VIOONGOZI IMTU KIZIMBANI DAR
Baadhi ya viongozi wa juu wa Hospitali na Chuo
cha Udaktari cha IMTU, wakiwa chini ya ulinzi wa askari katika
Mahakama ya Kinondoni jijini Dar es Salaam jana kusomewa mashtaka ya
kutupa viungo vya binadamu hadharani. Kutoka kushoto ni Venkat
Subbaiah, Appm Shankr, Prabhakar Rao na Dinnesh Kumar.
VIONGOZI wanne wa Chuo Kikuu cha Tiba na Teknolojia (IMTU), wamefikishwa
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, mjini Dar es Salaam jana, wakikabiliwa na mashtaka
mawili.
Viongozi hao ambao ni raia wa India, ni Venkat Subbaiah (57),
Appm Shankar (64), Prabhakar Rao (69) na Dinnesh Kumar (27).
Wakisomewa makosa hayo mbele ya Hakimu Kwey Rusema, Wakili wa
Serikali, Magoma Mtani, alidai tukio hilo lilitokea Julai 20, mwaka huu, katika
eneo la bonde la Mpiji Majohe, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Wakili Magoma alidai katika kosa la kwanza, washtakiwa wote
wanakabiliwa na shtaka la kushindwa kuhifadhi miili ya binadamu iliyokuwa
katika kituo hicho cha afya kwa ajili ya mazoezi kwa vitendo kwa wanafunzi.
Mtani alidai katika shtaka la pili, washtakiwa wote kwa pamoja
wanakabiliwa na kosa la kushindwa kuwa na kibali kutoka kwa mtu maalumu
anayetoa kibali cha kufukia ama kuteketeza miili hiyo (Coroner).
“Washtakiwa mlitenda kosa hili kinyume cha kifungu cha sheria
namba 128 cha utaratibu wa kuhifadhi miili ya binadamu,” alidai Wakili.
Washtakiwa walikana kuhusika na kosa hilo
na upelelezi wa shauri hilo
unaendelea.
Hakimu Rusema alisema shtaka hilo
linadhaminika kisheria, hivyo washtakiwa wanatakiwa kupeleka wadhamini wawili, wote
wawe raia wa Tanzania.
Hata hivyo, Hakimu Rusema baada ya kumaliza kuwasomea masharti
ya dhamana, alipokea ujumbe kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kwamba
jalada la washtakiwa hao lirudishwe kwake kwa ajili ya kuandaa upya mashtaka yao.
Kwa upande wake, Wakili wa Utetezi, Gaudiosus Ishengoma,
alishangazwa kurudishwa kwa jalada hilo
kwa DPP, kwani hiyo itakuwa ni mbinu za kuweka masharti magumu kwa wateja wake.
“Kisheria wateja wangu walishindwa kufuata utaratibu wa kuhifadhi ile miili baada
ya majaribio na kupata kibali kwa ‘Coroner’, hivyo kisheria kosa hili
linadhaminika, lakini jalada litakapokuja tena upya linaweza likawa na masharti
magumu,” alidai Ishengoma.
Washtakiwa hao walirudishwa rumande hadi jalada litakapotoka kwa
DPP kwa ajili ya kusomewa tena.
Julai 21, mwaka huu, viungo vya binadamu vilitupwa katika eneo
la Bonde la Mbweni Mpiji, Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam na uongozi wa Chuo cha IMTU na
kuzua mjadala mkubwa.
Katika eneo hilo,
MTANZANIA ilishuhudia mifuko mikubwa myeusi 85 ya nailoni ikiwa na viungo
mbalimbali vya binadamu vikiwa vimechunwa ngozi.
Viungo hivyo ambavyo vilionekana
nyama zake zikiwa zimekauka ni pamoja na mafuvu ya vichwa, sehemu ya
kifua cha binadamu, miguu, mikono, moyo na
mapafu.
Licha ya baadhi ya viungo kuonekana wazi, vilikuwa havitoi
harufu, jambo lililotafsiriwa kuwa vilikuwa vimepuliziwa dawa kali ya kuondoa
harufu.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo
waliiambia MTANZANIA kuwa miili hiyo ilitupwa eneo hilo tangu Julai 20, mwaka huu.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Super Kaijunga (45), alisema alikuwa
mtu wa kwanza kuona viungo hivyo.
Juzi Serikali ilitangaza kukifungia chuo hicho kwa muda
usiojulikana.
Mwisho
Comments
Post a Comment