WAZIRI MKENDA ATANGAZA TUME YA MIKOPO KWA WANAFUNZI ELIMU YA JUU

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda akitangaza tume ya kuchunguza utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu tarehe 29 Julai 2022 Jijini Dar es laam wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini juu ya mwelekeo wa Wizara, Vipaumbele na maeneo ya kimkakati katika utekelezaji kwa Mwaka wa fedha 2022/23.

Na
Mathias Canal, WEST

Wakati dirisha la maombi ya mikopo kwa mwaka wa masomo 2022/2023
likiwa wazi kwa muda wa siku 70 kuanzia Julai 19 hadi Septemba 30 mwaka huu, Serikali
imetangaza Tume ya watu watatu kuchunguza utoaji wa mikopo.

 

Tume hiyo itaongozwa na Prof Allan Mushi ambaye ni mhadhiri kutoka
Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro, Idd Makame kutoka Zanzibar na Dkt Martin
Chegeni ambao wote kwa pamoja ni wataalamu wa mifumo waliobobea katika sayansi
ya Kompyuta na Takwimu.

 

Tume hiyo itachunguza uhalali katika utoaji wa mikopo kwa
wanafunzi wa elimu ya juu kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2017/2018
mpaka 2021/2022 ili kubaini kama kulikuwa na upendeleo kwa watu wasiokuwa na
sifa.

 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ametangaza
tume hiyo tarehe 29 Julai 2022 Jijini Dar es laam wakati akizungumza na
wahariri wa vyombo vya habari nchini juu ya mwelekeo wa Wizara, Vipaumbele na
maeneo ya kimkakati katika utekelezaji kwa Mwaka wa fedha 2022/23.

 

Waziri Mkenda amesema kuwa Tume hiyo itapitia malalamiko ya
wanafunzi mbalimbali nchini ambao wamekuwa wakiyatoa kuhusu upendeleo wa utoaji
mikopo kwa kupata mikopo kwa wanafunzi wenye sifa huku wale wasiokuwa na sifa
stahiki wakikosa mikopo hiyo.

 

“Na kwenye hili tunakaribisha watu watoe taarifa kwa sababu kama
kuna mtoto wa Mkenda uliyesoma nae utakuwa unamjua baba yake ni nani na uwezo
wake, halafu wewe unaona mtu huyo amepewa mkopo toa taarifa” Amekaririwa Waziri
Mkenda na kuongeza kuwa

 

“Mtu yeyote ambaye ana wasiwasi na utoaji wa mikopo tunamkaribisha
ili aweze kuisaidia tume kufanya kazi yake kwa kuwa na taarifa zenye usahihi wa
hali ya juu kutoka kwa wanachi husika”

 

Prof Mkenda amesema kuwa tume hiyo itaangalia vigezo
vilivyoainishwa ili kuona kama kuna taarifa zingine za ziada zinaweza kutumika
katika utoaji wa mikopo ili fedha zinazotolewa na serikali zikopeshwe kwa haki.

 

Kadhalika, Waziri Mkenda amewahimiza waombaji mikopo ya elimu ya
juu kwa mwaka 2022/2023 kusoma na kuuzingatia ‘Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa mwaka
2022/2023’ ili kuwasilisha maombi kwa usahihi ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa
sahihi zilizowekwa kwa mujibu wa taratibu na sheria.

 

Katika mwaka wa masomo 2022/2023, Serikali imetenga kiasi cha TZS
573 bilioni kwa ajili ya kutoa mikopo na Udhamini (Scholaship) kwa wanafunzi wa
elimu ya juu nchini.


 

Comments

Popular posts from this blog

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?

AMANI YETU TUILINDE NAIBU WAZIRI CHANDE AZUNGUMZA KATIKA IJITIMAI JIJINI DODOMA

UNAMKUMBUKA AMINA CHIFUPA WA MPAKANJIAA.