TMDA YALONGA NA WANAHABARI KUHUSU MIKAKATI YAO

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),  Dkt. Adam Mitangu Fimbo,akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya habari Maelezo jijini Dodoma  ambapo alisema kuwa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba ni taasisi ya Serikali iliyopo chini ya wizara ya Afya yenye jukumu la kulinda afya ya jamii kwa kudhibiti ubora, Usalama na ufanisi wa dawa chanjo, vifaa tiba na vitendanishi pamoja na udhibiti wa bidhaa za Tumbaku.

Mkurugenzi huyo aliendelea kusema kwamba Kwa kipindi cha  Julai 2021 hadi 2022 kwa jumla malengo mkakati wa TMDA yametekelezwa kwa ufanisi  na kwa mafanikio makubwa.

TMDAemeendelea kushikilia cheti cha ithibati kwa  kiwango cha ISO 9001;2015 baada ya kukidhi vigezo kufuatia kaguzi zilizofanyika, Kaguzi hizo hufanyika kila baada ya miaka mitatu na wahakiki hutoka nje ya nchi.







Mkurugenzi akiwaonyesha wanahabari vyeti amabavyo hutolewa kwa ubora wa dawa

Wanahabari wakimsikiliza mkurugenzi alaipokuwa akizungumza



Mkurugenzi Msaidizi idara ya habari Maelezo Zamaladi Kawawa na Mkuu wa idara ya hjabari ya TMDA, Gaudencia Simwanza nao walikuwa katika mkutano huo
Mkurugenzi akipokea baadhi ya dawa kutoka kwa Zamaladi Kawawa, zilizoletwa kuonyeshwa waandishi wa habari ambazo hazifai kwa matumizi ya binadamu




Zamaladi Kawawa, akiongoza waandishi wa habari kuuliza maswali katika mkutano huo
Mkurugenzi na Zamaladi, wakiagana baada ya kumalizika mkutano huo

Zamaladi, akiwashukuru wanahabari kujitokeza katika mkutano huo. 

KWA TAARIFA ZAIDI FATILIA HOTUBA YA MKURUGENZI FIMBO;

TAARIFA YA MKURUGENZI MKUU WA TMDA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MAFANIKIO YA TAASISI KWA KIPINDI CHA MWAKA 2021/22 NA MATARAJIO KWA MWAKA 2022/23

Mkurugenzi, Idara ya Habari MAELEZO,
Waandishi wa Habari,

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ni taasisi ya Serikali iliyopo chini ya Wizara ya Afya yenye jukumu la kulinda afya ya jamii kwa kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa dawa, chanjo, vifaa tiba na vitendanishi pamoja na udhibiti wa bidhaa za tumbaku.

Taarifa ninayowasilisha hapa inaainisha hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa kazi na majukumu ya TMDA kwa kipindi cha Julai 2021 hadi Juni 2022 ambapo kwa ujumla Malengo Mkakati ya TMDA yametekelezwa kwa ufanisi na kwa mafanikio makubwa.  

Ni dhahiri kuwa mafanikio yaliyofikiwa na TMDA yametokana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita (6) chini ya uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata dawa, vifaa tiba, vitendanishi na chanjo zilizo bora, salama na fanisi.

Ndugu Waandishi wa Habari,

Katika kipindi cha Julai 2021 hadi Juni 2022, TMDA imefanikiwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba, Sura 219 kama ifuatavyo;

1.1 KUIMARISHA MIFUMO YA UTENDAJI KAZI (QUALITY MANAGEMENT SYSTEM)

TMDA imeendelea kushikilia cheti cha ithibati kwa kiwango cha ISO 9001: 2015 baada ya kukidhi vigezo kufuatia kaguzi zilizofanyika. Kaguzi hizi hufanyika kila baada ya miaka mitatu na wahakiki kutoka nje ya nchi. Hii imechangiwa na jitihada zinazofanywa katika kuboresha mifumo ya utoaji huduma sanjari na utekelezaji wa mifumo bora ya Utendaji Kazi (Quality Management System) katika kutoa huduma. Aidha huduma za TMDA zimeendelea kutolewa kwa kuzingatia viwango vya utoaji huduma vilivyoainishwa kwenye Mkataba wa Huduma kwa Wateja (Clients’ Service Charter - 2020 ili kukidhi mahitaji na matarajio ya wateja.

Aidha, Maabara ya TMDA imeendelea kushikilia hadhi kwa kutambuliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO prequalification) kwa kuwa na mifumo mahiri ya uchunguzi wa dawa. Kuendelea kutambuliwa kwa maabara ya TMDA kunatoa hakikisho la usalama, ubora na ufanisi wa bidhaa zinazodhibitiwa kwa wananchi na watumiaji.

Vile vile TMDA ni taasisi iliyohakikiwa na kuweza kufikia ngazi ya tatu kati ya nne (Maturity Level 3) ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya ubora wa mifumo ya udhibiti wa dawa. Mamlaka imeendelea kushikilia hadhi hii inayoashiria uwepo wa bidhaa bora salama na fanisi hapa nchini.

Ndugu Waandishi wa Habari,

1.2    UDHIBITI WA UBORA, USALAMA NA UFANISI WA DAWA, VIFAA TIBA NA VITENDANISHI

1.2.1    Tathmini na Usajili wa bidhaa za dawa, vifaa tiba na vitendanishi

Moja ya majukumu ya TMDA ni kutathmini na kusajili bidhaa za dawa, vifaa tiba na vitendanishi. Usajili wa bidhaa umeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka ambapo idadi ya bidhaa zilizosajiliwa imekuwa ikiongezeka. Katika kipindi cha mwaka 2021/22, Mamlaka imesajili jumla ya bidhaa 1,286 ambapo kati yake bidhaa za dawa za binadamu na mifugo ni 933 na vifaa tiba na vitendanishi ni 353. Kwa idadi hii jumla ya bidhaa zilizosajiliwa hadi sasa imefikia 8,831 ambapo kati yake bidhaa za dawa ni 6674 na vifaa tiba na vitendanishi ni 2,157. Hii inaashiria kiasi kikubwa cha dawa zinazotumika Tanzania zimehakikiwa na hivyo ni bora, salama na fanisi kwa matumizi ya binadamu.

1.2.2    Usajili wa majengo na ukaguzi    

Katika kipindi cha mwaka 2021/22, Mamlaka imesajili jumla ya maeneo 467 yanayojihusisha na biashara za bidhaa zinazodhibitiwa kwa lengo la kuhakikisha kuwa maeneo husika yanakidhi vigezo ili kutoathiri ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa.

Aidha, jumla ya maeneo 10,938 yanayojihusisha na biashara ya dawa, chanjo, vifaa tiba na vitendanishi yalikaguliwa kwa mwaka 2021/22 ikiwa ni ongezeko la maeneo 92 yaliyokaguliwa ikilinganishwa na maeneo 10,846 yaliyokaguliwa mwaka 2020/21.

1.2.3     Udhibiti wa uingizaji na usafirishaji wa bidhaa ndani na nje ya nchi

Kwa lengo la kuharakisha utoaji wa mizigo bandarini na kuboresha huduma, Mamlaka imeweka wakaguzi wake katika vituo vya forodha ambao hufanya kazi ya ukaguzi wa mizigo inayoingia na kutoka nje ya nchi. Jumla ya vituo vya forodha 32 vinatambulika kikanuni kuruhusu kuingia na kutoka kwa bidhaa zinazodhibitiwa na TMDA.

Kwa mwaka 2021/22, jumla ya vibali 15,478 (6,002 dawa na 9,476 vifaa tiba na vitendanishi) sawa na ongezeko la 116% ukilinganisha na vibali 13,259 vilivyotolewa mwaka 2020/21 vilitolewa. Kwa ujumla Mamlaka imetoa jumla ya vibali 63,871 vya kuingiza na kusafirisha bidhaa nje ya nchi hadi kufikia mwezi Juni 2022. Ongezeko hili limechangiwa na kuimarika kwa mfumo wa kieletroniki wa utoaji vibali vya kuingiza na kutoa nchini bidhaa unaomwezesha mteja kutuma maombi, kufanya malipo popote alipo na hatimaye kupata kibali ndani ya masaa 24.

1.2.4     Ukaguzi wa viwanda vya dawa na vifaa tiba
Viwanda 15 vya dawa (8 vilivyosajiliwa na 7 vipya) ndani ya nchi vilikaguliwa ambapo viwanda viwili (2) kati ya 7 vipya vimekidhi vigezo na vinatarajiwa kuanza uzalishaji hivi karibuni. Hili Ni ongezeko la viwanda 6 sawa na 67% ikilinganishwa na viwanda 9 vilivyokaguliwa mwaka 2020/21. Aidha, jumla ya viwanda vipya 21 vya vifaa tiba vilisajiliwa ikiwa ni ongezeko la viwanda 18 ikilinganishwa na viwanda vitatu (3) vilivyosajiliwa mwaka 2020/21. Hadi kufikia mwezi Juni 2022 jumla ya viwanda 17 vya dawa, 26 vya vifaa tiba na 6 gesi tiba vimesajiliwa na kuanza kufanya kazi.
    
1.2.5. Operesheni maalum kwenye soko  

Katika kipindi cha mwaka 2021/22 Mamlaka iliendesha operesheni tatu (3) maalum katika mikoa 14 ambapo maeneo 1,355 ya biashara yalikaguliwa. Operesheni hizi ziliwezesha kubainika na kukamatwa kwa dawa bandia aina nne (4), dawa duni aina tano (5), dawa za Serikali na dawa ambazo hazijasajiliwa. Thamani ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi vilivyokamatwa kwa kutosajiliwa ilikuwa TZS 353,839,338. Thamani ya dawa na vifaa tiba vya Serikali ilikuwa TZS 13,035,000 na thamani ya dawa zilizokwisha muda wa matumizi ilikuwa TZS 28,642,150. Hatua za kisheria zilichukuliwa dhidi ya watuhumiwa. Hata hivyo, kiasi cha bidhaa duni na bandia katika soko kimekuwa kikipungua ambapo hadi sasa tatizo la dawa duni na bandia liko kwa asilimia moja (1%).

Ndugu Waandishi wa Habari,

1.2.6     Ufuatiliaji wa ubora wa dawa na vifaa tiba na Udhibiti wa majaribio ya dawa

TMDA hufuatilia, kuondoa na kuteketeza bidhaa ambazo hazikidhi vigezo vya ubora, usalama na ufanisi ili kuepusha bidhaa husika zisitumiwe na walaji. Mpango wa Ufuatiliaji wa Ubora wa Bidhaa katika Soko (Post Marketing Surveillance Programme – PMS) hutumika wakati wa ufuatiliaji huu. Kwa mwaka wa fedha ninaoutolea taarifa, jumla ya sampuli 215 za dawa zilifuatiliwa na kuchunguzwa ambapo matokeo ya uchunguzi yalionesha kuwa dawa zote sawa na 100% zilifaulu vipimo vya kimaabara.

Kwa upande wa vifaa tiba na vitendanishi, jumla ya sampuli za matoleo 567 zilichunguzwa na sampuli 522 sawa na 92% zilikidhi vigezo. Hiki ni kiashiria kuwa kiasi kikubwa cha bidhaa za dawa na vifaa tiba kilichoko kwenye soko la Tanzania kinakidhi vigezo vya ubora.  

Aidha, idadi ya majaribio ya dawa yaliyoidhinishwa imeongezeka kutoka 11 mwaka 2020/21 na kufikia 34 mwaka 2021/22. TMDA hutathmini na kuidhinisha majaribio ya dawa yanayofanyika kwa binadamu hapa nchini ili kuhakikisha yanazingatia sheria, kanuni, miongozo na vigezo vya kulinda afya ya wale wanaofanyiwa majaribio hayo.

1.2.7     Kuteketeza bidhaa zisizofaa kwa matumizi

Katika mwaka 2020/21, kiasi na thamani ya bidhaa za dawa na vifaa tiba visivyofaa kwa matumizi ya binadamu zilizoteketezwa imeongezeka kutoka tani 14,704.80 zenye thamani ya TZS 8.5 bilioni zilizoteketezwa mwaka 2020/21 na kufikia jumla ya tani 35,547.47 zenye thamani ya takribani TZS 35.53 bilioni zilizoteketezwa mwaka 2021/22. Bidhaa hizi zinajumuisha bidhaa zilizotolewa taarifa na zile zilizokamatwa katika kaguzi mbalimbali. Kuongezeka kwa bidhaa zilizoteketezwa kunatokana na kuimarisha ukaguzi na elimu kwa umma inayosaidia wateja kutoa taarifa juu ya bidhaa zisizofaa kwa matumizi.
    
1.2.8     Udhibiti wa bidhaa za tumbaku

Mamlaka iliandaa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2021-26) wa Kitaifa wa Kupambana na Tumbaku pamoja na Mpango Kazi wa Miaka Mitano wa Udhibiti wa Tumbaku ambao umeanza kutekelezwa. Tumeweka tayari mfumo wa udhibiti wa bidhaa hizi na hadi sasa tumekwishatambua bidhaa zote za tumbaku zilizoko kwenye soko ambapo idadi yake hadi sasa ni bidhaa 51. Aidha, Mamlaka imeanzisha maabara ya upimaji wa bidhaa za tumbaku kwenye jengo lake lililoko hapa Dodoma.
    
1.2.9     Ufuatiliaji wa madhara yatokanayo na matumizi ya bidhaa

Mamlaka imeweka mifumo madhubuti ya ufuatiliaji wa madhara yatokanayo na matumizi ya dawa, chanjo na vifaa tiba (kitaalam vigilance system) ili kuweza kubaini, kutathmini na kuzuia madhara yasiyovumilika yasitokee kwa wananchi. Aidha, ili kuimarisha upatikanaji wa taarifa hizo, TMDA imeanzisha mfumo wa kielektroniki ujulikanao kama ADR Reporting Tool wa utoaji wa taarifa za madhara yatokanayo na matumizi ya dawa kwa kutumia simu za mkononi au kompyuta na kwa njia ya kutuma ujumbe mfupi kwenye simu. Kupitia mfumo huu TMDA imepokea jumla ya taarifa 4,898 katika kipindi husika na hadi sasa kuna jumla ya taarifa 31,666 kwenye Mfumo wa Taarifa unaosimamiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ujulikanao kama Vigibase. Hata hivyo taarifa hizi ni za maudhi madogo ambayo hayapelekei kuondoa dawa kwenye soko.

1.3    Uchunguzi wa sampuli katika Maabara za TMDA

1.3.1. Maabara za Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma

TMDA ina jumla ya Maabara tatu (3) hadi sasa ambazo zimejengwa jijini Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma. Maabara hizi jukumu lake ni kufanya uchunguzi wa sampuli za bidhaa kwa lengo la kujiridhisha na ubora na usalama  wake ili kuiwezesha Mamlaka kufanya maamuzi ya kiudhibiti kabla ya aidha kuruhusu au kutoruhusu bidhaa kutumika. Maabara ya kupima vifaa tiba kwenye Maabara iliyoko Dar es Salaam imeimarishwa na vile vile Maabara ya kupima bidhaa za tumbaku iliyoko hapa Dodoma imewekewa mitambo ya kisasa ya upimaji wa bidhaa hizi.

Katika kipindi cha mwaka 2021/22 maabara hizi zimefanya uchunguzi wa sampili 1,808 za dawa vifaa tiba, vitendanishi na vipukusi ambapo sampuli 1,644  sawa na 91% zilifaulu. Kiwango cha ufaulu wa bidhaa zilizochunguzwa umeongezeka kutoka 88% (mwaka 2020/21) hadi kufikia 91% (2021/22). Hii imetokana na kuongezeka kwa uelewa miongoni mwa wadau na kuimarika kwa udhibiti wa bidhaa katika soko.  

1.3.2 Maabara hamishika (Minilab kits)

Aidha, jumla ya sampuli 2,289 zilichunguzwa kupitia maabara hamishika kwenye vituo 25 nchini kwa lengo la kufanya uchunguzi wa awali wa dawa ambapo sampuli zote zilifaulu.

Ndugu Waandishi wa Habari,

1.4    UTOAJI ELIMU KWA UMMA NA HUDUMA KWA WATEJA

Katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi juu ya ubora, usalama na ufanisi wa dawa, chanjo, vifaa tiba na vitendanishi, elimu imeendelea kutolewa kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na mihadhara (outreach campaigns) katika mikoa 23 ya Tanzania, kipindi cha Televisheni cha TMDA NA JAMII, matangazo ya redioni na kupitia Mitandao ya kijamii. Aidha Mamlaka imeanzisha vilabu 55 vya masomo katika baadhi ya shule za sekondari katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Singida, Dodoma na Mtwara. Vilevile, kupitia mitandao ya kijamii idadi ya watu wanaofuatilia kurasa za mitandao husika imefikia 193,000 (Instagram 4362, facebook 15,000, Tweeter 174 na Youtube 40)

Ndugu Waandishi wa Habari,

1.5    USIMAMIZI WA RASILIMALI

1.5.1     Rasilimali Watu

Mamlaka imefanikiwa kuongeza ajira kwa kuzingatia Mpango wake wa Rasilimali Watu (Human Resources Plan) ambapo idadi ya watumishi imeongezeka kutoka 328 waliokuwepo mwezi Julai 2021 hadi kufikia 342 mwezi Juni 2022.  Vile vile, baada ya kupata kibali tumeweza kupandisha madaraja au vyeo jumla ya watumishi 97 na kubadilisha kazi (recartegorization) watumishi 5. Pia, jumla ya watumishi 53 wamehudhuria mafunzo ya muda mfupi na mrefu ndani na nje ya nchi. Watumishi wengine 82 wamepangwa kwenda kwenye mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa mwaka 2022/23.

1.5.2     Utekelezaji wa miradi ya Maendeleo

Pamoja na kukamilisha ujenzi wa Maabara iliyoko hapa Dodoma, Mamlaka pia imeanza kutekeleza mradi wa kusimika matanuru ya kuteketeza bidhaa zisizofaa kwa matumizi ya binadamu (incinerators) katika mikoa ya Pwani na Dodoma. Lengo hapa ni kusaidia kuteketeza bidhaa duni na bandia zinazokamatwa kwenye soko kupitia kaguzi na operesheni zinazofanyika mara kwa mara.

1.5.3     Mapato, Matumizi na Gawio kwa Serikali

Katika kipindi husika, TMDA imeweza kukusanya jumla ya TZS 39,904,191,503 ambayo ni asilimia 106 ya lengo la kukusanya TZS 37,799,195,573 kwa mwaka. Kati ya fedha hizi, TZS 35,377,240,188 ni makusanyo ya ndani. Matumizi kwa ujumla yalikuwa TZS 37,048,519,897.61. Gawio kwa Serikali tumekwishatoa jumla ya TZS 5,508,396,736.20.

Ndugu Waandishi wa Habari,

1.7    USHIRIKIANO WA KIKANDA NA KIMATAIFA

TMDA inashiriki kwenye mipango ya uwianisho wa taratibu za udhibiti wa dawa katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Bara la Afrika (SADC). Kupitia Mipango hii, taasisi za udhibiti wa dawa za nchi wanachama zimekuwa na mifumo thabiti ya pamoja ya udhibiti wa dawa na hivyo kusaidia upatikanaji wa dawa bora, salama na fanisi. Kupitia EAC hadi sasa jumla ya dawa 85 zimesajiliwa na sasa zinauzwa kwenye zote wanachama.

Kupitia mashirikiano haya, Mamlaka imeweza pia kutoa mafunzo kwa wenzetu kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa ya nchini Botswana (BOMRA), Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa nchini Uganda (NDA) na Taasisi ya Uchunguzi wa Magonjwa ya Binadamu ya Zanzibar (ZAHRI).

Ndugu Waandishi wa Habari,

Katika kuhakikisha TMDA inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, mambo yafuatayo yatapatiwa kipaumbele katika mwaka 2022/23.

a)    Kuimarisha ukaguzi wa bidhaa katika vituo vya forodha na maeneo ya biashara za dawa, vifaa tiba, vitendanishi na bidhaa za tumbaku,
b)    Maabara kuendelea kushikilia vyeti vya kimataifa na kuimarisha maabara zake za kupima bidhaa za tumbaku, dawa za mitishamba, vitendanishi na vipukusi.
c)    Kuimarisha usimamizi wa makusanyo ya maduhuli kutoka vyanzo vya ndani ili kufikia lengo na kuweza kuchangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali;
d)    Kutekeleza Mkakati wa Kuendeleza Viwanda vinavyozalisha dawa ndani ya nchi ili viweze kukidhi Taratibu za Utengenezaji Bora wa Dawa (kitaalam Good Manufacturing Practices - GMP);
e)    Kukamilisha ujenzi wa miradi ya matanuri ya kuteketeza bidhaa zisizofaa yatakayojengwa mikoa wa Pwani na Dodoma pamoja; na
f)    Kuendelea kuboresha mifumo ya utoaji huduma bora kwa wateja na kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya bidhaa inazozidhibiti ili jamii iweze kufanya maamuzi sahihi kabla na baada ya kutumia.
Ndugu Waandishi wa Habari, naomba kuhitimisha kwa kusema kuwa ili utekelezaji wa mipango yote ya udhibiti wa ubora, usalama  na ufanisi ifanikiwe, taarifa za idadi ya watu zinahitajika. Hivyo natoa rai kwa watu wote tujitokeze kuhesabiwa siku ya tarehe 23 Agosti, 2022 ili kwa pamoja tushiriki katika kulinda afya ya jamii. Kwa TMDA idadi ya watu inatusaidia sana kwa mfano kufahamu ni taarifa ngapi za madhara ya dawa zinatakiwa kwa kulinganisha idadi ya watu walioko hapa nchini.

Imetolewa na:

Adam Mitangu Fimbo
Mkurugenzi Mkuu
Dodoma
    29 Julai, 2022   

 

Comments

Popular posts from this blog

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?

AMANI YETU TUILINDE NAIBU WAZIRI CHANDE AZUNGUMZA KATIKA IJITIMAI JIJINI DODOMA

UNAMKUMBUKA AMINA CHIFUPA WA MPAKANJIAA.