RAIS DKT. MAGUFULI APOKEA TAARIFA YA ZOEZI LA UHAKIKI WA VYETI KWA WATUMISHI WA UMMA LEO MJINI DODOMA


  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Taarifa ya zoezi la uhakiki wa vyeti  kwa Watumishi wa umma kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora Angela Kairuki katika Ukumbi wa Chimwaga mjini Dodoma.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akikata utepe katika vitabu hivyo vya taarifa ya zoezi la uhakiki wa vyeti  kwa watumishi wa umma alivyopokea kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora Angela Kairuki katika Ukumbi wa Chimwaga mjini Dodoma. Katikati ni Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na wakwanza kushoto ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Profesa Idris Kikula.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akitoa kitabu cha Taarifa ya zoezi la uhakiki wa vyeti  kwa watumishi wa umma alivyopokea kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora Angela Kairuki katika Ukumbi wa Chimwaga mjini Dodoma. Katikati ni Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na wakwanza kushoto ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Profesa Idris Kikula.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akinyanyua juu Taarifa na vitabu vye majina 9,932 ya watumishi wenye vyeti vya kugushi.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akikata utepe na kufungua boksi kubwa lenye majina ya watumishi zaidi ya 9,932 waliobainika kuwa na vyeti vya kugushi mara baada ya kupokea Taarifa ya zoezi la uhakiki wa vyeti  kwa watumishi wa umma kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora Angela Kairuki katika Ukumbi wa Chimwaga mjini Dodoma.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiangalia majina hayo pamoja na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan  mara baada ya kufungua boksi kubwa lenye majina ya watumishi hao wa umma ambao wamegushi vyeti vyao .
  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisoma jina mojawapo la mtumishi aliyegushi cheti katika taarifa hiyo.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  akiwa pamoja na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan wakiangalia vitabu vyenye majina ya watumishi wa Umma zaidi ya 9,932 waliogushi vyeti vyao vya elimu ya Sekondari.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  akiwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa , Waziri wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako, Spika wa Bunge Job Ndugai, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora Angela Kairuki wakiminya kitufe kuashiria maadhimisho ya miaka 10 ya Chuo Kikuu cha Dodoma UDOM katika ukumbi wa Chimwaga mkoani Dodoma.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  akihutubia viongozi mbalimbali, wanafunzi wa UDOM, pamoja na watumishi wa Umma mara baada ya kupokea Taarifa ya zoezi la uhakiki wa vyeti  kwa watumishi wa umma kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora Angela Kairuki katika Ukumbi wa Chimwaga mjini Dodoma.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akagana na watumishi mbalimbali wa umma, viongozi pamoja wanafunzi wa UDOM mara baada ya kumaliza kuhutubia katika Ukumbi wa Chimwaga mjini Dodoma.
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akihutubia katika hadhara hiyo katika Chuo kikuu cha Dodoma UDOM.
 Wanafunzi wa UDOM wakisikiliza kwa makini Hotuba iliyokuwa ikitolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika maadhimisho ya miaka 10 toka kuanzishwa kwake.
 Baadhi ya viongozi mbalimbali wakifatilia kwa makini Hotuba iliyokuwa ikitolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika maadhimisho ya miaka 10 ya Chuo cha UDOM toka kuanzishwa kwake.
 Baadhi ya Makatibu wakuu pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali wakifatilia kwa makini hotuba iliyokuwa ikitolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika ukumbi wa Chimwaga mkoani Dodoma.
 Baadhi ya Makatibu wakuu pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, wanafunzi pamoja na walimu wa  UDOM wakipiga makofi wakati wakimkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wakati akiwasili katika ukumbi wa Chimwaga mkoani Dodoma.
 Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia katika Ukumbi wa Chimwaga.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Taarifa ya miaka 10 ya Chuo kikuu cha Dodoma UDOM katika ukumbi wa Chimwaga mkoani Dodoma. PICHA NA IKULU

Akana kujihusisha na kusafirisha wasichana nchini Kenya kwa ajili ya biashara ya Ngono.


Na Karama Kenyunko

Mshtakiwa Mary Amokowa, ameiomba mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imuachie huru kwani hakuhusika na tuhuma za kusafirisha wasichana 10 kutoka Tanzania Kwenda Kenya kwa ajili ya biashara ya ngono.

Mshtakiwa huyo ambaye ni raia wa Kenya ameiomba mahakama imuachie huru kwa kuwa madai ya kesi hiyo ni ya uongo na ya kutengenezwa.

Ameyasema hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Godifrey Mwambapa wakati akitoa utetezi wake dhidi ya kesi hiyo inayomkabili yeye,Jackline Milinga na Simon Alex Mgawe.

Akiongozwa na wakili wake Nehemia Nkoko,Mary amedai kuwa yeye ni mfanyakazi wa kampuni ya simu ya safari Com iliyopo Nairobi Kenya. Amedai kuwa, Septemba 4,2015 akiwa na rafiki yake Jackline walisafiri kwa kutumia basi la Mordem Coast kutoka Dar es Salaam kwenda Nairobi.

Ameongeza kuwa walikuwa na tiketi na pasi za kusafiria lakini walipofika Namanga mpakani mwa Kenya na Tanzania, akiwa tayari amekwisha gongewa mhuri wa kutoka Tanzania na akiwa katika foreni ya kusubiri kugongewa muhuri wa kuingia Kenya, askari wawili wa Uhamiaji wa Tanzania walimkamata Jackline.

Amedai walipomkamata walimwambia wana wasiwasi na hati yake ya kusafaria kwa sababu alikuwa na hati ya kusafiria ya kidiplomasia na baadaye walibaini haijaghushiwa ni halali.

Amedai kuwa, baada ya pasi ya rafiki yake kuonekana kuwa ni halali na wote wakati huo walikuwa chini ya ulinzi aliomba waachiwe huru, baada ya kutuchukua maelezo lakini hawakutuachia. Badala yake wakatuweka sehemu moja na hao wasichana 10, ambao tulikaa nao siku nne Uhamiaji Makao Makuu na kwamba walipohamishiwa uhamiaji mkoa hawakuwa na hao wasichana.

Ameileza mahakama kuwa hawajui wasichana anaotuhumiwa kuwasafirisha na wala hakuwahi kuwaona hadi siku Zulfa, Lea, Angelina na Amina walipopelekwa mahakamani kutoa ushahidi kwa upande wa mashtaka. “Shtaka hili ni la uongo na la kutengenezwa , sijawahi kusafirisha binadamu yoyote, mimi ni mfanyakazi wa Safari Com naomba mahakama iniachie huru kwa sababu tuhuma ni za uongo.”Mary alisema.

Kwa upande wa mshtakiwa Simon Alex Mgawe alidai kuwa tuhuma hizo si za kweli yeye hajawahi kusafiri nje ya Tanzania wala kukusanya binadamu kwa lengo la kuwasafirisha hivyo aliomba mahakama imuachie huru. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 11, mwaka huu itakapokujwa kwa ajili ya kuwasilisha hoja zao za majumuisho za kuishawishi mahakama iwaone washtakiwa wana hatia ama la.

Awali ilidiwa kuwa,Septemba 4 mwaka 2015, huko Magomeni, washtakiwa waliwaajiri wasichana 10 wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 22 na kuwasafirisha nchini Kenya kwa ajili ya biashara ya Ngono. Wasichana hao ni Najma Suleiman, Leah Mussa, Zulfa Ally, Rahma Mohammed, Salima Komba, Angelina Banzi, Leila Chorobi, Elizabeth Nalimu, Amina Abdi na Sada Hussein.

RAS TABORA AWATAKA WANAWAKE WASHIRIKIANE KATIKA SHUGHULI ZA MAENDELEO

Na Tiganya Vincent-RS-Tabora

Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Dkt. Thea Ntara ametoa wito kwa wanawake mkoani hapa kuungana na kushirikiana pamoja katika shughili za mbalimbali za ujasiriamali ili iwe rahisi kwao kunafaika na fursa mbalimbali mikopo ikiwemo asilimia tano inapaswa kutolewa na Halmashauri zao.
Dkt. Ntara alitoa kauli hiyo jana mjini Tabora wakati akizindua Jukwaa la Uwezeshaji wanawake kiuchumi la Mkoa huo.Alisema kuwa wanawake wakiendelea kufanyakazi kwa ubinafsi hawataweza kuendelea bali wataendelea kubaki nyuma.

Katibu Tawala huyo wa Mkoa alisema kuwa wanawake wakiungana na wakaunda vikiundi vinavyoaminika watapata fursa ya kukopeshwa na Taasisi za fedha zilizopo mkoani Tabora na hivyo kukuza mitaji yao ambapo hatimaye wanaweza kuwa na uwezo wa kuanzisha viwanda vyao.
Dkt. Ntara aliongeza kuwa wakiungana watapata fursa ya wao kuwa kichocheo cha kuleta maendeleo kuanzia ngazi za familia hadi taifa kutokana na wao kuwa wataalam wazuri wa matumizi ya fedha kidogo wanazopata.
Alisema kuwa mwanamke licha ya baadhi yao kutokwenda shule au kutopata fursa ya kusoma lakini bado Mungu amewajalia maarifa ambayo yanasaidia jamii kama vile kufahamu kuwa mtoto wake anaumwa wakati hajasomea udaktari, kufahamu umuhimu wa kilimo cha mboga mboga kuzungumza nyumba yake licha ya kutosomea ubwana au ubibi shamba, kuwa mtunza fedha mzuri licha ya kutosomea uhasibu.
Dkt. Ntara aliwasisitiza wanawake hao kuwa ni vema wakatumia tunu hiyo waliojaliwa katika kuunda vikundi mbalimbali katika maeneo yao na kuanzisha mradi ambapo utawasaidia wao na familia zao na hivyo kuonyesha kuwa wanawake wanaweza.
Alisema kuwa wakifanikiwa kuunda vikundi katika maeneo yao na vikaonekana havina matatizo atahakikisha kuwa anawabana Wakurugenzi watendaji wa Halmashauri zote za Mkoa huu kuhakikisha kuwa wanawapatia ile asilimia tano kama ilivyoagizwa.
Dkt. Ntara aliwakubusha wanawake hao kuwa ni vema wanapouungana wakakumbuka kuwa mtaji sio fedha pekee bali ni pamoja na kuwa na elimu ya mradi unataka kuunzisha , kuwa na watu ambao unawalenga katika mradi wao na watakaoshiriki katika mradi huo.
Aidha, Katibu Tawala huyo wa Mkoa aliwaasa wanawake hao kuunda mtandao wa mawasiliaono kwa Halmashauri zote ili iwe kwao fursa ya kubadilishana uzoefu na kuwa rahisi kupata masoko.
Uzinduzi wa Jukwaa la Uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi mkoani Tabora unalenga kusaidia kuongeza uelewa wa wanawake kiuchumi, kibiashara na upatikanaji wa mitaji.

WAZIRI MAHIGA AHITIMISHA ZIARA YA KIKAZI KATIKA JAMHURI YA KOREA 



Mhe. Balozi Dkt. Augustine Philip Mahiga (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alifanya ziara ya kikazi jijini Seoul, Jamhuri ya Korea tarehe 24 Aprili 2017 kwa mwaliko kutoka kwa Mhe. Yun Byung-se, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea. Ziara hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea mwaka 1992.

Wakati wa ziara hiyo, Mheshimiwa Mahiga alikutana na kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Mhe. Yun Byung-se ambapo Waziri Mahiga aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea kwa kumpatia mwaliko wa kutembelea taifa hilo hususan wakati huu inapoadhimishwa jubilee ya miaka 25. Mhe. Mahiga aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea kwa kuichagua Tanzania kuwa nchi ya kimkakati  katika uwekezaji kwa kipindi cha kuanzia 2016 -2020.

Kwa kipindi cha miaka 25, Serikali ya Korea imeisaidia Tanzania kufanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo Ujenzi wa Daraja la Kikwete katika Mto Malagarasi unaojumuisha madaraja matatu yenye jumla ya urefu wa meta 275  pamoja na barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 48; Ujenzi wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Kampasi ya Mloganzila yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 600 imejengwa na kufungwa vifaa tiba vya kisasa vya digitali, vinavyotumia zaidi teknolojia ya Tehama zikiwemo mashine za X-ray, MRI, CT-Scan, mashine maalum kwa ajili ya kupimia magonjwa ya wanawake. 

Vilevile, Ujenzi wa Hospitali ya mama na mtoto Chanika yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 160 inatarajiwa kufunguliwa siku za karibuni.Aidha, Watanzania zaidi ya 1000 wamenufaika kwa kupata ufadhili wa kusoma katika vyuo mbalimbali vya Jamhuri ya Korea.

Waziri Mahiga pia alikutana na baadhi ya Wanachama wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Jamhuri ya Korea ambapo alitumia fursa hiyo kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania mathalani ujenzi wa Reli ya Kati katika viwango vya kimataifa; uzalishaji na usambazaji wa nishati ya umeme; ujenzi wa maeneo ya viwanda; na huduma ya kutoa ushauri katika miradi mikubwa.

Aidha, Mhe. Waziri aliwahakikishia wawakilishi wa  makampuni ya Jamhuri ya Korea kuwa, Tanzania imeboresha mazingira ya uwekezaji na biashara pamoja na taasisi muhimu zinazotoa huduma mbalimbali katika sekta hiyo. 

Wakati huo huo, Mhe. Waziri Mahiga alitumia fursa hiyo kukutana na Balozi Sul Kyung-hoon Makamu wa Rais wa KOICA ambapo aliishukuru Taasisi hiyo kwa kuipatia zaidi misaada Tanzania kwa uwazi na bila ya masharti yeyote. Pia aliipongeza KOICA kwa kushirikisha jamii kuanzia wakati wa ubunifu wa mradi hadi kufikia utekelezaji pamoja na usimamizi. 
KOICA wameombwa kuongeza maeneo ya misaada na kujumuisha maeneo ya ujenzi wa miundombinu ya maji na nishati ya umeme wa jua, upepo na maji kwa ajili ya kusaidia maeneo ya vijijini. Aidha, Mhe. Waziri Mahiga alishauri KOICA kuangalia uwezekeno wa kuanzisha vituo vya kilimo cha kisasa, vituo vya kufugia na vituo vya kufundisha ujasiriamali ili jamii kubwa ya Watanzania iweze kunufaika.

Katika jitihada za kutafuta washirika kwa ajili ya kusaidia kuboresha Chuo cha Diplomasia, Mhe. Waziri akiwa Seoul alitembelea Chuo cha Taifa cha Diplomasia cha Jamhuri ya Korea na kufanya mazungumzo na Balozi Paik Ji-ah, Kaimu Mkuu wa Chuo. Lengo kuu lilikuwa kujifunza uendeshaji wa Chuo, mitaala iliyoandaliwa kutoa masomo, walengwa wa masomo hayo, aina ya wakufunzi, lugha zinazotumika kufundishia, utaratibu wa kuandaa wanadiplomasia na mifumo ya chuo hicho.

Vilevile kabla ya kuhitimisha ziara yake, Mhe. Waziri alikutana na Jumuiya ya Watanzania waishio Jamhuri ya Korea ambapo aliwahimiza kuheshimu Sheria na Taratibu za nchi hiyo ikiwa ni pamoja na kuleta utaalam utakaosaidia kuiendeleza Tanzania.

Aidha, akizungumza  na Watanzania hao ambao wengi wao ni wanafunzi, Mhe. Waziri aliwasihi kuzingatia masomo ili kufikia malengo waliyojiwekea na kuleta faida kwa familia zao na taifa kwa ujumla. Pamoja na mambo mengine, Mhe. Waziri aliwahakikishia Wanajumuiya hao kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kufungua Ubalozi wa Tanzania jijini Seoul na kuwaomba kutoa ushirikiano kwa Balozi wa kwanza wa Tanzania katika nchi hiyo. 
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 28 Aprili, 2017.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea, Mhe. Yun Byung-se. Mhe. Mahiga alikuwa nchini humo kwa ziara ya kikazi ikiwa pia ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 25 ya ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea.

Rais Magufuli Awataka Watumishi 9932 Waliogushi Vyeti Kuondoka Maeneo Yao ya Kazi

Na Nuru Juma na Beatrice Lyimo-MAELEZO .

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka watumishi 9932 waliogushi vyeti, kuondoka maeneo yao ya kazi haraka iwezekanavyo kabla hawajadhibiwa kwa mujibu wa sheria. 

Rais Magufuli ameyasema hayo leo mjini Dodoma alipokuwa akikabidhiwa taarifa ya uhakiki wa vyeti vya watumishi wa umma sambamba na uzinduzi wa maadhimisho ya miaka kumi ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM). 

“Watumishi 9932 wenye vyeti vya kugushi na feki mishahara yao ya mwezi huu ikatwe na waondoke kazini mara moja na hizo nafasi zitangwazwe ili wasomi waweze kuziomba na majina yao yawekwe kwenye magazeti ili wajulikane” amesema Rais Magufuli 

Aidha amesema kuwa hadi kufika tarehe 15 Mei, 2017 kila mkuu wa Idara mahali pake pa kazi ahakikishe watumishi hao wameondoka na watakao kaidi agizo hilo amevitaka vyombo vya usalama kuwashughulikia.
Hata hivyo Rais Magufuli ameongeza kuwa watumisi 1538 wanaotumia cheti zaidi ya mtu mmoja kutopewa mshahara hadi pale itakapojulikana nani mwenye cheti halali na kuwataka watumishi 11,769 kuwasilisha vyeti vilivyopungua. 

Mbali na hayo Rais Magufuli amewataka wanafunzi kusoma kwa bidii na kuachana na masuala ya siasa kwa lengo la kujenga nchi kwani watanzania wanahitaji maendeleo. 

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Angela Kairuki amesema kuwa mpaka sasa vyeti vilivyohakikiwa ni 435,000 ambapo imefanyika kwa awamu tatu iliyojumuisha Serikali za Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma, Tume na Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi na Wakala wa Serikali pamoja na Serikali Kuu. 

“Leo tunakabidhi taarifa ya awamu mbili iliyohusisha Serikali za Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma, Tume na Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi na Wakala wa Serikali ambapo imejumuisha uhakiki wa vyeti vya Kidato cha  Nne, Sita, vyeti vya ualimu kwa ngazi ya cheti na stashahada” amesema Waziri Kairuki. 

Amesema kuwa matokeo ya uhakiki wa vyeti kwa watumishi wa umma yapo ya aina nne ambapo watumishi 376,969 sawa na asilimia 94.23 wanavyeti halali, watumishi 9932 asilimia 2.4 wanavyeti vya kugushi, watumishi 1538 asilimia 0.3 vyeti vyao vinatumika kwa zaidi ya mtu mmoja na watumishi 11,769 asilimia 2.8 wanavyeti pungufu. 

Nae Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako alisema wizara yake inakumbana na changamoto ya watumishi wa umma kugushi vyeti hivyo aliwataka wanafunzi kusoma kwa bidii kwani serikali imeziba njia zote za mkato za kuajiriwa na Serikali. 

“Leo tunaandika historia ya kipekee kwani suala la uhakiki wa yveti limefanyika kwa mara ya kwanza nchini ambapo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ndio yenye jukumu la kuhakiki uhalali wa vyeti hivyo” amesema Prof. Ndalichako. 

Zoezi la uhakiki wa vyeti kwa Watumishi wa Umma limeendeshwa na Serikali ya Awamu ya Tano kuanzia Mwezi Oktoba, 2016 likiwa na lengo la kubaini uhalali wa vyeti kwa watumishi wake.

MAHAKAMA YA ARUSHA YAMWACHIA HURU ALIYEKUWA MWENYEKITI UVCCM ARUSHA KWA KOSA LA KUJIFANYA USALAMA WA TAIFA

Na Wankyo Gati,,ARUSHA

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Arusha, leo imemuachia huru aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Lengai Ole Sabaya baada ya kuona upande wa Jamuhuri wazembe wa kushindwa kuleta mashahidi katika kesi ya kujifanya Afisa Usalama wa Taifa (TISS).

Akisoma uamuzi wake jana uliotokana na ombi la Wakili wa Serikali Grace Madikenya la kuomba Mahakama hiyo kuiondoa kesi hiyo kwa sababu ya kukosa shahidi muhimu katika kesi hiyo na kupingwa na Upande wa Utetezi kuwa wanatumia vibaya mahakama kumtesa mteja wao, Gwantwa

Mwakuga, alisema Mahakama inasikitika kuona mwendesha mashitaka wa serikali, anatumia kigezo cha kuondoa kesi na kumkamata mshitakiwa kwa maslahi yake mwenyewe.

Alisema kesi hiyo imekuja mara ya pili baada ya kufunguliwa kesi namba 376/2016 na ilipofika katika utoaji wa ushahidi wa mpelelezi wa kesi hiyo, Mwendesha mashitaka aliomba Mahakama kuiondoa kesi hiyo kwa madai hawana nia ya kuendelea nayo na na mahakama ilikubaliana naye na kumwachia huru, lakini siku hiyo hiyo Desemba 14 Mshitakiwa alikamatwa.

“Kinachosikitisha Mahakama ilishuhudia kwa macho yake baada ya kumwachia mshitakiwa alipotoka nje alikamatwa tena na kuletwa tena Mahakamani hapa, kwa hakimu Mfawidhi Augustino Rwezile na mashitaka yalikuwa yale yale hakuna kilichorekebishwa na sasa wanaomba tena kuondoa kwa kigezo shahidi muhimu yupo nje ya nchi kwa miezi 18, hii ni utumiaji vibaya ofisi ya mwendesha mashitaka, ili kutesa watu,”alisema.

Gwantwa alisema Mahakama inatambua nguvu ya Mkurugenzi wa Mashitaka aliyonayo, lakini nguvu hiyo isitumike vibaya ni muhimu kuzingatia maslahi ya umma,haki na utedaji kazi wa Mahakama.Alisema Mahakama hiyo imejiuliza kipya kilichorekebishwa katika kesi hiyo ya pili namba 493/2016 na kuona hakuna, isipokuwa upande waJamuhuri wamefanya kwa kukidhi mataka yao wenyewe.

“Hapa upande wa jamuhuri wazembe wameshindwa kuleta mashahidi wakitakiwa kuleta wanaleta sababu wapo Kenya mara nje ya nchi, mara kuleta mashahidi ngumu, ili mradi kucheleesha kesi hii, mshitakiwa anazo haki zao za msingi za kuona kesi yake ikiendelea, lakini Jamuhuri inatesa Wadaawa kwa ajili ya maslahi yao, kitu ambacho mahakama hii haiko tayari kuona ikichezewa kwa namna hiyo,”alisema huku akinukuu kesi mbalimbali.

Alisema vema wadau wa Mahakama wakafahamu kuwa mahakama ni hekalu la kutenda haki kwa washitakiwa na walalamikaji sio vinginevyo na haki ya mshitakiwa kuona mashauri yafike mwisho na Mahakama haiwezi kuvumilia kuona mshitakiwa anakamatwa kwa kigezo cha kutumia mahakama vibaya.

Alimalizia kusema kimsingi kifungu cha 91 cha sheria ya mwendendo wa makosa ya Jinai ambacho upande wa Jamuhuri waliomba mahakama ikitumie kuondoa shauri hilo, inakikataa na kutumia kifungu cha 225 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai kumwachia huru mshitakiwa huyo.

Awali kabla ya hakimu Gwantwa kuanza kusoma uamuzi huo, Wakili wa serikali, Grace Madikenya aliiambia mahakama hiyo haipo tayari kuendelea kusikiliza shauri hilo kwani tayari ameomba kuliondoa na lipo kinyume cha sheria, huku Wakili wa utetezi Charles Adiel akiomba Mahakama hiyo kusoma uamuzi wa mahakama kwa niaba ya mteja  wake na atapokea.

Sabaya mwaka jana alifikishwa Mahakamani hapo na kusomewa mashitaka mawili ambapo la kwanza ni kuwa Mei 18 mwaka 2016, katika Hotel ya Sky Motel, Mshitakiwa Sabaya alijifanya Afisa usalama wa Taifa (TISS) na kupata huduma ya kulala katika hotel hiyo, kwa kupata chakula navinywaji wakati sio kweli.

Shitaka la pili Sabaya anashitakiwa kughushi kitambulisho ya TISS kilichosomeka MT.86117 wakati akijuwa wazi kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Sabaya alikuwa akitetewa na Wakili Edna Haraka na Charles Adiel

MIGODI INAYOMILIKIWA NA KAMPUNI YA ACACIA YAWA KIVUTIO KATIKA MAONESHO YA WIKI YA USALAMA NA AFYA MAHALA PA KAZI

Maonesho ya Wiki ya Usalama na Afya mahala pa kazi yanayofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro.
Maonesho haya yanayohusisha kampuni na Taasisi mbalimbali nchini yanaratibiwa na Wakala wa Usalama na Afya mahala pa Kazi (OSHA).
Baadhi ya Wafanyakazi wa Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu unaomilikiwa na Kampuni ya ACACIA,wakiweka sawa moja ya picha inayoonesha eneo ambalo shughuli za uchimbaji unafanyika.
Afisa Uhakiki na Usalama katika Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu unaomilikiwa na kampuni ya ACACIA,Amina Mohamed akitoa maelezo kwa wananchi waliotembelea banda hilo.
Baadhi ya Wafanyakazi wa Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu unaomilikiwa na Kampuni ya ACACIA,wakitoa maelezo kwa wananchi waliotembelea banda hilo katika maeonesho ya wiki ya usalama mahala pa kazi ndani ya viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika mjini Moshi.
Afisa Afya katika Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu ,Tumaini Sylivanus akitoa maelezo ya namna wanavyotoa huduma ya Afya kwa wafanyakazi wa Mgodi huo pindi wapatapo matatizo.
Mmoja wa Wakazi wa Kilimanjaro akipewa maelekezo ya namna ya kutumia kifaa maalumu kinachotumika katika zoezi la uzimaji wa moto pindi yatokeapo majanga ya Moto.Nyuma yake ni mmoja wa wafanyakazi wa Mgodi wa Bulyanhulu unaomilikiwa na kampuni ya ACACIA.
Afisa Viwango wa Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu,Setieli Kimaro akitoa ufafanuzi kwa wananchi waliotembelea banda la modi huo unaomilikiwa na kampuni ya ACACIA.
Afisa Usalama katika Mgodi wa Buzwagi unaomilikiwa na Kampuni ya ACACIA,Deogratius Nyantabano akitoa maelezo kwa wanafunzi waliotembelea banda la mgodi huo katika maonesho ya wiki ya usalama na afya mahala pa kazi yanyofanyika katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi ,Kilimanjaro.
Afisa Usalama katika Mgodi wa Buzwagi unaomilikiwa na Kampuni ya ACACIA,Mustapher Mlewa akieleza jambo kwa baadhi ya wananchi waliotembelea Banda hilo.
Daktari kutoka Mgodi wa Buzwagi unaomilikiwa na Kampuni ya ACACIA,Dkt Ludovick Silima akitoa maelezo juu ya usalama kwa mmoja wa wananchi waliofika katika banda la mgodi huo wakati wa maonesho ya wiki ya usalama na afya mahala pa kazi yanayoendelea katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi.
Afisa Mazingira katika Mgodi wa north Mara ,Sara Cyprian akionesha picha na maelezo kwa baadhi ya wananchi waliotembelea banda la Mgodi huo katika maonesho ya wiki ya usalama na afya mahala pa kazi.
Afisa Usalama katika mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaomilikiwa na kampuni ya ACACIA,Samweli Nansika (aliyenyoosha kidole) akitoa maelezo kwa baadhi ya wananchi waliotembelea banda la mgodi huo.
Mkuu wa Idara ya Usalama na uokoaji katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara ,Emanuel Erasto(katikati) akitoa maelezo namna amavyo wanaweza kumuokoa mtu aliyepata athari iliytokana na kemikali.
Eneo maalumu la kumuogesha mtu aliyepata athari ya kemikali.
Afisa usalama akita huduma ya kumsafisha mtu aliyepata athali ya kemikali akiwa nje ya bafu hilo la kumuogeshea ili na yeye asipate madhara.
Wafanyakazi wa Mgodi wa Buzwagi wakionesha namna ambavyo wanaweza msaidia mtu aliyepatwa na janga la Moto.
Kifaa Maalumu kinachotumika katika kubeba mwili wa mtu aliyepata madhara akiwa katika shimo wakati wa uchimbaji wa Dhahabu.
Mmoja wa wafanyakazi wa Mgodi wa Bulyanhulu akitoa maelezo kwa wananchi walitembelea banda hilo namna ambavyo wanaweza kunyanyua Gari pamoja na Mawe yaliyomuangukia mtu wakati akitekeleza majukumu yake kwa kutumia kifaa maalumu kinachojazwa upepo (Air Bag).
Mkuu wa Idara ya Usalama na Uokoaji katika Mgodi wa North Mara ,Emanuel Erasto akitoa maelezo namna wanavyoweza kumukoa mtu aliyepatwa madhara akiwa chini ya mgodi .
Dkt Ludovick Silima akitoa ufafanuzi kwa wananchi waliotembelea banda la Mgodi wa Buzwagi.
Afisa Mahusiano katika Mgodi wa Bulyanhulu akitoa maelezo ya namna Mgodi huo unavyo tekeleza majukumu yake ukitoa kipaumbele katika masuala ya Usalama na Afya kwa watumishi wake.
Afisa Uhusiano wa Mgodi wa Buzwagi ,Magesa Magesa akitoa maelezo namna mgodi huo ulivyoshiriki katika shughuli za maendeleo ikiwemo ujengaji wa vyumba vya madarasa,zahanati,maji pamoja na suala la kuhamasisha michezo katika maeneo yanayozunguka mgodi huo.

Na Dixon Buagaga wa Globu ya Jamii Kanda ya Kaskazini.

Comments

Popular posts from this blog

AMANI YETU TUILINDE NAIBU WAZIRI CHANDE AZUNGUMZA KATIKA IJITIMAI JIJINI DODOMA

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?

UNAMKUMBUKA AMINA CHIFUPA WA MPAKANJIAA.