WABUNGE WAHAKIKISHIWA HUDUMA BORA YA BIMA YA AFYA

Waziri wa Afya  Mohammed Mchengerwa, akisoma hotuba yake katika semina aliyoawaandalia wabunge iliyokuwa ikizungumzia huduma ya Bima ya Afya, warsha hiyo ilifanyika katika ukumbi wa Msekwa jijini Dodoma leo. Waziri Mchengerwa, aliwahakikishia wabunge wananchi kuanza kupatiwa huduma bora za matibabu tena kwa bei rahisi, ambapo kaya moja yenye familia ya watu 6 itatibiwa kwa ghalama ya Sh laki1.5 tu.  Aidha Katibu Mlkuu wa Wizara hiyo Gracy Magembe, aliwaambia wabunge Bima ya afya imelejea upya hakutakuwa na janjajanja  ya utoaji wa huduma za matibabu kwa wananchi huduma zitafanyika kidijitali aliwaambia wabunge sasa ni kazi yao kwenda kuwahakikishia wapiga kura wao kwamba matibabu ya uhakika yatatolewa waondoe wasiwasi. Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Dkt. Irene Isaka, aliwahakikishia wabunge kwamba matatizo ya nyuma yaliyokuwa yakifanyika yameshafanyiwa marekebisho makubwa  mfuko huo umejipanga kufanya kazi kisasa ili kuwaondolea kero wananchi, hawataki kumwangusha Rais Dkt Samia Suluhu Hassan juhudi zake alizoziweka kwa mfuko huo uweze kuwaondolea kero wananchi.

HOTUBA YA MHESHIMIWA MOHAMED O. MCHENGERWA, WAZIRI WA AFYA KATIKA SEMINA YA WAH. WABUNGE TAREHE 05 NOVEMBA, 2026

  • Mhe. Dkt. Florence George Samizi (Mb.), Naibu Waziri wa Afya;
  • Waheshimiwa Wabunge;

·       Wakurugenzi na Wakurugenzi Wasaidizi wa Wizara  Idara  na Taasisi za Serikali.

Nawasalimu kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania!

Waheshimiwa Wabunge,

Awali ya yote napenda kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kutujalia afya njema na kutuongoza vema katika kipindi chote cha Mkutano wa Tano wa Bunge la 13. Napenda pia kumshukuru Mhe. Mussa Azzan Zungu, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutupa nafasi kila wakati tunapoomba kushirikisha Bunge jitihada mbalimbali za maendeleo zinazotekelezwa katika sekta ya afya.

Waheshimiwa Wabunge,

Vilevile, naomba niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa utayari wenu wa kuitikia wito wa Wizara ninayoiongoza na hakika tunakiri kupata ushirikiano uliotukuka kutoka kwenu. Naomba mniruhusu kwa namna ya pekee nitambue Wenyeviti wa Kamati na Waheshimiwa Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti.  Hakika ushauri, maoni na maelekezo yao yamekuwa chachu katika utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.

Waheshimiwa Wabunge,

Dhumuni la Semina ya leo ni kujenga uelewa wa pamoja kuhusu awamu ya pili ya utekelezaji wa mpango wa bima ya afya kwa wote. Awamu hii imeanza kutekelezwa tarehe 22 Okotoba, 2026 ikihusisha wananchi wenye uwezo wa kulipia sambamba na Serikali kuendelea kugharamia bima ya afya kwa wananchi wasio na uwezo.

Waheshimiwa Wabunge,

Kabla ya kuwasilisha kwenu mwelekeo wa utekelezaji wa awamu ya pili, naomba nitoe taarifa ya utekelezaji wa awamu ya kwanza iliyohusisha uhakiki na ugharamiaji wa bima ya afya kwa wananchi wasio na uwezo pekee.

AWAMU YA KWANZA YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA BIMA YA AFYA KWA WOTE

Waheshimiwa Wabunge,

Katika awamu hiyo, jumla ya kaya 201,376 kati ya kaya 276,004 zisizo na uwezo zilihakikiwa na kupewa kadi za bima ya afya sawa na asilimia 73 ya lengo. Sambamba na kaya zisizo na uwezo, Serikali imehakiki na kugharamia bima ya afya kwa wazee na watoto wanaoishi katika makazi na makao maalum.

Waheshimiwa Wabunge,

Utekelezaji wa awamu ya kwanza umetupa uzoefu kuwa ushirikiano na umiliki wa ajenda kwa viongozi wa ngazi zote unaleta ufanisi katika kufikia malengo tarajiwa. Niendelee kutoa wito kwenu kuhamasisha wananchi ikiwemo wanaogharamiwa bima ya afya na Serikali kujitokeza ili waweze kuhakikiwa. Wananchi wafahamu kuwa kadi ya bima ya afya ina thamani kubwa kwa maisha yao. Hivyo, wajitokeze kuchukua kadi wanapoitwa na viongozi kwa kuwa afya njema ndiyo msingi wa kufanya kazi, kupata kipato na kutunza familia.

Waheshimiwa Wabunge,

Katika awamu ya kwanza ya utekelezaji, Bunge limeendelea kuidhinisha vyanzo vya mapato kwa ajili ya Mfuko wa Usawa wenye jukumu la kugharamia bima ya afya kwa wananchi wasio na uwezo. Kutokana na hatua hiyo, kwa mwaka wa fedha 2026/27 Serikali inatarajia kukusanya kiasi cha Shilingi bilioni 261.3 na kwa kipindi cha robo ya kwanza kuishia Septemba, 2026 shilingi bilioni 59.4 sawa na asilimia 22.8 kimeingia kwenye Mfuko. Aidha, Serikali imeshapewa idhini ya kutumia shilingi bilioni 164.5 kati ya Shilingi bilioni 192.8 zilizoingia kwenye Mfuko wa Usawa.

Waheshimiwa Wabunge,

Sambamba na usajili wa kaya zisizo na uwezo na jitihada za kuongeza rasilimali fedha katika Mfuko wa Usawa, Serikali imeendelea kutambua kaya mpya zisizo na uwezo. Itakumbukwa kuwa kwa kuanzia tulianza na kaya ambazo tayari zilikuwa kwenye kanzidata ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF). Moja ya uzoefu tulioupata wakati wa utekelezaji wa awamu ya kwanza ni uwepo wa kaya zinazostahili ambazo bado hazijatambuliwa.

Waheshimiwa Wabunge,

Kwa muktadha huo, TASAF imetambua kaya mpya 818,954 na matarajio ya mwaka 2026/27 ni kuongeza utambuzi wa kaya mpya 575,000. Katika kikao na Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa kilichofanyika tarehe 12 Oktoba, 2026 juu ya ajenda  hii ya utekelezaji wa awamu ya pili ya bima ya afya kwa wote niliwasihi kushirikiana na TASAF na mamlaka za vijiji na mitaa kuhakiki kaya kwa vigezo vilivyoidhinishwa. Hii itasaidia kuhakikisha hakuna kaya stahiki itakayoachwa kwa sababu haina mtu wa kuisemea, piahakuna kaya isiyostahili itakayoingizwa kwa sababu ina mtu wa kuipigia simu.

Vigezo vijulikane. Matokeo ya uhakiki yawekwe wazi kwa utaratibu unaolinda faragha na utu wa wahusika. Kaya iliyoachwa kimakosa ijue pa kuwasilisha malalamiko na ipate jibu. Sisi kama viongozi wa kisiasa katika maeneo yetu tutambue kuwa mwananchi anayechangia kwa jasho lake anaweza kuelewa kwa nini Serikali inamsaidia jirani asiyejiweza. Atapoteza imani akiona msaada huo umechukuliwa na mwenye uwezo kupitia mlango wa kujuana.

Waheshimiwa Wabunge,

Matunda ya utekelezaji wa awamu ya kwanza tayari yanaonekana! Idadi ya wananchi wasio na uwezo wanaogharamiwa bima ya afya inaendelea kuongezeka,  Idadi ya kaya mpya zisizo na uwezo zinatambuliwa, Wananchi waliochukua kadi zao za bima wameanza kunufaika kwa kupata matibabu wanapougua. Haya ndiyo matunda ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Serikali inayosema na kutenda! Na kazi haijaishia hapo, tunaendelea kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa na kunufaika na Bima ya Afya kwa Wote.

AWAMU YA PILI YA UTEKELEZAJI

Waheshimiwa Wabunge,

Kama nilivyosema katika utangulizi wa hotuba yangu kuwa Awamu ya Pili inahusisha wananchi wenye uwezo wa kujilipia wenyewe na wananchi wasio na uwezo ambao Serikali itaendelea kugharamia bima za afya kwa kundi hilo. Katika awamu hii tunaenda kuongeza wigo wa wananchi kujiunga na bima ya afya huku tukiwahakikishia kupata huduma bora za afya katika vituo vya kutolea huduma.

Waheshimiwa Wabunge,

Hatua hii ni ya kimageuzi na inayohitaji kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu na manufaa ya kuwa na bima ya afya, pamoja na kuwahamasisha kujiunga na mpango huu. Nilipokuwa mkoani Mtwara kule kwa watani zangu niliwapa mfano maana niliona kwa mifano watani watanielewa haraka zaidi nikawaambia Bima ya Afya ni kama kisima cha kijiji. Kila mmoja anachota maji yake, lakini kisima kinachimbwa na wote. Siku ya kiangazi, hakuna anayeulizwa "ulichimba kiasi gani?" Anapewa maji kwa sababu ni mwanakijiji. Ndivyo bima inavyofanya kazi: tunaweka kidogo kidogo tukiwa wazima, ili siku tukiugua, tunapata matibabu bila kulazimika kuuza chochote.

Waheshimiwa Wabunge,

Wananchi waeleweshwe kuwa Bima ya Afya kwa Wote haimaanishi kwamba kila mwananchi atapata bima bure. Hapana! Kisima hakichimbwi na mtu mmoja. Mwananchi mwenye uwezo atachangia bima yake na ya familia yake, kulingana na utaratibu uliowekwa. Lakini kwa wananchi ambao kweli hawana uwezo wa kujilipia, Serikali imeweka utaratibu wa kuwatambua kupitia mamlaka zinazohusika — kwa kushirikisha jamii yenyewe — na  Mfuko wa Maendeleo ya Jamii, TASAF.

Kwa hiyo: mwenye uwezo atachangia, na asiye na uwezo atasaidiwa na Serikali. Hakuna Mtanzania atakayebaki nje ya kisima hiki kwa sababu hana ndoo.

Waheshimiwa Wabunge,

Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alitambua maadui wakuu watatu wa maendeleo ya Taifa letu kuwa ni ujinga, maradhi na umaskini. Katika kuendeleza mapambano dhidi ya adui maradhi, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na malengo mahsusi, yanayopimika na yenye muda maalumu wa kuyafikia ili kuwezesha tathmini ya hatua zilizofikiwa na kuchukua hatua stahiki pale inapohitajika.

Waheshimiwa Wabunge,

Kwa kuzingatia msingi huo, Serikali imeweka lengo la kuongeza idadi ya wananchi wanaonufaika na bima ya afya kufikia milioni 25 ifikapo Juni, 2027. Lengo hili ni kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanakuwa na uhakika wa kupata huduma za afya bila kukabiliwa na mzigo mkubwa wa gharama za matibabu.

Waheshimiwa Wabunge,

Serikali kwa kushirikiana nanyi Waheshimiwa Wabunge tuna imani kuwa malengo ya kusajili wanufaika milioni 25 tutayafikia na kutimiza ahadi aliyoitoa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wananchi. Kwa kuwa Wakati wengine walisema haiwezekani, alisema "itawezekana." Wakati wengine walisema bajeti haitoshi, alisema "tutaipanga." Wakati wengine walisema wananchi hawataelewa, alisema "wananchi wa Tanzania ni waerevu — wanaelewa thamani ya afya kuliko mtu yeyote."

Waheshimiwa Wabunge,

Kwa hakika, ajenda ya Bima ya Afya kwa Wote haiwezi kufanikiwa kwa juhudi za Wizara ya Afya pekee, bali inahitaji ushirikiano na uwajibikaji wa ngazi zote za Serikali na wadau wote muhimu.

Waheshimiwa Wabunge,

Tunao wajibu kama viongozi ambao tuko karibu zaidi na wananchi kuhakikisha tunatoa ujumbe mmoja, sahihi na unaoeleweka. Katika mpango huu wa Bima ya Afya kwa Wote, wananchi wafahamu kuwa wanaweza kupata bima kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) au kampuni binafsi za bima ya afya zilizoidhinishwa na Serikali. Serikali imeweka utaratibu wa kuhakikisha kuna vifurushi vya bima vinavyozingatia mahitaji na uwezo wa wananchi kuchangia.

Waheshimiwa Wabunge,

Katika mpango huu, Serikali imewafikia wananchi wenye kipato cha kawaida! Tumeweka kifurushi cha bima ya afya kinachoitwa FAHARI AFYA, ambacho kina huduma muhimu za afya kwa gharama ya shilingi laki moja na nusu kwa kaya ya watu wasiozidi sita. Ukijiunga na Fahari Afya unapata huduma za afya kuanzia zahanati hadi hospitali ya Taifa, kwa kufuata utaratibu wa rufaa. Kabla ya kujiunga na bima, mwananchi asisitizwe kuelewe huduma atakazopata, maana ni haki yao kujua bima waliojiunga inawapatia nini!

 

UIMARISHAJI WA MIFUMO YA TEHAMA

Waheshimiwa Wabunge,

Bima ya Afya kwa Wote inahitaji mifumo inayomwezesha mwananchi kutambuliwa, kuhudumiwa na kupata haki yake bila kuzungushwa. Hatuwekezi katika teknolojia ili tuwe na kompyuta nyingi; tunawekeza ili mwananchi apate huduma bora, kwa wakati na bila usumbufu.

Katika kikao chake cha Januari 2026, Baraza la Mawaziri liliridhia Mkakati wa Mageuzi ya Kidijitali katika Sekta ya Afya. Hivyo, tunachotekeleza sasa ni uamuzi wa Serikali wenye mwelekeo mmoja wa kitaifa. Wajibu wetu ni kuugeuza uamuzi huo kuwa maboresho yanayoonekana katika huduma za kila siku.

Tayari mzabuni amepatikana kwa ajili ya kupanua matumizi ya mfumo wa AFYAEMS hadi katika hospitali 184 za wilaya. Mfumo wa GoTHOMIS utaendelea kutumika katika vituo vyote vilivyo chini ya ngazi ya hospitali za wilaya, ikiwemo vituo vya afya na zahanati.

Mgawanyo huu unaweka wazi mfumo utakaotumika katika kila ngazi. Hata hivyo, haupaswi kutengeneza mipaka ya taarifa. Mgonjwa anapohama kutoka ngazi moja ya huduma kwenda nyingine, taarifa zinazohitajika kumhudumia ziweze kufuatana naye kwa usalama. Ndiyo maana uunganishaji wa AFYAEMS, GoTHOMIS nisehemu ya kazi ya mkandarasi.

Tayari tuna msingi wa kujengea. GoTHOMIS inawezesha usajili wa wagonjwa, uhakiki wa bima na uwasilishaji wa madai kwa njia ya kielektroniki. Kazi iliyo mbele yetu ni kuhakikisha uwezo huu unatumiwa ipasavyo na mifumo inabadilishana taarifa kwa ufanisi.

Waheshimiwa Wabunge,

Wito wetu kama Sekta ya Afya nikuwaomba muendelee kuwa wasimamizi katika maeneo yenu ya utawala kwa kuhamasisha utayari wa vituo vya kutolea huduma za afya. Utayari katika uboreshaji wa miundombinu, upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, watumishi wa afya na mifumo ya TEHAMA.

 

UWEPO WA MSIMAMIZI WA BIMA YA AFYA KWA WOTE

Waheshimiwa Wabunge,

Utekelezaji wa mpango wa bima ya afya kwa wote inashirikisha Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali. Hata hivyo, baadhi ya Wizara au Taasisi zimepewa majukumu mahsusi na Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote Sura 161. Kwa umuhimu wake nitambue Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), ambaye kazi yake ni kuhakikisha kampuni za bima, vituo vya kutolea huduma za afya na wanachama wanafuata sheria na kutendewa haki. Kwa lugha rahisi, TIRA ni kama refa wa mpira! Anahakikisha kila upande unafuata sheria za mchezo na hakuna anayemwonea mwenzake. Hivi ndivyo Serikali ilivyojipanga kuhakikisha Bima ya Afya kwa Wote inawanufaisha wananchi!.

Waheshimiwa Wabunge,

TIRA imeendelea kusogeza huduma za usimamizi karibu na wananchi kwa kuanzisha ofisi za Kanda katika Kanda 10 na kwa kushirikiana na OWM-TAMISEMI katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwa na wataalam watakaojengewa uwezo wa majukumu yanayotekelezwa na TIRA na hivyo kuwa Waratibu wa TIRA katika ngazi ya Halmashauri ili mwananchi mwenye malalamiko au changamoto kuhusu huduma za bima ya afya anaweza kuwasiliana moja kwa moja na kupatiwa ufumbuzi.

 

KUZUIA VITENDO VYA UDANGANYIFU

Waheshimiwa Wabunge,

Uendelevu wa mpango wa bima ya afya unategemea uaminifu utakaojengwa miongoni mwa wadau wa mfumo huu wa bima ya afya. Bima ya Afya kwa Wote ni mali yetu sote, hivyo kila mmoja wetu ana wajibu wa kuulinda mpango huu ili utunufaishe sisi, watoto wetu na hata wajukuu zetu.Tusikubali kuuharibu mpango huu kwa udanganyifu!

Niwaombe tuwaelimishe wananchi wasitumie kadi ya bima ya mtu mwingine, wala kutoa taarifa za uongo ili kupata huduma wasizostahili. Udanganyifu wa mtu mmoja unaweza kuathiri manufaa ya wengi. Niwaombe tuwe walinzi wa mpango huu, kwa sababu tunachokijenga leo ni kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

HITIMISHO

Waheshimiwa Wabunge,

Kwa heshima kubwa nawashukuru sana kwa kunisikiliza na kuendelea kusisitiza katika kuhakikisha hakuna mdau anayeachwa nyuma katika Awamu ya Pili ya utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ili Taifa letu liweze kuwa miongoni mwa mataifa yaliyofikia malengo ya Huduma za Afya kwa Wote.

Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania.

 

Asanteni sana kwa kunisikiliza

 














Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Gracy Magembe





 

Comments

Popular posts from this blog

AJIRA MPYA 41,500 SERIKALINI ZATANGAZWA KATIBU MKUU UTUMISHI JUMA MKOMI

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?

WALIOPITA KURA ZA MAONI CCM HAWA HAPA