WAZIRI MHAGAMA AZINDUA MIFUMO NA VIFURUSHI VYA MFUKO WA BIMA YA AFYA KWA WOTE

Waziri wa Afya  Jenista Mhagama (kulia na Mkurugenzi wa Mfuko huo Dr. Irene Charles Isaka, wakifunua kitambaa kuashiria uzinduzi  huo uliofanyika jijini Dodoma leo
Wakiwa wameshikilia watoto baada ya kuzindua




HOTUBA YA MHE. JENISTA MHAGAMA (MB), WAZIRI WA AFYA
SIKU YA UZINDUZI WA MIFUMO YA NHIF YA USAJILI, UCHAKATAJI MADAI
NA TOTO AFYA KADI KATIKA UKUMBI WA TAKWIMU JIJINI DODOMA
TAREHE 17 DISEMBA 2024
● Katibu Mkuu -Wizara ya Afya, Dkt. John Jingu,
● Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Afya/Ukimwi
● Mganga Mkuu wa Serikali
● Mkurugenzi Mkuu-NHIF, Dkt. Irene Isaka,
● Viongozi kutoka Wizara ya Afya na Taasisi mbalimbali zilizoalikwa,
● Wadau wa Maendeleo(GIZ, KFW, KoICA,TCDC pamoja na NHIS Korea
● Menejimenti na Watumishi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya,
● Ndugu Waandishi wa Habari,
● Wageni Waalikwa
● Mabibi na Mabwana.
Nawasalimia kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.........
Awali ya yote nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha
kukutana hapa tukiwa na afya njema katika tukio hili muhimu.
Leo ni siku ya furaha kubwa sana kwangu binafsi, Wizara, Sekta ya Afya na
Umma wa Watanzania kwa ujumla, kwa sababu ya tukio hili muhimu la uzinduzi
wa Mifumo ya NHIF ambayo inakwenda kuleta mapinduzi makubwa katika
utoaji wa huduma kwa wanachama wake na wadau wake muhimu kama
Watoa Huduma. Hili ni tukio kubwa na la muhimu sana kwetu.
● Bima ya Afya kwa wote
Ndugu Washiriki,
1
Mtakumbuka Sheria ya Bima ya Afya kwa wote tayari ilishatangazwa kuanza
kutumika kupitia tangazo la Serikali Na. 700A la mwaka 2024 na kanuni zake
zimetangazwa kutumika kupitia tangazo la Serikali 809 la mwaka 2024 hivyo
Mifumo itawezesha Watanzania kupata taarifa muhimu kwa wakati na kuweza
kujihudumia kwa kujiunga kiurahisi.
Wageni Waalikwa
Suala la Bima ya Afya kwa Wote ni kipaumbele kwa Serikali yetu ya Awamu ya
Sita inayoongozwa na Mama yetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, sote
tutakumbuka tangu anaingia madarakani lilikuwa ni agizo lake kuhakikisha hili
linatekelezeka hivyo kwa upande wake amemaliza na sisi ndio tuna deni la
kuhakikisha mazingira yote yako sawa kwa wananchi kujiunga na kupata
huduma bora.
Serikali imehakikisha imeweka miundombinu imara katika maeneo yote ya
wananchi kwa kujenga Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali ngazi ya Wilaya,
Mkoa, Kanda hadi Taifa. Hivi sasa tuna takriban vituo 10,004 nchi nzima. Kati ya
vituo hivyo vituo 7,181ni vya serikali, vituo 1,975 ni vituo binafsi na 848 ni vituo
vinavyosimamiw na Taasisi za kidini. Serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa
Vifaa tiba na dawa kuwawezesha wananch kunufaika na huduma hizo ambazo
Serikali yao imewekeza. Nafurahi kuwajulisha kwamba Serikali ya awamu ya Sita
imekuja na suluhisho muhimu yaani BIMA YA AFYA KWA WOTE. Hii ni
kumwezesha mwananchi kupata huduma za afya bila kutetereka kutokana na
gharama za matibabu.
Tutambue kuwa tuna kazi kubwa kulingana na takwimu zilizopo za wananchi
walioko ndani ya mfumo wa bima ni asilimia 15 tu, ambapo NHIF inahudumia
asilimia nane (8) tu ya Watanzania hivyo unaweza kuona kuwa zaidi ya asilimia
2
85 ya watanzania wako nje ya Mfumo wa bima. Nitoe rai hapa kuwa kila mmoja
aliyeko hapa aone anawajibika moja kwa moja kuhakikisha anahamasisha na
kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa bima ya afya.
Kwa Watoa huduma sasa tambueni kuwa suala la kutoa huduma bora kwa
wananchi kupitia bima ya afya ni la lazima na sio hiari. Bima ya afya kwa wote ni
utekelezaji wa Sheria Na 13 ya mwaka 2023. Hivyo hakikisheni mnaweka
mazingira rafiki na yanayowavutia wananchi kuona umuhimu wa kuwa na bima
ya afya.
● Upatikanaji wa Huduma
Tunatambua kuwa upatikanaji wa huduma bora za matibabu hasa kwa
mwananchi wa kawaida pamoja na upatikanaji wa huduma ya dawa kwa sasa
umeongezeka sana kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali yetu
hususan kuongeza fedha katika eneo hilo. Pamoja na mafanikio haya, Wizara
imeendelea kusimamia na kudhibiti mianya yote ya upotevu wa dawa ili
kuhakikisha wananchi na wanachama wa Mfuko huu wanapata huduma bora
wanapokuwa katika vituo vya kutolea huduma.
Wakati Wizara ikichukua hatua hizi, naiagiza NHIF kuangalia namna Mfuko
unavyoweza kuendeleza ushiriki wake katika suala zima la uboreshaji wa
huduma katika vituo vya kutolea huduma kutokana na fursa zilizopo. Natambua
Mfuko umekuwa ukitoa mikopo nafuu kwa hospitali za Serikali, Taasisi za Dini na
Hospitali binafsi. Mikopo kwa ajili ya vifaa tiba ( 74.2%), Ukarabati vituo vya afya
21.4%) na dawa (4.3%).
3
Nina uhakika kuwa ushiriki wa NHIF katika kuwekeza kwenye uboreshaji wa
miundombinu ya vituo vya matibabu na upatikanaji wa vifaa tiba na dawa
utaendelea kuimarisha sana upatikanaji wa huduma na utapunguza malalamiko
kwa wanachama wake na wananchi kwa ujumla. Wizara yangu iko tayari
kuwashika mkono pale mtakapoona mnakwama ili kuhakikisha Mfuko huu
unatimiza malengo yake na wakati huo huo unabaki kuwa endelevu.
Aidha pongezi hizi pia nazitoa kwa Mkurugenzi Mkuu Dkt. Irene Isaka ambaye
amekabidhiwa taasisi hii nyeti kuiongoza hasa katika wakati huu ambao kama
nchi yetu inatekeleza magauzi makubwa katika sekta ya Bima ya Afya kwa wote,
Hongera sana.
● Uzinduzi wa Mifumo
Tukio la leo ambalo limetukutanisha hapa ni uzinduzi wa Mifumo ambayo
inaanza kutumika katika kuwahudumia wananchi moja kwa moja bila kulazimika
kufika katika Ofisi za NHIF, jambo hili ni kubwa na niwapongeze sana. Kama
mnavyokumbuka hili lilikuwa ni agizo la Mhe. Rais wetu Dkt. Samia Suluhu
Hassan ambaye aliagiza Mifumo yote ya Serikali sasa ianze kusomana na agizo
hili lilikuwa hadi Desemba mwaka huu, hivyo kwa Taasisi yetu NHIF mmefanya
vizuri kulifanyia kazi na kuhakikisha mifumo yenu sasa inasomana na Taasisi
zingine lakini imezingatia mahitaji ya kuwahudumia wananchi.
Ndugu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi,
Kama alivyodokeza Mkurugenzi Mkuu kwenye taarifa yake kuwa, Mifumo
ninayozindua leo ni pamoja na Mfumo wa Usajili wa Wanachama ambao
unamwezesha mwananchi kujihudumia popote alipo kwa njia ya mtandao.
4
Mwanachama ataweza kuona taarifa zake na kuhuisha pale anapohitaji. Mfumo
mwingine ni wa uwasilishaji madai na uchakataji madai hayo. Nimejulishwa
kwamba kwa upande wa uwasilishaji wa madai, tayari asilimia 80 ya vituo
vimeshaunganishwa. Hivyo kurahisha uchakataji wa madai, kudhibiti
udanganyifu na kulipa mapema watoa Huduma.
Nipongeze sana hatua hii kutokana na ukweli kuwa, hapo awali NHIF ilikuwa ni
Taasisi ambayo imegubikwa na changamoto nyingi zikiwemo za ucheleweshaji
huduma kwa wanachama, kuchelewesha malipo kwa watoa huduma pamoja na
udanganyifu. Mifumo hii inakwenda kusaidia kuondoa changamoto hizi na
hatimaye kutoa huduma zenye ubora unaotakiwa.
Waheshimiwa wageni Waalikwa
Sasa naomba niseme kidogo kuhusu hili la Mpango wa Toto Afya Kadi. Mpango
huu ulisaidia sana familia za wananchi hasa zile zilizokuwa na changamoto za
kiafya. Mpango huu pamoja na uzuri wake ulileta hasara kwa kuwa kwa kila
shilingi 100 mtoto alitumia takriban shilingi 600. Natambua NHIF imekuja na
mpango wa kusajili makundi ya watoto na hivyo kupunguza athari. Nimejulishwa
pia kwamba leo nitazindua mpango wa usajili wa mtoto mmoja mmoja iwapo
itatokea kwamba mtoto hayupo shule. kwa dhati kabisa niwapongeze kwa
kuwa wasikivu na kufanyia kazi maoni kutoka kwa wananchi na wadau
wengine ambapo mmefanyia kazi na leo tunazindua utaratibu wa
kumwezesha mtoto kujiunga kwa makundi au mmoja mmoja.
Sasa nitumie fursa hii kuwaomba wananchi kuwasajili watoto wao ili waweze
kuhudumiwa kwa utaratibu wa bima ya afya lakini pia kuhakikisha mnakuwa
walinzi wa hizi huduma ili Mfuko usiibiwe kupitia huduma za watoto
5
watakaojiunga kwani kwa kufanya hivyo mtakuwa sehemu ya kulinda uhai wa
Mfuko.
Wageni waalikwa mabibi na mabwana
Moja ya wadau wakubwa wa Mfuko huu ni Watoa huduma ambao wanahudumia
wanachama wenu na mnawalipa kwa huduma hizo. Kama alivyosema
Mkurugenzi Mkuu kuwa kwa sasa Mfuko umeweza kushughulika na changamoto
ya makato ya madai ya watoa huduma lakini pia Mfuko kwa sasa unalipa Madai
kwa wakati na ujio wa Mifumo hii sasa NHIF inakwenda kuondoa kabisa
malalamiko ya Watoa huduma.
Kutokana na hili, Wizara yangu inatarajia kuona Watoa huduma wakiwahudumia
wanachama kwa ubora na kuwapa taarifa sahihi wanazopaswa kupewa lakini pia
hakikisheni sasa mnawasilisha Madai sahihi ili muweze kulipwa madai ambayo ni
halali. Vitendo vya udanganyifu havivumiliki hata kidgo tutachukua hatua kali
dhidi ya vituo vitakavyojihusisha na udanganyifu au mwanachama yeyote.
Serikali inayo matarajio makubwa sana kwa Mfuko huu, niwaombe mjielekeze
katika maeneo yafuatayo:-
a. Pamoja na maboresho haya ya Mifumo yaliyofanyika na tunayokwenda
kuzindua muda mfupi ujao, endeleeni kubuni namna bora za kufanya
tathnimi na kuongeza wigo wa wanachama na huduma ili kuondoa
changamoto zinazolalamikiwa bila kuathiri uhai na uendelevu wa Mfuko.
b. Najua Mfuko uko katika hatua za kuja na vifurushi mbalimbali ili
kuwezesha wananchi kujiunga kupitia sheria ya bima ya afya kwa wote,
hakikisheni mnawashirikisha wadau muhimu ili kuweza kupata maoni
6
kutoka makundi yote ili kuwezesha kupata vifurushi vinatakavyosaidia
wanachi moja kwa moja.
c. Natambua Mfuko una Kituo cha Huduma kwa Wateja kwa njia ya simu bila
malipo kinochotoa huduma masaa 24 siku 7 za wiki. Hata hivyo,
hakikisheni mnaweka watumishi wenye ujuzi wa aina mbalimbali
wakiwemo Madaktari wauguzi na wafamasia ili kuweza kutatua
changamoto zinazowasilishwa kwa wakati.
d. Aidha, hakikisheni mnatoa taarifa kwa umma kwa wakati kwa maeneo
yanayohitaji ufafanuzi ili kuepusha wananchi kupata taarifa zisizo sahihi
kupitia vyanzo vingine.
e. Eneo jingine hakikisheni Menejimenti inatekeleza maelekezo mbalimbali
yanayotolewa na mamlaka za usimamizi ikiwemo Wizara yangu, Kamati za
Kudumu za Bunge, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali,
Benki Kuu ya Tanzania na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA).
f. Natambua Mfuko unafanya jitihada mbalimbali za kudhibiti vitendo vya
udanganyifu, nitumie nafasi hii kupongeza NHIF na kukemea tabia ya
baadhi ya watoa huduma kutumia Mfuko kujipatia mapato yasiyo halali na
kwa udanganyifu lakini pia Mfuko utuletee taarifa ya wanaobainika na
vitendo hivi.
Nilianza kwa kuwashukuru naomba nimalizie kwa kuwashukuru. Naishukuru pia
Menejimenti ya Mfuko kwa maandalizi mazuri ya shughuli hii. Baada ya kusema
7
hayo niko tayari sasa kwa ajili ya kuizindua rasmi Mifumo yetu ya Usajili wa
Wanachama na Uchakataji wa madai pamoja na kuzindua TOTO Afya!
Asanteni sana kwa kunisikiliza.





Wageni waliikwa wakimsikiliza Waziri Mhagama.

Baadhi ya watoto na baadhi ya wanafunzi walioalikwa katika uzinduzi huo












Baadhi ya wanahabari wakipiga picha baada ya kumalizika hafla hiyo

HOTUBA YA MKURUGENZI MKUU DKT. IRENE ISAKA KWENYE UZINDUZI
WA MIFUMO NA MPANGO WA TOTO AFYA KADI
DODOMA, TAREHE 17 DESEMBA, 2024

● Waziri wa Afya na Mgeni Rasmi, Mhe. Jenista Mhagama (Mb),
● Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge – Afya na Ukimwi
● Katibu Mkuu-Wizara ya Afya, Dkt. John Jingu,
● Viongozi kutoka Wizara ya Afya
● Viongozi wa Taasisi mbalimbali zilizoalikwa,
● Washirika na Wadau wa Maendeleo (baadhi tuna ushirikiano wa
muda mrefu)
GIZ – 2014 (CHF)- (kwa UHI 2023),
KfW- 2011 (Tumaini la Mama), (kwa UHI Juni, 2024),
PharmAccess – 2014 (kwa UHI April 2024),
NHIS-Korea - Septemba 2024,
Benjamin Mkapa Foundation - Januari 2024,
FSDT/TCDC - Septemba 2024 .
● Menejimenti na Watumishi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya,
● Ndugu Waandishi wa Habari,
● Wageni Waalikwa
● Mabibi na Mabwana.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
1
Mhe. Waziri na Wageni waalikwa,
Awali ya yote, naomba nimshukuru Mungu Mwenyezi, mwingi wa rehema kwa
kutupa afya njema na kutuwezesha sote kukutana kwa pamoja siku ya leo ambayo
ni muhimu sana kwetu kama NHIF katika utendaji au utoaji wa huduma zetu kwa
wadau.
Naomba nitoe shukrani za pekee kabisa kwako Mhe. Waziri wa Afya kwa kutenga
muda ndani ya ratiba yako ngumu kuja kuzindua Mifumo ya Mfuko wa Bima ya Afya
pamoja na Mpango wa Toto Afya Kadi ambao umekuwa ukisubiriwa kwa hamu
kubwa na wananchi kutokana na umuhimu wake kwa kundi la Watoto wenye umri
chini ya miaka 18.
Lengo la hafla hii,
Mhe. Waziri na Waalikwa wote,
Lengo la halfa hii ni kuzindua Mifumo miwili ambayo ni Mfumo wa Usajili wa
wanachama na Mfumo wa uchakaji wa Madai. Mbali na Mifumo, Mhe. Waziri pia
utatuzindua vifurushi vya ziada pamoja na Mpango wa Toto Afya Kadi ambao
unakwenda kurejesha utaratibu wa kumsajili mtoto mmoja mmoja.
● Utekelezaji wa Shughuli za Mfuko,
Kabla sijaongelea shughuli ya leo naomba kuongelea utendaji wa Mfuko
Mheshimiwa Mgeni rasmi
Mfuko umeendelea kuongeza Wigo wa Wanachama ili kuhakikisha wananchi wengi
wanapata huduma kupitia Mfumo wa bima ya afya na Wanufaika. kipindi cha Julai
2023 hadi Oktoba 2024, Mfuko ulifanikiwa kusajili wanachama wapya 839,331
sawa na asilimia 94 ya lengo. Idadi hiyo ya wanachama waliosajiliwa, imewezesha
Mfuko kuwa na wanachama wachangiaji 1,359,772 na wanufaika 5,106,957 sawa
na asilimia 8.4 ya Watanzania wote.
2
● Mapato ya Mfuko
Katika kipindi cha mwaka 2023/24 Mfuko ulikusanya mapato jumla ya shilingi
bilioni 756.48 ukilinganisha na shilingi bilioni 696.72 zilizokusanywa mwaka
2022/23. Hii ni sawa na asilimia 108.6 ya lengo.
Kwa upande wa michango ya wanachama, lengo ilikuwa kukusanya shilingi bilioni
668.03 ambapo uliweza kukusanya michango jumla ya shilingi bilioni 699.26
sawa na asilimia 105 ya lengo. Kutokana na jihada mbalimbali zikiwemo za
kubana matumizi, Mfuko kwa sasa umeongeza uhimilivu wake kutoka miezi 6 hadi
mwaka mmoja.
● Urari wa Mapato na Matumizi
Hadi kufikia tarehe 31 Oktoba, 2024 ya Mwaka wa Fedha 2024/25, Mfuko ulikuwa
umekusanya jumla ya shilingi bilioni 294.55 na jumla ya matumizi yalikuwa shilingi
billioni 217.43 sawa na ziada ya shilingi billioni 77.12
● Usajili wa Vituo vya kutolea huduma
Hadi kufikia mwezi Juni 2024, Mfuko ulikuwa umesajili jumla ya vituo vya
matibabu 10,004 nchini kote. Kati ya vituo hivi, vituo vya Serikali ni 7,181
(72%), vituo vya Mashirika ya Dini ni 848 (8%), na vituo vya watu binafsi
ni 1,975(20%).
● Udhibiti wa vitendo vya udanganyifu
Hadi Oktoba, 2024 Mfuko ulitekeleza kazi zilizolenga kudhibiti na kuibua vitendo vya
udanganyifu Mfuko ulibaini jumla ya shilingi bilioni 7.94 kinachotakiwa kurejeshwa
kilichotokana na madai yenye udanganyifu kutoka kwa watoa huduma. Mfuko
umeokoa Zaidi ya shilingi billion 18 kupitia uhakiki kwenye vituo vya kutolea
3
Huduma. Jumla ya Kadi za wanachama 12,685 zilifungiwa na shilingi bilioni
2.59 zilirejeshwa. Mfuko utaendelea kutekeleza shughuli za kukabiliana na
udanganyifu kwa kuimarishaji ugunduzi na udhibiti kwa kutumia mifumo ya
TEHAMA, kuendelea kushirikiana na wadau wakuu katika kupambana na vitendo
vya udanganyifu na kuongeza elimu ya uelewa kwa wadau wote wa Mfuko.
● Mikopo Nafuu kwa Watoa Huduma
Kwa ujumla tangu kuanzishwa kwa mpango huo hadi Juni, 2024, Mfuko umetoa
mikopo ya vifaa tiba yenye thamani ya shilling billioni 32.131 kwa vituo vya afya
vilivyoidhinishwa 287; mikopo ya dawa yenye jumla ya shillingi bilioni 3.907 kwa
vituo 45 na mikopo ya uboreshaji wa miundombinu ya shilling billioni 11.918 kwa
vituo 96.
UZINDUZI WA MIFUMO
Mheshimiwa Mgeni rasmi,
Nikianza na Mfumo wa Usajili, Mfumo huu umetengenezwa na Wataalam wetu wa
ndani kwa sh. Millioni 445 ikilinganishwa na sh. Bln 3.5 iwapo tungetumia
akandarasi za nje. Mifumo yetu inasomana na (NIDA, RITA, NECTA, NACTVET,
NSSF, WCF, MCT, GEPG, UTUMISHI, MOF, BRELA). Mifumo hii miwili imerahisisha
sana utendaji, Mfumo wa usajili wanachama unawawezesha wanachama
kujihudumia wenyewe bila kulazimika kufika katika Ofisi za Mfuko wa Taifa wa Bima
ya Afya. Kwa kurahisisha kujiunga na kutuma michango Mfumo utaondoa
malalamiko ambayo awali yalisababishwa na mapungufu ya kibinadamu lakini
kubwa zaidi na kuondoa gharama za fedha au muda ambao awali ulitumika kwenda
kwenye Ofisi zetu. Mfumo umehakikiwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao eGa na
hivyo kuahikikisha kuwa ni salama.
4
Kwa upande wa Mfumo wa Uchakataji Madai, Mfumo huu pia nao umetengenezwa
na Wataalam wa ndani ambao umeleta mapinduzi makubwa katika eneo la
uwasilishaji na uchakataji wa madai. Tulikuwa na malalamiko mengi kutoka kwa
wanachama na Watoa huduma ya ucheleweshaji wa huduma au ulipaji wa madai
Madai yalichukua hadi siku 90 wakati kwa mujibu wa Sheria tunapaswa kuchukua
siku 60. Hivi sasa tuna wastan wa siku 45 kwa yale madai ambayo yamewasilishwa
kwa wakati na hayana viashiria vya udanganyifu. Kwa mwezi tunapokea madai toka
vituo zaidi ya 5010 yakiwa na wastan wa folio 1, 190,000.
Mheshimiwa tulikuwa na malalamiko mengi ya kukata madai yaani rejection rates
hadi asilimia 20 ila sasa kwa kutumia mifumo rejection zimepungua hadi kufikia
wastan wa 9% lengo letu ni kufika asilimia 5.
● Toto Afya Kadi
Mhe. Waziri na Wageni Waalikwa, Mpango wa Toto Afya Kadi ni mpango
ambao ulianzishwa mwaka 2016 lakini kutokana na mwitikio mdogo, wtt
waliojiunga walikuwa ni wagonjwa tu kwa hiyo iliondoa dhana ya bima ya afya kwa
kuwa mtoto mmoja alitumia wastan wa mara 6 zaidi yakiwango kilichochangwa.
Mfuko umepokea maelekezo yako ya kufanya mapitio ya fao la Toto Afya
lililositishwa, kwa lengo la kulifanya liwe endelevu na stahimilivu. Watoto
wataendelea kuandikishwa kupitia makundi yao ya shule kwa michango ya awali ya
shilingi 50,400.00 kwa mwaka, Aidha watoto watakaojiunga kwa utaratibu wa
hiyari wajiunga kwa viwango vilivyorejewa kama inavyoonyeshwa katika jedwali
lifuatalo:-
Jedwali: Marejeo ya fao la Toto Afya na viwango vya Ukomo
Maelezo Chaguo 1 Chaguo 2 Chaguo 3
Malipo 658,000 237,000 150,000
Kiwango cha Ukomo
Wanaolazwa 22,000,000 8,000,000 2,000,000
Wagonjwa wa
Nje 3,000,000 2,000,000 1,000,000
5
Maeneo makubwa ambayo Mfuko umejiandaa na umeanza utekelezaji wake ni
pamoja na usajili wa kundi la Wanafunzi kuanzia ngazi ya Awali hadi ngazi ya Chuo
Kikuu. Aidha, Mifumo hii ambayo utaizindua muda mfupi ujao itawezesha
Watanzania kupata taarifa muhimu kwa wakati na kuweza kujihudumia kwa
kujiunga kiurahisi kama nilivyoeleza huko awali.
Kutokana na haya, niwaombe sana wananchi watumie fursa hii kujiunga na NHIF ili
waweze kunufaika na huduma zilizoboreshwa kwa kuzingatia mahitaji hali na
gharama kulingana na vipato vya wananchi wetu.
Mhe. Waziri na Wageni Waalikwa,
Baada ya kusema haya, naomba sasa nimkaribishe ili aweze kukukaribisha kwa
hatua inayofuata.
Asanteni kwa kunisikiliza.


Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri tanzania (TEF) Deodatus Balile, akisoma hotuba yake katika uzinduzi huo
 

Comments

Popular posts from this blog

AJIRA MPYA 41,500 SERIKALINI ZATANGAZWA KATIBU MKUU UTUMISHI JUMA MKOMI

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?

WALIOPITA KURA ZA MAONI CCM HAWA HAPA