HATIMAYE MANSOUR WA CCM ATUA CUF JUMLA JUMLA LEO HII
Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, akimpongeza Mansour Yussuf Himid baada ya kuamua kujiunga na chama hicho na kumkabidhi rasmi kadi ya CUF katika viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja.
Mwanachama mpya wa CUF Mansour Yussuf Himid akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui, baada ya kujiunga na chama hicho katika viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja.
Mwanachama mpya wa CUF Mansour Yussuf Himid akizungumza na wanachama wenzake , baada ya kujiunga na chama hicho katika viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja
Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, akihutubia mkutano wa hadhara wa chama hicho katika viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja.
Wanachama wa CUF wakionyesha
kuunga mkono uamuzi wa Mansour Yussuf Himid kujiunga rasmi na chama hicho
kwenye viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja. (Picha na Salmin Said, OMKR).
28/12/2014.
Na:
Hassan Hamad (OMKR).
Aliyekuwa Mwakilishi
wa jimbo la Kiembesamaki Mhe. Mansour Yussuf Himid, amejiunga rasmi na chama
cha wananchi CUF.
Mhe. Mansour ambaye
amewahi kuitumikia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushika nyadhifa mbali
mbali ikiwemo ya Waziri wa Kilimo, amechukua uamuzi huo leo kwenye mkutano wa
hadhara wa CUF uliofanyika viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja.
Baada ya kukabidhiwa
kadi ya CUF na Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad, Mhe.
Mansour amesema ameamua kujiunga na CUF baada ya kubaini na kuridhika kuwa
chama hicho kimebeba matumaini mapya ya wazanzibari.
Mhe. Mansour ambaye
tayari alishateuliwa na chama hicho kuwa mshauri wa mikakati wa Katibu Mkuu wa
CUF, amechukua kadi hiyo akiwa miongoni mwa wanachama wapya 108 waliojiunga na
CUF kwenye mkutano huo.
Mapema akizungumza
kwenye mkutano huo, Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, amempongeza
Mhe. Mansour kwa kuamua kujiunga na chama hicho hadharani, na kukiita kitendo
hicho kuwa ni cha kijasiri.
Akizungumzia
mafanikio ya chama hicho, Maalim Seif amesema kimepata mafanikio makubwa katika
mwaka unaomalizika wa 2014, na kutangaza maazimia mapya ya chama hicho kwa
mwaka 2015.
Ametaja mafanikio
yaliyopatikana kuwa ni pamoja na kuendelea kukubalika kwa chama hicho katika
pembe zote za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Kuhusu maazimio ya
Chama hicho kwa mwaka 2015, Maalim Seif amesema kimejipanga kuhakikisha kuwa
kinashinda kwa asilimia kubwa katika uchaguzi mkuu ujao na kuweza kuongoza
serikali ya umoja wa kitaifa.
Hata hivyo amewataka
wanachama wasibetweke kutokana na mafanikio yaliyopatikana, bali waongeze nguvu
kuhakikisha kuwa malengo ya chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao yanafikiwa.
Ameongeza kuwa CUF
pia kimejipanga kuimarisha uchumi na kujenga Zanzibar mpya itakayokuwa ya
matumaini kwa Wazanzibari wote.
Katika hatua
nyengine, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
amesema katika uchaguzi mkuu ujao hatowazuia vijana kutetea haki yao iwapo
watadhulumiwa.
“Katika uchaguzi mkuu
wa mwaka 2010 nilifanya kazi kubwa ya kuwazuia vijana wasifanye vurugu pale
hoteli ya Bwawani.
Mwanzo niliwatuma wasaidizi wangu waende kuwaondosha lakini
hakuna aliyesikia hadi nilipokwenda mwenyewe, tena waliondoka kwa shingo upande
kabisa. Kwa hivyo uchaguzi mkuu ujao sina namna yoyote ya kuwazuia vijana
kutetea haki yao”, alifafanua Maalim Seif.
Kabla ya mkutano huo
Maalim Seif alifanya ziara ya kukagua uhai wa chama hicho katika vijiji vya
Michamvi, Bwejuu, Jambiani na Paje ambako aliweka mawe ya msingi kwenye matawi
ya chama hicho, pamoja na kupandisha bendera kwenye barza ya DAY OUT ya Paje.
………………………………………………………………………………
Comments
Post a Comment