NASEMA HATUTAVUMILIA UZEMBE SERIKALINI- KENANI
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimewataka mawaziri na manaibu waziri walioapishwa jana kuwa kinatarajia utendaji wa juu na matokeo yanayoonekana, kikisisitiza kuwa hakitasita kuchukua hatua kali dhidi ya kiongozi yeyote atakayeshindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi, amesema mawaziri, manaibu waziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wengine wote walioteuliwa au kuchaguliwa na Mwenyekiti wa Chama hicho ambaye ndiye Rais wasiowajibika kwa wananchi, chama kitawawajibisha.
Kihongosi Amesema kuwa kila kiongozi wa serikali atapimwa kulingana na vigezo vitakavyowekwa, na kiongozi yeyote atakayeshindwa kufikia viwango vya ufanisi hatasita kuchukuliwa hatua mara moja, huku akisisitiza kuwa dhamira ya chama ni kuona viongozi wanafanya kazi kwa kujituma na kwa kuzingatia maslahi ya wananchi.
Aidha amebainisha kuwa mawaziri, manaibu mawaziri na viongozi wa ngazi mbalimbali wanapaswa kufanya kazi kwa juhudi na weledi ili kuhakikisha matarajio na maelekezo ya Rais yanatekelezwa kikamilifu na kwa muda mwafaka.
Hayo ameyasema leo 19, 2025 jijini Dodoma na Kihongosi, ambaye amesema kuwa uteuzi wa viongozi hao ni dhamana kubwa waliyopewa na Rais Samia Suluhu Hassan, hivyo hawapaswi kuichukulia kwa urahisi.
Chama kinawataka mawaziri na manaibu waziri waende kufanya kazi kwa weledi na wasimuangushe Rais, akibainisha kuwa wengi wao ni wapya, na licha ya kufurahia uteuzi, wakumbuke kuwa Rais anataka kazi, matokeo na utendaji uliotukuka unaozingatia utu kwa Watanzania wote.
Aidha amebainisha kuwa CCM haitavumilia aina yoyote ya uzembe au kutozingatia maadili ya kazi katika Serikali inayotekeleza Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho, na viongozi walioteuliwa wanapaswa kufanya kazi kwa bidii, uwajibikaji na kwa kuwatumikia wananchi kama Taifa linavyotarajia huku wakionyesha matokeo safi kwa kazi iliyotukuka.
Pia, Amebainisha kuwa Chama cha Mapinduzi hakitasita kuchukua hatua kali kwa kiongozi yeyote mzembe ndani ya Serikali, akisema kuwa viongozi walioteuliwa wanapaswa kwenda kuwatumikia wananchi na si vinginevyo.
Comments
Post a Comment