HOSPITALI YA BENJAMINI MKAPA YAZINDUA SAFARI YA MAADHIMISHO YA MIAKA 10

BMH  YAZINDUA SAFARI YA MAADHIMISHO YA MIAKA 10 YA HUDUMA ZA TIBA, NA YATAKIWA KUENDELEA KUWA KITOVU CHA  UBUNIFU WA HUDUMA BORA NA UTALII WA MATIBABU. 

Na Ludovick Kazoka, Dodoma. Oktoba 13, 2025

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) leo imetimiza miaka 10 ya huduma, ikitakiwa kuwa tumaini jipya la kitovu cha ubunifu wa huduma bora za matibabu na utalii wa matibabu kutokana na uwekezaji mkubwa wa zaidi ya Tsh Billion 230 uliowekwa na serikali katika Hospitali hiyo.


Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma (RC) wakati wa uzinduzi wa maadhimisho hayo, Mhe. Rosemary Senyamule, akisema BMH imekuwa tumaini la waaliokata tamaa na magonjwa makubwa.

"Hospitali hii imekuwa ni alama ya mafanikio ya mkoa na Taifa kwa ujumla," amesema Mkuu wa Mkoa baada ya kukata utepe kuashiria uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 10 ya kutoa huduma shughuli ambayo itahitimishwa mwezi Februari, mwakani.

Shughuli hii inaambatana na kutoa huduma bure za vipimo na matibabu katika viwanja vya vya Nyerere Square.

RC Senyamule amepongeza Serikali kwa kufanya mapinduzi makubwa ya kuimarisha huduma katika Hospitali hii ya Rufaa ya Kanda ya Kati.

"Hospitali sasa inatoa huduma za ubingwa wa juu 17 na huduma za ubingwa bobezi 20. Huduma hizi zimeokoa sana fedha za kigeni ambazo Serikali ingetumia kwa ajili ya rufaa za nje ya nchi," amesema Bi Senyamule.

Mkuu wa Mkoa pia ametumia fursa hiyo kuipongeza Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kutoa wauguzi bora wa mwaka kwa mara ya pili mfululizo mwaka uliopita na mwaka huu.

"BMH imekuwa ni moja ya taasisi mahiri za afya nchini na kuleta maendeleo chanya katika sekta ya afya nchini," ameongeza Bi Senyamule.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof Abel Makubi, mpaka sasa BMH imehudumia wananchi 1.6m toka ianzishwe 2015.

"Kwa sasa, tunahudumia wananchi wagonjwa 1000 mpaka 1200 kwa siku.

"Dhamira yetu sasa ni kuwa Hospitali ya pili ya Taifa," amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali.


Prof Makubi ameelezea mafanikio makubwa ambayo Hospitali imeyapata kwa muda wa miaka 10 kuwa ni pamoja upandikizaji wa figo kwa wagonjwa 54 na upandikizaji wa uloto kwa watoto 21.

"Tunamshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kugharamia  75% za gharama za matibabu ya selimundu kwa watoto waliokuwa na Selimundu," amesema.

Prof Makubi ameongeza pia kuwa Hospitali imeimarisha huduma kwa  kupunguza mizunguko ya kupata huduma  na kuboresha huduma kwa jamii.

"Hospitali imechaguliwa kuwa Hospitali bora ya Rufaa ya Kanda kwa mwaka huu. Muelekeo ni kuwa Hospitali ya pili ya Taifa na kuwa Kituo cha Tiba Utalii nchini," amesema.


Aidha Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe Jabiri Shekimweri, ameipongeza BMH kuunganisha maono ya Mkoa na Hospitali ya kuifanya kuwa Kituo cha Tiba Utalii.


"BMH imejiunganisha na maono ya Mkoa kuwa Kituo cha Tiba Utalii. Hii ni ishara ya huduma bora zinazotolewa Hospitalini  hapo," ameongeza Mhe. Shekimweri.

 

Comments

Popular posts from this blog

UNAMKUMBUKA AMINA CHIFUPA WA MPAKANJIAA.

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?

KADA MGEJA AHUDHURIA MAZIKO YA MAMA MZAZI WA MWANDISHI MWANDAMIZI WA HABARI KAHAMA