SIKU YA KIFUA KIKUU DUNIANI MKOA WA SHINYANGA



Maadhimisho ya siku ya Kifua Kikuu Duniani “World TB Day” mkoa wa Shinyanga yamefanyika katika machimbo ya dhahabu ya Nyangarata kata ya Lunguya halmashauri ya Msalala wilayani Kahama.

CHAMA CHA WATU WENYE UALBINO CHATOA ELIMU MASUALA YA UALBINO KANISA KUU LA KKKT SHINYANGA


Chama cha watu wenye ualbino nchini (Tanzania Albinism Society-TAS) kimeanza kampeni ya kutoa elimu kuhusu masuala ya ualbino katika nyumba za ibada ambapo leo viongozi wa chama hicho taifa wametoa elimu katika kanisa la KKKT Usharika wa Ebenezer Kanisa Kuu Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria lililopo mjini Shinyanga.

Balozi Seif atembelea Kampuni ya Kimataifa ya Uhandisi wa miundombinu ya Ujenzi ya Garware mjini Mumbai, India

Na Othman Khamis Ame, OMPR
Kampuni ya Kimataifa ya Uhandisi wa miundombinu ya Ujenzi ya Garware yenye Makao Makuu yake Mjini Mumbai Nchini India imeonyesha nia yake ya kutaka kujenga Ukumbi Mpya wa Kisasa wa Kimataifa wa Mikutano Zanzibar endapo itapata fursa ya kufanya kazi hiyo. 
Uwamuzi huo umekuja kufuatia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa na mpango wa Kutaka kujenga Ukumbi wenye hadhi hiyo katika azma yake ya kuimarisha Sekta ya Utalii inayoonekana kuimarika na kuleta ufanisi mkubwa. 
Mkurugenzi Miradi wa Kamuni Garware Bwana Deepak Menghnani alithibitisha hilo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mwishoni mwa ziara ya Wiki Moja ya Ujumbe wa Zanzibar hapo katika Hoteli ya Kimataifa ya Eros Mjini New Delhi India. 
Bwana Deepak Menghnani alimthibitishia Balozi Seif kwamba Wahandisi wa Kampuni ya Garware iliyoanzishwa karibu miaka sita iliyopita wana uwezo wa Kujenga Jengo la Mikutano katika kipindi kisichozidi miaka Mitatu kwa mujibu wa uwezo wa mahitaji ya muhusika. 
Alisema teknolojia rahisi inayotumika katika Kampuni hiyo imewawezesha Wataalamu na Wahandisi wake kuendesha ujenzi wa Mjengo tofauti ikiwemo Hospitali, Skuli, Ofisi za Serikali na hata Taasisi Binafsi pamoja na nyumba za Makaazi kwa bei inayomuwezesha mtu wa kawaida kumudu kununua. Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya Kimataifa ya Uhandisi wa miundombinu ya Ujenzi ya Garware alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Taasisi hiyo ya ujenzi imekuwa ikishirikiana na Wahandisi waliobobea kutoka Nchini Misri ili kuiwezesha kuwa na uhimili wa Kimataifa. Bwana Deepak Menghnani alisema Garware tayari imeshatoa huduma za ujenzi katika Mataifa ya Bukinafaso,Sri Lanka na Dubai ndani ya kipindi cha miaka Minane tokea kuanzishwa kwake. 
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kuuandalikia barua ya mualiko Ujumbe wa Viongozi wa Kampuni hiyo katika muda mfupi ujao ili kujionea mazingira ya Zanzibar na kuona hatua gani zinastahiki kuchukuliwa katika mwanzao wa kuelekea kwenye mpango huo wa ujenzi wa Ukumbi wa Kimataifa. 
Balozi Seif alisema Zanzibar imeshafanikiwa kwa kiasi kikubwa katika uimarishaji wa Sekta ya Utalii lakini kinachokosekana kwa wakati huu ni uwepo wa Ukumbi wa Kimataifa unaotoa fursa kwa Wageni na hata 
Nchi rafiki kuelekeza nguvu zao za kufanya makongamano, Mikutano na hata Vikao vya Kimataifa. “ Zipo kumbi za Mikutano zinazotumika katika baadhi ya Mahoteli Mjini na sehemu za Vijijini Zanzibar lakini hazikidhi mahitaji halisi kutokana na udogo wake ”. Alisema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar. 
Balozi Seif alisema ipo mikutano na baadhi ya semina za Kimataifa zinazopangwa kufanyika Visiwani Zanzibar lakini wajumbe wa Mikutano hiyo hulazimika kuishi mbali na maeneo yao ya mikutano jambo ambalo huleta usumbufu wa kujipangia mambo yao mengine binafsi. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amemaliza ziara yake Nchini India na sasa amewasili Dubai kwa Mapumziko mafupi ya siku mbili na baadae atarejea Nchini Tanzania kuendelea na majukumu yake.

KAMATI YA BUNGE YA KUDUMU YA UTAWALA NA SERIKALI ZA MITAA YARIDHISHWA NA MIRADI YA TASAF, TAMISEMI , MKURABITA NA MFUKO WA RAIS WA KUJITEGEMEA MKOANI NJOMBE.

Kamati ya kudumu ya bunge Utawala na Serikali za Mitaa imetembelea mkoani Njombe na kukagua baadhi ya miradi inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF,TAMISEMI, Mfuko wa Rais wa Kujitegemea na MKURABITA na kuridhishwa na mchango wa taasisi hizo katika kupiga vita umasikini kwa kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Wakiwa mkoani humo,wajumbe wa Kamati hiyo walikutana na Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaotekelezwa na TASAF ambapo licha ya kuvutiwa na hatua ya kujiongezea kipato kutokana na ruzuku kwa kuanzisha miradi midogo midogo, lakini pia walipongeza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta za elimu, afya na lishe katika kaya za walengwa hao.

Aidha wajumbe wa kamati hiyo ambao waliongozana na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah Kairuki pia wamepongeza hatua ya TASAF ya kupunguza tatizo la makazi ya walimu kwa kujenga nyumba katika kijiji cha Uwemba nje kidogo ya mji wa Njombe.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mhe.Kairuki amesema serikali itaendelea kuweka mkazo katika miradi inayolenga kuwapunguzia wananchi adha ya umasikini hivyo akataka wananchi kuitumia fursa hiyo vizuri ili waweze kuboresha maisha yao.Waziri huyo alionyesha kuridhika na baadhi ya wananchi mkoani Njombe kwa kutumia fursa zilizowekwa na serikali kuendesha shughuli za kiuchumi kikiwemo kilimo,ufugaji ,biashara na uanzishaji wa vikundi vya kuweka akiba.

Kwa Upande wa MKURABITA,Wajumbe wa Kamati hiyo walipata ushuhuda kutoka kwa baadhi ya wananchi ambao wamepata mikopo kwa kutumia hati za ardhi iliyopimwa chini ya Mpango huo ambao baadhi yao wameweza kupanua biashara zao baada ya kukopa fedha kwa wastani wa shilingi milioni 80 na kurejesha mikopo hiyo kwa wakati 

Kwa upande wake Mwenyekiti aliyeongoza wajumbe hao,Mhe. Venance Mwamoto alitoa wito kwa wataalamu walioko kwenye maeneo ya wananchi kutumia muda wao mwingi kuwapatia elimu na mafunzo yatakayowawezesha kuboresha miradi wanayoianzisha ili iwe endelevu na yenye kuleta tija.

Hata hivyo wanufaika wa mikopo kutoka taasisi za fedha walionyesha kilio chao kutokana na riba kubwa wanayotozwa jambo ambalo wamedai kuwa linaathiri maendeleo ya biashara zao na kufifisha nia ya kuendelea kukopa .Zifuatazo ni picha za ziara hiyo ya kamati ya bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa mkoani Njombe.
 Wajumbe wa kamati ya bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakikagua ujenzi wa nyumba ya Walimu inayojengwa na TASAF katika kijiji cha Ulembwe nje kidogo ya mji wa Njombe. 
 Wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali Mitaa wakipata maelezo ya mradi wa ujenzi wa nyumba ya Walimu katika kijiji cha Ulembwe inayojengwa TASAF ikiwa ni jitihada za serikali za kutatua tatizo la makazi kwa walimu.
 Baadhi ya wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa , wakisalimiana na walengwa ya TASAF katika kijiji cha Ulembwe mkoani Njombe katika ziara ya kamati hiyo kukagua miradi ya TASAF,MKURABITA,TAMISEMI na Mfuko wa Rais wa Kujitegemea.
 Mkuu wa mkoa wa Njombe ,Christopher ole Sendeka (watatu  kulia), baadhi ya wabunge na Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Ladislaus Mwamanga (aliyevaa Kaunda suti nyeusi ) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini katika kijiji cha Uwemba mkoani Njombe.
 Baadhi ya walengwa wa TASAF katika wa kijiji cha Ulembwe ,nje kidogo ya mji wa Njombe wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge waliofanya ziara kijijini hapo .Wakiwa kijijini hapo ule usemi wa mgeni njoo mwenyeji apone ulidhihirika baada ya Waziri Kairuki kuahidi kumsomesha mmoja wa watoto kutoka kaya ya mlengwa hadi kidato cha nne. 
 Wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya utawala na serikali za mitaa wakipata maelezo kutoka kwa mmoja wa wananchi walionufaika na fedha kutoka mfuko wa Rais wa kujitegemea katika mji wa Makambako mkoani Njombe ambaye anaendesha kilimo cha viazi mviringo.
 Waziri Kairuki na Wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya Utawala bora na Serikali za Mitaa wakiangalia bidhaa za ususi zinazofanywa na baadi ya wanawake kupitia kikundi chao kilichowezeshwa na Mfuko wa Rais wa Kujitegemea mjini Njombe.
 Baadhi ya Wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya utawala na serikali za mitaa wakipata maelezo kutoka kwa mmoja wa wanufaika wa Mfuko wa Rais wa kujitegemea mkoani Njombe aliyetumia fedha alizokopeshwa na mfuko huo kuanzisha mradi wa kufuga n’gombe.
 Waziri Kairuki wa kwanza kushoto akifuatiwa na mhe. Mwamoto,wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa mkoa wa Njombe akiwemo mkuu wa mkoa huo Christopher Ole Sendeka ,nyuma yao ni baadhi ya wanufaika wa MKURABITA. 
 Waziri Kairuki aliyevaa gauni lenye rangi nyekundu na Mwenyekiti wa kamati ya bunge ya utawala na serikali za mitaa mhe. Venance Mwamoto wakitoa nasaha kwa baadhi ya wanufaika wa MKURABITA mkoani Njombe.
 ‘’Karibuni tena Mkoani Njombe’’ndivyo wanavyoelekea kusema wenyeji kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa waliotembelea mkoa huo kukagua miradi ya TASAF,TAMISEMI ,MKURABITA na Mfuko wa Rais wa Kujitegemea.
Waziri Angellah Kairuki watatu kutoka kushoto mstari wa mbele akiwa na Mhe.Magreth Sitta na Mhe.Ruth Mollel ambao ni wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge wa utawala na serikali za mitaa wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Walengwa wa TASAF katika kijiji cha Ulembwe nje kidogo ya mji wa Njombe.

AICC yashauriwa kuwekeza Dodoma

Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeushauri uongozi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) kuelekeza nguvu ya uwekezji katika mji wa Dodoma ili kuziba kukidhi ongezeko la huduma za kumbi za kufanyia muikutano linalosababishwa na serikali kuhamia katika mji huo.

Akizungumza katika kikao cha majumuisho baada ya Kamati ya PIC kutembelea AICC mwishoni mwa wiki na kukagua miradi miwili, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Albert Obama ameshauri AICC kuupa kipaumbele mkoa wa Dodoma katika mkakati wa kujenga kituo kingine cha kisasa cha Mikutano.

“Tunahitaji kuiona taasisi hii ikipanuka na kujenga vituo vingine vya mikutano huko mikoani na moja ya mikoa ambayo tungependa muipe kipaumbele ni Dodoma maana huko ndio serikali inahamia na mahitaji ya huduma ya kumbi za mikutano yanakwenda kuongezeka”, alisisitiza Obama.

Nae Mjumbe wa Kamati hiyo, Amina Mollel alieleza kufurahishwa na juhudi za uongozi wa AICC kumilisha ujenzi wa mradi wa nyumba za kisasa (apartment) 48 ambapo azote zina wapangaji na kuwa sehemu muhimu ya kuongeza mapato ya shirika.

Aidha ameushauri uongozi wa AICC kuzingati uwekaji wa miundombinu ya walemavu katika miradi mingine inayotekelezwa ukiwemo mradi wa ujenzi wa ukumbi wa kisasa kwa ajili ya maonesho ambao unatarajiwa kukamilika mwezi Mei mwaka huu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mwendeshaji wa AICC, Elishilia Kaaya aliieleza Kamati ya PIC kuwa Kituo kina mipango ya baadae ya kujenga Kituo kingine cha Kisasa cha Mikutano kitakachojulikana kama Mount Kilimanjaro International Convention Centre (MKICC) ili kukabiliana na ushindani wa biashara ya mikutano kutoka nchi za jirani kama Rwanda ambayo tayari ina Kituo cha kisasa cha Kigali na Kenya ambayo tayari inatarajia kujenga Kituo cha kisasa cha Mikutano huko Mombasa.

Kaaya ameeleza kuwa AICC imefanikiwa kununua ekari 23 katika mji wa Mtwara na pia inatafuta ardhi katika mikoa ya Dodoma, Mwanza na Iringa kwa ajili ya kujenga Vituo vingine vya Mikutano. Aidha alieleza Kamati kuwa mbali na kujenga Vituo vya Mikutano, AICC inatarajia kujenga miundombinu kwa ajili ya Wanajuiya ya Kidiplomasia eneo la Laki Laki nje kidogo ya mji wa Arusha ambapo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imetenga eneo kubwa kwa ajili ya taasisi mbalimbali za kimataifa kujenga ofisi. 

Mbali na biashara ya mikutano, AICC inajishughulisha pia na upangishaji wa ofisi na nyumba na pia inatoa huduma za afya kupitia hospitali yake. Pia AICC inamiliki Kituo cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) kilichopo Dar es Salaam.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma wakiwa katika mradi wa nyumba za kisasa za kupangisha za AICC ambapo mradi huu umekamilika na tayari nyumba hizo zimeisha pata wapangaji. 
Mkurugenzi wa Miliki na Miradi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Victor Kamagenge (kushoto) akitoa maelezo kwa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji Mitaji ya Umma, juu ya ujenzi wa ukumbi wa kisasa wa maonesho. Kamati hiyo ilitembelea AICC mwishoni mwa wiki kukagua miradi miwili ya ujenzi wa ukumbi wa maonesho ambapo ujenzi wa unaendelea na mradi mwingine wa nyumba za kisasa 48 ambao tayari umekamilika.

Comments

Popular posts from this blog

AMANI YETU TUILINDE NAIBU WAZIRI CHANDE AZUNGUMZA KATIKA IJITIMAI JIJINI DODOMA

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?

UNAMKUMBUKA AMINA CHIFUPA WA MPAKANJIAA.