SERIKALI YAWASILISHA MPANGO WA GRIDI YA TAIFA YA MAJI COP 30

 

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewasilisha Mpango wa Gridi ya Taifa ya Maji katika Mkutano wa 30 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (COP 30) unaofanyika jijini Belem, nchini Brazil.

Gridi ya Taifa ya Maji ni Mkakati wa Taifa uliopo katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, wenye lengo la kuhakikisha upatikanaji wa huduma endelevu ya maji kwa jamii, viwanda, kilimo, mifugo na mazingira, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa wasilisho hilo, Naibu Katibu Mkuu (Muungano), Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi, amesema mpango huo wa Gridi ya Taifa ya Maji utasaidia kutatua changamoto za upatikanaji wa huduma hiyo kwa kuwa na vyanzo vya uhakika kutoka Maziwa Makuu na mito mikubwa.

Amebainisha kuwa Tanzania ni kinara wa ajenda ya maji Afrika kupitia uwekezaji wa miradi mikubwa ya maji inayotekelezwa na Serikali ili kukabiliana na uhaba wa huduma hiyo muhimu kwa binadamu.

Akiendelea kuzungumza, Bw. Mitawi amesema kuwa pamoja na mambo mbalimbali, Gridi ya Taifa ya Maji itasaidia kuwezesha ukuaji wa uchumi na kuhakikisha huduma za maji zinakuwa endelevu na za uhakika.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu Mitawi amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikisha washirika wa maendeleo kutoka sekta binafsi na asasi za kiraia ili kuhakikisha maandalizi ya Gridi ya Taifa ya Maji yanakamilika kama ilivyopangwa.

Kwa mantiki hiyo, amesema kuwa ni wajibu wa kila mmoja kulinda vyanzo vya maji vikiwemo maziwa ya Victoria, Nyasa na Tanganyika pamoja na mito, ili kuhakikisha usalama wa maji unabaki kuwa endelevu wakati wote.

Alitumia nafasi hiyo kuwashukuru washirika wa maendeleo kama Shirika la Kimataifa la WaterAid, NDC Partners na Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto (UNICEF) kwa kushirikiana na Serikali katika kuboresha huduma za maji kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa WaterAid Tanzania, Bi. Manka Mushi, amesema mpango wa Gridi ya Taifa ya Maji unaendana na mikakati ya Serikali ya kutatua changamoto ya upungufu wa maji.

Hivyo, alibainisha kuwa upatikanaji wa maji ya uhakika si tu unamaliza changamoto ya huduma hiyo, bali unaimarisha sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, uvuvi, nishati, viwanda, afya na elimu.

Bi. Manka ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada za kuanzisha Gridi ya Taifa ya Maji, mpango ambao utasaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.

Itakumbukwa kuwa Machi 22, 2025, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Maji Duniani, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alielekeza kuanzishwa kwa Gridi ya Taifa ya Maji ili huduma hiyo iweze kufika katika maeneo yote nchini. Aidha, wakati akifungua Bunge la 13, amesisitiza utekelezaji wa Gridi ya Taifa ya Maji kukamilika ifikapo mwaka 2030.   

Comments

Popular posts from this blog

WALIOPITA KURA ZA MAONI CCM HAWA HAPA

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?

UNAMKUMBUKA AMINA CHIFUPA WA MPAKANJIAA.