. Kamati hiyo ilianza kutekeleza zoezi hilo katika mkoa wa Dar es Salaam tarehe 01 hadi 05 Agosti, 2022 na kufanikiwa kupokea malalamiko 386 kutoka kwa wananchi wa Halmashauri tano za Mkoa wa Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani katika Wilaya za Kibaha na Kisarawe. 

Katika zoezi hilo, Kamati ilibaini vyanzo nane (8) vya migogoro/malalamiko ya ardhi katika Mkoa Dar es Salaam moja ya vyanzo hivyo ni Uvamizi wa maeneo yenye milki za watu wengine (25.3%), uelewa mdogo wa taratibu za ardhi na masuala ya mikataba (24.3%); na migogoro iliyotolewa uamuzi na mahakama (16.6%).

Zoezi hilo limeendelea tarehe 26-30 Septemba, 2022 katika Mkoa wa Dodoma kwa upande Jiji la Dodoma pekee, ambapo jumla ya malalamiko 809 yamepokelewa. Hii inaonesha wazi kuwa wengi wa wananchi hatukamilishi masuala yao ipasavyo na hatutoi elimu ya kutosha kuhusu masuala ya ardhi hali inayopelekea kuwepo kwa malalamiko mengi ambayo yanasababisha wananchi kupoteza imani na Serikali yao pia kuiingizia Serikali hasara.

 Naelekeza kuwa kila Halmashauri na Mkoa ihuishe register za migogoro ya ardhi ya maeneo yake na pia kilniki za utatuzi wa migogoro kwa kila Halmashauri na Mkoa zitekelezwe na taarifa ziwasilishwe kila ifikapo tarehe ya mwisho ya kila mwezi. Aidha, kila Halmashauri na Mkoa leo hii iwasilishe jina na mawasiliano ya simu ya mratibu wa utatuzi wa kero/malalamiko na migogoro ya ardhi. 

Pamoja na maelekezo hapo juu, naagiza kuwa moja wapo ya kazi ya mratibu wa migogoro ni kuratibu na kusimamia ipasavyo suala dawati la utatuzi wa migogoro ya ardhi yaliyopo katika maeneo yao na kuhakikisha migogoro ya ardhi inasajiliwa na kutatuliwa kwa wakati chini ya usimamizi wenu wateule na makamishna wa ardhi.

 Ndugu Watumishi; Suala la kufanya kazi kwa Weledi na Uadilifu ni la lazima kwa kila mtumishi wa umma; baadhi ya maafisa ardhi siyo waadilifu, wanafanya kazi bila kuzingatia Sheria, Kanuni, taratibu na Miongozo iliyopo. Hali inayopelekea kuongezeka kwa malalamiko ya wananchi juu ya uwepo wa milki pandikizi, wananchi kuombwa rushwa, ucheleweshaji wa kupatiwa hatimilki na huduma zinginezo. 

Naelekeza ninyi wasimamizi wa walio chini yenu mhakikishe mnawasimia watumishi ili watekeleze  majukumu yao kwa mujibu wa Sheria na taratibu zote na ambaye atakiuka, hatua stahiki za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa.

 Ndugu Watumishi; Kutokana na maelezo hayo na kwa kuwa leo mpo hapa, kila mtumishi abainishe changamoto zilizopo kwenye eneo lenu na mapendekezo ya utatuzi wake, lengo likiwa ni kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Ni matumaini yangu kuwa kila mtumishi atashiriki katika kubainisha changamoto hizo na kutoa mapendekezo ya utatuzi wake. Baada ya maelezo hayo, nawashukuru sana kwa usikivu wenu na nawatakiwa majadiliano na kikao chema.

 

Asanteni kwa kunisikiliza.

Comments

Popular posts from this blog

UNAMKUMBUKA AMINA CHIFUPA WA MPAKANJIAA.

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?

KADA MGEJA AHUDHURIA MAZIKO YA MAMA MZAZI WA MWANDISHI MWANDAMIZI WA HABARI KAHAMA