TLS,TWAWEZA: MUSWADA HUU WA SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI MZURI
Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na Taasisi ya
Twaweza wamesema kuwa Muswaada wa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ni
bora kuliko Miswada iliyowahi kuwasilishwa nchini.
Haya yamebainishwa katika maoni yao waliyowasilisha
kwenye Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii leo Mjini Dodoma katika
juhudi za kuufanya Muswada huo kuwa bora zaidi na kupelekea kuapa sheria yenye
tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
TLS na Twaweza wamebainisha kuwa Muswada huu ni bora
zaidi na utasaidia kuwajengea wadau wa
habari nchini heshima kwa kutoa huduma bora kupitia vyombo vya habari kwa kuzingatia taaluma ya
Habari waliyonayo hatua ambayo inautofautisha na muswada uliowasilishwa Bungeni
mwaka 2015.
Kwa mujibu wa maoni yalitolewa na Chama cha Wanasheria
Tanganyika (TLS) yamesema Muswada huo mzuri zaidi na unaifuta Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976 hatua ambayo
wameipongeza Serikali kwani Sheria hiyo
iliwahi kuainishwa kuwa miongoni mwa Sheria 40 na kusadikiwa na Tume ya
Jaji Francis Nyalali kama Sheria kandamizi.
Kwa upande wa Taasisi ya Twaweza wao wamesema kuwa Muswada
huo utaanzisha utaratibu ambao utawatambua waandishi wa habari kwa kuanzisha
Baraza Huru la Habari pamoja na Bodi ya Ithibati ya wanahabari amabazo
zitasimamia kanuni na maadili ya wanahabari, kusimamia viwango na mienendo ya
kitaaluma na kuendeleza vigezo bora vya maadili na nidhamu miongoni mwa
wanahabari.
Kwa mantiki hiyo, maoni yaliyowasilishwa kwa Kamati hiyo
yanaendana na Muswada ambao unasisitiza kuanzisha
mahusiano na taasisi nyingine za taaluma ya habari ndani na nje ya nchi ili
wadau wa habari waweze kubadilishana mawazo na kuwa na namna bora ya
kuhabarisha umma katika masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.
Aidha, Baraza huru la habari kutakuwa suluhisho katika kusimamia
na kusikiliza malalamiko ambayo yatawasilishwa kwenye baraza hilo kulingana na
kanuni za maadili ya taaluma ya habari hatimaye kuifanya tasnia ya habari
kuheshimika tofauti na hali ilivyokuwa hapo awali.
Uboreshwaji wa Muswada huo unalenga kuleta Sheria
itakayosimamia Tasnia ya Habari ili iweze kuendana na wakati pamoja na Sheria
za kimataifa na namna bora ya kuwahudumia wananchi.
Comments
Post a Comment