WAKULIMA WANUFAIKA NA HUDUMA ZA STAKABADHI GHALA WRRB
Mwaka huu ni mwaka wa kihistoria kwa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala na Taifa kwa ujumla. Tarehe 19 Mei 2026, Mfumo wa Stakabadhi za Ghala uliadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2006. Katika kipindi hiki, Mfumo umebadilisha kabisa namna biashara ya mazao inavyofanyika nchini kwa kuweka msingi wa biashara yenye uwazi, ushindani na usalama wa masoko ya wakulima.
Mafanikio haya yasingewezekana bila uongozi madhubuti wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye ameendelea kusimamia sera zinazoweka mazingira bora ya biashara, uwekezaji, matumizi ya TEHAMA na maendeleo ya sekta ya kilimo na biashara.
Vilevile, tunatoa shukrani za dhati kwa Wizara ya Viwanda na Biashara chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Judith Salvio Kapinga, Waziri wa Viwanda na Biashara, ambaye ameendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa majukumu ya WRRB, kutoa miongozo ya kisera na kuhakikisha Mfumo wa Stakabadhi za Ghala unaendelea kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Mfumo unaendelea kukua nchini
Ndugu Waandishi wa Habari,
Mfumo wa Stakabadhi za Ghala umeendelea kukua na kuimarika mwaka hadi mwaka. Ulipoanza kutekelezwa, mfumo ulihusisha zao moja tu la korosho. Kutokana na mafanikio yake, kwa sasa unahusisha mazao na bidhaa 18 zilizokusanywa kupitia mfumo huu ambazo ni Kunde, Njungumawe, Karanga, Asali, Maharage, Mihogo, Dengu, Kahawa, Kakao, Choroko, Mahindi, Mpunga, Mbaazi, Korosho, Ufuta, Soya, Mchele, Chai na Vitunguu swaumu, na wigo wa utekelezaji wake kwasasa umefikia Mikoa 23 ambayo ni Arusha, Dodoma, Geita, Iringa, Kagera, Katavi, Kigoma, Lindi, Manyara, Mara, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Pwani, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga , Simiyu, Singida, Songwe, Tabora na Tanga. Ukuaji huu unaonyesha kuongezeka kwa imani ya wadau, kupanuka kwa matumizi ya mfumo na mchango wake katika kuimarisha masoko ya mazao na bidhaa nchini.
Mchango wa Serikali katika kuimarisha WRRB
Ndugu Waandishi wa Habari,
Katika mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali ilitoa Shilingi milioni 950 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya WRRB.
Fedha hizi zilitumika katika maeneo muhimu ambayo yameongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi, ikiwemo:
- kutoa elimu na uhamasishaji kuhusu Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa wakulima na wadau mbalimbali nchini;
- kuboresha miundombinu ya TEHAMA na mifumo ya kidijitali ya usimamizi wa shughuli za Stakabadhi za Ghala;
- kuimarisha usimamizi na ukaguzi wa maghala nchini;
- kununua vitendea kazi na vifaa vya kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya Bodi.
Uwekezaji huu wa Serikali umeongeza uwezo wa WRRB kusimamia Mfumo kwa ufanisi zaidi na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma bora.
Mafanikio makubwa ya mwaka wa fedha 2025/2026
Ndugu Waandishi wa Habari,
Mfumo huu umeendelea kuwa na mafanikio makubwa ambapo kwa Mwaka wa fedha 2025/2026 jumla ya kilo 1,122,246,475 za mazao tisa ya korosho, ufuta, kahawa, kakao, mbaazi, dengu, choroko, soya na chai zimeuzwa kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala katika minada ya kidigitali inayosimamiwa na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), ikilinganishwa na kilo 781,659,285 zilizouzwa mwaka uliopita, hii ni sawa na ongezeko la asilimia 43.6.
Kwa lugha rahisi, ndani ya mwaka mmoja kiasi cha mazao kilichouzwa kupitia Mfumo kimeongezeka kwa zaidi ya kilo milioni 340. Ongezeko hili linaonesha kuwa wakulima wengi zaidi wameendelea kuuamini Mfumo na kuamua kuuza mazao yao kupitia utaratibu rasmi wenye ushindani.
Mafanikio haya yameleta manufaa makubwa kwa wakulima, Serikali na uchumi wa nchi kwa ujumla. Kutokana na mauzo hayo:
• Wakulima
na wauzaji walilipwa jumla ya Shilingi trilioni 2.298;
• Serikali za Mitaa zilikusanya Shilingi bilioni
61.05 kupitia ushuru wa mazao (CESS);
• Thamani ya biashara yote iliyofanyika kupitia
Mfumo ilifikia Shilingi trilioni 2.679.
Kwa lugha rahisi, zaidi ya Shilingi trilioni 2.2 zimefika moja kwa moja mikononi mwa wakulima na wazalishaji kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala. Fedha hizi zimechangia kuboresha ustawi wa kaya kwa kuongeza uwezo wa wananchi kugharamia mahitaji muhimu kama elimu, afya, makazi, pamoja na kuwekeza katika shughuli mbalimbali za uzalishaji na maendeleo.
Vilevile, zaidi ya Shilingi bilioni 61 zilizokusanywa kupitia ushuru wa mazao (CESS) zimeongeza mapato ya Halmashauri, na hivyo kuziwezesha kuboresha utoaji wa huduma za jamii, ikiwemo ujenzi na matengenezo ya barabara, shule, vituo vya afya, masoko na miundombinu mingine muhimu kwa maendeleo ya wananchi.
Mafanikio kwa mazao mbalimbali
Ndugu Waandishi wa Habari,
Katika mwaka wa fedha 2025/2026, makusanyo ya mazao na mauzo kupitia mfumo wa Stakabadhi za Ghala yalikuwa kama ifuatavyo:
- Korosho kilo milioni 439.6
- Mbaazi kilo milioni 269.9
- Ufuta kilo milioni 199.6
- Dengu kilo milioni 131.4
- Choroko kilo milioni 37.0
- Kahawa kilo milioni 29.2
- Kakao kilo milioni 12.8
- Soya kilo milioni 2.1
- Chai kilo 381,440
Takwimu hizi zinaonesha kuwa Mfumo umeendelea kupanuka katika mazao mengi zaidi na kuongeza mchango wake katika biashara ya ndani na mauzo ya nje.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kupitia Mfumo huu:
- wakulima wanauza mazao kupitia minada ya ushindani badala ya kuuza holela kwa wanunuzi bila kuwa na nguvu ya makubaliano ;
- wakulima hawalazimiki kuuza mazao mara baada ya kuvuna wakati bei ikiwa chini;
- mazao yanahifadhiwa katika maghala yenye viwango hivyo kupunguza upotevu baada ya mavuno;
- wakulima hulipwa kupitia benki na taasisi za fedha hivyo kuongeza ujumuishaji wa kifedha (financial inclusion);
- Stakabadhi za Ghala zimeendelea kutumika kama dhamana ya kupata mikopo.
Matokeo yake ni kuongezeka kwa kipato cha wakulima, kuimarika kwa biashara na kuongezeka kwa uwekezaji katika sekta ya kilimo.
Mchango kwa uchumi wa Taifa
Ndugu Waandishi wa Habari,
Mfumo wa Stakabadhi za Ghala umeendelea kuwa miongoni mwa nyenzo muhimu za Serikali katika kukuza uchumi, kuwawezesha wazalishaji kupata masoko yenye ushindani na kuongeza ufanisi katika biashara ya mazao. Sambamba na ukuaji wa matumizi ya Mfumo huo, mapato ya ndani ya Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) yameendelea kuongezeka kwa kasi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Mapato hayo yameongezeka kutoka Shilingi bilioni 1.998 katika mwaka wa fedha 2023/2024, hadi Shilingi bilioni 2.944 mwaka 2024/2025, na kufikia Shilingi bilioni 5.870 katika mwaka wa fedha 2025/2026. Hii ina maana kuwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu, mapato ya ndani ya WRRB yameongezeka kwa karibu mara tatu.
Ongezeko hili linaonesha kuimarika kwa utekelezaji wa majukumu ya WRRB, kuongezeka kwa idadi ya wadau wanaotumia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, pamoja na kupanuka kwa shughuli za kibiashara zinazoratibiwa kupitia Mfumo huo.
Pia Ongezeko hili limeenda sambamba na kuongezeka kwa fursa za ajira zinazotokana na utekelezaji wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala. Katika mwaka wa fedha 2025/2026, Mfumo ulizalisha jumla ya ajira 31,875 kupitia shughuli mbalimbali za mnyororo wa thamani, ikiwemo ukusanyaji wa mazao na bidhaa, uhifadhi ghalani, upimaji wa ubora, usafirishaji, upakiaji na upakuaji, pamoja na huduma nyingine zinazohusiana na biashara kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala. Hii inaonesha kuwa Mfumo unaendelea kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi kwa kuongeza fursa za ajira na kipato kwa wananchi.
Kutokana na kuimarika kwa mapato yake ya ndani, WRRB imeweza kugharamia asilimia 67.57 ya bajeti yake katika mwaka wa fedha 2025/2026, ikilinganishwa na asilimia 53.12 mwaka wa fedha uliotangulia. Hali hii inaonesha hatua kubwa ya Bodi kuelekea kujitegemea kifedha, kupunguza utegemezi wa fedha za Serikali na kuendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na wadau wa Mfumo.
Aidha, mchango wa WRRB katika kuongeza mapato ya Serikali umeendelea kuimarika, ambapo fedha zilizorejeshwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali zimeongezeka kutoka Shilingi milioni 22 mwaka 2023/2024 hadi kufikia Shilingi milioni 140 mwaka 2025/2026.
Kuimarisha usimamizi wa Mfumo
Ndugu Waandishi wa Habari,
Katika mwaka wa fedha 2025/2026, WRRB iliendelea kufanya ukaguzi wa maghala kabla, wakati na baada ya msimu wa biashara.
Jumla ya magunia 19,041,651, yenye uzito wa zaidi ya kilo bilioni 1.114, zilikaguliwa na kuthibitishwa ubora wake.
Aidha, kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, WRRB imeendelea kuchangia kutatua changamoto ya lumbesa katika biashara ya mazao. Mazao yote yanayouzwa kupitia Mfumo hukaguliwa ubora wake, hupimwa kwa kutumia vipimo vinavyokubalika na kuhifadhiwa kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa kabla ya kuuzwa sokoni. Hatua hii huongeza uwazi katika biashara, huondoa migogoro inayotokana na vipimo visivyo sahihi na kuwapa wanunuzi na wauzaji uhakika wa ubora na kiasi cha bidhaa wanazofanyia biashara. Katika kuimarisha juhudi hizi, WRRB itaendelea kushirikiana kwa karibu na Wakala wa Vipimo (WMA) kuhakikisha matumizi ya vipimo sahihi na kudhibiti vitendo vya lumbesa katika biashara ya mazao nchini.
Pia, WRRB imeendelea kuboresha Mfumo wa WRMS (Warehouse Receipts Management System) na kuendeleza Mfumo wa WRS-MIS (Warehouse Receipts System Management Information System) utakaounganisha taarifa za leseni, ukaguzi na biashara kwa njia ya kidijitali.
Mwelekeo wa Baadaye wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala
Ndugu Waandishi wa Habari,
Pamoja na mafanikio yaliyopatikana, WRRB imejipanga kuendelea kupanua wigo wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ili uweze kunufaisha sekta nyingi zaidi za uzalishaji na kuchangia kwa kiwango kikubwa zaidi katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo kuanzia 2026/27 hadi 2030/31, Bodi imeweka mikakati mbalimbali ambayo itaendelea kutekeleza kwa lengo la kuimarisha Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma na kuhakikisha manufaa zaidi yanawafikia wakulima, wafanyabiashara na wadau wengine wa Mfumo. Mikakati hiyo ni pamoja na;
i. Kupanua Mfumo katika sekta mpya za uzalishaji
WRRB itaendelea kupanua wigo wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ili uwezeshe biashara ya bidhaa mbalimbali na si mazao ya kilimo pekee. Kupitia mkakati huu, Bodi inaendelea na majadiliano ya kisera na kitaalamu kwa kushirikiana na Wizara mbalimbali, taasisi za Serikali, sekta binafsi, wafugaji, wakulima, vyama vya ushirika pamoja na washirika wa maendeleo ili kuweka mazingira wezeshi ya kuingiza bidhaa mpya katika Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.
Katika mwaka wa fedha 2026/27, WRRB itaanza utekelezaji wa mkakati huu kwa kuingiza sekta ya mifugo katika Mfumo, ambapo mnada wa kwanza wa mifugo kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala unatarajiwa kufanyika Wilaya ya Mvomero hivi karibuni. Aidha, Mfumo utaendelea kupanuliwa kwenye bidhaa nyingine zikiwemo mwani, ngozi, mazao ya bustani na bidhaa nyingine zitakazokidhi vigezo vya kuingia katika Mfumo.
Upanuzi huu wa Mfumo pia utafungua fursa mpya za uwekezaji na biashara nchini. Halmashauri zitanufaika kwa kujenga na kuendeleza maghala ya kisasa yatakayokidhi viwango vya Mfumo, hatua itakayochochea ukusanyaji wa mapato ya ndani na maendeleo ya uchumi wa maeneo husika. Vilevile, kutakuwa na fursa zaidi kwa sekta binafsi na vyama vya ushirika kuwekeza katika uendeshaji na usimamizi wa maghala yaliyosajiliwa, huduma za uhifadhi, usafirishaji, upimaji wa ubora wa bidhaa, pamoja na huduma nyingine zinazohusiana na mnyororo wa thamani.
Pia Bodi inaendelea kuandaa kanuni, miongozo na taratibu za kiutendaji zitakazowezesha biashara ya bidhaa hizo kufanyika kwa kuzingatia viwango vya ubora, usalama wa bidhaa na mahitaji ya masoko ya ndani na kimataifa.
Lengo ni kuwafanya wazalishaji wa sekta hizo wanufaike na huduma zinazotolewa kupitia Mfumo, ikiwemo uhifadhi salama, masoko yenye ushindani, upatikanaji wa mikopo kwa kutumia stakabadhi za ghala na kuongeza thamani ya bidhaa zao.
ii. Kuongeza matumizi ya TEHAMA katika usimamizi wa Mfumo
WRRB itaendelea kuboresha mifumo ya kidijitali ili kuongeza uwazi, ufanisi na kasi ya utoaji wa huduma. Hii ni pamoja na kuendeleza Mfumo wa WRS-MIS, kuboresha Mfumo wa WRMS, kuongeza matumizi ya stakabadhi za kielektroniki na kuunganisha taarifa za leseni, ukaguzi, biashara na malipo katika mfumo mmoja wa kidijitali.
Hatua hizi zitaongeza ufanisi wa usimamizi wa Mfumo, kupunguza gharama za uendeshaji na kuwezesha wadau kupata huduma kwa haraka zaidi.
iii. Kuimarisha ushiriki wa taasisi za fedha
Bodi itaendelea kushirikiana kwa karibu na Benki Kuu ya Tanzania(BoT), benki za biashara, taasisi za fedha na wadau wengine ili kuongeza huduma za mikopo zinazotumia Stakabadhi za Ghala kama dhamana.
Lengo ni kuhakikisha wakulima, wafugaji, vyama vya ushirika na wawekezaji wengi zaidi wanapata mitaji ya kuendeleza shughuli zao bila kulazimika kuuza bidhaa zao kwa bei ya hasara.
Sambamba na hilo, WRRB imeendelea kuimarisha mazingira ya upatikanaji wa huduma za kifedha kwa kusimamia utoaji wa leseni na uendeshaji wa Mameneja Dhamana (Collateral Managers) wanaohakikisha bidhaa zinazotumika kama dhamana zinatunzwa kwa usalama na kuzingatia viwango vinavyotakiwa. Hatua hii imeongeza imani ya taasisi za fedha katika utoaji wa mikopo inayotumia Stakabadhi za Ghala na kuchangia kupunguza hatari ya mikopo chechefu.
Aidha, katika maadhimisho ya miaka 20 ya WRRB na Mfumo wa Stakabadhi za Ghala yaliyofanyika mwaka huu, WRRB iliingia makubaliano ya ushirikiano na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Benki ya NBC, yenye lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha, kuwezesha matumizi ya Stakabadhi za Ghala kama dhamana ya mikopo na kuongeza ujumuishaji wa kifedha kwa wazalishaji, wafanyabiashara na wadau wengine wa Mfumo.
iv. Kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya maghala na huduma za biashara
WRRB itaendelea kuhamasisha uwekezaji katika ujenzi wa maghala ya kisasa, vituo vya ukusanyaji mazao, miundombinu ya kuhifadhi bidhaa zinazohitaji mazingira maalumu pamoja na huduma za kuongeza thamani ya mazao na bidhaa nyingine zinazotarajiwa kuingia katika Mfumo.
Hatua hii itaongeza uwezo wa nchi kuhifadhi mazao kwa usalama, kupunguza upotevu baada ya mavuno na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa.
v. Kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na wadau
WRRB itaendelea kutoa elimu kwa wakulima, wafugaji, vyama vya ushirika, waendeshaji wa maghala, wanunuzi, taasisi za fedha na wananchi kwa ujumla kuhusu fursa na manufaa ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala. Elimu hiyo inalenga kuongeza uelewa wa matumizi ya Mfumo, kuhamasisha ushiriki wa wadau wengi zaidi na kuhakikisha wanatumia fursa zinazotokana na Mfumo katika kuongeza tija na kuboresha biashara zao.
Elimu hiyo itatolewa kupitia mikutano ya wadau, mafunzo, vyombo vya habari, maonesho ya biashara, majukwaa ya kidijitali na programu mbalimbali za uhamasishaji, ili kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanashiriki na kunufaika na Mfumo huu.
Aidha, WRRB itaendelea kuutangaza na kuukuza Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kama jukwaa linalowezesha biashara ya mazao na bidhaa mbalimbali, kwa kuendelea kupanua wigo wa matumizi yake kutoka katika mazao ya kilimo pekee hadi bidhaa nyingine zenye fursa za kibiashara. Hatua hii itaongeza ushiriki wa wadau katika minyororo mbalimbali ya thamani na kuimarisha upatikanaji wa masoko yenye ushindani.
Sambamba na hilo, WRRB itaendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia za kidijitali katika utekelezaji wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ili kuwa sehemu muhimu ya kukuza mifumo ya kidijitali ya biashara nchini. Kupitia maboresho ya mifumo ya TEHAMA, Mfumo utaendelea kurahisisha upatikanaji wa taarifa za masoko, kuongeza uwazi wa miamala, kuboresha ufanisi wa huduma na kuwaunganisha wazalishaji, wanunuzi na wadau wengine wa biashara kwa njia rahisi na salama.
Katika kuimarisha mnyororo wa biashara kidigitali ndani na nje ya nchi, WRRB itaendelea kujenga ushirikiano na taasisi mbalimbali ili kuongeza matumizi ya teknolojia, elimu na huduma zinazowawezesha wadau wa Mfumo kufanya biashara kwa ufanisi zaidi. Katika maadhimisho ya miaka 20 ya WRRB, Bodi iliingia makubaliano ya ushirikiano na Shirika la Posta Tanzania (TPC), Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) pamoja na East Africa Grain Council (EAGC). Ushirikiano huo unalenga kuimarisha utoaji wa elimu kwa wadau, kuongeza matumizi ya majukwaa ya kidigitali katika biashara, kuboresha usambazaji wa taarifa za masoko, pamoja na kuwezesha biashara ya mazao na bidhaa kuvuka mipaka kwa kuzingatia viwango vya kikanda na kimataifa.
Kwa ujumla, mwelekeo huu unaendana na azma ya Serikali ya kuendelea kujenga uchumi shindani, kuongeza thamani ya mazao na bidhaa za Tanzania, kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza ajira na kuchochea maendeleo endelevu kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.
Mchango katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050
Ndugu Waandishi wa Habari,
Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ni nyenzo muhimu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa:
- kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya dunia;
- kuongeza thamani ya mazao ya kilimo;
- kuimarisha ujumuishaji wa kifedha kwa wakulima;
- kuongeza mapato ya Serikali na Halmashauri;
- kuchochea uwekezaji katika maghala na miundombinu ya biashara;
- kuongeza matumizi ya TEHAMA katika biashara ya mazao;
- kuongeza ajira na ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi.
HITIMISHO
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kwa mara nyingine, napenda kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi wake mahiri na maono yanayoendelea kuweka mazingira wezeshi kwa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuchangia maendeleo ya sekta ya kilimo na uchumi wa Taifa.
Vilevile, tunatoa shukrani zetu za dhati kwa Wizara ya Viwanda na Biashara kwa usimamizi na mwongozo wake katika kuimarisha utekelezaji wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala. Aidha, tunawashukuru wadau wetu wote wakiwemo Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), taasisi za fedha, vyama vya ushirika, waendeshaji wa maghala, wanunuzi, wakulima pamoja na wadau wengine wote wanaoendelea kushirikiana nasi katika kukuza na kuimarisha mfumo huu.
Mwisho, tunawashukuru sana ninyi waandishi wa habari kwa ushirikiano wenu na kwa kuendelea kuwa kiungo muhimu cha kuhabarisha na kuelimisha umma kuhusu shughuli na mafanikio ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala. Tunaamini ushirikiano huu utaendelea kuimarika kwa manufaa ya Watanzania wote.
Wanahabari wakimsikiliza kwa makini mkurugenzi huyo alipokuwa akizungumza
Comments
Post a Comment