WABUNGE WAIPONGEZA MIFUKO YA JAMII YA PSSSF NA NSSF
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, akifungua warsha ya siku moja ya wabunge na maofisa wa mifugo ya NSSF na PSSSF iliyofanyika ukumbi wa Msekwa jijini Dodoma leo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Fortunatus Makore Magambo (pichani), amewataka Wabunge kuwa mabalozi wa bidhaa za ngozi zinazozalishwa nchini kwa kuzitumia na kuzitangaza, hatua itakayosaidia kukuza viwanda vya ndani, kuongeza ajira na kuimarisha uchumi wa taifa.
Akizungumza katika Ukumbi wa Msekwa leo Jun 15,2026 Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya shughuli na mafanikio ya Kiwanda cha Ngozi cha Kilimanjaro (Kilimanjaro International Leather Industries Company Limited - KLICL), Magambo amesema Tanzania ina uwezo mkubwa wa kuzalisha bidhaa bora za ngozi zinazoweza kushindana katika soko la kikanda na kimataifa kutokana na upatikanaji wa malighafi za kutosha na uwekezaji uliofanywa katika sekta hiyo.
Amesema KLICL, imeendelea kuwa miongoni mwa viwanda vikubwa vya uchakataji wa ngozi nchini kwa kuzalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo viatu, mikanda, mabegi na bidhaa nyingine zinazokidhi viwango vya ubora vya kimataifa.
“Tunawaomba Waheshimiwa Wabunge muwe mabalozi wa bidhaa za ngozi zinazozalishwa hapa nchini. Mkitumia na kuzitangaza, mtasaidia kujenga imani kwa wananchi na kuongeza soko la bidhaa zetu za ndani,” amesema Magambo.
Ameeleza kuwa matumizi makubwa ya bidhaa zinazozalishwa nchini yatasaidia kuongeza thamani ya mazao ya mifugo, kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda, kuongeza ajira kwa vijana na kuimarisha mapato ya fedha za kigeni kupitia mauzo ya bidhaa hizo nje ya nchi.
Magambo amesema kiwanda hicho kinaendelea kutekeleza mkakati wa kupanua masoko yake ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha uwezo mkubwa wa uzalishaji uliowekezwa unatumika kikamilifu. Alitaja masoko yanayolengwa kuwa ni pamoja na nchi za Afrika Mashariki na mataifa mengine kama China, Saudi Arabia, Italia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Misri, Pakistan na Uturuki.
Katika hatua inayoonyesha kuongezeka kwa ushindani wa bidhaa za ngozi za Tanzania katika soko la dunia, menejimenti ya KLICL ilieleza kuwa wanunuzi kutoka China tayari wameidhinisha sampuli za bidhaa zake, jambo linalotarajiwa kufungua fursa za oda kubwa zaidi katika siku zijazo.
Comments
Post a Comment