MGEJA ASEMA URAIS SI MAJARIBIO, DKT. SAMIA ANATOSHA

Na Mwandishi Wetu, Kahama na Nzega
Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mwanasiasa mkongwe nchini, Ndugu Khamisi Mgeja (anayeongea pichani), amewatahadharisha Watanzania kutofanya makosa kwa kuchagua wagombea wa urais wasiokuwa na uzoefu wa kiuongozi na ambao hawajawahi kufanya kazi yoyote ya serikali, hata katika ngazi za mitaa, akisema kufanya hivyo ni kosa la kujitakia.
Mgeja alikumbusha usia wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyewahi kusema kuwa kiongozi bora wa nchi hii hatatoka nje ya CCM, bali atatoka ndani ya CCM. Amesema kuwa kiongozi huyo si mwingine bali ni Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni chaguo sahihi la Watanzania.
Mgeja alitoa kauli hiyo katika mikutano ya kampeni iliyofanyika katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Nzega mkoani Tabora na Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, alipokuwa akinadi wagombea wa ubunge akiwemo Hussein Bashe (Nzega) na Benjamini Ng’ayiwa (Kahama Mjini).
Akiwa katika vijiji vya Nyanhembe na Ufala wilayani Kahama, Mgeja aliwaomba wananchi wa Jimbo la Kahama Mjini kumpigia kura za kishindo mgombea urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na mgombea ubunge Benjamini Ng’ayiwa na mgombea udiwani Betha Daud.
Amesema Watanzania wana kila sababu ya kumuunga mkono Dkt. Samia kwa sababu amefanya mambo makubwa ya kimaendeleo katika sekta zote nchini. “Dkt. Samia ameleta mafanikio makubwa yanayoonekana kwa macho. Tunawajibu wa kumlipa kwa kura za heshima na kishindo tarehe 29 mwezi huu,” alisema Mgeja.
Aidha, alimwelezea Ng’ayiwa kuwa ni kijana mwenye ari kubwa ya kuwatumikia wananchi wa Kahama, akiwataka wamchague ili aendelee kuleta maendeleo katika jimbo hilo.
Akiwa wilayani Nzega, Mgeja alimiminia sifa kemkem mgombea urais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisema utendaji wake bora umejidhihirisha kupitia miradi mikubwa ya maendeleo iliyoanzishwa na kukamilishwa katika kipindi kifupi. “Dkt. Samia ni mama muungwana, mchapa kazi, mwenye maono makubwa, mwadilifu, mpenda maendeleo na mwenye upendo wa dhati kwa wananchi wake,” alisema.
Ameongeza kuwa chini ya uongozi wake wa awamu ya sita, maendeleo yamekuwa yakionekana kama uyoga, na kwamba Watanzania wajiandae kuona mambo makubwa zaidi katika miaka ijayo.
Kuhusu Mgombea Ubunge wa Jimbo la Nzega, Hussein Bashe, Mgeja aliwapongeza wana CCM na wananchi kwa kuendelea kumuunga mkono, akisema ni kiongozi mchapa kazi, mwenye maono makubwa, na mchango wake katika Wizara ya Kilimo umeleta mabadiliko makubwa nchini. “Wananzega mna kila sababu ya kumuunga mkono na kumlinda kama mboni ya jicho. Hakikisheni tarehe 29 mwezi huu mnampigia kura za heshima na kishindo ili aendelee kuwatumikia wananchi wa Nzega na taifa kwa ujumla,” alisema.
Akihitimisha, Mgeja aliwataka Watanzania kudumisha umoja na mshikamano, akisema taifa lipo imara chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan licha ya kuwepo kwa kikundi kidogo cha watu wanaotumika kujaribu kuvuruga amani. “Mama yetu Rais Dkt. Samia yuko imara kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani, umoja na mshikamano wa kitaifa. Wale wanaojaribu kuleta chokochoko wajue hawawezi kutugawa Watanzania,” alisisitiza.
Mgeja aliwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi tarehe 29 Oktoba kupiga kura bila hofu, akisema taifa liko katika mikono salama chini ya uongozi thabiti na shupavu wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Comments
Post a Comment