TLS KULINDA UTAWALA WA SHERIA, KUMSHTAKI MAKONDA TAARIFA KWA UMMA

 Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika  (TLS), Tundu Lissu, akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana kuhusu maazimio yaliyofikiwa na Baraza la Uongozi la chma hicho na hatua  za kuchukus dhidi ys Serikali. Kushoto ni Makamu wa Chama hicho Godwin Ngwilimi na Kulia ni Wakili na Mwenyeji wao Stephine Kuwayawaya. 


Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) limemaliza kikao chake cha kawaida cha siku mbili kilichofanyika Dodoma kwa kuazimia kuchukua hatua kadhaa zenye lengo la kulinda Utawala wa Sheria na uwajibikaji katika nchi yetu. 


Akitangaza maazimio ya Baraza hilo, Rais wa TLS na Mwenyekiti wa kikao hicho, Mh. Tundu A.M. Lissu, alizitaja hatua zitakazochukuliwa kuwa ni pamoja na TLS kufungua mashtaka binafsi ya jinai dhidi ya Mkuu wa Dar es Salaam, Paul Makonda aka Daudi Albert Bashite, kwa tuhuma za makosa mbali mbali ya jinai ikiwamo kutumia vyeti feki, ujambazi wa kutumia silaha, matumizi mabaya ya madaraka, n.k.
 

Mh. Lissu alisema: "Dhana ya Utawala wa Sheria ina maana, pamoja na mambo mengine, sio tu kwamba hakuna mtu aliyeko juu ya sheria, bali pia kwa kila mtu, bila kujali cheo au nasaba au hali yake kiuchumi na kijamii yuko chini ya udhibiti wa sheria za kawaida za nchi yetu na yuko chini ya mamlaka ya mahakama za kawaida zilizoanzishwa kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Nchi.
 

"Kwa bahati mbaya, katika nchi yetu, kumejitokeza dhana ya hatari na imani potofu: kwamba Rais yuko juu ya sheria. Kwamba Rais anatawala sheria na sio sheria inayomtawala Rais. Kwamba Rais na watu wake wanaweza kufanya chochote wanachotaka kufanya bila kujali sheria za nchi na bila kuwa na hofu ya kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria.
 

"Utovu wa uwajibikaji wa viongozi, matumizi mabaya ya madaraka na vitendo vya wazi wazi vya kijinai vimekuwa ndio kanuni kuu za utawala katika kipindi hiki. Utekaji nyara, upotezaji, kuweka watu vizuizini na utesaji wa watu wanaohisiwa au kutuhumiwa kuwa wakosoaji wa serikali au wahalifu vimekuwa ni vitu vya kawaida katika utawala huu. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aka Daudi Albert Bashite, ni kielelezo kizuri cha vitendo hivi."
Kuna tuhuma za muda mrefu sasa kwamba Mkuu huyo wa Mkoa ametumia vyeti vya shule ya sekondari visivyokuwa vyake. 


Kwamba yeye sio Paul Makonda bali ni Daudi Albert Bashite; kwamba Paul Makonda halisi yupo na ndiye mwenye vyeti vinavyoaminika kutumiwa na Bashite. Kitendo hiki ni kosa la jinai kwa mujibu wa sheria za Tanzania.
Kifungu cha 120 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria za 


Tanzania, kinasema: "Mtu yeyote aliye kwenye utumishi wa umma ambaye, wakati akitekeleza majukumu ya ofisi yake, akifanya kitendo cha udanganyifu au akikiuka dhamana ya mamlaka yake na kuathiri umma, kama udanganyifu au ukiukaji dhamana huo ungekuwa ni kosa la jinai kama ungefanywa na mtu binafsi au la, anafanya kosa na endapo atapatikana na hatia atapata adhabu ya kifungo cha miaka saba jela."
 

Kwa kutumia vyeti vya shule visivyokuwa vyake; kwa kutumia majina ya mtu mwingine wakati akiwa mtumishi wa umma, Daudi 

Bashite ameathiri imani ya wananchi kwa serikali iliyopo madarakani kwamba inaajiri na kulinda watu wadanganyifu na wasiokuwa na vyeti halali vya kitaaluma. Mtu huyu amefanya kosa la jinai ambalo kwalo anastahili kushtakiwa mahakamani na kuadhibiwa endapo atapatikana na hatia anastahili kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria za kawaida za nchi yetu.
 

Mh. Lissu alisema kwamba Paul Makonda aka daudi Bashite hajafanya kosa hilo peke yake. Kwa kitendo chake cha kuvamia kituo cha kurushia matangazo cha Clouds Media Group yapata miezi miwili iliyopita, Mkuu huyo wa Mkoa amefanya makosa mengine mengi ya jinai kama ifuatavyo:
1)    Kosa la matumizi mabaya ya madaraka kinyume na kifungu cha 7(9) cha Sheria ya Tawala za Mikoa, 1997, kikisomwa pamoja na kifungu cha 96 cha Kanuni ya Adhabu;

2)    Kosa la kutumia vitisho (threatening violence) kinyume na kifungu cha 89 cha Kanuni ya Adhabu kwa kuingia kwa nguvu kwenye studio za Clouds Media Group na kutishia kuwadhuru wafanyakazi wa Clouds Media Group;

3)    Kosa la kutishia (intimidation) kinyume na kifungu cha 89B cha Kanuni ya Adhabu, kwa kuingia kwa nguvu Clouds Media Group na kuchukua vitendea kazi vya studio huku akiwa na silaha;
4)    Kosa la kukiuka sheria nyingine yoyote iliyotungwa kwa kufanya kitendo kinachokatazwa na sheria hiyo kinyume na kifungu cha 123 cha Kanuni ya Adhabu;

5)    Kosa la wizi wa kutumia nguvu (robbery) kinyume na kifungu cha 285 cha Kanuni ya Adhabu kwa kutumia nguvu kunyang'anya vitendea kazi (rekodi ya matangazo) vya Clouds Media Group;

6)    Kosa la wizi wa kutumia silaha (armed robbery) kinyume na kifungu cha 287A cha Kanuni ya Adhabu kwa kuvamia studio za Clouds Media Group na kunyang'anya vitendea kazi vya studio hiyo kwa kutumia silaha za moto;

7)    Kosa la shambulio kwa lengo la kuiba kinyume na kifungu cha 288 cha Kanuni ya Adhabu kwa kuwashambulia wafanyakazi wa Clouds Media Group kwa lengo la kuwaibia vitendea kazi vya matangazo;

8)    Kosa la kuvunja na kuingia katika nyumba au jengo wakati wa usiku kwa lengo la kufanya uhalifu kinyume na vifungu vya 293, 294(2), 296 na 297 vya Kanuni ya Adhabu kwa kitendo cha kuvamia studio za Clouds Media Group kwa lengo la kufanya uhalifu na kwa kufanya vitendo vya uhalifu;

9)    Kosa la kutembea na silaha kwa lengo la kufanya uhalifu kinyume na kifungu cha 298(a), (b) na (f) cha Kanuni ya Adhabu kwa kutembea na silaha wakati wa uvamizi wao wa studio za Clouds Media Group kwa lengo la kufanya uhalifu;

10)    Kosa la kuingilia kijinai (criminal trespass) kinyume na kifungu cha 299(a) cha Kanuni ya Adhabu kwa kuingia kwa nguvu na bila uhalali wowote studio za Clouds Media Group kwa lengo la kufanya uhalifu au kwa lengo la kutishia, kutukana au kuwaudhi wamiliki au watumiaji wa studio hizo.
 

Kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Makonda aka Bashite alipaswa kuchukuliwa hatua za jinai na Jeshi la Polisi, pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kwa mujibu wa ibara ya 59B(2) ya Katiba ya nchi yetu. Ibara ya 59B(4) ya Katiba inaelekeza kwamba katika kutekeleza mamlaka yake, "Mkurugenzi wa Mashtaka atakuwa huru, hataingiliwa na mtu yeyote au na mamlaka yeyote na atazingatia ... nia ya kutenda haki, kuzuia matumizi mabaya ya taratibu za utoaji haki na maslahi ya umma."
 

Kanuni hii kuu pia imefafanuliwa na kutiliwa nguvu na kifungu cha 8 cha Sheria ya Mamlaka ya Mashtaka ya Taifa, 2008 (National Prosecutions Service Act, 2008). Kwa mujibu wa Sheria hii, 
Mkurugenzi wa Mashtaka ana mamlaka sio tu ya kudhibiti mashtaka yote ya jinai bali pia kuratibu shughuli za upelelezi wa makosa ya jinai [kifungu cha 16(1)].
Aidha, kwa mujibu wa kifungu cha 17(1) na (3), Mkurugenzi ana uwezo wa kutoa maelekezo ya maandishi kwa ofisa yeyote wa umma ili apatiwe taarifa yoyote inayohusu upelelezi au uendeshaji wa mashtaka ya jinai na ofisa huyo anatakiwa kutii maelekezo hayo.
 

Hadi sasa, sio Jeshi la Polisi wala Mkurugenzi wa Mashtaka, waliochukua hatua stahiki za kijinai dhidi ya Mkuu wa Mkoa Makonda aka Bashite. Mamlaka hizi, kwa sababu wanazozijua wao, zimeamua kukalia kimya na kunyamazia vitendo vya kihalifu vilivyofanywa na Mkuu wa Mkoa huyo.
 

Hata hivyo, sheria za Tanzania hazijafunga milango yote ya kudhibiti wahalifu wa aina hii. Kifungu cha 128(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Jinai, Sura ya 20 ya Sheria za Tanzania, kinaruhusu mtu binafsi (pamoja na taasisi, makampuni au mashirika kama TLS) kupeleka malalamiko kwa hakimu mwenye mamlaka pale anapoamini kuna sababu za msingi zinazoonyesha kuwa kosa la jinai limetendwa.
 

Kwa mujibu wa kifungu cha 128(4) cha Sheria hiyo, malalamiko hayo yanaweza kuwa ya mdomo au ya maandishi. Kwa kifungu cha 128(5), endapo hakimu ataridhika kwamba malalamiko aliyopelekewa yanaonyesha kosa la jinai basi anatakiwa kuandaa hati ya mashtaka na, kwa mujibu wa kifungu cha 130, anaweza kutoa hati ya ukamataji (arrest warrant) au hati ya wito (summons) ili mhalifu huyo afike au afikishwe mahakamani.
 

TLS itatumia utaratibu huu kuhakikisha kwamba Mkuu wa Mkoa Makonda aka Bashite anafika au anafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizi.
Baadhi ya makosa, kama vile matumizi mabaya ya madaraka na kutishia (intimidation) yanahitaji ridhaa ya Mkurugenzi wa 


 Mashtaka kabla ya kufunguliwa. Baada ya kupeleka malalamiko mahakamani na kufungua mashtaka dhidi ya Mkuu wa Mkoa 
Makonda aka Bashite, TLS itamwandikia Mkurugenzi wa Mashtaka kumwomba ridhaa yake kwa makosa hayo mawili.
Na endapo Mkurugenzi wa Mashtaka atakataa kutoa ridhaa yake, TLS itamfungulia mashtaka ya rejea ya kimahakama (judicial review) katika Mahakama Kuu ili alazimishwe kutoa ridhaa hiyo. Kwa vyovyote vile, TLS itahakikisha Utawala wa Sheria unalindwa katika nchi yetu na wenye mamlaka ya umma wanafuata na kuheshimu sheria za nchi yetu.
 

Baraza la Uongozi la TLS limeazimia vile vile kufungua mashauri katika Mahakama Kuu ya Tanzania kuhoji uhalali kikatiba wa Rais John Pombe Magufuli kushindwa hadi sasa kuteua Kiongozi Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, yaani Jaji Mkuu. Tangu Jaji Mkuu Mohamed Chande Othman astaafu rasmi mnamo tarehe Mosi Januari ya mwaka huu, Rais Magufuli hajateua Jaji Mkuu mpya kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Mkuu Chande Othman. Badala yake, Rais Magufuli amemteua Jaji wa Rufaa Prof. Ibrahim Hamisi Juma kuwa Kaimu Jaji Mkuu.
 


TLS inaamini kwamba Rais Magufuli anakiuka Katiba ya nchi yetu. Ijapokuwa ibara ya 118(4) ya Katiba yetu inamruhusu Rais kuteua Kaimu Jaji Mkuu iwapo itatokea kiti cha Jaji Mkuu kitakuwa wazi; au Jaji Mkuu hayupo Tanzania; na au Jaji Mkuu atashindwa kutekeleza kazi yake kwa sababu yoyote, na Rais akaona kuwa kwa muda wa tukio lolote kati ya hayo matatu inafaa kumteua Kaimu Jaji Mkuu, TLS inaamini kwamba ibara ya 118(4) haikutungwa kwa lengo la kumwezesha Rais kuteua Kaimu Jaji Mkuu bila kikomo cha muda.
 

Kama ilivyo kwa sheria zote, ibara ya 118(4) ina sababu yake maalum. Ibara hiyo imewekwa kwa makusudi ya kuhakikisha kwamba kwa muda wote kunakuwa na kiongozi wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania pamoja na kiongozi wa Mahakama ya Tanzania, wakati Jaji Mkuu kamili anasubiriwa kuteuliwa. Kaimu Jaji Mkuu ni sawa ni kile kinachoitwa na wanasheria 'interlocutory position.' Kaimu Jaji Mkuu ni nafasi ya muda inayoshikiliwa na mtu mwenye sifa za kuwa Jaji Mkuu kabla nafasi hiyo haijajazwa na Jaji 

Mkuu kamili. Hata hivyo, Serikali, kwa kupitia Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba JAM Kabudi, imetamka bungeni kwamba mamlaka ya Kaimu Jaji Mkuu hayana kikomo cha muda. Kwa sababu hiyo, suala hili sasa linahitaji tafsiri ya vifungu hivi vya Katiba yetu, na Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kutoa tafsiri hiyo.
 

Licha ya kauli za Serikali bungeni hivi karibuni, haijawahi kutokea, katika historia yetu yote tangu uhuru, Rais wa nchi yetu akashindwa kuteua Jaji Mkuu kamili kujaza nafasi iliyo wazi ya Jaji Mkuu. Bunge letu, kama mmojawapo wa mihimili mikuu ya dola ya 

Tanzania, lina kiongozi wake mkuu muda wote: Spika Job Ndugai au Naibu Spika Tulia Ackson. Serikali yetu, kama mhimili mwingine mkuu, ina kiongozi wake mkuu muda wote: Rais Magufuli au Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan.
 

Kwa Mahakama ya Tanzania, mhimili mkuu wa tatu wa dola ya 
Tanzania, kutokuwa na kiongozi wake mkuu kamili takriban miezi mitano baada ya kustaafu kwa Jaji Mkuu Chande Othman, kunatoa taswira potofu kwamba Mahakama ina hadhi hafifu au ya chini ikilinganishwa na Bunge na Serikali. Dhana hii potofu inaathiri moja kwa moja heshima, hadhi na uhuru wa Mahakama ya Tanzania na haiwezi kuruhusiwa kujengeka miongoni mwa jamii yetu.
 

Kitendo hiki vile vile kinatoa taswira potofu kwamba pengine Kaimu Jaji Mkuu wa sasa hatoshelezi nafasi hiyo; au kwamba miongoni mwa Majaji wote wa Rufaa au wa Mahakama Kuu ya Tanzania au mawakili na wanasheria wengine wa nchi hii pamoja na wale wa nchi za Jumuia ya Madola hakuna hata mmoja wao mwenye uwezo au sifa za kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania. TLS itaondoa taswira hii potofu kwa kuteua jopo la mawakili wenye ujuzi na uzoefu mkubwa wa kesi za kikatiba ili kutekeleza uamuzi huu.
 

Baraza la Uongozi la TLS vile vile limeazimia kuandaa Kongamano la Kitaifa juu ya Mchakato wa Katiba Mpya ili kujadili hatma ya mchakato wa Katiba Mpya kwa nchi yetu. Kongamano hilo litajumuisha vyama vya siasa, taasisi zisizokuwa za kiserikali, taasisi za kitaaluma, mashirika ya dini na wataalamu wa masuala ya siasa na katiba wa ndani na nje ya nchi yetu. 

Baraza la Uongozi limeazimia kuwaalika pia wajumbe wote wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuhudhuria Kongamano hilo. Kongamano lenyewe litafanyika kwa muda na tarehe zitakazotangazwa baadae.
 

Aidha, Baraza la Uongozi limeazimia kwamba TLS itachukua hatua, kwa kushirikiana na wadau wengine, za kuhoji masuala mbali mbali ambayo yameathiri ustawi wa jamii ya Tanzania, hususan masuala ya mafao na haki za wafanyakazi kuhusiana na makato ya madeni yao kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu na fao la kujitoa uanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii.
 

TLS itashughulikia vile vile tatizo linaloelekea kuwa sugu la migogoro kati ya wakulima na wafugaji na ukiukaji mkubwa wa haki za wafugaji katika maeneo mengi hapa nchini. Tatizo hili limekuwa kubwa kiasi kwamba sasa wafugaji wa Tanzania hawaelewi tena kama wana haki yoyote katika nchi yao, kwa maana wamekuwa wakifukuzwa kila mahali wanapoenda na mifugo yao.
 

Imetolewa kwa idhini na mamlaka ya Baraza la Uongozi la Tanganyika Law Society, leo hii tarehe 30 Aprili, 2017.
-------------------------------------------------------------
Mh. Tundu Antiphas Mughwai Lissu (MB)
RAIS



Baadhi ni wajumbe wa kamatyi hiyo waliotoa maadhimio hayo

 Tundu Lissu Rais wa TLS kwa mwaka 2017 aliyechaguliwa kwa kishindo pamoja na Serikali kutoa matamko ya hapa na pale dhidi yake na kuwekwa ndani lakini haikuzuia hiyo kwa mawakili wengi vijana kumchagua kijana mwenzao, kukiamsha chama chao wanachodai kilikuwa kimelala tena kimeegemea upande mmoja tu wa Chama cha Mapinduzi wa Serikali yake huku wananchi wakitabika.

 Picha ya pamoja wajumbe wa kamati hiyo ya TLS iliyokutana mjini Dodoma

Comments

Popular posts from this blog

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?

AMANI YETU TUILINDE NAIBU WAZIRI CHANDE AZUNGUMZA KATIKA IJITIMAI JIJINI DODOMA

UNAMKUMBUKA AMINA CHIFUPA WA MPAKANJIAA.