MAJALIWA Azitaka zisiwe pango la wezi, wazembe
Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa akihutubia leo wakati wa
kufungua baraza la ushauri (RCC) Mkoa wa Dodoma ambapo lilishirikisha
Wizara,Idara na Wadau mbalimbali wanaoratibu ujio wa Serikali kuhamia Makao
makuu Dodoma Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Chuo cha mipango ya
Maendeleo Vijijini Dodoma ( Picha na PMO)
30 JANUARI, 2017
TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI
HALMASHAURI ZIFANYE KAZI KWA WELEDI-MAJALIWA
*Azitaka zisiwe pango la wezi, wazembe
WAZIRI MKUU Kassm Majaliwa amesema wakati umefika wa kuwa
na watumishi wenye weledi wa kutosha kwenye Halmashauri zote nchini na pia
hazitakiwi kuwa pango la wezi, wazembe au jalala la kutupa wabadhilifu
walioshindikana kwingineko.
Aidha, Waziri Mkuu amesemma
Serikali za Mitaa na Halmashauri zote nchini zinatakiwa zianze kujitathmini na
kujipanga vizuri zaidi kuona ni kwa namna gani zitakuwa chachu ya maendeleo ya
viwanda vinavyotarajiwa.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Januari 30,
2017) wakati akifungua Kikao cha Baraza la Mashauriano (RCC) mkoani Dodoma.
Amesema kikao ni chombo muhimu na endapo kitatumika vizuri kitaweza
kusaidia kusukuma maendeleo ya Mkoa na kupunguza migogoro kwenye Halmashauri.
Amesema Serikali itaendelea
kuongeza kiwango cha ruzuku kwa Halmashauri zote nchini kwa kadiri uwezo
utakavyoruhusu na kusisitiza kwamba fedha hizo lazima zisimamiwe vizuri na
zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo inayowagusa wananchi.
“Endapo
itabainika kwamba kuna baadhi ya Sheria zinazokwamisha utendaji katika Mamlaka
za Serikali za Mitaa, hatutasita kuzifanyia mapitio na hatimaye kuzibadili ili
ziendane na azma yetu ya kutoa huduma bora kwa wananchi,” amesema.
Amesema
Serikali ina maslahi makubwa kwa Serikali za Mitaa, sio tu kwa kuwa ni Serikali
kamili katika ngazi hiyo, bali pia kutokana na ukweli kwamba kero nyingi za
wananchi ziko katika ngazi hiyo.
Waziri Mkuu amesema vyanzo vingi vya mapato ya
Serikali vinapatikana kwenye Halmashauri huku changamoto kubwa ikiwa ni
kulegalega kwa Halmashauri nyingi katika ukusanyaji wa mapato ya kodi na
yasiyo ya kodi jambo linalozorotesha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Hivyo
Waziri Mkuu ametoa rai kwa Halmashauri hizo kuendelea kuboresha huduma kwa
wananchi na kutatua kero zao kikamilifu na kwa wakati pamoja na kubuni vyanzo
vipya vya mapato na kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato.
Pia
zihakikishe malipo yote yanafanyika kwa njia za kielektoniki na zihamasishe
vijana na akina mama wajiunge kwenye vikundi vya uzalishaji mali na kuwapatia
stadi za kazi na mikopo yenye masharti nafuu ili waweze kuwa chanzo cha mapato
hapo baadaye.
Amesema
watendaji wa Halmashauri wanatakiwa kujiepusha na vitendo vya rushwa na
ubadhilifu wa mali za umma na uzembe kazini na watakaobainika kufanya vitendo
hivyo wachukuliwe hatua kali za kisheria na kinidhamu.
“Someni
taarifa ya CAG (Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali) na kutoa majibu
ya kina ya namna mtakavyodhibiti mianya ya rushwa na ubadhilifu kama
ilivyoainishwa kwenye ripoti hizo,” amesema.
Hata
hivyo amesema kila Halmashauri iandae mpango wa utekelezaji wa Ilani ya CCM
kwenye maeneo makubwa ya kipaumbele kama vile ujenzi wa miundombinu ya shule, maboresho kwenye sekta
ya afya (ujenzi wa hospitali, zahanati na vituo vya afya).
“Endeleeni
kuwa na mahusiano mazuri miongoni mwenu, mfanye kazi kwa kuzingatia sheria,
kanuni na taratibu. Kila mmoja kwa nafasi aliyonayo atimize wajibu wake
na kuzingatia mipaka ya nafasi yake. Punguzeni migogoro, matusi, dharau, bezo
na vitisho. Mshirikiane na jamii ione mpo wamoja,” amesema.
(mwisho)
IMETOLEWA
NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMATATU, JANUARI 30, 2017
Comments
Post a Comment