MKURUGENZI MTENDAJI WA TPDC AZUNGUMZIA HALI YA GES NA MAFUTA NCHINI

 Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mussa Makame, akizungumza na wanahabari katika ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO jijini Dodoma  akielezea mafanikio ya shirika hilo tangu kuanzishwa kwake, upatikanaji wa gesi na mafuta hebu fuatana nae katika hotuba yake kisha kwenye Mhagale Online TV

SHIRIKA LA MAENDELEO YA PETROLI TANZANIA

 

 

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MAFANIKIO YA SHIRIKA

KWA MWAKA WA FEDHA 2025/26

PAMOJA NA MIRADI YA MAENDELEO INAYOTEKELEZWA NA TPDC

KWA MWAKA WA FEDHA 2026/27

 

TAREHE: 21 SEPTEMBA 2026


 

1.       UTANGULIZI

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ni Shirika la Taifa la Mafuta linalomilikiwa na Serikali na lenye jukumu la kusimamia na kuendeleza shughuli za kibiashara za mafuta na gesi asilia nchini kwa niaba ya Serikali. Katika mwaka wa fedha 2025/26, TPDC iliendelea kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya mafuta na gesi asilia - ikihusisha kutafuta, kuendeleza, kuzalisha, kusafirisha na kusambaza rasilimali za mafuta na gesi asilia, kuimarisha miundombinu ya mafuta na gesi asilia na kuhakikisha Watanzania wananufaika kutokana na fursa zinazotokana na maendeleo ya sekta hii.

Katika kipindi hicho, Shirika liliendelea kufanya kazi kwa ufanisi na kibiashara, huku likiendelea kutekeleza na kushiriki katika miradi ya kimkakati yenye umuhimu kwa usalama wa nishati na uchumi wa Taifa. Aidha, TPDC iliendelea kuwekeza katika watu, teknolojia na mifumo ili kuongeza ufanisi na tija katika utekelezaji wa majukumu yake.

2.       MAFANIKIO YA KIBIASHARA NA MCHANGO KWA TAIFA

Katika mwaka wa fedha 2025/26, TPDC iliendelea kuimarisha uendeshaji wake kwa ufanisi wa hali ya juu na kupata mafanikio makubwa ya kibiashara. Baadhi ya viashiria vya mafanikio haya ni:

·       TPDC ilipata faida ya kiasi cha shilingi bilioni 72.98;

·       TPDC ililipa kodi za ujumla wa kiasi cha shiling bilioni 50.04;

·       TPDC ililipa mgawo wa faida na mrabaha (profit gas share and royalty) kwenye mfuko wa mapato ya mafuta na gesi jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 142.61; na

·       TPDC ililipa gawio (dividend) kiasi cha shilingi bilioni 15.118.

Mafanikio haya yanaendelea kuimarisha uwezo wa TPDC wa kutekeleza majukumu ya kimkakati kwa Taifa na kujenga Shirika lenye uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi na kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.

3.       SHUGHULI ZA UZALISHAJI WA GESI ASILIA

Katika mwaka wa fedha wa 2025/26, TPDC kwa kushirikiana na Waendeshaji wa Vitalu vya Songosongo (Panafrican Energy Tanzania - PAET) na Mnazi Bay (maurel & Prom – M&P) tumeendelea na shughuli za uzalishaji wa gesi asilia katika vitalu hivyo kwa wastani wa futi za ujazo milioni 170 kwa siku Sehemu kubwa ya uzalishaji huo umeendelea kutumika katika uzalishaji wa umeme na sehemu iliyobaki imetumiwa na viwanda, kwenye Taasisi na majumbani.

4.       MIRADI MIKUU YA MAENDELEO NA SHUGHULI ZILIZOTEKELEZWA NA TPDC

4.1       Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP)

Serikali kupitia TPDC ina umiliki wa asilimia 15 katika mradi wa EACOP. Mradi huu tayari unaendelea kutekelezwa ukihusisha ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga nchini Tanzania. Hadi kufikia sasa, mradi umefikia asilimia 92.7 ya utekelezaji. Kupitia utekelezaji wake, Serikali na Watanzania wanaendelea kunufaika na ajira, fursa za kandarasi na zabuni mbalimbali za utoaji huduma, pamoja na ufaulishaji wa teknolojia na ujuzi kama ifuatavyo:

(i)          Mradi umeendelea kutoa manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi kupitia ajira, biashara na maendeleo ya jamii. Katika kipindi cha ujenzi, jumla ya ajira 10,000 zimezalishwa, ambapo ajira 7,500 sawa na asilimia 75 zimenufaisha Watanzania. Vilevile, kampuni zaidi ya 200 za Kitanzania zimepewa kandarasi za ugavi wa bidhaa na huduma zenye thamani inayozidi Shilingi Trilioni 1.325, hatua ambayo imeongeza ushiriki wa sekta binafsi ya ndani na kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.

(ii)         Kwa upande wa mapato ya Serikali, utekelezaji wa mradi umewezesha kukusanywa kwa zaidi ya Shilingi Bilioni 100 kupitia kodi, ada, ushuru na tozo mbalimbali. Mradi unatarajiwa kuongeza zaidi mchango wake kwa uchumi wa Taifa mara utakapoanza rasmi hatua ya uendeshaji.

(iii)       Mradi umeendelea kuchangia miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) katika nyanja za elimu, afya na mazingira ikiwemo mradi wa maji wenye thamani ya takribani Shilingi Bilioni 4.4 unaowanufaisha wananchi zaidi ya 26,000, ujenzi na uboreshaji wa huduma za afya katika Kata ya Chongoleani, ugawaji wa miche ya minazi milioni mbili, pamoja na ujenzi wa kituo cha kisasa cha michezo. Aidha, vijana 800 wamepatiwa mafunzo ya stadi za kazi ili kuwawezesha kujiajiri na kuajiriwa katika sekta mbalimbali. 

Tunatarajia tone la kwanza la mafuta (First Drop) kuingia katika Pump Station No. 1, iliyopo nchini Uganda, mwezi Disemba 2026. Baada ya hapo, mafuta ghafi yatasukumwa katika mfumo wa bomba kutoka Uganda mpaka Tanzania kwa muda wa miezi miwili na kufika Chongoleani, Tanga mwezi Februari 2027. Baada ya kufika Tanga, mafuta ghafi yatajazwa katika matenki manne yenye uwezo wa kuhifadhi mafuta mapipa milioni mbili (2) kwa pamoja. Baada ya kukamilika kwa majaribio ya uwezo wa matenki kuhifadhi mafuta, upakiaji wa shehena ya kwanza ya mafuta ghafi mkatika meli unatarajiwa kuanza mwezi Machi 2027. Hatua hii itaashiria kuhitimisha rasmi awamu ya ujenzi na kuanza kwa awamu ya uendeshaji wa mradi kwa kipindi cha miaka 25 ijayo. 

4.2       Mradi wa Uchakataji na Usindikaji wa Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG).

Kupitia timu ya Majadiliano ya Serikali, katika mwaka wa fedha 2025/26 Serikali imefikia makubaliano na Makampuni ya Kimataifa ya nishati (international Energy Companies – IECs) katika maeneo ya kibiashara, kikodi na namna ya ugawanaji mapato. Kwa sasa, Serikali inaendelea na zoezi la kukamilisha mazungumzo katika upande wa sheria zitakazosimamia ujenzi na uendeshaji wa mradi.

Mradi huu utakuwa ni uwekezaji mkubwa na wa kihistoria katika sekta ya nishati nchini, unaotarajiwa kuibadilisha Tanzania kuwa kitovu muhimu cha biashara ya gesi asilia katika ukanda na kimataifa.

TPDC itashikilia umiliki na kusimamia nafasi ya Taifa kwenye mradi huu hivyo tayari imeanza maandalizi ya kitaasisi na kiufundi kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, ikiwa ni pamoja na maandalizi ya rasilimali watu, mifumo na usimamizi wa miundombinu.

Eneo la kutekeleza mradi huu lilishapatikana na Wananchi kulipwa fidia. Serikali, chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu imeunda timu itakayochambua na kuweka mpango wa ushiriki wa Watanzania katika mradi huu. Timu hii imeshaanza kukutana na tutarajie mrejesho toka kwao katika siku za karibuni.

4.3       Mradi wa Uchorongaji wa Visima Vipya vya Gesi Asilia – Mnazi Bay

Shirika kwa kushirikiana na mbia wake, Kampuni ya Maurel & Prom (M&P), limefanikiwa kuchoronga visima vitatu vya gesi asilia katika Kitalu cha Mnazi Bay, ambapo visima viwili ni vya kuongeza uzalishaji na kisima kimoja ni cha utafiti. Visima viwili vya kuongeza uzalishaji tayari vimekamilika na kuunganishwa katika mnyororo wa uchakataji wa gesi asilia ambapo visima hivyo viwili kwa pamoja vina uwezo kwa kuzalisha takribani futi za ujazo milioni 65 kwa siku, hivyo kuongeza uwezo wa uzalishaji wa gesi asilia na kuimarisha upatikanaji wa nishati nchini. Uchorongaji wa Kisima kimoja cha utafiti nao umekamilika na zoezi la uchukuaji na uchakataji wa taarifa kwenye kisima unaendelea ili kubaini uwepo na kiasi cha gesi asilia katika kisima husika. 

Kwa ujumla, utekelezaji wa mradi huu umegharimu Dola za Marekani milioni 90 na umefungua fursa kwa kampuni 35 za Kitanzania kushiriki katika utoaji wa huduma mbalimbali. Aidha, mradi huu umezalisha fursa za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa Watanzania.

4.4       Mradi wa Kitalu cha Ruvuma (Ntorya) na Ujenzi wa Bomba la Ntorya hadi Madimba

TPDC inaweka mkazo mkubwa katika uendelezaji wa gesi iliyogunduliwa katika Kitalu cha Ruvuma, eneo la Ntorya, pamoja na ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi ghafi kutoka Ntorya hadi Madimba, Mtwara. Mradi huu ni wa kimkakati wenye lengo la kuongeza uzalishaji wa gesi asilia na miundombinu ya usafirishaji, uchakataji na usambazaji wake.

Mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka eneo la Ntorya hadi Kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha madimba utahusisha bomba la chuma, lenye kipenyo cha inchi 14, urefu wa kilometa 34.2 na uwezo wa kusafirisha gesi ghafi hadi futi za ujazo milioni 140 kwa siku, pamoja na miundombinu yake (initial station, block valve station na receiving station).  Thamani ya mradi ni Shilingi za Kitanzania Bilioni 122.7 na hadi kufikia sasa, utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 67 na mradi unatarajiwa kukamilika katika robo ya mwisho ya mwaka 2026.

4.5       Mradi wa Uchukuaji wa Taarifa za Mitetemo 3D – Kitalu cha Lindi-Mtwara

TPDC inaendelea na uchukuaji wa taarifa za mitetemo kwa mfumo wa 3D katika eneo la takribani kilometa za mraba 736 katika Kitalu cha Lindi-Mtwara. Taarifa hizi ni muhimu katika kubaini kwa usahihi maeneo yenye uwezekano wa kuhifadhi mafuta au gesi asilia na kuongeza uwezekano wa ugunduzi mpya. Mradi huu ni sehemu ya uwekezaji wa TPDC katika utafutaji wa rasilimali mpya ambazo zinaweza kuongeza kiwango cha rasilimali za mafuta na gesi asilia nchini. Mradi huu unakadiriwa kugharimu kiasi cha shillingi bilioni 107, hadi sasa utekelezaji wa mradi umefika asilimia 50 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Julai, mwaka 2027.

4.6       Mradi wa Utafutaji wa Mafuta na Gesi – Kitalu cha Eyasi-Wembere

TPDC inaendelea na utafutaji wa mafuta katika Kitalu cha Eyasi-Wembere kinachohusisha maeneo yaliyopo katika mikoa ya Singida, Tabora, Simiyu, Arusha na Shinyanga. Utafiti huu unajumuisha uchukuaji wa taarifa za mitetemo kwa mfumo wa 2D na ni sehemu ya jitihada za kutafuta rasilimali mpya za mafuta nchini. TPDC imekamilisha uchukuaji wa kilomita za urefu 779 na inaendelea na utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi yenye urefu wa kilomita 325.7. Awamu hii inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu wa fedha, na jumla ya mradi utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 53.  

4.7       Upanuzi wa Usambazaji wa Gesi Asilia kwa Viwanda, Majumbani, Taasisi na Magari

Katika mwaka wa fedha 2025/26, TPDC iliunganisha nyumba 1,000 katika mikoa ya Pwani na Lindi na kuunganisha viwanda viwili. Shirika pia liliendelea kutoa huduma kwa katika kituo chake cha CNG Mlimani chini ya uendeshaji wa Kampuni yake GASCO. Vile vile, Shirika liliunganisha vituo vitatu (03) vya CNG ambavyo vinamilikiwa na wawekezaji binafsi.

TPDC inaendelea kupanua miundombinu ya gesi asilia katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara, huku ikiendelea na hatua mbalimbali za kufikisha huduma katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Tanga, Kilimanjaro na Arusha. Sambamba na hilo, Shirika kupitia mkandarasi wake nchini China, linaendelea na usanifu na uzalishaji wa vituo vya CNG-V na CNG-V Mobile Stations ambavyo vitaletwa nchini na kuwekwa katika mikoa tajwa.

Upanuzi huu unalenga kuongeza matumizi ya gesi asilia katika usafirishaji, viwandani na majumbani, kupunguza utegemezi wa mafuta yanayoagizwa kutoka nje, kupunguza gharama za uendeshaji na kuchangia matumizi ya nishati safi na maendeleo endelevu.

4.8       Mradi wa Bomba la Gesi Asilia kutoka Kinyerezi hadi Chalinze

Mradi huu unalenga kufikisha gesi asilia kwa njia ya bomba kutoka Kinyerezi-Dar es Salaam hadi Chalinze - Pwani ili kufikia Kongani za Viwanda za Mkoa wa Pwani (Zegereni, Kwala, n.k) pamoja na viwanda vingine vinavyoendelea kujengwa katika maeneo hayo. Tayari mkuza wa ujenzi wa mradi umepatikana na kazi zinazoendelea kwa sasa chini ya Mshauri Elekezi ni Upembuzi Yakinifu wa mradi ambao umefikia 90.4% na Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii iliyofikia 81%. Baada ya kukamilika kwa kazi hizo, taratibu za kumpata Mkandarasi wa ujenzi zitaendelea. 

4.9       Miradi Midogo ya Gesi Kimiminika (Mini-LNG)

Teknolojia ya miradi midogo ya kubadili gesi asilia kuwa kimiminika (Mini-LNG) imethibitika kibiashara kuweza kufikisha gesi asilia zaidi ya kilomita 500 kwa faida, ikisafirishwa kwenye malori maalum kufikia maeneo yasiyo na miundombinu ya mabomba. Shirika limeanza majadiliano na wawekezaji wa teknolojia hii ili kuweza kupata miradi ya aina hii itakayowezesha gesi asilia kufikishwa nchi nzima. Hadi sasa mazungumzo yanaendelea na Kampuni 6 ambapo kati ya hizo tayari TPDC imesaini makubaliano ya mauziano ya gesi asilia na Kampuni 3 na tayari zinaendelea na hatua mbalimbali za utekelezaji ikiwa ni pamoja na kukamilisha ununuzi wa ardhi na Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii (ESIA) kabla ya kutafuta Wakandarasi wa ujenzi.

4.10   Biashara ya Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja

Biashara ya mafuta inahusisha TPDC kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi kupitia mfumo wa uagizaji kwa pamoja ambao huratibiwa na Petroleum Bulk Procurement Agency (PBPA). Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26, TPDC ilishiriki na kushinda zabuni sita (6) za kuingiza mafuta nchini. Kufuatia changamoto ya vita vya Marekani na Israeli dhidi ya Irani iliyoanza mwezi Februari, 2026 ambapo ilipelekea ongezeko la bei ya mafuta, Mwezi Machi 2026 baada ya kushindanishwa, TPDC ilifanikiwa kupewa jukumu la kuingiza mafuta yote ya nchi kwa kipindi cha miezi mitatu (Mei, Juni na Julai). Katika kipindi hiki TPDC ilitakiwa kuingiza jumla ya meli 34 na zote zilishawasili nchini kwa utaratibu na ratiba iliyopangwa na PBPA.

4.11    Miradi ya Kusafirisha Gesi na Mafuta kwenda Nchi Jirani

Miradi hii kwa sasa inahusisha nchi za Kenya, Uganda, Zambia na Msumbiji na inahusu miundombinu ifuatayo:

(i)          Mradi wa bomba la gesi asilia kwenda Uganda: Mshauri Mwelekezi ameshaanza Upembuzi Yakinifu wa mradi. Kukamilika kwa Upembuzi Yakinifu kutaruhusu makubaliano ya namna ya uendeshaji wa mradi baina ya nchi husika kabla ya kutafuta Mkandarasi wa ujenzi wa mradi.

(ii)         Mradi wa bomba la mafuta safi kwenda Uganda: Mshauri Mwelekezi anaendelea na Upembuzi Yakinifu wa mradi unaotarajiwa kukamilika Machi 2027. Baada ya Upembuzi Yakinifu nchi husika zitakubaliana namna ya uendeshaji wa mradi kabla ya ujenzi kuanza.

(iii)       Mradi wa kusafirisha gesi asilia kwenda Kenya (Mombasa): Timu za Watalaam inaboresha nyaraka za maridhiano (Bilateral Agreements) ili kuruhusu kuanza taratibu za kutafuta Mshauri Mwelekezi wa kufanya Upembuzi Yakinifu wa mradi.

(iv)       Mradi wa bomba jipya la mafuta safi kwenda Zambia: mradi huu unatekelezwa kwa utaratibu wa Public-Private-Partnership (PPP) ambapo kwa sasa upekuzi (due diligence) wa mwendelezaji wa mradi (project developer) unaendelea kabla ya kukabidhiwa mradi.

(v)        Mradi wa bomba la gesi asilia kutoka Msumbiji kuja Tanzania: pamoja na vikao mbalimbali vya majadiliano vinavyoendelea baina ya Timu za Wataalam kutoka nchi hizi mbili, Rasimu ya Hati ya Makubaliano (Memorandum of Understanding - MoU) imekamilishwa na kuwasilishwa Wizara na Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mapitio na idhini ili kuweza kusainiwa. Kusainiwa kwa MoU kutawezesha kuweka msingi wa makubaliano ya kitaalam juu ya utekelezaji wa mradi huu.

5.       UTEKELEZAJI WA MIRADI YA CSR (UWAJIBIKAJI KWA JAMII)

Katika mwaka wa fedha 2025/26, TPDC iliendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na huduma kwa jamii katika maeneo ambayo Shirika linaendesha shughuli zake. Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa kivuko (Ferry) cha kisasa katika Kisiwa cha Songosongo, unaogharimu takribani TZS bilioni 5.7, kinacholenga kurahisisha usafiri wa wananchi kutoka kisiwani Songosongo kwenda Kilwa Masoko na Kilwa Kivinje. Ujenzi wa kivuko hicho umefikia asilimia 55 na unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba 2026, ambapo kitaanza kutoa huduma kwa wananchi.

Aidha, Shirika limeendelea na ujenzi wa Vituo vya Afya vya Dihimba na Madimba mkoani Mtwara, vinavyogharimu takribani TZS bilioni 2.4, pamoja na kutekeleza miradi mbalimbali ya maji, elimu na afya katika maeneo mbalimbali nchini ambako TPDC inatekeleza shughuli na miradi yake. Hatua hizi zinaakisi dhamira ya Shirika ya kushirikiana na jamii na kuchangia katika kuboresha huduma za msingi na ustawi wa wananchi na kuendeleza mahusiano na mashirikiano na jamii na kuweza kupata dhamana ya kuendesha shughuli zake (Social License to Operate).

6.       FAIDA ZA MIRADI HII NA FURSA KWA VIJANA

Miradi hii yote si tu kwamba inachochea ukuaji wa uchumi wa Taifa, bali pia inafungua milango ya ajira, ujuzi na ushiriki wa vijana katika sekta ya nishati.

Kupitia miradi hii, vijana wanapata fursa za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, mafunzo ya vitendo (on-job training), zabuni za huduma mbalimbali katika nyanja za uhandisi, usafirishaji, ujenzi, ugavi, teknolojia na huduma za kitaalamu. Aidha, kupitia utekelezaji wa Sera ya Ushiriki wa Watanzania Kiuchumi (Local Content Policy), TPDC inaendelea kuhakikisha kuwa Watanzania, hususan vijana, wanashiriki kikamilifu katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya mafuta na gesi.

TPDC itaendelea kushirikiana na Serikali, sekta binafsi na wadau wengine kuhakikisha rasilimali za mafuta na gesi asilia zinatumika kwa tija, uwazi na manufaa mapana ya Taifa, kwa kizazi cha sasa na kijacho.

7.       CHANGAMOTO NA FURSA

Mahitaji ya gesi asilia nchini yameongezeka na kwa sasa yanazidi uwezo wa uzalishaji wa gesi asilia kutoka katika vitalu vya Songosongo na Mnazi Bay vinavyozalisha kwa sasa. TPDC inaliona ongezeko hili la mahitaji si changamoto pekee, bali pia ni fursa kubwa ya kuongeza uzalishaji, kuendeleza maeneo mapya ya gesi na kuhakikisha mahitaji ya Taifa na nchi jirani yanakidhiwa.

8.       MWELEKEO WA TPDC KWA MWAKA 2026/27

Katika kipindi cha mwaka wa fedha tulionao, Mwelekeo wa Shirika unaendelea kuwa tuhakikisha tunaweka nguvu, jitihada na rasilimali zetu ikiwemo rasilimali fedha na watu katika kuhakikisha tunaongeza uzalishaji wa gesi asilia na upatikanaji wake ili kukidhi mahitaji makubwa ya gesi asilia hapa nchini na nchi za jirani. Tutaendelea kuweka mkazo katika shughuli za kuongeza uzalishaji katika Vitalu vya Mnazi Bay na Songosongo lakini pia tutaweka mkazo mkubwa katika Kitalu cha Ruvuma eneo la Ntorya kwa kushiriki shughuli za uendelezaji wa gesi iliyogunduliwa pamoja na kukamilisha ujenzi wa bomba la kusafirishia gesi kutoka eneo la Ntorya hadi Madimba. Sambamba na hayo, tutaweka mkazo mkubwa katika shughuli zinazoendelea za utafutaji katika Vitalu vyetu ya Kimkakati vya TPDC ikiwemo:

(i)    Kitalu cha Lindi-Mtwara kwa kuendelea kukusanya taarifa za mtetemo za 3D na kuzitafsiri tayari kwa maandalizi ya mpango wa uchorongaji;

(ii)  Kitalu cha Eyasi Wembere kwa kumalizia uchukuaji wa taarifa za mtetemo za 2D pamoja na kuzitafsiri tayari kwa maandalizi ya uchukuaji wa taarifa za 3D na uchorongaji wa visima vya utafutaji;

(iii) Kitalu cha Songo Songo Magharibi kwa uchukuaji wa taarifa za mtetemo za 3D tayari kwa ajili ya kuandaa mpango wa uchorongaji;

(iv) Kitalu cha Mnazi Bay Kaskazini kwa kuendelea kutafuta wabia wa kimkakati wa kushirikiana nao kuchoronga visima vya utafutaji;

Vilevile, Shirika litaendelea na jitihada za uunganishwaji wa wateja wapya wa viwanda, taasisi na majumbani na kuhakikisha gesi asilia inafika maeneo mbalimbali ya nchi kwa njia mbalimbali ikiwemo mabomba pamoja na teknolojia mbadala kama vile miradi midogo ya gesi kimiminika (Mini-LNG) na CNG. Kwa upande wa njia za mabomba mkazo utakuwa kuanza ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Kinyerezi hadi Chalinze. Mkazo pia utawekwa kwa Kampuni zetu Tanzu za GASCO na TANOIL kuhakikisha zinaendelea kuleta tija katika majukumu yao.

Mradi wa Uendelezaji wa mkoa wa Tanga kama Kitovu cha biashara ya Mafuta

Mradi huu unaotarajiwa kuendelezwa kwa ushirikiano na Kampuni za UNOC na Vitol Bahrain unalenga ujenzi wa miundombinu ya kuchakata mafuta ghafi (Refinery), sehemu za kuhifadhia mafuta ghafi na safi, mabomba ya kusafirishia mafuta safi na miundombinu mingine wezeshi. Kufuatia kusainiwa kwa Hati za Makubaliano (MoU) kati ya Watekelezaji wa mradi huu, Timu za Kuratibu mradi zimeundwa na zimeanza kazi mbalimbali zitakazowezesha utekelezaji wa mradi kwa ufanisi.

9.       UJUMBE MKUU KWA VYOMBO VYA HABARI

            i.       TPDC imeendelea kufanya vizuri kibiashara na kutekeleza majukumu ya kimkakati kwa Taifa.

           ii.       Shirika linaendelea kuwekeza katika shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini.

         iii.       Upanuzi wa usambazaji wa gesi asilia unaongeza fursa kwa kaya, viwanda, taasisi na sekta ya usafirishaji.

         iv.       Miradi ya kimkakati inafungua fursa za ajira, biashara, ujuzi, teknolojia na ushiriki wa kampuni za Kitanzania.

          v.       Vijana ni sehemu muhimu ya nguvu kazi na mustakabali wa sekta ya mafuta na gesi.

10.   HITIMISHO

TPDC chini ya Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi na wadau wengine kuhakikisha rasilimali za mafuta na gesi asilia zinatumika kwa tija, uwazi na manufaa mapana ya Taifa, kwa kizazi cha sasa na kijacho.

 

Imetolewa na:
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji,
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)







Wanahabari wakiwa tayari kumsikiliza kwa makini 






 

Comments

Popular posts from this blog

AJIRA MPYA 41,500 SERIKALINI ZATANGAZWA KATIBU MKUU UTUMISHI JUMA MKOMI

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?

WALIOPITA KURA ZA MAONI CCM HAWA HAPA