CHUO CHA KODI KUWAJENGEA UWEZO MAWAKALA WA FORODHA ZANZIBAR
Mkuu
wa Chuo cha Kodi Prof. Isaya Jairo (Kulia) pamoja na Mwenyekiti wa
Chama cha Mawakala wa Forodha Zanzibar (ZFB) Omar Hussein Mussa
wakibadilishana hati za makubaliano ya ushirikiano katika kuwajengea
uwezo wanachama wa ZFB.
Mkuu
wa Chuo cha Kodi Prof. Isaya Jairo (Kulia) pamoja na Mwenyekiti wa
Chama cha Mawakala wa Forodha Zanzibar Omar Hussein Mussa wakizungumza
na wajumbe wa Kamati ya Makubaliano kutoka Chuo cha Kodi (Kulia) na
Zanzibar (kushoto) kabla ya kusaini hati za makubaliano katika chumba
cha mikutano ITA.
Mkuu
wa Chuo cha Kodi Prof. Isaya Jairo (wa pili kushoto), Mwenyekiti wa
Chama cha Mawakala wa Forodha Zanzibar (ZFB) Omar Hussein Mussa (wa pili
Kulia) pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala Tanzania (TAFFA)
Stephen Ngatunga (wa kwanza kulia) katika picha ya pamoja na wajumbe wa
kamati ya ushirikiano mara baada ya kusaini makubaliano ya kuwajengea
uwezo mawakala wa Forodha Zanzibar. (PICHA ZOTE NA OLIVER NJUNWA).
…………………………………………………………………………………..
Na Oliver Njunwa- Dar es Salaam
Chuo
cha Kodi (ITA) pamoja na Chama cha Mawakala wa Forodha Zanzibar (ZFB),
vimeingia katika makubaliano ya kushirikiana katika kuwajengea uwezo
Mawakala wa Forodha Zanzibar.
Akizungumza
mara baada ya hafla fupi ya kutiliana saini makubaliano hayo,
iliyofanyika hivi karibuni katika Chuo cha Kodi jijini Dar es salaam,
Mkuu wa Chuo hicho Prof. Isaya Jairo amesema kwamba, makubaliano hayo ni
muhimu kwani kila upande una watalaam wa kutosha kuwasaidia Mawakala wa
Forodha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
“ITA
inajivunia utaalam wake wa kufundisha na ZFB ina utaalamu katika
masuala ya kiforodha. Kwa hiyo wote kwa pamoja tutashirikiana ili
malengo ya makubaliano haya yaweze kufikiwa”, alisema Prof. Jairo.
Prof.
Jairo aliongeza kuwa, katika makubaliano hayo, Chuo cha Kodi kitatoa
mafunzo ya muda mfupi na utaalamu wa masuala ya forodha kwa ZFB ili
kuhakikisha kuwa kunakuwa na Mawakala wa Forodha wanaofanya kazi kwa
weledi.
Mkuu
wa Chuo cha Kodi pia amesema kwamba lengo la vyuo sio kupata fedha bali
kutoa wataalamu wa kutosha ambapo uwezo wa Chuo hupimwa kwa idadi ya
wanafunzi wanaohitimu na aina ya sifa walizonazo.
Aidha,
Prof. Jairo ameiomba ZFB kulinda hadhi ya jina la Chuo cha Kodi kwani
kina jina zuri kutokana na uzoefu wake wa kutekeleza makubaliano ya
ushirikiano na taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi.
“ITA
ina makubaliano na Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA)
pamoja na Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB) na kwa nchi za nje ina
makubaliano na Malawi, Zambia, Botswana na iliisadia Sudan Kusini
kuanzisha Mamlaka ya Mapato nchini humo”, alisema Prof. Jairo.
Makubaliano
hayo yamefanyika katika Chuo cha Kodi Dar es salaam Ijumaa tarehe 26
Januari 2017 na kutiwa saini kati ya Mkuu wa Chuo cha Kodi Prof. Isaya
Jairo na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Forodha Zanzibar Omar
Hussein Mussa na kushuhudiwa na Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha
Tanzania (TAFFA) Stephen Ngatunga.
Naye
Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Forodha Zanzibar ZFB, Omar Hussein
Mussa amesema kwamba makubaliano hayo ni msingi mzuri wa kupata Mawakala
wa Forodha wenye weledi na hivyo kupunguza changamoto zinazojitokeza
katika tasnia ya uwakala wa forodha.
“Makubaliano
haya ni jambo jema na yatakuwa endelevu kwa kuwa sisi tuko tayari
kuhakikisha yanaleta mabadiliko katika utendaji wa mawakala wetu wa
Forodha”, alisema Bw. Mussa.
Kwa
upande wake Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania Stephen
Ngatunga ambaye alihudhuria hafla hiyo, amekipongeza Chuo cha Kodi
pamoja na ZFB kwa makubaliano hayo muhimu na kusema kwamba anafarijika
kuona jitihada zake zimefanikiwa kwani yeye alichangia kufanikisha suala
hilo.
Katika
makubaliano hayo, Chuo cha Kodi kitasimamia kiwango cha taaluma
itakayotolewa kwa kuzingatia vigezo vya Baraza la Taifa la Mafunzo ya
Ufundi (NACTE) na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU). Aidha, Chuo hicho pia
kitasimamia udahili, mitihani, kutoa walimu na vyeti baada ya kuhitimu
wakati Chama cha Mawakala wa Forodha Zanzibar kitapokea ada, kutoa
wanafunzi, madarasa pamoja na vitendea kazi.
Chuo
cha Kodi ni sehemu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania ambacho kilipata
ithbati kutoka Baraza la Taifa la Mafunzo ya Ufundi kutoa mafunzo ya
muda mfupi na mrefu kwa watumishi wa TRA pamoja na wadau mbalimbali
katika fani za Kodi na Forodha.
Comments
Post a Comment