WAZIRI MKUU DKT . MWIGULU AKUTANA NA MZEE JOSEPH BUTIKU
- Get link
- X
- Other Apps
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Mzee Joseph Butiku, akizungumza na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, wakati wa mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Oysterbay, jijini Dar es Salaam, Julai 20, 2026.
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, akipokea nyaraka kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Mzee Joseph Butiku, baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika katika Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Oysterbay, jijini Dar es Salaam, Julai 20, 2026.
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Mzee Joseph Butiku, na ujumbe wake baada ya mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Oysterbay, jijini Dar es Salaam, Julai 20, 2026.
@@@@@@@@@@@@@@@@@@
WAZIRI MKUU AKUTANA NA MZEE JOSEPH BUTIKU
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema maendeleo ya kweli ya Taifa yanategemea kujenga wananchi wenye maadili, uzalendo, uwajibikaji na mshikamano, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha utawala wa sheria na taasisi za umma.
“Hakuna maendeleo ya kudumu bila kujenga watu wenye maadili, uzalendo na uwajibikaji. Kama Taifa tuna kila sababu ya kuendelea kuwekeza katika kujenga tabia ya wananchi pamoja na kuimarisha taasisi zetu,” amesema.
Waziri Mkuu amesema hayo leo (Jumatatu, Julai 20, 2026) alipokutana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Mzee Joseph Butiku, katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Oysterbay, jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo, Mzee Butiku alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake na juhudi anazoendelea kuzifanya katika kuiongoza nchi. Pia, alimpongeza Waziri Mkuu kwa mchango wake katika kumsaidia Mheshimiwa Rais kusimamia Serikali na kuhakikisha utekelezaji wa majukumu ya Serikali unaendelea kwa ufanisi. Amesema amekuwa akifuatilia kwa ukaribu ziara za Waziri Mkuu mikoani na kujionea namna zilivyochangia kutatua changamoto za wananchi na kuimarisha utoaji wa huduma.
Aidha, aliishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana na Taasisi ya Mwalimu Nyerere na kuipatia mazingira mazuri ya kutekeleza majukumu yake, ikiwemo kupata eneo la ujenzi wa Mwalimu Nyerere World Leadership Institute, pamoja na kuitambua Taasisi hiyo kama mshirika wa maendeleo ya Taifa.
Mzee Butiku pia alisisitiza umuhimu wa kuendelea kujenga jamii inayoheshimiana, inayovumiliana na inayozingatia maadili, uzalendo, utawala wa sheria, haki za watu na misingi ya demokrasia. Alisema kumekuwepo na mwenendo wa baadhi ya watu kuwavunjia heshima viongozi, wazee, viongozi wastaafu na viongozi wa dini, jambo ambalo halijengi utaifa wala haliendani na misingi ya Taifa.
Aliongeza kuwa ni muhimu Watanzania wakaendelea kukosoana kwa hoja na kwa kuzingatia sheria, huku kila mmoja akitimiza wajibu wake kwa lengo la kulinda amani, usalama, umoja na mshikamano wa Taifa. Amesema Taasisi ya Mwalimu Nyerere itaendelea kutoa elimu ya amani, maadili na uzalendo kwa manufaa ya Taifa.
Vilevile, Mzee Butiku ameipongeza Serikali kwa hatua inazoendelea kuchukua katika kuimarisha amani, utulivu, haki za watu, Serikali za Mitaa na misingi ya demokrasia. Amesema hatua hizo zimeendelea kuimarisha mshikamano wa Taifa na kurejesha hali ya utulivu nchini. Pia amepongeza hatua ya kuendelea kutoa kipaumbele suala la Katiba Mpya kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025–2030.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuimarisha utawala wa sheria, uwajibikaji, utoaji wa haki na utendaji wa taasisi za umma ili kulinda haki za wananchi na kuimarisha amani na utulivu nchini.
Amesema Serikali itaendelea kuimarisha Serikali za Mitaa na taasisi nyingine za umma ili ziweze kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi, sambamba na kuendelea kujenga Taifa linalozingatia maadili, uzalendo, mshikamano na demokrasia.
Aidha, Waziri Mkuu amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Taasisi ya Mwalimu Nyerere katika kukuza maadili, uzalendo, umoja wa kitaifa na maendeleo, ikiwemo kuunga mkono ujenzi wa Mwalimu Nyerere World Leadership Institute (Centre of Excellence).
- Get link
- X
- Other Apps
Comments
Post a Comment