MELI KUBWA ZAIDI DUNIANI YATUA BANDARI YA DAR ES SALAAM LEO
JUHUDI za serikali kuifufua Bandari ya Dar es Salaam na
kuifanya kuwa ya ushindani zimenoga ambapo sasa imefungua milango kwa meli
kubwa zaidi kutia nanga katika bandari hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA),
Mhandisi Deusdedit Kakoko (PICHANI),alisema hayo jana jijini Dar es Salaam mara baada ya manahodha wa Mamlaka hiyo
kufanikiwa kuingiza meli kubwa zaidi katika historia ya bandari hiyo yenye
urefu wa mita 261.
Alisema meli hiyo iitwayo MV Hammonia Grenada ina uwezo wa
kubeba makasha 4,256 imetia nanga katika bandari ya Dar es Salaam na kushusha makasha
483 na kupakia makasha 656 kabla ya kuelekea nchini Thailand.
“Milango sasa ipo
wazi kwa meli kubwa zaidi kutia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam, kwani
teknolojia ya meli za kisasa inaruhusu,” alisema.
Alisema mbali na teknolojia iliyotumika kutengeneza meli
hizo, Mamlaka imeboresha ujuzi wa manahodha wake baada ya kuwapeleka katika
nchi za Afrika Kusini, Denmark na Ufaransa kupata mafunzo jinsi ya kuingiza
meli za aina hiyo bandarini.
Alisema kuingia kwa meli hiyo ya MV Hammonia Grenada na
kutia nanga ni uthibitisho tosha kwamba bandari ina uwezo wa kuhudumia meli
kubwa kwa kutumia miundombinu iliyopo na kwa ufanisi mkubwa.
“Bandari yetu ina uwezo wa kuhudumia meli zenye ukubwa huo
katika gati zake nne, gati hizo ni namba 8,9,10 na 11 ambazo zina kina chenye
urefu mita 11,” alisema.
Alisema kwamba ujio wa meli hiyo ni ushahidi tosha kwamba
bandari ina uwezo wa kupokea meli kubwa za aina hiyo ambazo awali zilikuwa
zikiishia bandari ya Mombasa pekee.
“Wapo waliokuwa wakifikiri kwamba bandari yetu sasa
haifanyi kazi lakini ukweli ni kwamba bandari yetu ipo sawa na inaendelea
kupokea meli kama kawaida.
“Na kuwathibitishia hilo, hata Rais John Magufuli wakati
alipokuja kufanya ziara hapa bandarini kulikuwa na meli nyingine saba zimetia
nanga.
“Napenda niwatoa hofu wateja wetu kwamba bandari yetu ina
uwezo wa kuhudumia meli kubwa bila shida yoyote na ujio wa meli hii umefungua
milango ya meli nyingine kubwa kuja katika bandari yetu,” alisema Kakoko.
Naye Rubani Mkuu wa Mamlaka, Kepteni Abdullah Mwingamno alisema meli hiyo ndiyo kubwa
kuliko zote ambazo zimewahi kuingia katika bandari ya Dar es Salaam.
“Hapo mwanzo mlango wa bandari yetu ulitengenezwa kuweza
kuhudumia meli zenye urefu wa mita 234 tu lakini kutokana na mabadiliko ya
teknolojia na jinsi meli zenyewe zinavyojengwa imeweza kuingiza hata meli za
urefu mkubwa zaidi,” alisema Mwingamno ambaye ndiye aliyeingiza meli.
Pamoja na suala la teknolojia, Kepteni Mwingamno alisema hivi sasa TPA ina wataalamu
wa kutosha ambao wamepata mafunzo sehemu mbalimbali Duniani ili kuweza kuingiza
meli kubwa za namna hiyo.
“Tumepeleka kundi la kwanza la vijana wetu nchini Afrika
Kusini kupata mafunzo ya jinsi ya kuingiza meli kubwa katika bandari yenye lango
kama la kwetu na kundi la pili la vijana hawa tumelipeleka Copenhagen,
Denmark,” alisema.
Alisema kundi la tatu la vijana hao walilipeleka Nantes
nchini Ufaransa kupata mafunzo kama hayo.
“Kwa hiyo napenda kuwahakikishia wateja wetu kwamba tunao
wataalamu wa kutosha kuifanya kazi hii,” alisema.
Alisema hapo awali, TPA iliwahi kuingiza meli nyingine
kubwa yenye urefu wa mita 250 na baadae ikaingiza meli nyingine yeenye urefu wa
mita 255.
Kwa mujibu wa Kepteni huyo, meli zenye urefu wa mita 261
mara nyingi huishia Bandari ya Mombasa kutokana na udogo wa lango letu lakini
ujio wa meli hiyo umefungua rasmi milango ya kibiashara.
“Ujio wa meli hii umefungua rasmi njia kwa meli nyingine
kubwa za aina hii ambazo zilidhani zisingiweza kuingia katika bandari ya Dar es
Saam na hivyo kufungua rasmi ushindani na bandari nyingine,” amesema.
MV Hammonia Grenada ikiwasili katika Bandari ya Dar es Salaam (2)
MV Hammonia Grenada ikiwasili katika Bandari ya Dar es Salaam
Comments
Post a Comment