Polisi wapekua nyumba ya Mbunge Lema

JESHI la Polisi mkoa wa Arusha jana limefanya upekuzi wa zaidi ya Saa 1 katika nyumba anayoishi Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini Godbless Lema (Chadema) iliyopo Njiro mjini hapa.

Lema anaedelea kushikiliwa na polisi mkoani hapa kwa ajili ya mahojiano tangu Alhamisi baada ya kukamatwa akiwa bungeni Dodoma na kusafirishwa hadi mkoani hapa.
Aidha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Charles Mkumbo akizungumza na MTANZANIA Jumapili kwa njia ya simu jana, ili kupata uhakika wa habari za kupekuwaliwa nyumbani kwa kiongozi alisema, hawezi kutoa taarifa za mambo ya kipelelezi.

"Hayo ni mambo ya kiuchunguzi hatuwezi kutangaza taarifa leo tunamhoji au kupekua mtu nyumbani kwake hapana. Hatuwezi kutoa taarifa za kila kitu tunachofanya,"alidai Kamanda Mkumbo.

Hata hivyo Mke wa mbunge huyo Neema Lema, akizungumza kwa njia ya simu alidai kwamba ni kweli askari polisi wakiwa na magari manne, askari wenye silaha wakiongozana na OC CID Damass Massawe walifika nyumbani kwake kupekua.

"Sikuwepo nyumbani kwa wakati huo. Nilikuwa nje kidogo ya mji eneo la Kisongo kumuona dada yangu, wakati wao wakipekua. Lakini taarifa zote nimezipata kwamba wamepekua nyumba nzima kasoro chumba tunacholala kwani nilikifunga na kuondoka na ufunguo," alidai Neema na kuongeza:

"Kwa kweli hawakuondoka na kitu chochote. Lakini pia hawakusema wanatafuta nini, na ili tu uone hakuna wanachokitafuta ni kwamba tangu juzi walipoanza kumshikilia mpaka leo (jana) walikuwa hawajamhoji," alidai.

Wiki iliyopita Lema akiwa bungeni mjini Dodoma mara baada ya kumalizika kwa vikao kwa Bunge alitiwa nguvuni na jeshi la polisi kisha kusafirishwa usiku hadi mkoani Arusha kwa ajili ya kuhojiwa dhidi ya tuhuma zinazodaiwa kumkabili.
Akithibitisha kushikiliwa na kuhojiwa kwa Lema, ofisini kwake juzi mjini hapa Kamanda 

Mkumbo alisema, ni kweli kiongozi huyo alikuwa anaendelea kushikiliwa katika mahabusu iliyopo kituo Kikuu cha Polisi mjini hapa.
"Ni kweli tunamshikilia yupo mahabusu, tunaendelea kumhoji kuna mambo bado tunakamilisha ya kiuchunguzi,tukimaliza kumhoji tutamfikisha mahakamani,"alisema Kamanda Mkumbo

Novemba Mosi, Mwaka huu Lema alikamatwa na polisi akidaiwa kutoa lugha zenye uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli, katika mikutano yake hadhara ya Jimbo ambapo alihojiwa na kuachiwa kwa dhamana.
Akifafanua madai hayo Kamanda Mkumbo alisema zipo baadhi ya tuhuma ambazo hawakuwa wamemuhoji. Hivyo kukamatwa kwake ni muendelezo wa upelelezi kabla hawajamfikisha mahakamani.

"Tunamshikilia Lema hatutampa dhamana mpaka tumalize kumhoji, kuna masuala tulikuwa hatujamhoji juzi na akimaliza kuhojiwa atapelekwa mahakamani,"alidai.

Alisema wanaendelea kumhoji Lema kwa tuhuma za kutoa lugha zenye uchochezi dhidi ya Rais Dkt. Magufuli, kupitia mikutano ya hadhara aliyoifanya katika jimbo hilo.
“Alitoa lugha zenye uchochezi kinyume cha sheria na baadhi ya maneno aliyotoa yenye uchochezi ni kama “Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiendelea kugandamiza dekomrasia siasa za ugandamizaji taifa litaingia katika umwagaji wa damu,”alinukuu Kamanda Mkumbo na kuongeza:
\
“Nchi hii inaandaliwa kwenda katika utawala wa kidikteta na pia aliwataka wananchi wawe tayari kwa lolote na waache kabisa uoga kwani uoga ni dhambi mbaya kuliko dhambi zote duniani,” alisema.

Comments

Popular posts from this blog

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?

UNAMKUMBUKA AMINA CHIFUPA WA MPAKANJIAA.

AMANI YETU TUILINDE NAIBU WAZIRI CHANDE AZUNGUMZA KATIKA IJITIMAI JIJINI DODOMA