Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?

 Kangaroo hupatikana Australia pekee
 Miamba Bahari ya Australia ni mikubwa kuliko yote Duniani na kivutio kwa watalii
 Ramani ya Australia




Robo tatu ya Waustralia wanaishi katika majiji makubwa na maeneo ya pwani. Fukwe pia ni sehemu za utambulisho wa Australia





SAYARI tuishimo yaani dunia ina mabara saba, ambayo tukianzia kwa mtiririko wa bara kubwa hadi dogo ni Asia, Afrika, Amerika Kaskazini, Amerika Kusini, Ulaya, Antarctica na Australia

Mbali ya mabara hayo ambayo Antartica ni pekee lisilokaliwa na watu kutokana na kufunikwa na barafu kwa asilimia 89, dunia ina nchi huru kati ya 180 na 195 huku ikiwa na mamia kwa maelfu ya visiwa.

Katika makundi hayo matatu, Australia ni pekee duniani iliyobeba sifa zote tatu yaani bara, nchi na kisiwa, kwani nyingi zimeishia kuwa na sifa moja au mbili yaani nchi na au kisiwa.

Australia ni bara dogo kuliko yote duniani, lakini pia kisiwa kikubwa kuliko vyote katika sayari hii.

Mbali ya sifa hizo mbili pia ni nchi ya sita kwa ukubwa duniani.

Australia, au kama inavyojulikana rasmi Jumuiya ya Madola ya Australia, ni nchi iliyo katika kizio cha kusini mwa dunia.

Inahusisha bara Australia, kisiwa cha Tasmania na visiwa vingi katika Bahari za Hindi na Pasifiki.

Nchi jirani ni pamoja na Indonesia, Timor Mashariki na Papua New Guinea kwa upande wa Kaskazini.

Upande wa Kusini Mashariki kuna visiwa vya Solomon, Vanuatu na New Caledonia kwa upande wa Kaskazini Mashariki na New Zealand kwa upande wa Kusini Mashariki.
New Zealand mara nyingi huhesabiwa kuwa sehemu ya Bara la Australia.

Aidha Australia huangaliwa pamoja na visiwa vya Pasifiki katika orodha la mabara ya dunia kama ‘Australia na Pasifiki’.

Kwa karibu miaka 50,000 kabla ya kuja kwa walowezi kutoka Ulaya mwishoni mwa karne ya 18, Australia ilikuwa ikikaliwa na wazalendo wa asili wa eneo hilo, Waustralia, ambao wametokana na moja au zaidi ya makundi yanayozungumza lugha 250.

Baada ya kugunduliwa na wapelelezi wa Kiholanzi mwaka 1606, nusu ya mashariki ya Australia ikaangukia mikononi mwa Uingereza mwaka 1770 na kuitwa rasmi Wales ya Kusini Mpya Februari 7, 1788.

Idadi ya watu ikaongezeka kwa miongo iliyofuata na ikagawanywa katika majimbo sita chini magavana wa kikoloni.

Januari Mosi 1901, makoloni sita yakawa Shirikisho na Jumuiya ya Madola ya Australia ikaundwa.

Ina idadi ya watu milioni 22 huku karibu asilimia 60 ya watu hao wakiishi katika majimbo yenye miji mikuu ya Sydney, Melbourne, Brisbane, Perth na Adelaide.

Mji mkuu wa taifa hili ni Canberra.

Karibu asilimia 56 ya idadi ya watu Australia wanaishi Victoria au Wales Mpya ya Kusini na karibu asilimia 77 huishi bara katika pwani za mashariki.

Australia ni nchi ya 13 kwa uchumi mkubwa duniani.
Na iko juu duniani katika ufanisi wa kitaifa wa maeneo kama vile maendeleo ya mwanadamu, ubora wa maisha, huduma za afya, wastani wa umri wa kuishi, elimu ya jamii, uhuru wa kiuchumi na ulindaji wa haki za kiraia na za kisiasa.

Australia ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Madola, Jukwaa la Visiwa vya Pasikifi, G20 na jumuiya nyingine za ANZUS, OECD, APEC.

Bara hili lililo juu ya bamba la Australia lina eneo la ukubwa wa kilomita mraba 7,617,930.

Umbali kati ya Magharibi na Mashariki ni kilomita 4,000 na kati ya Kaskazini na Kusini ni kilomita 3,700.

Kwa jumla ina pwani yenye urefu wa kilomita 34,218 ikiwa imezungukwa na Bahari ya Hindi, Pasifiki na Bahari ya Kusini.

Bara linakaa kwenye sehemu imara ya bamba la Australia bila mipaka ya gandadunia na kwa sababu hiyo nchi hii haikumbwi sana na matetemeko ya ardhi na hakuna volkano.

Kuna miamba ya bahari mikubwa kabisa duniani zaidi ya 2,900 ikiwa imesambaa katika eneo la karibu kilomita za eneo 350,000 na kutengeneza visiwa zaidi ya 900.

Wasafiri zaidi ya milioni mbili huitembelea miamba hii bahari pamoja na kwamba sehemu kubwa inalindwa dhidi ya shughuli zozote za kibinadamu.

Sehemu kubwa ya bara ni jangwa au maeneo yabisi sana.

Takriban asilimia 40 ya eneo limefunikwa na matuta ya mchanga.

Ardhi yenye rutuba iko kusini mashariki na kona ya kusini magharibi pamoja na hali ya hewa isiyo na joto kali.

Hali ya hewa kaskazini mwa nchi ni kitropiki na kuna misitu minene pamoja na savana na jangwa.

Sehemu kubwa ya uso wa nchi ni tambarare na jangwa.

Kwenye pwani ya mashariki na pia upande wa magharibi kuna safu za milima inayopanda hadi kimo cha mita 2,200.
Sehemu ya juu kabisa huitwa milima ya theluji au Alpi za Australia na mlima wa Kosciuszko unafikia kimo cha mita 2,229. Hapa kuna barafu za kudumu.

Kuna beseni la Ziwa Eyre iliyopo mita 17 chini ya usawa wa bahari.
Tako za beseni hili mara nyingi ni kavu kabisa hujaa mara chache tu baada ya mvua mkubwa sana.

Mahali pakavu kabisa ni jangwa la Simpson lenye mvua chini ya milimita 200 kwa mwaka.

Sehemu kubwa ya bara haina watu.

Wakazi wengi pamoja na miji yote wako kwenye pwani la mashariki na kusini.
Uchumi katika maeneo yabisi hutegemea zaidi ufugaji wa kondoo ambao wanafikia milioni 130 na ng'ombe milioni 25.

Mji mkuu wa Canberra ulijengwa kati ya Sydney na Melbourne baada ya miji hiyo miwili kushindwa kukubaliana kati yao upi ulistahili kuwa mji mkuu.

Mito muhimu inaanza katika safu za Australia ni Murray na Darling na kuunda ukanda muhimu kwa kilimo nchini Australia.

Mingine ni Mto Snowy na Mto Murrumbidgee, Fitzroy (Queensland), Ord, Swan (Australia ya Magharibi).
Aidha kuna Mto Derwent, Tamar (Tasmania) na Hawkesbury uliopo Wales Mpya ya Kusini.

Australia ilitengwa na mabara mengine mamilioni ya miaka iliyopita.

Kwa sababu hiyo kuna aina nyingi za pekee za mimea na wanyama zisizopatikana mahali pengine duniani miongoni mwao akiwa kangaroo.

Miti ya Australia kama vile mkalatusi imesambazwa kote duniani katika nchi zenye hali ya hewa ya kufaa.

Watu wa kwanza walifika Australia takriban miaka 50,000 iliyopita na walitunza utamaduni wa wavindaji-wakusanyaji hadi kufika kwa ukoloni.

Hakuna taarifa rasmi iwapo watu wa Asia walifika Australia lakini tangu karne ya 17 Baada ya Kristo, Waholanzi walifika wakafuatia Waingereza kwa kutumia majahazi.
Australia ikawa mahali pa koloni la Kiingereza na wafungwa kutoka Uingereza walioletwa hapa katika karne ya 19. Baadaye walifika pia walowezi huru.

Idadi ya Waustralia asilia imepungua sana kutokana na magonjwa mapya wakiambukizwa na Wazungu pia kutokana na ukandamizaji na kufukuzwa kutoka sehemu kubwa ya nchi yao.

Australia ilipata uhuru wake mwaka 1901 lakini imeendelea kumkubali Malkia wa Uingereza kama Mkuu wa Dola akiwakilishwa na Gavana Mkuu.

Tangu kuundwa kwa Shirikisho, Australia imeendeleza mfumo thabiti wa demokrasia ya kisiasa ikiwamo utawala wa Kifalme.

Mamlaka za kiserikali ziko mikononi mwa Waziri Mkuu.

Muundo wa utawala ni ya shirikisho. Kuna majimbo sita ya kujitawala pamoja na maeneo ambayo moja kwa moja yako chini ya Serikali ya Shirikisho.


Comments

Popular posts from this blog

UNAMKUMBUKA AMINA CHIFUPA WA MPAKANJIAA.

KADA MGEJA AHUDHURIA MAZIKO YA MAMA MZAZI WA MWANDISHI MWANDAMIZI WA HABARI KAHAMA