ASHA BARAKA KIELELEZO CHA MWANAMKE WA SHOKA KATIKA MUZIKI WA DANS TANZANIA MIAKA 30 BADO NYOTA INAWAKA
Kwa Asha Baraka hakuna adui wa kudumu na ndiyo maana inapotokea msanii wa Twanga Pepeta anahama bendi, bado ataambiwa mlango wa kurejea uko wazi hata kama aliondoka kwa kuchafua hali ya hewa.
Asilimia kubwa ya wasanii nyota wa Twanga Pepeta waliohama bendi, walirejea kundini.
Sina haja ya kutaja majina ya watu, lakini haihitaji taasisi ya utafiti kubaini kuwa wasanii wengi walioweka alama kubwa Twanga Pepeta, walipojaribu kuhama, walirejea.
Jumamosi hii Asha Baraka anakwenda kufanya tukio kubwa la kiburudani pale Brake Point Makumbusho jijini Dar es Salaam.
Ni miaka 30 ya Asha Baraka kwenye utumishi wa muziki wa dansi, waimbaji nyota waliowahi kupita kwenye mikono yake kama Nyoshi el Saadat, Ally Chocky, Mwinjuma Muumini na Kalala Jr ambao wote hao kwasasa wanamiliki bendi zao, watasindikiza tukio hilo.
Inawezekana Asha Baraka kama binaadamu yeyote yule, ana madhaifu yake, lakini inawezekana pia ana mazuri mengi na anajua namna ya kutengeneza undugu na watu waliomzunguka, kuanzia wasanii hadi wadau wa muziki.
Asha Baraka wakati mwingine hajali ukorofi, usumbufu wala utukutu wa msanii, yeye anaheshimu kipaji cha mtu huku akiamini mengine yatarekebishika.
Anajua ubora na udhaifu wao na anatambua namna ya kuishi na kila mmoja na ndiyo maana leo wasanii wake wa zamani wamekubali kwenda kumuunga mkono kwenye jambo lake.
Onyesho hili la miaka 30 ya Asha Baraka kwenye 'game' linasubiriwa kwa hamu kubwa hasa kutokana na ukweli kuwa mwanamama huyu hajawahi kuwa na jambo dogo pale anapoandaa matamasha mbali mbali.
Lakini napenda kumpa tahadhari Asha Baraka na timu yote inayohusika na maandalizi ya onyesho hili. Idadi ya watumbuizaji nyota ni kubwa hivyo umakini wa hali ya juu unahitajika.
Mbali na Chocky, Nyoshi, Muumini na Kalala Junior, kwenye onyesho hilo wapo pia TID, Dully Sykes na Mr Nice, achilia mbali Twanga Pepeta na Twanga Digital.
Kama jukwaa litakuwa sehemu ya baraza la gumzo kwa Ma MC na kamati ya maandalizi, kama muda wa kila tukio hautazingatiwa, basi onyesho hili linaweza kugeuka kuwa kero.
Na ndio maana namtaka Asha Baraka akailinde heshima aliyojiwekea kwenye ubora wa kuandaa maonyesho makubwa.
Asha Baraka hajawahi kufanya tukio hili hapo kabla, hajafanya ilipotimu miaka kumi wala ishirini, hivyo tukio hili linachukuliwa kama la kipekee na linastahili kutendewa haki katika kila idara kuanzia ratiba, utunzaji wa muda, 'sound' na muonekano wa ukumbi (mapambo).
Yote kwa yote, kwa wale wadau kindakindaki wa muziki wa dansi, watakuwa watu wa ajabu sana kama watalikosa onyesho hili bila sababu zisizozuilika.
Ili ujuwe kwamba mwanamama huyu kiboka Twanga Pepeta ilianzia na kiingilio kinywaji chako tu pale Mango Garden na Leaders Clab Kinondoni jiji la Dar es salaam, hadi leo hii kufikia kiingilio cha maelfu ya shilingi, wengi waliopambana naye katika muziki wengine tumewasahahu hongera

Comments
Post a Comment