MKURUGENZI MKUU WA VETA, CPA ANTHONY MZEE KASORE KATIKA MKUTANO NA WANAHABARI LEO JIJINI DODOMA
Ndugu Wanahabari,
Awali ya yote napenda kuwashukuru kwa kuitikia wito wa kushiriki mkutano huu muhimu unaolenga kuhabarisha Watanzania kuhusu jitihada za Serikali katika uendelezaji ufundi stadi nchini na fursa zilizopo VETA kwa ajili ya kuwawezesha vijana na wananchi kwa ujumla kuajirika na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
Leo hatuzungumzii nadharia. Tunazungumzia maisha ya vijana kubadilika; Tunazungumzia ajira kuundwa; Tunazungumzia uchumi kujengwa kwa mikono ya Watanzania wenye ujuzi.
KUHUSU VETA
Ndugu wanahabari,
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ni Wakala wa Serikali iliyoanzishwa kwa Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Sura ya 82 ikiwa na majukumu ya utoaji, ugharamiaji na uratibu wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini. Kwa lugha rahisi zaidi, VETA ndiyo inazalisha watu wanaojenga Tanzania kwa vitendo. Nyumba tunazoishi, barabara tunazopita, umeme tunaotumia, mashine viwandani, huduma za utalii, teknolojia za kilimo, hadi matengenezo ya magari, yote yanategemea mafundi stadi. Ndiyo maana dira yetu ni: “Tanzania yenye Mafundi Stadi Mahiri na wa Kutosha,” na kaulimbiu yetu ni, “Ufundi Stadi, Fursa Kama Zote, Kwa Watu Wote.”
MSISITIZO WA SERIKALI YA AWAMU YA SITA KWENYE ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI STADI
Ndugu wanahabari,
![]()
![]()
Katika Serikali
ya Awamu ya Sita, chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, elimu ujuzi (Amali) imepewa nafasi ya
kipekee kama mhimili wa ajira, uzalishaji na maendeleo
ya Taifa.
![]()
![]()
Naomba
ninukuu maneno machache ya Mheshimiwa Rais katika Hotuba yake ya Ufunguzi wa Bunge la 13, tarehe
14 Novemba 2025, Dodoma.
![]()
“Kwa
kuwa zaidi ya asilimia 60 ya watu wa Nchi hii ni Vijana, tutaweka kipaumbele
kwenye sera na programu zitakazopanua fursa za kiuchumi, kutengeneza kazi na
ajira, kuongeza wigo wa hifadhi za jamii, na kuwajengea kesho iliyo bora zaidi.
…………..Vile vile, kupitia vyuo vyetu vya ufundi stadi, VETA, tutaongeza programu
maalum za mafunzo ya ufundi stadi na kuunganisha programu hizi na miradi ya
mikakati kama reli ya kisasa (SGR), uendelezaji wa bandari, uchumi wa buluu,
madini na gesi ili vijana hawa wapate uzoefu na waweze kuajirika… Aidha,
tutaweka mazingira ya kuhakikisha tunakuza vijana kwenye uongozi kwa kuwezesha
vyuo vyetu kufanya mafunzo ya ulezi na ukuzaji wa vijana viongozi
(mentorship).” Mwisho
wa kunukuu.
Kauli hii ni dira inayochora mustakabali wa Taifa. Hii ina maana kwamba Kijana anayepata ujuzi leo, anapata nafasi ya kazi kesho.
Katika
kutafsiri ahadi hii kuwa vitendo, VETA ndiyo inayobeba jukumu kuu la kutoa
elimu na mafunzo ya ufundi stadi, ambayo yanahitajika kwa umuhimu mkubwa katika
uzalishaji viwandani na kwenye sekta zote za kiuchumi kwa kuzingatia muelekeo
na maelekezo ya Mheshimiwa Rais.
JUHUDI ZA VETA KATIKA UENDELEZAJI UFUNDI STADI NA FURSA KWA VIJANA NA WANANCHI KWA UJUMLA
Ndugu wanahabari,
Serikali kupitia VETA imeongeza fursa za mafunzo ya ufundi stadi kwa kujenga na kupanua vyuo vya ufundi stadi, kuhuisha mitaala, na kubuni programu mahsusi za kuwawezesha vijana, wanawake, na makundi mbalimbali katika jamii kupata ujuzi utakao wawezesha kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za kiuchumi na kijamii hapa nchini.
Ø Ujenzi na Upanuzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi
Ndugu wanahabari,
VETA sasa ina vyuo 80 vilivyosambaa kote nchini, vikihudumia zaidi ya wanachuo 86,000 kwa mwaka. Huu ni mtandao wa matumaini unaogusa maisha ya maelfu ya vijana na wananchi wanaotafuta nafasi yao katika uchumi wa sasa na ujao. Serikali ina nia ya kuhakikisha kila Wilaya inakuwa na angalau chuo kimoja kinachomilikiwa na VETA. Ujenzi unaendelea katika wilaya 64 na kimoja cha mkoa wa Songwe (ujenzi huu unagharimu takribani bilioni 100), huku pia kukiwa na matarajio ya kukabidhiwa vyuo viwili kutoka halmashauri za wilaya za Bumbuli na Sengerema. Vilevile, maandalizi ya ujenzi wa vyuo vitano vya Kanda (TVET Polytechnics) yanaendelea. Matarajio ni kuwa, ifikapo mwaka 2027, VETA itakuwa na vyuo 152, hatua itakayoongeza udahili hadi wanafunzi 250,000 kwa mwaka.
Vilevile, VETA imeendelea kuongeza miundombinu ya vyuo vilivyopo, ikiwemo kujenga karakana mpya, mabweni na madarasa ili kuongeza udahili na fursa zaidi za mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana wa kitanzania.
Ø
Unyumbufu katika utoaji mafunzo ili kuwezesha kila mwenye
uhitaji kupata mafunzo ya ufundi stadi
Ndugu Wanahabari,
Msimamo wetu ni kwamba VETA ni ya wote, bila kujali kiwango cha elimu, jinsia, hali ya kimwili au mahali alipo mwananchi, pamoja na kuwa shirikishi. VETA imekuwa ikipanga na kutekeleza afua mbalimbali zinazolenga kufikia maono hayo yanayoenda sambamba na DIRA 2050, Sera ya Elimu na Mafunzo 2014 toleo la 2023, Mpango Mkakati wa Kuendeleza ujuzi nchini na Ilani ya CCM chama Tawala 2025.
Kwa sasa, VETA imefanya yafuatayo:
i) Uboreshaji wa utaratibu wa kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi
Mwaka huu VETA imefanya uboreshaji mkubwa katika taratibu za kujiunga na elimu na mafunzo ya ufundi stadi, ikiwemo kuondoa Mtihani wa Mchujo (Aptitude test). Uboreshaji huo umelenga kuongeza fursa kwa waombaji wengi zaidi, ambapo waombaji wote 18,875 wa mwaka huu wamechaguliwa kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi. Hadi kufikia Februari 10, 2025 jumla ya wanachuo 7, 952 wameripoti vyuoni.
ii) Kupunguza baadhi ya Masomo (Exemption) kwa Wenye Elimu ya Juu
Mwamko wa vijana wenye sifa za elimu mbalimbali kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi unaendelea kuongezeka. Mwaka huu jumla ya waombaji 134 kwenye vyuo vyetu walikuwa ni wahitimu wa Astashahada, Shahada, na Shahada za Uzamili waliodahiliwa katika mafunzo ya muda mrefu. Waombaji kwenye kundi hili wameondolewa masomo ambayo walishayasoma wakati wanajipatia elimu kulingana na taaluma zao, jambo linalowawezesha kuhitimu kwa muda mfupi zaidi na kuongeza idadi ya watanzania wenye ujuzi mahiri katika soko la ajira na kazi pamoja na kuweka motisha ya kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi. Mathalani, wale wenye shahada za uhandisi wameondolewa masomo kama Uchoraji wa Kiufundi (Technical Drawing) na Sayansi ya Kihandisi (Engineering Science) na wale wenye shahada za sanaa wameondolewa masomo kama stadi za mawasiliano.
Kwa kufanya hivyo, kutawawezesha kuhitimu mapema zaidi. Mathalani, badala kujifunza stadi za Ngazi ya Kwanza na ya Pili kwa miaka miwili, watafanya kwa mwaka mmoja tu.
Napenda kuwahamasisha
wahitimu wa vyuo vya elimu ya juu kutumia fursa hii kujiunga na vyuo vyetu ili
kupata stadi mbalimbali kwa ajili ya uendeshaji shughuli mbalimbali za
kiuchumi.
iii) Kukuza Ushiriki wa Wenye Mahitaji Maalum
Mpango wa VETA ni kuwezesha watu wenye mahitaji maalum, wakiwemo wenye ulemavu kupata fursa zaidi za kujiunga na kujifunza ufundi stadi. Serikali kupitia VETA inataka kuwezesha kundi hili kupata ujuzi, kuajiriwa au kujiajiri, hivyo kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Afua
mahsusi ambayo VETA imefanya mwaka huu ni kufadhili wanafunzi wote 195 wenye
ulemavu waliodahiliwa katika vyuo vya VETA kwa ajili ya mafunzo ya muda mrefu.
VETA itagharamia ada za mafunzo kwa miaka yote ya mafunzo, kuanzia Ngazi ya
kwanza hadi ya Pili.
Napenda kutumia fursa hii kuwahamasisha wazazi na walezi wa watoto wenye ulemavu kuwaleta watoto wao kwenye vyuo vyetu tushauriane ili nao wajiunge na mafunzo ya ufundi stadi, hivyo kupata ujuzi unaowawezesha kujikwamua kiuchumii na kimaisha kwa ujumla.
iv) Kuanzisha Mafunzo ya Jioni
Mpango wa VETA ni kuhakikisha inawafikia wananchi wengi zaidi katika kuwapa ujuzi na kuwawezesha kushiriki kikamilifu kwenye shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Tumeanzisha Mafunzo ya Jioni (Evening Session), ambapo jumla ya wanafunzi 1,741 walichaguliwa kujiunga na mafunzo ya muda mrefu kwa kujifunza muda wa jioni, hadi sasa waliodahiliwa (walioripoti chuoni) ni 1050. Licha ya kuchangia katika kuongeza udahili, hatua hii inalenga kuwahudumia wale waliopo kazini au wenye majukumu mengine ya asubuhi hadi mchana.
v)
Kuboresha utaratibu wa utunuku
kwa wanafunzi wa kozi za muda mfupi
Tumepanga kuufanya utunuku wetu kuwa nyumbufu na unaozingatia mkusanyiko wa alama (credits) ili kutoa fursa kwa wanafunzi wa kozi za muda mfupi kusoma moduli zilizogawanywa kwa mfumo wa umahiri na kukusanya alama zao za mafunzo hatua kwa hatua.
Kupitia mfumo huu, kila moduli itakuwa na idadi maalumu ya credits kulingana na uzito na umahiri unaohitajika. Mwanafunzi atakapokamilisha moduli na kufaulu tathmini husika, atapewa credits zinazotambuliwa rasmi. credits hizi zitahifadhiwa kwenye kumbukumbu rasmi za mwanafunzi na zitaweza kujumlishwa pale atakapojisajili kujifunza moduli nyingine zinazohusiana na stadi hiyo. Mwanafunzi atakapokamilisha idadi ya credits zinazotakiwa katika ngazi husika, ataweza kutunukiwa Tunuku za Kitaifa za Ufundi Stadi katika Ngazi ya 1, ya 2 au ya 3.
vi) Mafunzo kwa njia ya Kielektroni (Simu, vishkwambi na kompyuta) kupitia VSOMO
Ili kuwapa vijana na wananchi wengine uhuru zaidi wa kujifunza mafunzo ya ufundi stadi popote walipo na kwa muda wao, VETA ilianzisha mfumo (application) uitwao VSOMO. Mfumo huu humwezesha mwanafunzi kujifunza maarifa yote ya ufundi stadi kwa kutumia simu ya mkononi, kufanya mtihani kwenye simu hadi mwisho wa mpango wa mafunzo ya nadharia. Baada ya hapo, atapangiwa kufanya mafunzo ya vitendo kwenye chuo kimojawapo cha VETA. Hii inapunguza muda wa kukaa chuoni na inaongeza matumizi bora ya simu za mkononi na muda wa mafunzo. Vilevile, mpango huu unawapa fursa watu walio mbali na vyuo kupata mafunzo ya ufundi stadi.
VSOMO ilikuwa ikitekelezwa kwa ushirikiano wa VETA, Airtel na Kampuni ya Magilla Tech. Hata hivyo, mwaka jana, VETA ilikabidhiwa rasmi mfumo huu ambapo kwa sasa VSOMO inapatikana kupitia mitandao yote ya simu iliyopo nchini.
Hadi sasa stadi zipatazo ishirini (20) zinazotolewa kupitia mfumo wa VSOMO. Stadi hizo ni Ufundi wa Pikipiki; Ufundi wa Umeme; Ufundi wa Aluminium na PVC; Umeme wa Magari; Utandazaji na Ufungaji Mabomba; Utengenezaji wa Kompyuta; Upishi na Utoaji Huduma ya Chakula (Catering); Uokaji Mikate na Upambaji; Usafi wa Majengo Makubwa na Maeneo ya Umma; Maua na Upambaji kwenye Shughuli; Ujasiriamali; Utengenezaji wa Simu za Mkononi; Ufungaji Mabomba Viwandani; Umeme wa Viwandani; Uungaji Vyuma Viwandani na Urembo.
Mpaka sasa Takribani wanafunzi 533 wamemaliza kozi mbalimbali kupitia mfumo huu wa VSOMO na kutunikiwa vyeti.
vii) Urasimishaji Ujuzi Uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi wa Mafunzo
Urasimishaji Ujuzi Uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi wa Mafunzo (Recognition of Prior Learning -RPL) ni programu nyingine inayotoa fursa muhimu kwa vijana ambao wana ujuzi uliopatikana mahali pa kazi na kukosa vyeti tambuzi, kupata fursa ya kurasimisha ujuzi huo na kupata tunuku stahiki. VETA hufanya tathmini ya mafundi hao (wanagenzi) na kuwapatia vyeti kupitia mpango huu, hivyo kuwarasimisha. Kwa kufanya hivyo, wanaweza kunufaika zaidi na ujuzi wao kwa kupata zabuni na kupata ajira rasmi.
Hadi kufikia
Januari,2026 jumla ya wanagenzi 25,523 (wakiume 21,547 na wakike 3,976)
wamenufaika na Programu ya Urasimishaji Ujuzi (RPL).
Kwa mwaka wa
fedha 2025/2026, VETA ina shabaha ya kurasimisha ujuzi wa jumla ya mafundi
30,000. Lengo hili ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Mama Samia ya
Urasimishaji wa Ujuzi inayolenga kurasimisha ujuzi kwa vijana 80,000 nchini
kote ifikapo Juni,2027.
Hii ni fursa kwa vijana mafundi ambao wamepata mafunzo kupitia sehemu za kazi kurasimishiwa ujuzi.
viii) Mafunzo kwa wajasiriamali kwenye sekta isiyo rasmi
VETA huendesha mpango wa Mafunzo Jumuishi ya Kukuza Ujasiriamali kwenye Sekta Isiyo Rasmi (Integrated Training for Entrepreneurship Promotion-INTEP). Mpango huu hufanyika kwenye jamii kwa kuhusisha vijana na wanawake wanaoendesha shughuli zao za uzalishaji au za kiuchumi kwenye mfumo usio rasmi. Mfano Mama na Baba Lishe; Mafundi Nguo; Seremala na Wasindikaji. Kupitia mpango huu, wahusika wakiwa katika vikundi huandaliwa mafunzo ya kuwaongezea maarifa na ujuzi ili kuboresha shughuli zao na kuongeza tija.
Kupitia mpango huu, VETA imepanga kutoa mafunzo kwa vijana na wanawake 2000 kila mwaka, katika kipindi cha miaka mitano. Hadi kufikia Januari, 2026 wajasiriamali 7040 amenufaika na mpango wa Mafunzo Jumuishi ya Kukuza Ujasiriamali kwenye Sekta Isiyo Rasmi.
VETA inawaalika vijana na wanawake waliojiunga pamoja katika vikundi vya ujasiriamali kuchangamkia fursa za mafunzo kupitia mpango huu. Wanaweza kuandika barua za maombi ya kupatiwa mafunzo kupitia Kanda zetu.
Ø Fursa za mafunzo kupitia miradi ya ushirikiano na wadau
Ndugu wanahabari,
VETA kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendesha mafunzo ya muda mfupi kwa makundi maalum kwenye sekta mbalimbali nchini, hivyo kuwapa vijana na makundi mengine fursa pana zaidi. Miongoni mwa miradi ya mafunzo kwa sasa ni:
i) Mradi wa Ujasiriliamali wa Vijana kwa Mustakabali wa Chakula na Kilimo (Youth Entrepreneurship for the Future of Food and Agriculture -YEFFA)-Vijana 5,631 kunufaika
VETA inashirikiana na
taasisi za AMSHA, RUATI, TAMA na MIBOS katika utekelezaji wa Mradi wa
Ujasiriamali wa Vijana kwa Mustakabali wa Chakula na Kilimo (YEFFA). Mradi huo
unafadhiliwa na AGRA Tanzania na unatekelezwa kupitia vyuo vya VETA Kihonda,
Manyara, Mpanda na Arusha (Oljoro). Kupitia mradi huo, vyuo husika vinatoa
mafunzo ya muda mfupi katika stadi za Ufundi wa Zana za
Kilimo (Agro-mechanics); Teknolojia ya Umwagiliaji (Irrigation
Technology) na Teknolojia ya Uhifadhi wa Mazao Baada ya Mavuno
(Post-harvest Technology). Mafunzo hayo yanatarajiwa kutolewa kwa awamu nne,
ambapo awamu ya kwanza imeanza Januari mwaka huu.
Mafunzo hayo yatawanufaisha
vijana 5,631 kutoka mikoa 19 ambayo ni Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Lindi,
Morogoro, Pwani, Ruvuma, Njombe, Iringa, Manyara, Singida, Dodoma, Tabora,
Katavi, Kigoma, Rukwa, Mbeya, Songwe na Kagera.
ii) Timiza Malengo
Mradi wa Timiza Malengo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya VETA na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS). Mradi huu unalenga kuwawezesha vijana wa Kike walio katika hatari ya kupata maambukizi ya VVU kwa kuwapatia mafunzo ya ufundi stadi, stadi za Maisha na elimu ya UKIMWI, afya na ujasiliamali. Mradi ulianza kutelekezwa na VETA Desemba 2024 katika mikoa sita (6) ya Ruvuma, Njombe, Lindi, Tanga, Tabora na Mara, yenye Jumla ya Halmashauri 18 ukihusisha vyuo 24 vya VETA ambavyo ni Urambo, Igunga, Nyasa, Makete, Wanging’ombe, Mbarali, Uyui, Ukerewe, Korogwe, Lushoto, Butiama, Songea, Ulyankulu, Mara, Njombe, Iringa, Geita, Ruangwa, Mtwara, Newala, Gorowa, Namtumbo, Lindi na Masasi.
Hadi kufikia Januari,2026 jumla ya wasichana 2,269 wamehitimu mafunzo katika stadi mbalimbali, huku 2,771 wakitarajiwa kuendelea na mafunzo ili kufikia lengo la kuwafikia wanufaika 5,040 ifikapo Desemba 2026.
Hivyo tunatoa rai kwa wale wanaopata fursa hizi kuzitumia kwa wakati na kwa manufaa yao binafsi na Taifa.
iii) Wezesha Binti na Inclu-Cities
Mradi wa Wezesha Binti na Inclu-cities ni miradi inayofadhiliwa wa Shirika
la Maendeleo la Ubelgiji la Enabel. Miradi hii inatekelezwa katika Mikoa ya Kigoma (Wezesha Binti); na
Mwanza na Tanga (Inclu-cities). Miradi hii inatarajiwa kuwanufaisha Vijana 1,400
kupitia mafunzo ya ufundi stadi ambapo Wezesha Binti vijana 700 na Inclu-cities
vijana 700 ifikapo 2028.
Hadi sasa vijana 531 wamenufaika.
iv) Vijana, Elimu, Malezi na Ajira - VEMA
![]()
![]()
Mradi wa Vijana, Elimu, Malezi na Ajira unatekelezwa kupitia chuo cha
VETA Mwanza. Mradi huu unatekelezwa kwa miaka miwili, 2024 hadi 2026 na unalenga
kuwanufaisha vijana 800 katika stadi za Umeme wa Majumbani, Useremala,
Aluminium, Uandaaji Chakula, Ufundi Magari, Ufundi Umeme wa Magari, Uungaji na
Uundaji Vyuma, Ufundi wa Utandazaji na Ufungaji Mabomba, Uashi na Ushonaji. Hadi
sasa vijana 600 wamenufaika na mafunzo hayo.
v) Mafunzo kwa Wafanyakazi wa majumbani (Domestic Workers)
VETA inashirikiana na shirika la Kiitaliano lijulikanalo kama CVM kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wafanyakazi wa majumbani kwa lengo la kuwapatia ujuzi, maarifa na kuwafanya waboreshe utendaji kazi wao, waheshimike, wapate haki zao na kuthaminiwa utu wao. Mradi huu unatekelezwa kupitia vyuo vya VETA Dar es Salaam, Lindi, Tanga, Dodoma, Mikumi na Iringa. Kupitia ushirikiano huu VETA imewajengea uwezo wasichana 1,244 ili kuwawezesha kufanya kazi za majumbani ndani na nje ya nchi.
Kupitia mradi huu, mitaala ya Mafunzo kwa Wafanyakazi Majumbani imeandaliwa, ikiwemo inayowezesha kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa kipindi cha mwezi mmoja, miezi mitatu au miezi sita. Kutokana na kuandaliwa kwa mitaala hiyo, mafunzo hayo sasa yanaweza kutolewa kwenye vyuo vya VETA kwa wenye uhitaji wakati wowote ule.
Hili ni eneo jingine la fursa kwa vijana, hasa wale wanaofanya kazi hizo hapa nchini au wenye nia ya kwenda nje ya nchi kufanya kazi za namna hiyo. Kwa sasa mafunzo haya yanaendelea kutolewa katika vyuo vya VETA Dar es Salaam, Lindi, Tanga, Dodoma, Mikumi na Iringa.
vi) Uwezeshaji wa wanawake
Mwaka jana 2025 tuliendesha mkakati maalum kwa kushirikiana na Asasi ya Wanawake na Samia ambapo tuliweza kuwafikia wanawake 16,000. Wanawake hao walijengewa uwezo kwenye stadi za Ushonaji, Upishi, Ufungaji na Utandazaji Mabomba, Mapambo na Udereva. Wanawake wengi waliokuwa katika mpango huu wameunda vikundi na wanatarajiwa kunufaika na fursa ya kushiriki kwenye zabuni za umma kwa kutumia dirisha la makundi maalum. Sheria ya Ununuzi wa Umma inaelekeza asilimia 30 ya ununuzi wa umma itolewe kwa makundi maalum. VETA iliingia makubaliano na PPRA kuhamasisha na kuwezesha makundi maalum yaliyotajwa kwenye sheria kushiriki katika zabuni za umma.
Kwa mwaka 2026 suala hili litafanyika tena kwa wanawake 3,000.
Ø Uimarishaji Ubora wa Mafunzo
Ndugu wanahabari,
Jitihada mbalimbali zinafanyika katika kuimarisha ubora wa mafunzo ya ufundi stadi katika vyuo vya VETA ili kutoa wahitimu mahiri wanaokidhi mahitaji ya soko la ajira, ndani na hata nje ya nchi. Miongoni mwa jitihada za hivi karibuni ni pamoja na:
i)
Ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia
![]()
Katika kipindi cha mwaka wa fedha
2024/2025 Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kupitia VETA imefanikiwa
kununua vifaa, zana na mitambo ya kufundishia vyenye thamani ya Shilingi
Billion 8.4 katika fani mbalimbali ikiwemo Uchomeleaji Uungaji na Uundaji
Vyuma; Ubunifu, Ushonaji na Teknolojia ya Nguo; Uashi, Utandazaji na Ufungaji
Mabomba; Mekatroniki na Uandaaji Chakula, na kuvisambaza katika jumla ya vyuo
vya ufundi stadi 69 nchi nzima kati ya vyuo 80 vinavyo fanya kazi kwa sasa.
![]()
Sambamba na hilo, Serikali
kupitia kwa wadau wa maendeleo, imeweza kununua na kupokea vifaa, zana na
mitambo ya kufundishia yenye thamani ya Shilingi milioni 892.
Kwa mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali imetenga bajeti ya Shilingi Bilioni 2.5 kwa ajili ya kuweka vifaa, zana na mitambo ya kisasa ya mafunzo katika vyuo vikongwe vya mikoa ya Moshi, Dodoma na Dar es salaam.
Serikali ina mpango Madhubuti wa kuhakikisha vyuo vyetu vikongwe vinaboreshwa na kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia.
Lengo la serikali ni
kuhakikisha kuwa vyuo vyote vya ufundi Stadi vinakuwa na vifaa na mitambo ya
kufundishia ya kisasa ili kuhakikisha vinatoa ujuzi unaoendana na mahitaji ya
waajiri nchini, jamii pamoja na mabadiliko ya sayansi na technolojia. ![]()
![]()
![]()
![]()
ii)
Utafiti wa soko la ajira: Tafiti
13 za soko la ajira zimefanyika, ikiwemo uchambuzi wa mahitaji ya ujuzi (Skills
Mapping) katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini. Lengo ni kuandaa mafunzo
yanayoendana na shughuli za kiuchumi na mahitaji ya ujuzi kwa kila eneo.
iii) Ujengeaji uwezo watumishi: Watumishi 479 wamejengewa uwezo, ili kutoa mafunzo kwa ubora zaidi.
iv) Ushirikiano na Makampuni: Kupitia utekelezaji wa mfumo wa Uanagenzi Pacha (DATS), ulioenezwazwa katika vyuo 11, VETA imeweza kushirikiana na Makampuni/viwanda 351 katika utoaji wa mafunzo, hivyo kuwezesha wanachuo kuongeza umahiri wao kwa kupata mafunzo ya mahala pa kazi.
v)
Kutoa Tunuku za
Kimataifa: kutokana na kuongezeka kwa fursa na uwekezaji
mkubwa unaoendelea kufanywa na Serikali katika Nyanja mbalimbali, makampuni
mengi yakiwemo ya kigeni yanahitaji mafundi wenye ujuzi unaokubalika kimataifa.
Kwa hiyo, umeandaliwa mkakati wa kuanza kutoa Mafunzo yatakayowezesha kutoa
tunuku za kimataifa. Tutafanya hivyo kupitia Vituo vya Umahiri (Centres of
Excellence) ambapo tumepanga kuwa na vituo kumi na vinne (14) vya umahiri
nchini kote. Kwa kuanzia tumenunua vifaa vya mafunzo zikiwemo simulators katika
vyuo vya VETA Moshi na Dodoma na kuboresha karakana za kufundishia.
vi) Ushirikiano na mafundi mahiri katika kutoa mafunzo: Wakati tukitoa mafunzo tumebaini kuwa kuna mafundi wengi mahiri katika nyanja mbalimbali. Wapo waliopata umahiri mkubwa baada ya kuhitimu mafunzo kutoka kwenye vyuo vyetu na wengine wamejifunza kupitia mfumo usio rasmi (au sehemu za kazi). Tumeanzisha mpango wa kuwatambua na kushirikiana na Fundi Mahiri hao katika kutoa Mafunzo. Hadi kufikia Januari, 2026 tumekwisha watambua na kuingia kwenye ushirikiano na mafundi mahiri 1,086.
Tunawakaribisha mafundi mahiri katika maeneo mbalimbali kushirikiana na VETA kupitia vyuo vyake katika utoaji wa mafunzo kwa vijana, ambapo pia watanufaika na nguvukazi inayotokana na vijana waliopo mafunzoni.
Ø Ushirikiano na wadau
Serikali imeandaa Mpango wa Kitaifa wa Ushirikiano kati ya Vyuo na Viwanda ambao ulizinduliwa na Mheshimiwa Daktari Emmanuel Nchimbi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 9 Februari, 2026. Mpango huo unatafsiri maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuifanya elimu ujuzi iwe daraja la moja kwa moja kati ya kijana na ajira kwa kushirikiana na viwanda.
Kwa mwelekeo huu, mpango wa Rais wa kuunganisha viwanda na vyuo vya mafunzo unajidhihirisha vyema.
Ø Ujumbe kwa vijana wa Tanzania
Ndugu wanahabari,
Dunia ya leo haihitaji vyeti pekee. Inahitaji uwezo wa kufanya kazi.
ü Ujuzi ni mtaji
ü Ujuzi ni ajira
ü Ujuzi ni kujitegemea
ü Ujuzi ni heshima
Nawahamasisha vijana
kujifunza ujuzi ili wapate ajira, wajiajiri na hata kuajiri wengine
.
HITIMISHO
Kupitia
uwekezaji huu mkubwa unaofanywa na Serikali ya Awamu ya
Sita
, VETA inakuwa injini
ya kuzalisha ajira, ujuzi na uchumi shindani.
Hivyo niwaase watanzania wote kuchangamkia fursa hii na kwa kuzingatia kuwa vyuo vya VETA sasa vipo katika kila Mikoa na Wilaya nchini na kila chuo kinatoa kipaumbele kwenye mafunzo yanayolengo kuwezesha jamii husika kutumia vizuri fursa na rasilimali mbalimbali zinazopatikana katika maeneo yao ili kujiletea maendeleo.
![]()
Ninawaomba Wanahabari
muendelee kuwa mabalozi wa kuelimisha jamii kuhusu fursa hizi, ili kila kijana
wa Tanzania ajue kuwa: Mustakabali wake uko mikononi mwake na VETA ipo
kumwezesha.
Ufundi Stadi Fursa kama zote kwa watu wote.
Asanteni kwa kunisikiliza.
--------------------------
Comments
Post a Comment