VIKWAZO KWA URUSI KUWA JANGA KWA MABILIONEA

Bilionea Alisher Usmanov akiwa na mkewe Irina


  Bilionea wa Urusi Roman Abramovich, akiwa na rafiki yake  Dasha Zhukova






Vikwazo vyawatisha mabilionea wa Urusi.
ROHO za mabilionea wa Urusi ziko juu kwa uwezekano wa kuwekewa vikwazo vitakavyoporomosha si tu uchumi wao bali pia wa  taifa hilo.
Uwezekano huo unatokana na mjadala unaoendelea katika mataifa ya Magharibi yasiyofurahishwa na ushiriki wa Moscow katika machafuko yanayoendelea mashariki mwa Ukraine.
Mabilionea hao wana neno kuhusu uwezekano huo hata nini cha kufanya ili kuviepuka, lakini wanamgwaya Rais wa Urusi Vladimir Putin, hivyo kushindwa kuzungumza waziwazi.

Marekani tayari imeweka mlolongo wa vikwazo dhidi ya kampuni za Urusi na mtu mmoja moja huku Uingereza na Uholanzi zikiongoza ajenda katika Umoja wa Ulaya (EU) juu ya vikwazo vikali zaidi kufuatia kuangushwa kwa ndege ya Shirika la Ndege la Malaysia, MH17.
Wataalamu wa fedha wanaonya kuwa vikwazo vya ziada dhidi ya Urusi vinavyoweza kuwekwa kipindi cha wiki mbili zijazo vinaweza kuupeleka uchumi wa Urusi wa dola trilioni mbili katika mfadhaiko mkuu.
Kwa mujibu wa Igor Bunin, ambaye anaongoza Kituo cha Teknolojia ya Siasa mjini Moscow, wafanyabiashara wa Urusi wanavigwaya vikwazo lakini pia wanamwogopa zaidi Rais Putin.
Bunin aliuambia mtandao wa Bloomberg.com: “Uchumi na kundi la wateule wa kibiashara wako katika kihoro.
“Hakuna mtu anayeweza kuzungumza hilo wazi kwa sababu ya tishio la kushughulikiwa. Ishara yoyote ya uasi, inatosha kabisa kukuangusha hadi magotini kwa dakika chache,”.
Vikwazo vya Marekani vilivyowekwa kabla ya msiba wa MH17 uliogharimu maisha ya watu 295 wengi wao wakiwa raia wa Uholanzi, tayari vimeathiri kampuni zinazomilikiwa na serikali ya Urusi pamoja na wafanyabiashara kadhaa walio karibu na Putin.
Kampuni ya OAO Novatek (NVTK), inayozalisha gesi ambayo kwa sehemu fulani inamilikiwa na mshirika wa Putin, Gennady Timchenko, ilishuhudia thamani yake sokoni ikipungua kwa karibu dola bilioni tatu baada ya kuzuiwa nchini Marekani.
Wamiliki wa Benki ya SMP na Benki ya Invest Capita, ambao ni mtu na kaka yake; Arkady na Boris Rotenburg, ni marafiki wa siku nyingi na washirika wa Putin katika mchezo wa judo pia wamekumbwa na orodha nyeusi ya Marekani.
Wakati Uingereza ikiihamasisha EU kuweka vikwazo dhidi ya wateule wa Putin, baadhi yao huenda wakawa wale waliopiga kambi mjini London.
Hata hivyo, Makazi ya Waziri Mkuu wa Uingereza, 10 Downing Street (No 10) yalikataa kutoa ufafanuzi juu ya watu watakaokumbwa na vikwazo hivyo.
Lakini minong’ono inaeleza huenda ikahusisha mabilionea maarufu kama vile Roman Abramovich, mmiliki wa Klabu ya Chelsea inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza.
Abromovich, mwenye utajiri wa pauni milioni 5.5, ana ukaribu na utawala wa Putin.
Mwingine anayetajwa ni pamoja mwanahisa mkuu wa Klabu ya Arsenal FC, inayoshiriki pia Ligi Kuu ya Uingereza, Alisher Usmanov (60), mwenye utajiri wa pauni bilioni 11.
No10 ilipuuza uwezekano wa Putin, ambaye anadhaniwa kuhamisha mabilioni ya pauni kipindi hiki kulengwa binafsi na hatua hiyo.
Vikwazo vya EU pia vinaweza kuhusisha dhidi ya kuiuzia Urusi silaha na kukomoa uwezo wa kampuni za nishati za Urusi kupata fedha barani Ulaya.
Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron, alisema msimamo wa Putin katika mzozo wa Ukraine haukubaliki kabisa.
Katika mahojiano mbalimbali, Cameron amekiri kuwa Uingereza haitakwepa athari za kuichukulia hatua Moscow.
Hata hivyo Cameroon alisema athari itakazopata kiuchumi haziwezi kulinganishwa na zile zinazoweza kujitokeza iwapo hatua hazitachukuliwa.
Cameroon amemtaka Putin atumie ushawishi wake kuwazuia waasi wanaotaka kujitenga na Ukraine kuendelea na harakati zao, akimkumbushia raia wake 10 walikuwa miongoni mwa abiria waliokufa katika MH 17 inayodaiwa kudunguliwa na waasi hao.
Chanzo cha habari NO 10, kilisema Uingereza inatarajia kuongeza majina ya ziada ya orodha ya Warusi watakaokabiliwa na marufuku ya kusafiri barani Ulaya na kutaifishwa mali zao chini ya masharti ya sasa ya vikwazo vya EU.
Hatua hiyo inaweza kuhusisha kampuni au taasisi pamoja na watu wanaohusika na harakati za kuidhoofisha Ukraine.
Lakini pia kutakuwa na hatua za kusukuma wigo wa vikwazo ili vibane wale wenye ushawishi au kuusaidia utawala wa Urusi, ikimaanisha matajiri waliomzunguka Putin.
Chanzo hicho kilisema: “Mbinu yetu ya kushughulika na Putin itakuwa kwa namna ambayo tunadhani itamshawishi ashirikiane nasi na kuwabana waasi na kuleta matokeo mazuri kwa amani.'
Mabilionea wa Urusi wamekuwa wakionesha hofu lakini wakisita kuzungumza lolote, lakini mmoja wao kwa sharti la kutotajwa alisema Putin anahatarisha kutengwa.
“Wengi hawawezi kukubaliana na pigo litakalowakumba, matajiri na watu wenye nguvu wamekuwa wakizungumza chini chini uwezekano wa kujitenga na Putin ili kulinda fedha zao,” bilionea huyo alisema.
Na wiki iliyopita Rais wa Marekani Barack Obama aliipiga marufuku kampuni ya silaha ya Kalashnikov, ambayo inatengeneza bunduki maarufu za AK-47, kuuzwa nchini Marekani, hali iliyosababisha wateja wengi kupigana vikumbo kununua shehena ya silaha iliyokuwa imebakia sokoni.
Wafanyabiashara wa rejareja wa bunduki walisema tangu amri hiyo itolewe wiki iliyopita, mahitaji yake yameongezeka kwa vile wanunuzi wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kununua silaha zilizobaki sokoni.
Wizara ya Fedha ya Marekani ilitoa taarifa katika tovuti yake kuwa raia wa Marekani wanaruhusiwa kununua na kutumia Kalashnikov iwapo tu silaha hizo ziliingizwa kabla ya kuanza kwa vikwazo.
Robert Keller, meneja wa kampuni ya usambazaji wa bunduki hizo mjini Las Vegas, K-Var Corp, aliliambia Shirika la Habari Marekani (CNN): Bidhaa hizi zina mahitaji makubwa nchini hapa. Tumeuza sana  Kalashnikov,”.
Miongoni mwa silaha zinazozalishwa na kampuni hiyo ni AK-47, maarufu zaidi duiniani na ile iliyoboreshwa AK-74.
Msemaji wa Kalashinkov alisema wateja wa Marekani wanaadhibiwa kutokana na marufuku hiyo.



Comments

Popular posts from this blog

AJIRA MPYA 41,500 SERIKALINI ZATANGAZWA KATIBU MKUU UTUMISHI JUMA MKOMI

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?

WALIOPITA KURA ZA MAONI CCM HAWA HAPA