WAZIRI MKUU MWIGULU ALIFUNGA BUNGE NA KUWATAKA WATANZANIA WATUNZE AMANI

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. MWIGULU LAMECK NCHEMBA (MB.), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUAHIRISHA MKUTANO WA TATU (3) WA BUNGE LA 13 LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA TAREHE 26 JUNI, 2026

JIJINI DODOMA

 

1.            Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa fadhili zake zilizotuwezesha sote kuiona siku hii muhimu katika historia ya Bunge la 13. Kama mnavyofahamu, tumekutana leo kwa ajili ya kuhitimisha mkutano wa Tatu ambao ulikuwa mahsusi kwa ajili ya kupokea na kujadili bajeti ya serikali.

 

2.            Mheshimiwa Spika, nimesema leo ni siku muhimu na ya kihistoria kwa sababu, hii ni Bajeti ya kwanza ya Serikali kupitishwa na Bunge la 13 baada ya uchaguzi mkuu wa 2025. Hongereni sana waheshimiwa Wabunge!

 

3.            Mheshimiwa Spika, kwa unyenyekevu mkubwa, ninaomba nitoe shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maono na uongozi wake thabiti wakati wote wa kipindi cha mkutano huu wa Tatu (3) wa bunge la bajeti. Wakati wote amekuwa akinipa maelekezo yenye tija na kuifanya kazi yangu kuwa nyepesi.

 

4.            Mheshimiwa Spika, sina shaka nyote mtakubaliana nami kuwa utayari wake na hamasa kubwa aliyokuwa nayo katika kuwatumikia watanzania imekuwa ni mfano wa kuigwa. Pia, hulka yake na ustahimilivu wake umekuwa faraja kwetu sisi wasaidizi wake, watumishi wote wa umma na Watanzania wote kwa ujumla.

 

5.             Mheshimiwa Spika, ninamshukuru sana Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano wake alionipatia wakati wote nikitekeleza majukumu yangu. Busara zake na weledi wake umekuwa msaada na mfano wa kuigwa katika utendaji kazi Serikalini.

 

6.            Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa ushirikiano mkubwa alionipatia wakati wote. Kadhalika, ninatoa shukrani kwa Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Ofisi yote ya Makamu wa Pili wa Rais kwa ushirikiano wakati nikitekeleza majukumu yangu.

 

7.            Kipekee nitumie nafasi hii kukushukuru sana wewe binafsi Mheshimiwa Mussa Azan Zungu, Mbunge wa Ilala, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hakika umeendelea kudhihirisha uzoefu wako kwenye shughuli za Kibunge na umekuwa tafsiri sahihi ya kiongozi shupavu na mwenye uweledi mkubwa katika kuliongoza Bunge hili la 13.

 

8.             Mheshimiwa Spika, uzoefu wako wakati wote umeendelea kuwa na tija kubwa katika utendaji wa shughuli za serikali bungeni. Ninakushukuru sana kwa namna ulivyoendesha mijadala yote ya bajeti za kisekta katika mkutano huu wa tatu pamoja na kupitisha makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2026/2027.

 

9.            Mheshimiwa Spika, vilevile, nitumie nafasi hii kutoa shukrani kwa Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini na Naibu wa Spika pamoja na Mheshimiwa Najma Murtaza Giga (Mbunge wa Viti Maalum), Mheshimiwa Deodatus Philip Mwanyika Mbunge wa Njombe Mjini na Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, (Mbunge wa Viti Maalum) kwa nafasi zao za Wenyeviti wa Bunge. Wakati wote mmekuwa mkinipa ushirikiano wa kutosha wakati mlipokuwa mkimsadia Mheshimiwa Spika katika shughuli za kuendesha Bunge hili tukufu.

 

10.        Mheshimiwa Spika, ninatoa shukrani zangu za dhati kwa Waheshimiwa Wabunge wote kwa kufanya kazi kubwa kipindi chote cha utekelezaji wa shughuli za Mkutano wa tatu mahususi wa kupitisha mpango na bajeti. Waheshimiwa wabunge mmefanya kazi kubwa, hakika mnastahili pongezi.

 

11.        Mheshimiwa Spika, maoni, ushauri na michango yenu katika mkutano huu yamekuwa yakitoa mwelekeo sahihi katika mipango na utendaji wa shughuli za Serikali na imegusa moja kwa moja maisha ya wananchi wote. Pia ninawapongeza kwa kazi kubwa mliyoifanya tarehe 23 Juni, 2026 ya kupitisha kwa kura ya ndiyo Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/2027 ya shilingi trilioni 62.33 kwa kura za asilimia 97.66 Hongereni sana waheshimiwa wabunge na hiyo kazi kubwa mliyoifanya na kwa imani mliyokuwa nayo kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Serikali ilijipanga, imesikiliza hoja zenu na kutoa ufafanuzi na sasa ipo tayari kwenda kutekeleza Bajeti kwa kuzingatia yote mliyoshauri.

 

12.        Mheshimiwa Spika, ninaomba sasa nitumie nafasi hii kuwapongeza Mawaziri, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Naibu Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Katibu Mkuu Kiongozi, Makatibu Wakuu, Makatibu Tawala, Naibu Makatibu Wakuu, Watendaji Wakuu wa Taasisi za Serikali na Watumishi wote umma kwa kufanikisha kupitishwa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

 

Pongezi za Teuzi na Chaguzi Mbalimbali

 

13.        Mheshimiwa Spika, kama mtakavyokumbuka ninaomba niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kutoa pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Emmanuela K. Mtatifikolo, Mbunge wa Jimbo la Ismani kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo hilo kufuatia uchaguzi mdogo uliofanyika hivi karibuni (wakati mkutano huu ukiendelea). Ushindi huo, unadhihirisha kwamba wananchi jimbo la Ismani wana imani kubwa na Chama cha Mapinduzi kutokana uongozi thabiti, sera makini pamoja na Ilani ya Uchaguzi inayotekelezeka. Nitumie fursa hii kumkaribisha sana Mheshimiwa Emmanuela K. Mtatifikolo na nimhakikishie kuwa Waheshimiwa Wabunge wote tutampa ushirikiano mkubwa ili aweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu ya kuwakilisha wananchi wa jimbo la Ismani.

 

14.        Mheshimiwa Spika, wakati mkutano wa tatu wa Bunge ukiendelea, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya teuzi mbalimbali.  Teuzi hizo zilifanywa kwa lengo la kutekeleza na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na shughuli mbalimbali za serikali na mihimili mingine.

 

15.        Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 02 Mei, 2026 Mheshimiwa Rais, alimteua Mheshimiwa Dkt. Evaline Wilbard Munisi (Mb.), kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano). Pia, Mheshimiwa Rais alimteua Dkt. John Antony Jingu kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.

 

16.        Mheshimiwa Spika, vilevile aliteua wakuu wa taasisi, mabalozi na wateule wengine katika nafasi mbalimbali. Nitumie nafasi hii kuwatakia wateule wote kila la heri katika utekelezaji wa majukumu yao mapya na kuwakumbusha wajibu wao wa kutanguliza mbele maslahi ya Taifa letu mbele na kuwahudumia watanzania wote.

 

Salamu za Pole

 

17.        Mheshimiwa Spika, wapo Watanzania wenzetu waliokumbwa na majanga mbalimbali zikiwemo ajali za barabarani. Ninatoa pole kwa wananchi wote waliopoteza wapendwa wao katika ajali hizo. Vilevile, ninatoa pole kwa majeruhi wote na ninawaombea kwa Mwenyezi Mungu awape uponyaji wa haraka.  Nitumie nafasi hii pia, kutoa pole kwa waathirika wa majanga mengine yote yaliyotokea na hatujayataja.

 

2.0        SHUGHULI ZA BUNGE

 

Maswali na Majibu

 

18.        Mheshimiwa Spika, leo wakati tunahitimisha shughuli za mkutano wa tatu wa Bunge la 13, tumefanikiwa kutekeleza masuala mbalimbali ikiwemo wajibu wa msingi kutunga sheria, kupitisha bajeti na hoja mbalimbali zilizojitokeza. Shughuli hizo ni kujibu maswali na hoja zilizowasilishwa na Waheshimiwa Wabunge; kujadili na kupitisha Miswada ya Sheria ya Serikali; na kujadili na kutoa Maazimio mbalimbali. Katika mkutano huu, maswali ya msingi 696 na ya nyongeza 2,591 na maswali 31 ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu yaliulizwa na kupatiwa majibu.

 

Miswada

19.        Mheshimiwa Spika, kwa upande wa miswada bunge lako tukufu katika Mkutano huu, Bunge lako tukufu limepokea Miswada mitano (05) ambayo ilisomwa katika hatua mbalimbali ambayo ni:

 

Moja:       Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2026 (The Finance Bill, 2026), uliosomwa kwa hatua zote;

Mbili:        Muswada wa Sheria ya Matumizi wa Mwaka 2026 (The Appropriation Bill, 2026) , uliosomwa kwa hatua zote;

Tatu:        Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 02) wa Mwaka, 2026 [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No. 02) Bill, 2026], uliosomwa kwa mara ya kwanza;

Nne:         Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Kilimo wa Mwaka 2026 [The Agricultural (Amendments) Bill, 2026], uliosomwa kwa mara ya kwanza; na

Tano:       Muswada wa Sheria ya Kufuta Sheria ya Tasnia ya Pareto wa Mwaka 2026,  nao uliosomwa kwa mara ya kwanza.

 

Azimio

 

20.        Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 61 na 107 hadi 112 za Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Februari 2023, na kwa kuzingatia wajibu wa Bunge, Bunge lako tukufu lilipokea na kujadili Azimio moja ambalo ni:

 

Azimio la Bunge kuhusu Kuipongeza Timu ya Taifa ya Vijana Wanaume Chini ya Umri wa Miaka 17 yaani (Serengeti Boys) kwa Kufuzu Fainali za AFCON 2026 na Kukata Tiketi ya Kushiriki Mashindano ya Kombe la Dunia la Vijana Chini ya Umri wa Miaka 17 kwa Mwaka 2026. Nirejee kuwapongeza sana vijana wetu kwa kuweka historia hiyo!

 

3.0        MAFANIKIO NA VIPAUMBELE VYA SERIKALI

 

Mafanikio ya Utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2025/2026

 

21.        Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake thabiti na dhamira yake ya kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa weledi mkubwa katika kutekeleza miradi ya maendeleo. Dhamira hiyo imekuwa msingi wa mafanikio makubwa tunayoyashuhudia katika mwaka wa fedha ambao tunaouhitimisha.

 

22.        Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia maono na maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali ya Awamu ya Sita imepata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa Ilani ya Mwaka 2020 na Dira ya 2025 kupitia sekta mbalimbali. Mafanikio hayo yamebainishwa kwa kina wakati nilipowasilisha Bungeni Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2026/2027.

 

23.        Mheshimiwa Spika, pia, mafanikio hayo katika maeneo ya miundombinu, sekta za uzalishaji, huduma za jamii na masuala mtambuka  na yamebainishwa kwa ufasaha na Mawaziri wa Kisekta kupitia bajeti za wizara zao katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/2026. Mafanikio kwenye sekta na maeneo hayo yameendelea kuwa faraja na ukombozi kwa wananchi wa kipato cha chini ikiwemo wakulima, wafanyabiashara wadogo, waendesha bodaboda na mama/babalishe na maeneo mengine. Haya yote ni matunda ya uongozi makini wa Mheshimiwa Rais na dhamira yake ya dhati ya kustawisha maisha ya Watanzania kuwa ya staha na utu bila kumwacha mtu nyuma.

 

Kuimarisha Diplomasia Kiuchumi na Ushirikiano wa Kimataifa

 

24.        Mheshimiwa Spika, ni jambo la kujivunia kuona jinsi Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alivyoendelea kuitangaza na kuiwakilisha vema Tanzania katika jukwaa la kimataifa. Mheshimiwa Rais, ameendelea kuonesha uongozi wa hekima na kuendelea kushirikiana na mataifa mbalimbali na asasi za kimataifa.

 

25.        Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ameendelea kusukuma mbele ajenda ya diplomasia ya kiuchumi kwa vitendo, akithibitisha kuwa Tanzania ni mshirika wa kuaminika katika biashara na kiuwekezaji. Tumeshuhudia ziara za viongozi wenzake kutoka Ghana, Kenya, Uganda, Rwanda, Singapore na  hivi majuzi kiongozi kutoka Namibia.

 

26.        Mheshimiwa Spika, ziara hizo zilifanikisha makubaliano pamoja na kusaini mikataba muhimu katika maeneo ya biashara, uchukuzi, nishati na miundombinu. Aidha, Mheshimiwa Rais, alipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Mabalozi wanane, akisisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuongeza thamani ya rasilimali zake.

 

27.        Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais pia ameitangaza Tanzania kama kituo cha uwekezaji wa kimataifa kupitia ziara zake za kikazi nje ya nchi. Akiwa amefanya ziara na kushiriki mikutano ya kikazi na kiserikali katika nchi za Falme za Kiarabu (Dubai) na Urusi. Akiwa nchini Urusi, Mheshimiwa Rais alitoa wito wa uwekezaji zaidi katika Bara la Afrika, akiitangaza Tanzania kama lango la kimkakati la biashara katika eneo lenye soko la zaidi ya watu milioni 500.

 

Kutunukiwa Shahada ya Uzamivu

 

28.        Mheshimiwa Spika, ni heshima kubwa kwa Taifa letu kuona Mheshimiwa Rais akitunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu na Chuo Kikuu cha Urafiki wa Watu wa Urusi kwa mchango wake mkubwa katika elimu, ushirikiano wa kimataifa na urafiki kati ya mataifa haya. Heshima hii hutolewa kwa nadra kwa viongozi wachache duniani, ni kielelezo cha namna jamii ya Kimataifa inavyothamini uongozi wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tunampongeza kwa dhati Mheshimiwa Rais kwa heshima hii inayotuangazia sote kama Taifa.

 

4.0        MAMBO YALIYOTILIWA MSISITIZO KATIKA MJADALA WA BAJETI YA 2026/2027 

 

Vipaumbele vya Sekta kwa Mwaka 2026/2027

29.        Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kulihakikishia Bunge lako na wananchi kwa ujumla kwamba vipaumbele vya Bajeti ya mwaka 2026/2027 kwa kila Wizara za Kisekta vimezingatia maslahi mapana ya Taifa. Bajeti hii, itaendelea kuimarisha uwekezaji katika sekta za uzalishaji, miundombinu na huduma za jamii. Serikali imejipanga kuendelea kuimarisha mikakati na mifumo mapato ya ndani na kupunguza utegemezi wa mikopo na misaada kutoka nje. Mikakati moja wapo ni kupunguza utegemezi kutoka nje. Nimpongeze mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa wasilisho la Bajeti hiyo!

 

Kuimarisha Uwezeshaji wa Makundi Maalum

 

30.        Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujumla wameshuhudia kusomwa kwa bajeti ya mwaka 2026/2027. Bajeti hiyo, inaenda kugusa na kuweka mazingira wezeshi ya kuvutia urasimishaji wa sekta isiyo rasmi ambayo inaajiri zaidi vijana na wanawake.

 

31.        Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azma hiyo, Serikali kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa inaenda kutenga asilimia 15 ya mapato yao ya ndani badala ya asilimia 10 iliyopo sasa ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Kati ya asilimia 15 itakayotengwa, asilimia 10 itaelekezwa kwenye mikopo ya wanawake, vijana na wenye ulemavu kwa uwiano kama ilivyokuwa awali. Aidha, asilimia tano itatumika kwa ajili ya uwekezaji kwenye miradi ya ujenzi na maboresho ya masoko na maeneo ya biashara na ujasiriamali ili kuvutia na kuongeza fursa za ajira hususan kwa vijana, wanawake na makundi maalum.

 

32.        Mheshimiwa Spika, nizielekeze mamlaka za serikali za mitaa kutenga maeneo ya wajasiriamali kwa kuzingatia urahisi  wa kufikika na kuwezesha kufanya biashara kwa tija. Hivyo, kupitia asilimia 5 ya uboreshaji wa miundombinu ya wajasiriamali, pale inapohitajika halmashauri zilipe fidia wazidishe kufanya hivyo ili kuwezesha upatikanaji wa maeneo yenye sifa kwa wajasiriamali kupata tija katika shughuli zao ili tuache kufukuzana na wajasiriamali tuwapatie maeneo ya kufanya biashara ili yakidhi tija zao.

 

33.        Mheshimiwa Spika,  aidha, kupitia utaratibu mpya wa utoaji mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri. Ninazielekeza taasisi za fedha na waratibu wa mikopo hiyo kuondoa masharti magumu yanayokwamisha wajasiriamali kunufaika na mikopo hiyo. Mfano ulazima wa wahitaji kwa upande wa watu (walemavu) kuunda vikundi na ulazima wa wahitaji kuwasilisha dhamana kubwa kama vile hati za nyumba kwa asili ya biashara zao hawawezi kuwa nazo. Nitumie fursa kwa vijana kutumia hiyo vizuri.

 

Maeneo Yaliyofanyiwa Maboresho ya Kodi

 

34.        Mheshimiwa Spika, ili kuwavutia wajasiriamali, Serikali itatoa msamaha wa kodi ya mapato kwa wafanyabiashara wadogo ambao ni wapya kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu tarehe ya kupata namba ya utambulisho wa mlipakodi. Hatua hii itawezesha mama na baba lishe, waendesha bodaboda na bajaji, mafundi seremala na wachomeleaji na wengine wenye shughuli ndogondogo n.k kuanzisha biashara zao pasipo kuwepo changamoto ya kudaiwa kodi ndani ya mwaka mmoja, muda huo unatoa fursa ya kujiimarisha katika biashara wanazozianzisha. Mheshimiwa tumetolea mfano kwa wafugaji wenye ndama wao ili waweze kuwakuza na kufanya biashara.

 

Kukamilisha Miradi na Programu za Maendeleo

 

35.        Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuweka nafuu mbalimbali za kikodi zinazochochea matumizi ya nishati ya umeme na gesi asilia majumbani na katika sekta ya usafiri ili kukabiliana na athari kutokana na migogoro mashariki ya kati. Hivyo, Serikali itasamehe kodi kwenye vifaa vitakavyotumika katika vituo vya kuchaji magari yanayotumia umeme na kupunguza ushuru wa forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 10. Nitoe rai kwa wawekezaji na sekta binafsi kwa ujumla watumie fursa hiyo kuagiza mashine na vipuri vitakavyotumika kwenye vituo hivyo.

 

Kuendelea Kuimarisha Sekta za Uzalishaji

 

36.        Mheshimiwa Spika, katika kutambua kuwa sekta ya kilimo nchini inabeba makundi mengi katika uzalishaji na biashara, Serikali imeweka vivutio mbalimbali vya kikodi ili kuhamasisha kilimo na matumizi ya mbegu za mafuta zinazozalishwa nchini. Aidha, nafuu hii ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa hii kwa gharama nafuu na kulinda viwanda vya ndani vinavyochakata na kuzalisha mafuta ya kula yanayotokana na michikichi, soya, karanga pamoja na nazi.

 

37.        Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuweka mazingira bora kwa kuhakikisha viwanda vya ndani vinazalisha na kuwa shindani dhidi ya bidhaa zinazoingizwa nchini. Hatua hiyo, ni sehemu ya kuongeza kiwango cha Ushuru wa Forodha kwenye bidhaa mbalimbali zinazoagizwa kutoka nje ya nchi kwa lengo la kulinda viwanda vya ndani na kuhamasisha uwekezaji nchini.

 

38.        Mheshimiwa Spika, niendelee kutoa rai kwa Watanzania wote, kutumia nafuu hizi za kikodi zilizotolewa na Serikali kufuatia hotuba nzuri iliyotolewa na Waziri wa Fedha kwa kuongeza uwekezaji katika sekta ya uzalishaji kuliko kufuata faida binafsi. Hatua hii, itaendelea kutanua wigo wa kutoa ajira kwa vijana ambao kwa sehemu kubwa ndio wamekuwa kwenye changamoto ya ukosefu wa ajira.

 

Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini

 

39.        Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa sekta ya biashara na uwekezaji nchini, Serikali imefanya maboresho katika sheria 55 ambapo pamoja na mambo mengine ada na tozo 374 zimepunguzwa au kufutwa. Lengo la hatua hiyo, ni kupunguza gharama za kufanya biashara, kuimarisha mazingira ya uwekezaji pamoja na kuongeza usajili wa biashara na uwekezaji hapa nchini. Hizi ni hatua muhimu za kuweka mazingira muhimu ya uzalishaji na kutoa tozo.

 

40.        Mheshimiwa Spika, serikali imezingatia maoni ya waheshimiwa wabunge kuhusu kero ya wingi wa ada, tozo na adhabu zinazotolewa na mamlaka za udhibiti  wa ufanyaji biashara na uwekezaji. Hivyo, Serikali imedhamiria kuanzisha mfumo jumuishi ili kutatua kero hizo bila kuathiri majukumu ya msingi yanayofanywa na taasisi za udhibiti.

 

Sekta za Kimkakati Zilizoongezewa Fedha

 

41.        Mheshimiwa Spika, Serikali imetoa fedha zaidi kwa baadhi ya sekta za kimkakati ili kuziwezesha kukamilisha miundombinu na kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu karibu na maeneo ya wananchi. Lengo ni kukamilisha miundombinu ya Reli ya SGR,  ujenzi wa barabara, upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam na viwanja vingine. Pia, itashusha gharama za usafiri na usafirishaji na kuleta unafuu kwa mwananchi. Tutaweka nguvu kubwa kwenye vipande vya reli ambavyo hajakamilika ili mpaka mwaka 2030 tuna na treni kutoka da es salaam hadi mwaza.

 

42.        Mheshimiwa Spika, katika sekta ya madini, serikali imetenga fedha za kuweka mazingira wezeshi kwenye ujenzi wa viwanda vya kusafisha dhahabu, nickel, graphite, uranium na uboreshaji wa ramani za kina za madini nchini. Hatua hiyo itavutia uwekezaji na kusaidia wachimbaji wadogo kupata masoko, teknolojia na kuacha kuuza madini ghafi yanayopunguza thamani ya madini yao.

 

Hali ya Upatikanaji wa Nishati ya Mafuta Nchini

 

43.        Mheshimiwa Spika, nimpongeze waziri wa sekta na Serikali itaendelea kusimamia  mpango wa kupunguza makali ya nishati ya mafuta. tangu kuanza kwa vita Mashariki ya Kati Serikali ilichukua hatua za haraka kuhakikisha nishati ya mafuta inapatikana nchini. Serikali ilitoa ruzuku ya shilingi bilioni 50 kwa mwezi Mei, 2026 na shilingi bilioni 90 kwa mwezi Juni, 2026 ili kuwa na bei himilivu tofauti na ilivyotarajiwa endapo ruzuku isingekuwepo. Serikali itaendelea kufanya tathmini ya mwenendo wa bei za mafuta katika soko la dunia na kuchukua hatua stahiki ili kupunguza athari na kuhakikisha upatikanaji wa mafuta wakati wote.

 

Kuimarisha Mtiririko wa Fedha katika Mifuko ya Miradi ya Maendeleo

 

44.        Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwapongeza waheshimiwa wabunge kwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wananchi katika majimbo yao wanapata maendeleo kwenye sekta mbalimbali ikiwemo maji, barabara na umeme. Kwa umahiri mkubwa, waheshimiwa wabunge wameishauri Serikali kuchukua hatua za haraka kuwezesha sekta hizo kupata fedha kwa wakati.

 

45.        Mheshimiwa Spika, Serikali imepokea ushauri huo na itaendelea kuboresha utaratibu wa utoaji wa fedha hizo kama ilivyoshauriwa. Kwa sasa asilimia 70 ya fedha za mifuko ya maendeleo zitaelekezwa moja kwa moja kwenye mifuko husika ili uweze kutekeleza majukumu yake ya kimsingi. Uamuzi huo utaongeza kasi na uhakika wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kupanua wigo wa huduma za jamii na kuongeza fursa za uzalishaji.

 

46.        Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwakumbusha watendaji wa Taasisi ambazo zitapelekewa fedha hizo kuhakikisha wanakamilisha miradi iliyokusudiwa tena kwa kuzingatia thamani ya fedha na miradi iwe na uimara. Wakumbuke kuwa dhamira na maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kutekeleza kikamilifu miradi ya maendeleo kwa ajili ya ustawi wa Watanzania. Serikali itachukua hatua kwa watendaji wote ambao watashindwa kutekeleza maelekezo hayo.

 

47.        Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Serikali, Wabunge na Watanzania wote, ninaomba nitoe shukrani za pekee kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo kwa uwazi na uwajibikaji. Tumuombee Mungu aendelee kuwa na afya njema na hekima zaidi ili aendelee kuiongoza nchi yetu kwa mafanikio makubwa.  Ameendelea kuziongezea fedha taasisi za ukaguzi ili waendelee kufanya ukaguzi wakati miradi inaendelea ikiwa ni dhamira ya kuleta ustawi kwa watanzania.

 

Masuala ya Ardhi

48.        Mheshimiwa Spika, katika ziara nilizofanya maeneo mengi nchini, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusiana na migogoro ya ardhi. Baadhi ya masuala yao yalifikishwa kwenye Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya lakini hayakupata ufumbuzi kamili. Itakumbukwa kwamba, Mfumo wa Mabaraza ya Ardhi ulianzishwa miaka ya nyuma wakati mahakama za hakimu mkazi na wilaya zikiwa chache katika maeneo mengi.

 

49.        Mheshimiwa Spika, kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali ya awamu ya sita, sote tumeshuhudia ongezeko kubwa la mahakama za wilaya hapa nchini. Ili kuongeza ufanisi wa kushughulikia maamuzi ya migogoro ya ardhi, katika mkutano ujao wa Bunge, Serikali itawasilisha mapendekezo ya kuhamishia masuala hayo kutoka Mabaraza ya Ardhi kwenda kwenye mfumo rasmi wa mahakama. Nitoe rai kwa watanzania wote tuache kuaminiana na kutoa ardhi bila ya kufuata misingi ya kisheria.

 

Masuala ya Utoaji Haki

 

50.        Mheshimiwa Spika, pia kwa nyakati mbalimbali, nimepokea changamoto wanazokutana nazo baadhi ya wafugaji kwa mifugo yao kutaifishwa baada ya kukamatwa kwenye maeneo yaliyohifadhiwa wabunge wengi wameongelea suala hilo. Baada ya mashauri haya kuhitimishwa katika vyombo vya sheria kwa wafugaji kupata ushindi na kuamriwa warejeshewe mifugo yao, taasisi husika hazijatekeleza maamuzi ya mahakama na kuishia kuwaambia mifugo yao imekufa, imepokea ama sababu nyingine. Vitendo hivi vinaidhoofisha sekta ya mifugo na kuwaacha wananchi hawa katika ufukara.

 

51.        Mheshimiwa Spika, Ili kuimarisha misingi ya utawala wa kisheria na utoaji haki kwa wananchi, kupitia mkutano ujao wa bunge, Serikali itawasilisha mapendekezo ya marekebisho ya sheria zinazosimamia utaifishaji mifugo na mali kwenye maeneo yaliyohifadhiwa tunakwenda kuifuta sheria inayotaifisha mifugo ya watanzania. Kwa sasa, Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii wahakikishe wanatekeleza maamuzi yaliyotolewa na mahakama ya kuwarejeshea  wananchi mifugo yao na kama mifugo hiyo ilikufa au kupotea walipe fidia kwa mifugo iliyopotea.

 

Ukamataji wa Mali na Mitaji ya Wajasiriamali

 

52.        Mheshimiwa Spika, katika maeneo mengi nchini, kumejitokeza vitendo vya baadhi ya watendaji wa mamlaka za udhibiti na usimamizi wa sheria kunyang’anya bidhaa, mitaji na vitendea kazi vya wajasiriamali mbalimbali. Vitendo hivi, havikubaliki na vinarudisha nyuma jitihada za wananchi kujikwamua kiuchumi, licha ya serikali kuweka mazingira mazuri ya kuwawezesha wananchi hao waweze kutekeleza majukumu yao. Kama msimamizi wa shughuli za kiserikali nitaendelea kuchukua hatua kali ili kukomesha tabia hii.

 

53.        Mheshimiwa Spika, niendelee kusisitiza maelekezo ya serikali kwa watendaji kuheshimu jasho la mtanzania, shughuli zainazofanywa na mtanzania, mitaji na shughuli zinazofanywa na wajasiriamali kote nchini. Dosari zozote zinazojitokeza katika shughuli zao zishughulikiwe kwa kutumia njia zisizohusisha kukamata mali  na mitaji yao isipokuwa kwa makosa ya kijinai na yanayohatarisha usalama.

 

5.0        UWAJIBIKAJI WA WATUMISHI WA UMMA

 

Mahusiano ya Viongozi na Watendaji

 

54.        Mheshimiwa Spika, ili utoaji wa huduma kwa wananchi na utekelezaji wa shughuli za Serikali  vifanyike kwa ufanisi, ni muhimu sana kwa  viongozi, watendaji na watumishi wote kuwa na mahusiano mazuri katika dhana hii ya uwajibikaji. Hali hiyo itachangia kuepusha migogoro na migongano baina ya viongozi, watendaji na watumishi, na hivyo kupunguza tija katika shughuli za serikali na kuwahudumia wananchi.

 

55.        Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba serikali imeanza kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025 na kuanzia tarehe 01 Julai 2026, Serikali itaanza kutekeleza rasmi Dira 2050 na ndio kwa mara ya kwanza tuanenda kutekeleza Bajeti ya Kwanza ya Serikali ya Awamu ya Sita. Hivyo ni wajibu wa kila mmoja kujielekeza katika kuwezesha wananchi kupata manufaa ya mipango ambayo imesomwa na Waziri wa Mipango. Viongozi waepuke kuendeleza makundi na makovu ya uchaguzi uliopita na kupanga safu za uchaguzi  ujao. Hali hiyo inaweza kuchochea migogoro itakayosababisha kuchelewesha utekelezaji wa Ilani na kutoa huduma bora kwa wananchi.

 

Muda wa Uongozi wa Naibu Meya na Makamu Mwenyekiti

 

56.        Mheshimiwa Spika, katika usimamizi wa shughuli kwenye mamlaka za serikali za mitaa, kila mwaka serikali inaingia gharama za uchaguzi ambapo viongozi na watendaji kuwa katika mchakato wa uchaguzi. Mazingira hayo yanazorotesha utendaji, yanachochea migongano na kuondoa utulivu kwenye mamlaka za serikali za mitaa.

 

57.        Mheshimiwa Spika, ninapenda kulijulisha Bunge lako tukufu katika mkutano ujao, Serikali itawasilisha mapendekezo ya marekebisho ya sheria kuhusu nafasi za Naibu Meya na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri. Tuaondoa uchaguzi kufanyika kila mwaka. Lengo ni kubadilisha mfumo wa sasa na kuwa na Naibu Meya na Makamu Mwenyekiti kuwa kiongozi kwa kipindi chote cha uhai wa Baraza la Madiwani. Marekebisho hayo yanatarajia kuleta utulivu, viongozi wajikite katika kufanya kazi na kujiekeleza kwenye shughuli za maendeleo ya wananchi katika maeneo yao. Mambo ya safu na kuwaza uongozi ni ubinafsi.

 

Utatuzi wa Kero za Wananchi

 

58.        Mheshimiwa Spika, ziara za viongozi wa kitaifa katika maeneo mbalimbali nchini ni sehemu ya majukumu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa shughuli za serikali ikiwemo utoaji wa huduma bora kwa wananchi. Katika ziara hizo wananchi wengi wamekuwa wanajitokeza kuwasilisha kero mbalimbali. Baadhi ya kero hizo, ilitarajiwa ziwe zimetatuliwa na viongozi waliopo kwenye mamlaka za serikali za mitaa.

 

59.        Mheshimiwa Spika, ninawakumbusha viongozi na watumishi wote wa umma kwamba utatuzi wa kero za wananchi ni sehemu ya majukumu yao ya kila siku. Aidha, ziara za viongozi wa Kitaifa ikiwemo ziara ya Waziri Mkuu siyo mbadala wa kutoa huduma hizo kwa wananchi. Hivyo ninatoa maelekezo yafuatayo:

 

Mosi:   Wizara, Idara, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zihakikishe Mifumo iliyopo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kuanzia ngazi ya mtaa/kijiji inatoa huduma kwa wananchi ipasavyo;

Pili:     Viongozi waendelee kutekeleza majukumu yao badala kusubiri teuzi “PDF/MKEKA”. Suala la uteuzi lisiathiri utendaji kazi na dhamana ambazo zimetolewa na mamlaka ya uteuzi. Mamlaka inaendelea kufanya tathmini na wote wasiotimiza wajibu wao ipasavyo ikiwemo kuwahudumia wananchi watachukuliwa hatua; na

Tatu:   Viongozi na watendaji katika kila ngazi wasimamie na kutekeleza kwa ukamilifu maagizo na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na viongozi wa kitaifa ikiwemo kwenye ziara ikiwemo kutatua na kusikiliza kero za wananchi. Taasisi zote zitenge muda wa kusikiliza changamoto za utoaji huduma katika maeneo yao. Ufuatiliaji unaendelea kufanyika na viongozi  watapimwa kwa namna wanavyotekeleza maagizo hayo.

 

Wananchi Kuzingatia Mifumo ya Serikali

60.        Mheshimiwa Spika, ninatoa rai kwa wananchi wote kuwa pamoja na uwepo wa ziara za viongozi wa kitaifa kwenye maeneo yao, waithamini, waiamini na kuitumia mifumo ya kiutawala iliyopo nchini ili kupata utatuzi wa kero na malalamiko mbalimbali. Ziara tunazofanya sio mbadala wa mifumo rasmi iliyopo hivyo wasisubiri ziara za viongozi wa kitaifa.

 

61.        Mheshimiwa Spika, Nina hakika Wizara, Idara, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmshauri na watendaji wengine wanao uwezo wa kutatua kero mbalimbali. Mheshimiwa Rais amewapa dhamana ya kuwawakilisha kwenye maeneo yaliyopo watimize wajibu wao.

 

62.        Mheshimiwa Spika, sambamba na mifumo hii ya kiutawala iliyopo, Serikali imeweka mifumo ya kieletroniki kwa ajili ya wananchi kuwasilisha kero na maoni mbalimbali Serikalini. Mifumo hiyo ni pamoja na e-mrejesho, e-kiongozi, sema na waziri (wizara mbalimbali), pamoja na Kituo cha Kitaifa cha Mawasiliano ya Simu (Call Center).

 

63.        Mheshimiwa Spika, nilielekeza kituo cha mawasiliano ya simu (call center) kuwepo kimeongeza wigo wa kuwafikia wananchi bila kuingia gharama. Kituo hicho kilichopo chini ya ofisi yangu kunawezesha wananchi kuwasiliana moja kwa moja na Serikali kwa lengo la kutoa taarifa, kero, malalamiko na maoni kuhusu huduma zinazotolewa na Wizara, Idara na Taasisi za Serikali.

 

64.        Mheshimiwa Spika, huduma hiyo ni ya bure na inapatikana kupitia chaguo la pili baada ya kupiga namba 180 na mwananchi anaweza kutuma ujumbe mfupi wa maneno, kuongea na kuambatisha picha mnato, picha mjongeo (video clip) na nyaraka. Kupitia kituo hiki wananchi wanapatiwa majibu ya moja kwa moja au kuunganishwa kwenye taasisi husika kulingana na hoja iliyotolewa.

 

6.0        MAELEKEZO MAHSUSI

 

Kuzingatia Utekelezaji wa Vipaumbele vya Bajeti Mpya

 

65.        Mheshimiwa Spika, Mkutano wa Tatu wa Bunge la 13 ulikuwa mahsusi kwa ajili ya kujadili na kupitisha Bajeti na Mipango ya Serikali. Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa 2026/2027 ni nyenzo ya kwanza katika kutekeleza Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027- 2030/2031 ambao unatafsiri kwa vitendo Dira 2050.

 

66.        Mheshimiwa Spika, Bajeti iliyopitishwa na Bunge lako inalenga kuimarisha miundombinu, kuongeza uzalishaji, kuboresha huduma za kijamii, na kuhamasisha uwekezaji wa ndani ili kufikia uchumi shindani na ustawi wa wananchi. Ili kufanikisha azma hii, tutaendelea kusimamia yale ambayo Waziri wa Fedha ameyatolea ufafanuzi.

 

Wito kwa Wadau Kushiriki Katika Maandalizi ya Mapokezi ya Wanafunzi Wanaotarajiwa Kujiunga Kidato cha Kwanza Mwaka 2028.

 

67.        Mheshimiwa Spika, Hili ni badiliko la kihistoria baada ya ya lile la Mwalimu nyerere kuongeza muda wa elimu ya msingi. Serikali inaendelea na maandalizi muhimu ya kupokea wanafunzi 3,021,177 wa makundirika mawili yanayotarajiwa kujiunga na elimu ya sekondari ifikapo mwaka 2028. Takriban kata 315 zimebainika kuwa na changamoto ya msongamano wa wanafunzi kutokana na uchache wa miundombinu.

 

68.        Mheshimiwa Spika, shilingi trilioni 1.7 zinahitajika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu kabla ya Januari, 2028. Hivyo, ninatoa wito kwa wadau wote wa elimu kushiriki kikamilifu katika kufanikisha maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi wa makundirika mawili mwaka 2028. Kila mmoja wetu anayo nafasi ya kuchangia mabadiliko haya ili kufikia azma ya kupata miundombinu muhimu na kuweza kuhudumia wanafunzi tarajiwa.

 

7.0        USALAMA, AMANI NA UTULIVU

 

69.        Mheshimiwa Spika, uwepo wa amani umeendelea kuwa msingi muhimu wa shughuli za kiuchumi, kijamii na kisiasa, hivyo kuifanya nchi kuendelea kuvutia uwekezaji na kuimarisha ustawi wa wananchi. Watanzania tunao wajibu wa kutunza hali hii bila kujali tofauti zetu za kisiasa, kidini au kikabila.

 

70.        Mheshimiwa Spika, nitoe rai kwa kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa analinda na kuitunza tunu ya amani na utulivu wa nchi yetu. Nawasisitiza Watanzania wenzangu tuendelee kulinda amani tuliyoirithi kwa wazee wetu kwa kuzingatia sheria, kuheshimu haki za wengine na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kusababisha migawanyiko. Tuzingatie matumizi ya lugha ya staha katika mijadala ya kijamii na kisiasa kwani yana mchango mkubwa katika kuvunja mshikamano wa kitaifa. Amani ikivunjika, hakuna anayejihakikishia usalama, hasa hasa wale wanaoishi nje ya Tanzania waituongoze kuvunja amani ya nchi yetu. Tusidanganyane amani, ulinzi na usalama sio suala la kujadiliwa.

 

71.        Mheshimiwa Spika, Tanzania imeendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki katika masuala ya kisiasa kwa njia ya amani na ustaarabu. Demokrasia inatoa nafasi kwa watu kutoa maoni yao, kuchagua viongozi na kushiriki katika maendeleo ya Taifa kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.

 

72.        Mheshimiwa Spika, sina shaka mtakubaliana nami kuwa kuendesha siasa za kistaarabu ni msingi wa kuimarisha amani na demokrasia. Viongozi wa vyama vya siasa, wafuasi wao pamoja na wananchi kwa ujumla wanapaswa kujenga utamaduni wa kuheshimu tofauti za mawazo, kuepuka lugha za uchochezi na kuweka mbele maslahi ya Taifa letu.

 

73.        Mheshimiwa Spika, unapotaja suala la uendelezaji wa demokrasia nchini Tanzania, huwezi kuliongelea jambo hili bila kugusia jitihada binafsi za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wakati wote amekuwa kinara katika kuimarisha demokrasia, haki za binadamu na utawala bora. Katika kipindi chote cha uongozi wake, tumeshuhudia utekelezaji falsafa yake ya 4R yaani maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na mabadiliko ambayo kwa hakika yamekuwa chachu ya kuimarisha siasa za ndani ya nchi yetu.

 

74.        Mheshimiwa Spika, kutokana na utashi wake huo, sote tumeshuhudia nchi yetu ikiendelea kuwa na mshikamano, amani na umoja wa kitaifa. Hii ni kutokana na msisitizo wake kuhusu utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu, utawala bora na demokrasia. Isitoshe, tumeshuhudia maboresho mbalimbali ya upande wa mifumo, sheria na uendeshaji wa shughuli za kisiasa.

 

75.        Mheshimiwa Spika, vilevile, tumeshuhudia uwepo wa fursa zaidi za mijadala na maridhiano miongoni mwa makundi ya wadau wa demokrasia na masuala ya siasa. Ni lazima tukubali kuwa kupitia kuimarisha maridhiano baada ya uchaguzi, kuendeleza demokrasia na kuendesha siasa za kistaarabu, Taifa linaweza kuendelea na kustawi kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.

 

76.        Mheshimiwa Spika, kabla sijamaliza eneo hili, ninaomba kumnukuu aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Mandela ambaye katika uhai wake alifafanua vizuri sana suala la maridhiano kwa maneno yafuatayo:

 

In the end, reconciliation is a spiritual process, which requires more than just a legal framework. It has to happen in the hearts and minds of people.”  Mwisho wa kunukuu.

 

77.        Mheshimiwa Spika, kwa tafsiri isiyo rasmi, Mzee wetu Mandela alimaanisha kuwa: “... upatanisho ni mchakato wa kiroho, ambao unaenda ndani zaidi ya mfumo wa kisheria. Unapaswa kudhihirika katika mioyo na akili za watu.”

 

78.        Mheshimiwa Spika, ninaendelea kuamini kwamba bila kujali tofauti zetu za kifikra, kiitikadi na imani zetu na hata kama tukifarakana na kutofautiana kiasi gani, namna pekee ya kuonesha uzalendo na mapenzi mema kwa nchi yetu ni pale tunapokubali kuwa tayari kukaa kwenye meza ya mapatano na huo ndiyo uongozi, uzalendo na ukomavu wa kisiasa. Tunapaswa kuijali nchi yetu kwanza kwa kukaa kwenye meza ya maridhiano na kutanguliza utaifa wetu kwanza.

 

79.        Mheshimiwa Spika, amani, utulivu na mshikamano wa Taifa hili si vitu vya kuchezewa kwani vimejengwa kwa jasho, uzalendo, damu na hekima za waasisi wetu. Kwa namna yoyote ile hatutaruhusu viharibiwe kwa tamaa za kisiasa au maslahi ya wachache. Tanzania ni nchi yetu sote, na hatutakuwa tayari kuona mtu yeyote, kikundi chochote au maslahi yoyote yakilitumbukiza Taifa letu katika mgawanyiko, vurugu au machafuko.

 

80.        Mheshimiwa Spika, umoja wa Watanzania si jambo la mjadala; ni msingi wa uwepo wa Taifa letu na ni wajibu wa kila mmoja kuutunza. Hivyo, tuipende, tuilinde na kuipigania nchi yetu na tusikubali kugawanyika kwa misingi ya rangi, ukabila, dini au ukanda ili tuendelee kuwa na amani na kufikia kiwango cha juu cha ustawi na maendeleo.

 

81.        Mheshimiwa Spika, suala la usalama, amani na utulivu ni kipaumbele namba moja na hakuna mjadala katika hilo. Niwahakikishie waheshimiwa wabunge na wananchi kwa ujumla, vitendo vya uvunjifu wa amani, uchochezi na fujo za aina yoyote havitavumiliwa na mamlaka husika. Hatua stahiki zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

 

82.        Mheshimiwa Spika, ninawasihi Watanzania wote kuheshimu misingi ya utawala bora na kuhakikisha shughuli mbalimbali za kijamii, kiutamaduni, kidemokrasia na kisiasa zinaendelea kufanyika kwa kuzingatia sheria, taratibu, mila, desturi na Katiba ya nchi yetu.  Aidha, Serikali iko Imara na itaendelea kutimiza kikamilifu wajibu wa kulinda mipaka ya nchi yetu, usalama wa raia, mali na tunu za Taifa ikiwemo umoja, amani, mshikamano na muungano.

 

8.0        MICHEZO

 

83.        Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa sekta ya michezo, serikali ya awamu ya sita imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali na kuchukua hatua mahsusi za kuinua sekta hii muhimu kwa uchumi wa Taifa letu.  Baadhi ya mikakati hiyo ni pamoja na kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Michezo, kuanzisha Tuzo za Michezo za Baraza la Michezo la Taifa kwa lugha nyingine “National Sports Council Sports Awards”, Kuziwezesha Timu za Taifa kushiriki mashindano mbalimbali, kuimarisha miundombinu ya michezo na kutenga fedha kupitia bajeti.

 

84.        Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuratibu mashindano ya UMMISETA na UMITASHUMTA kwa lengo la kuinua vipawa vya watoto na kuendelea kuvilea. Hatua hiyo inatekelezwa sambamba na kuwekeza kwenye akademia za michezo, kuwezesha makundi maalum kushiriki katika mashindano mbalimbali pamoja na kuhamasisha mashindano ya michezo kuanzia ngazi za chini kuratibu na kuwezesha mashindano ya kimataifa kwa timu chini ya miaka 18.

 

85.        Mheshimiwa Spika, licha ya kutoa burudani, sekta ya michezo imekuwa na mchango mkubwa katika kutoa ajira kwa vijana, kujenga umoja wa kitaifa, kuitangaza nchi yetu na kuvutia utalii, kuimarisha uchumi endelevu na kuchangia Pato la Taifa. Vilevile, inao mchango mkubwa katika kuimarisha afya lakini pia, kupunguza gharama za matibabu kwa maradhi yasiyoambukiza. Kutokana na umuhimu huo sekta ya michezo imeendelea kuwa moja ya sekta za kipaumbele cha serikali.

 

86.        Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine, mafanikio ya sekta ya michezo yametokana na uwepo wa utashi mkubwa wa kuendeleza michezo wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Wakati wote mwelekeo wake ni kwamba michezo si burudani pekee bali ni nyenzo muhimu ya maendeleo endelevu na diplomasia ya nchi. Mwelekeo huu unaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa yenye sekta ya michezo imara Barani Afrika.

 

87.        Mheshimiwa Spika, kutokana na hatua hizo, vilabu vyetu vimeendelea kung’ara katika mashindano mbalimbali kikanda na kimatifa na kuliwezesha Taifa letu kuwa na mvuto wa kipekee katika tasnia ya michezo. Licha ya vilabu, wanamichezo wetu wameendelea kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali. Nitumie nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa wanamichezo wetu waliofanya vizuri na kuibuka kidedea katika mashindano hayo.

 

88.        Mheshimiwa spika, ninatoa pongezi kwa Timu ya Taifa ya Wanawake chini ya miaka 20 (Tanzanite Queens) kwa kufuzu kihistoria kushiriki Kombe la Dunia la FIFA la Wanawake litakalofanyika nchini Poland kuanzia tarehe 5 hadi 27 Septemba, 2026. Vilevile, Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu wanawake “Twiga Stars” imefuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON 2026) yatakayofanyika mwezi Julai, 2026 nchini Morocco.

 

89.        Mheshimiwa Spika, vilevile, ninaipongeza timu ya Taifa ya Vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Boys) kwa kufanikiwa kufuzu Fainali za Kombe la Dunia za FIFA 2026 zitakazofanyika nchini Qatar kuanzia tarehe 19 Novemba hadi 13 Desemba 2026. Timu hiyo pia ilimaliza mshindi wa pili katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Vijana (AFCON U-17) zilizomalizika Juni 2026 nchini Morocco. Mafanikio hayo ni kielelezo cha uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika kuwekeza kwenye ukuzaji wa vipaji vya michezo kuanzia ngazi za chini.

 

90.        Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mchezo wa ngumi, ninatoa pongezi kwa Bondia Ibrahim Class ambaye amefanikiwa kutwaa mikanda miwili mikubwa ya WBC. Mikanda hiyo ni WBC International Silver Belt na WBC International Gold Belt katika uzito wa Super Featherweight. Mikanda hiyo imeweka historia kubwa kwenye nchi yetu.

 

91.        Mheshimiwa Spika, sambamba na ushindi katika michezo hiyo, Klabu ya Mpira wa Kikapu ya Dar City ilifuzu na kushiriki mashindano ya Basketball Africa League (BAL) kwa mara ya kwanza yaliyofanyika Mwezi Mei 2026 Kigali, Rwanda. Timu hiyo ilifanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

 

9.0        SHUKRAN NA KUTOA HOJA

 

92.        Mheshimiwa Spika, leo tunapoenda kuhitimisha Mkutano wa Tatu wa Bunge la 13, nimshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt, Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Dkt. Emmanuel Jihn Nchimbi, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Huseni Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na mwenyekeiti wa Baraza la Mapinduzi. Pia nikushurkuru wewe mwenye Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge.

 

93.        Mheshimiwa Spika, nina kila sababu ya kuwashukuru wote waliowezesha kufanikisha kwa njia moja au nyingine majukumu yangu kwa mujibu wa ratiba iliyokuwa imepangwa. Kwa dhati ya moyo wangu ninawashukuru viongozi na watendaji wote wa Serikali kwa kazi kubwa waliyoifanya.

 

94.        Mheshimiwa Spika, kipekee nimshukuru Mheshimiwa Prof. Palamagamba Aidan Mwaluko Kabudi, Mbunge wa Kilosa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu); Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Kwela na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano); Mheshimiwa Prof. Riziki Silas Shemdoe, Mbunge wa Lushoto na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) pamoja na Naibu Mawaziri wote. Hakika nyote mmekuwa msaada mkubwa kwangu wakati wote nilipokuwa nikitekeleza majukumu ya serikali.

 

95.        Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii pia, kuwashukuru sana Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri wa kisekta kwa kazi nzuri mliyoifanya ya kujibu maswali yote yaliyoulizwa na kutoa ufafanuzi wa hoja mahsusi zilizowasilishwa wakati wote wa Mkutano huu wa tatu na mijadala ya bajeti. Vilevile, ninatoa shukrani kwa Wakuu wote wa Mikoa, kwa ushirikiano mkubwa mlionionesha wakati wa kutekeleza majukumu yangu. Ninawapongeza pia, Makatibu Tawala wa Mikoa yote ambao mlikuwa mkifanya kazi bega kwa bega na Wakuu wa Mikoa kuhakikisha majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu yanatekelezwa kikamilifu.

 

96.        Mheshimiwa Spika, ninatoa shukrani zangu za dhati kwa watendaji wakuu na watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu. Nikianza na Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Wakurugenzi, na Wafanyakazi wote kwa ushirikiano mkubwa wanaonipatia katika kutekeleza majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

 

97.        Mheshimiwa Spika, ninamshukuru sana Balozi Dkt. Moses Mpogole Kusiluka, Katibu Mkuu Kiongozi, kwa ushirikiano wake wakati wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali na amekuwa kiungo muhimu kwenye kutekeleza majukumu ya Serikali. Ninawashukuru pia, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara zote pamoja na wakuu wote wa taasisi Wakurugenzi wa Halmashauri na Wakuu wa Mashirika, Wakala na Idara Zinazojitegemea kwa ushirikiano mkubwa walionipatia kwa kipindi chote cha Mkutano huu.

 

98.        Mheshimiwa Spika, kipekee ninamshukuru sana Mheshimiwa Hamza Saidi Johari, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa ushauri wake wa kisheria ambao umewezesha miswada yote ya kisheria kukamilishwa kwa weledi wa hali ya juu.

 

99.        Mheshimiwa Spika, ninatoa shukrani za dhati kwa  Ndugu Baraka Ildephonce Leonard, Katibu wa Bunge kwa kuhakikisha kuwa shughuli zote za ratiba ya Mkutano wa tatu zimekamilishwa kama sote tunavyoshuhudia leo. Ninawashukuru pia, wafanyakazi wote wa Ofisi ya Bunge kwa kuhudumia vema Mkutano huu. Sina shaka Waheshimiwa Wabunge mtakubaliana nami kwamba Mkutano huu umeendeshwa kwa weledi wa hali ya juu.

 

100.     Mheshimiwa Spika, ninatoa pongezi kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vikiongozwa na Mwenyekiti wao CDF Jenerali Jacob John Mkunda na Wakuu wengine wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama. Ni jambo la faraja na la kujivunia kuona kuwa sote tumekuwa salama katika kipindi chote cha Mkutano huu. Amani na utulivu tulioupata wakati wa kutekeleza majukumu ya Bunge ni kwa kuwa wapo wenzetu waliofanya kazi usiku na mchana kuhakikisha usalama wetu. Kwa dhati ya moyo wangu ninawashukuru sana. 

 

101.     Mheshimiwa Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa George Mcheche Masaju, Jaji Mkuu wa Tanzania kwa kutekeleza msingi ya uwajibikaji katika utoaji haki. Kadhalika, ninawapongeza watendaji wote wa Mahakama kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya ya kuwahudumia wananchi na kuhakikisha haki inapatikana kwa wote.

 

102.     Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa wananchi wa Jimbo la Iramba Magharibi kwa mambo mengi sana. Kwanza, kwa kuendelea kuniunga mkono wakati wote ninapotekeleza majukumu yangu. Pili, kwa uvumilivu mkubwa walionao kwa kipindi chote ninapokuwa katika maeneo mengine nikiwahudumia Watanzania. Kadhalika, kwa kuendelea kutoa ushirikiano na kuonesha mshikamano na viongozi wote wanaonisaidia kutekeleza majukumu yangu jimboni.

 

103.     Mheshimiwa Spika, kwa moyo wa upendo ninatoa shukrani kwa familia yangu. Ama kwa hakika wamekuwa chanzo kikuu cha utulivu wakati ninapotekeleza majukumu yangu. Ninamshukuru mke wangu mpendwa Bi. Neema Mwigulu Nchemba pamoja na watoto wetu Joshua, Gracious, Isaac na Bernice kwa upendo wanaoendelea kuuonesha kwangu. Ahsanteni sana nami ninawapenda sana.

 

104.     Mheshimiwa Spika, ninatoa shukrani kwa viongozi wote wa madhehebu ya dini. Sina shaka Waheshimiwa Wabunge wote mtakubaliana nami kuwa tumefika hatma ya Mkutano huu muhimu kwa ustawi wa Taifa letu kwa kuwa wapo waliokuwa wanaomba kwa ajili yetu. Ahsanteni sana nami ninawasihi sana endeleeni kutuombea.

 

105.     Mheshimiwa Spika, ninatoa shukrani kwa wananchi wote wa Tanzania kwa ushirikiano wanaoendelea kuuonesha kwa serikali ya awamu ya sita. Pia, ninawashukuru sana kwa kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali kwa maendeleo ya Taifa letu.

 

106.     Mheshimiwa Spika, ninatoa shukrani kwa vyombo vya Habari, mitandao ya kijamii pamoja na wanahabari wote waliokuwa mstari wa mbele kuhakikisha umma wote unapata taarifa sahihi ya masuala muhimu yaliyojiri hapa bungeni. Kundi hili limefanya kazi kubwa na nzuri kwa kuwa licha ya kutangaza limefanya uchambuzi na kuwezesha umma kuelewa kwa mapana zaidi kuhusu bajeti inayohusu maisha yao ya kila siku.

 

107.     Mheshimiwa Spika, nikamilishe salamu zangu za shukrani kwa watumishi wote wa sekta ya umma na sekta binafsi kwa hakika mmefanya kazi kubwa na nzuri katika kuhakikisha Mkutano huu unahitimishwa kwa mafanikio makubwa. Ninawasihi sana endeleeni kufanya kazi kwa bidii, weledi na uadilifu, ninyi ni nguzo muhimu ya utekelezaji wa mipango na mikakati ya serikali, Ahsanteni sana.

 

108.      Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitatambua kazi kubwa iliyofanywa na madereva kwa kipindi chote cha mkutano huu. Ahsanteni sana kwa kufanya kazi kwa weledi na nidhamu ya hali ya juu. 

 

109.      Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, ninaomba sasa Bunge lako tukufu liahirishwe hadi tutakapokutana tena tarehe 25 Agosti, 2026 saa tatu kamili asubuhi hapa katika Ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma.

                

110.      Mheshimiwa Spika, ninaomba kutoa hoja.

 

 

 



Mbunge wa Bagamoyo Subnira Mgalu akiuliza mwongozo kuhusu mafuta




Waziri Ndejembi akijibu mwongozo wa Mgalu akisema mafuta yatashuka bei hivi karibuni


Waziri Katambi akipiga mafruku mikutano ya vyama vya kisiasa ikiwemo CCM
Makofi ya Waziri Katambi wakati akizungumza














 

Comments

Popular posts from this blog

WALIOPITA KURA ZA MAONI CCM HAWA HAPA

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?

WAZIRI MKUU MAJALIWA ASHIRIKI IBADA YA KUSIMIKWA ASKOFU