MARAIS DKT.JOHN MAGUFULI NA DKT.SAMIA SULUHU HASSAN WALIHESHIMISHA J W T Z.
Helkopta zikilipamba jengo jipya la Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa (MMUT) lililopo eneo la Kikombo Mkoani Dodoma, awali Makao Makuu hayo yalikuwa Upanga jijini Dar es Salaam. Jengo hilo la kisasa liliasisiwa na Rais wa awamu ya Tano marehemu Dkt. John Pombe Magufuli na kumaliziwa ujenzi wake na Rais wa Awamu ya Sita Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Rais Samia amesema hakuna uwekezaji unaoweza kuja bila kuwepo mazingira salama, na kwamba haiwezekani kujenga ustawi wa wananchi bila amani. Ameeleza kuwa hivi karibuni shirika la kimataifa la tathmini ya ukuaji wa uchumi duniani, The Modes, limeipa nchi daraja la I, kiwango alichokieleza kuwa ni kizuri kwa mustakabali wa ukuaji wa uchumi.
Ameongeza kuwa kadri taifa linavyoimarika kiuchumi, uwekezaji katika sekta ya ulinzi unakuwa jambo lisiloepukika kutokana na umuhimu wake kwa maendeleo na ustawi wa wananchi. Amesema Serikali itaendelea kuliwezesha Jeshi kuwa na mazingira bora ya kazi ili liwe tayari wakati wote kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Aidha, amebainisha kuwa Taifa linalotaka kuheshimiwa halina budi kuwekeza katika Taasisi imara za kulinda uhuru, mipaka, rasilimali na watu wake. Amesema majengo hayo mapya ni nyenzo ya kusaidia utekelezaji wa majukumu, lakini nguvu ya Jeshi haitokani na majengo au vifaa pekee.
Katika hafla hiyo alinukuu maneno ya Baba wa Taifa, Julius Kambarage Nyerere, aliyewahi kusema, “Moyo kabla ya silaha,” akisisitiza kuwa msingi wa Jeshi imara ni moyo wa kizalendo, nidhamu, weledi, utii, dhamira safi, uadilifu na uaminifu kwa taifa.
Rais Samia ameongeza kuwa utii kwa mamlaka ya kikatiba na uaminifu kwa taifa ndiyo silaha ya kwanza ya Jeshi linaloheshimika. Amewasihi viongozi, makamanda na wapiganaji kuendelea kuishi kwa misingi ya kiapo chao na kuepuka mienendo inayoweza kuharibu heshima ya Jeshi.
Aidha, amesisitiza kuwa Taifa lina imani kubwa na Jeshi, na kwamba hiyo ni dhamana waliyopewa na Watanzania. Ametoa wito kwa wananchi wote kutekeleza wajibu wao wa kikatiba katika kulinda amani na utulivu wa nchi.
Amebainisha pia kuwa tarehe 15 Desemba mwaka jana alipata fursa ya kufungua Mkutano wa Tisa wa Wakuu wa Majeshi ya Ulinzi na Makamanda mkoani Tanga, katika Kituo cha Square, uliobeba kaulimbiu isemayo “Ulinzi imara na amani ndio msingi wa maendeleo ya nchi yetu.” Amesema kaulimbiu hiyo inakumbusha kuwa kila hatua ya maendeleo iliyofikiwa imejengwa juu ya msingi wa utulivu, nidhamu na ulinzi thabiti kwa wananchi, na kwamba bila uimara wa hali ya ulinzi na usalama, isingewezekana kufikia hatua iliyopo leo.
Hafla hiyo ilihudhuliwa pia na waliowahi kuwa wakuu wa Jeshi hilo Jenerali George Waitara ,Jenerali Devis Mwamunyanga na Mwaisisi wa jengo hilo Jenerali Venance Mabeyo.
Aidha Baadhi ya mawaziri, Naibu Mawazi na Makatibu Wakuu walihudhulia pia pamojo na mamwambata wa kijeshi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini



Comments
Post a Comment