USALAMA KWA NCHI ZA AFRIKA NI MUHIMU WAZIRI DKT. NYANSAHO



Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Rhimo Nyansaho (Mb), tarehe 11 Novemba 2026, jijini Arusha, amesisitiza dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuendeleza misingi ya Umoja wa Afrika, usalama wa pamoja na ushirikiano wa kikanda. Ameyasema hayo wakati akifunga rasmi Mkutano wa 20 wa Makamanda wa Vyuo vya Ukamanda na Mafunzo ya Kijeshi barani Afrika (African Conference of Commandants ( ACoC).
Katika hotuba yake, Mheshimiwa Dkt. Nyansaho aliwasilisha salamu za pongezi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa washiriki wote wa mkutano huo. 
Aidha, aliwapongeza makamanda na wajumbe kwa ushiriki wao na michango yenye tija katika kuimarisha elimu ya kijeshi na kukuza ushirikiano baina ya taasisi za kijeshi barani Afrika. Alisisitiza kuwa elimu na mafunzo ya kitaaluma ya kijeshi yana nafasi muhimu katika kuandaa viongozi wenye maarifa, maono na uwezo wa kukabiliana na changamoto za kiusalama zinazozikabili nchi za Afrika, zikiwemo ugaidi, uhalifu wa kupangwa unaovuka mipaka ya nchi na vitisho vya kimtandao. Aidha, alihimiza kuimarishwa kwa ushirikiano baina ya vyuo vya kijeshi kupitia mafunzo ya pamoja, kubadilishana wanafunzi na wakufunzi pamoja na kuoanisha mitaala ya mafunzo ya kijeshi, hususan katika maeneo ya Operesheni za Kusaidia Amani, Sheria za Kimataifa za Kibinadamu na Ulinzi wa Raia.
Mkutano huo uliwakutanisha viongozi waandamizi wa kijeshi na wajumbe kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, akiwemo Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Salumu Haji Othman, Mkuu wa Chuo cha Ukamanda na Unadhimu Tanzania na Mwenyekiti wa Mkutano wa Makamanda wa Vyuo vya Kijeshi vya Afrika (ACoC), Meja Jenerali Stephen Justice Mnkande, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Rajabu Mabele, wawakilishi wa Umoja wa Afrika, makamanda wa vyuo vya kijeshi, wakufunzi wakuu na maafisa waandamizi wa kijeshi.
Mkutano huo umekuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu, maarifa na mbinu bora za mafunzo ya kijeshi, kwa lengo la kuimarisha uwezo wa pamoja wa majeshi ya Afrika na kuendeleza ushirikiano katika kukabiliana na changamoto za kiusalama, hivyo kuchangia juhudi za kudumisha amani, usalama na utulivu wa kudumu barani Afrika.


Waziri Dkt. Nyansaho, akiwa mkatika picha ya pamoja na washiriki wa mkutano huo







 

Comments

Popular posts from this blog

AJIRA MPYA 41,500 SERIKALINI ZATANGAZWA KATIBU MKUU UTUMISHI JUMA MKOMI

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?

WALIOPITA KURA ZA MAONI CCM HAWA HAPA