WAKASUVI AMEFIKWA MAUTI KATIKATI YA JUKUMU ZITO: DKT. NCHIMBI.
Katibu
Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi
amesema kuwa kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Ndugu
Hassan Mohamed Wakasuvi ni pigo kubwa, si kwa mkoa huo pekee, bali
Chama, Serikali na taifa zima kwa ujumla, ambapo amefikwa na mauti akiwa
ni Mwenyekiti wa Kamati Ndogo, iliyopewa jukumu la kuangalia namna ya
kukiboresha Chama Cha Mapinduzi.
Dk.
Nchimbi amesema kuwa Komredi Wakasuvi alikuwa mmoja wa viongozi shupavu
wa Chama Cha Mapinduzi, kuanzia mkoani kwake, hadi ngazi ya taifa,
ambapo kutokana na uwezo na uadilifu wake katika kutimiza majukumu yake
kwa ufanisi na ushirikiano tangu alipochanguliwa kuwa Mwenyekiti wa Mkoa
wa CCM, mwaka 2007, aliendelea kuaminiwa hadi kuchaguliwa kuwa Mjumbe
wa Kamati Kuu ya CCM, nafasi aliyokuwa nayo hadi mauti yalipomfika.
Katibu
Mkuu wa CCM, Dk. Nchimbi amesema hayo alipokuwa akitoa salaam za pole
na rambirambi kwenye msiba wa Mzee Wakasuvi, kabla ya mazishi ya
kiongozi huyo, Jumamosi Februari 24, 2024, katika Kijiji cha Mabama,
Wilaya ya Uyui, mkoani Tabora, uliohudhuriwa pia na Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Mhe.
Kassim Majaliwa Majaliwa, aliyemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Kiwango
cha kuaminiwa Mzee Wakasuvi kilikuwa ni kikubwa sana. Mbali ya kuwa
Mwenyekiti wa Mkoa na Mjumbe wa NEC ya CCM Taifa, pia alikuwa Mjumbe wa
Kamati Kuu. Lakini pia alikuwa Mwenyekiti wa Kamati iliyopewa jukumu la
kuangalia namna ya kukiboresha chetu. Makamu wake alikuwa ni Mzee
Wassira (Steven).
“Wanauliza
watu maswali mbalimbali. Mimi ilikuwa imepangwa niwatembelee na kuonana
nao Jumatatu (keshokutwa). Wakaniulize maswali waliyopanga kuniuliza
nami nilikuwa nimejiandaa kwenda kujibu maswali hayo,” amesema Dk.
Nchimbi na kuongeza;
“Ameanza
uongozi muda mrefu sana tangu Umoja wa Vijana. Wenzake wengine wako
hapa akina Mzee Lukuvi (William), Mzee Luhavi (Rajabu) na wengine. Muda
wote alikuwa anahamasisha maendeleo ya nchi yetu na kuchochea uimara wa
CCM. Chama kimepoteza, Serikali imepoteza na Wananchi kwa ujumla
wamepoteza kiongozi mahiri na shupavu. Tuna kila sababu ya kulinda na
kuenzi kazi zake, kwa kuendelea umoja, kushikamana, amani na utulivu
thabiti bila kujali tofauti zetu za kisiasa, dini, kabila wala maeneo.”
Mbali
ya salaam hizo, Dk. Nchimbi pia aliwasilisha salaam za Mwenyekiti wa
CCM, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo Katibu Mkuu wa CCM huyo
amesema kuwa msiba huo umemgusa Mheshimiwa Rais moja kwa moja lakini
hakuweza kuhuduria kutokana na ratiba ya majukumu mengine ya kikazi, nje
ya nchi.
“Kama
ambavyo imekuwa kawaida kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kila
kunapojitokeza jambo kama hili, hapa pia amejitoa kwa uzito mkubwa tangu
tu zilipotokea taarifa za msiba huu. Washauri wake wa siasa wote wako
hapa. Pia ametutuma sisi wasaidizi wake, Mhe. Waziri Mkuu kwa upande wa
Serikali na mimi kwa upande wa Chama kuleta salaam zake za pole kwa
wanaCCM wote na Tabora kwa ujumla wenu. Nasi pia tutafikisha salaam na
shukrani zenu mlizompatia yeye kwa jinsi alivyojitoa kushiriki katika
msiba huu,” amesema Dk. Nchimbi.
Mzee
Hassan Mohamed Wakasuvi alifikwa na mauti siku ya Alhamis, Februari 22,
2024, baada ya kuugua kwa muda mfupi, ambapo pia alikuwa katika
maandalizi ya kusafiri kikazi kwenda mkoani Pwani, Jumapili, Februari
25, 2024 kwa ratiba ya majukumu mengine ya kazi za Chama.
Comments
Post a Comment