PROF. SHEMDOE: SERIKALI IMEWEKEZA BILIONI 2.8 KUBORESHA AFYA, BARABARA, ELIMU YA AMALI GAIRO

Na. OWM–TAMISEMI, Gairo
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza Shilingi bilioni 2.8 katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Kituo cha Afya Chanjale, Barabara ya Confort Pub–Magoweko na Shule ya Amali Kwipipa, hatua iliyoboresha upatikanaji wa huduma za afya, kurahisisha usafiri na usafirishaji pamoja na kupanua fursa za elimu ya amali kwa wananchi wa wilaya ya Gairo.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, Julai 17, 2026 katika kijiji cha Kwipipa, kata ya Rubeho, wilaya ya Gairo, baada ya kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi hiyo ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma.
Prof. Shemdoe amesema miradi hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora karibu na maeneo wanayoishi kupitia uwekezaji unaogusa maisha yao ya kila siku.
“Leo nimekagua miradi mitatu muhimu. Mradi wa Kituo cha Afya Chanjale wenye thamani ya Shilingi Milioni 680, Barabara ya Confort Pub–Magoweko yenye thamani ya Shilingi Milioni 470 na Shule ya Amali Kwipipa yenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.6. Miradi hii ni matokeo ya fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi,” amesema Prof. Shemdoe.
Akizungumzia Shule ya Amali Kwipipa, Prof. Shemdoe amesema shule hiyo imebobea katika mafunzo ya uhandisi na itakuwa chachu ya kuandaa wataalamu wenye ujuzi watakaoshiriki katika ujenzi wa taifa na maendeleo ya sekta mbalimbali za uzalishaji na amewataka wanafunzi wa shule hiyo kuitunza miundombinu yake ili idumu kwa muda mrefu na kuendelea kunufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.
Prof. Shemdoe ameainisha kuwa, uwekezaji huo ni sehemu ya jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, akieleza kuwa tangu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, Halmashauri ya Wilaya ya Gairo imepokea zaidi ya Shilingi Bilioni 100 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Gairo, Mhe. Ahmed Shabiby, amewapongeza wananchi wa kijiji cha Kwipipa kwa kujitolea eneo lililowezesha ujenzi wa shule ya Amali, yenye manufaa kwa wananchi wa Gairo na taifa kwa ujumla, Aidha ameipongeza TAMISEMI kwa kutenga bajeti ya chakula kwa wanafunzi wa shule hiyo, hatua itakayochangia kuboresha mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia.
Naye, Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Josephine Kapoma, amesema Shule ya Amali Kwipipa itasaidia taifa kupata wahandisi wazawa wenye ujuzi na tija kwa taifa, hivyo amemuomba Prof. Shemdoe amfikishie salamu Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa wananchi wa Kwipipa wameipokea shule hiyo kwa furaha kutokana na mchango wake katika kuinua elimu ya ufundi nchini.









Comments
Post a Comment