MKOA WA ARUSHA MAFANIKIO YA SERIKALI YA AWAMU YA SITA KATIKA MKOA WA ARUSHA

Awali ya yote nichukue nafasi hii kumshuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema, kwa kutujalia kukutana  hapa siku ya leo tukiwa wazima na afya njema, huku tukijivunia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne (2021 hadi 2025) ya Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya jemedari makini sana Mheshimiwa Dkt Sami Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Niliyepo mbele yenu kuzungumzia mafanikio ya Mkoa wa Arusha ni Kenani Laban Kihongosi, niliyepewa heshima na dhamana na Mhe Rais ya kusimamia shughuli mbalimbali za Serikali katika Mkoa wa Arusha.

Ndugu Waandishi wa Habari;

Mkoa wa Arusha ni miongoni mwa Mikoa 31 nchini, wenye Wilaya sita, Halmashauri saba, Tarafa 23, Kata 158, Vijiji 394, Mitaa 154, na Vitongoji 1,505 wenye jumla ya wakazi 2,356,255, kulingana na Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022. Kati ya watu hao wanaume ni 1,125,616 na wanawake ni 1,230,639, kukiwa na wastani wa ongezeko watu kwa asilimia 3.4% kwa mwaka.

Ndugu Waandishi wa Habari;

Mkoa wa Arusha ni miongoni mwa mikoa yenye kasi kubwa ya maendeleo. Wananchi wa Arusha wanaoshuhudia mapinduzi ya maendeleo katika sekta zote. Katika kipindi cha  miaka minne ya Serikali ya Awamu ya sita, chini ya uongozi mahiri wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mkoa wa Arusha umejikita katika kuboresha miundombinu katika Sekta za Elimu, Afya, Maji na Miundombinu ya Barabara, Nishati, Kilimo & Mifugo, Utalii pamoja na Utawala Bora.

Ndugu Waandishi wa Habari;

Lengo Serikali kwa kuzingatia Ilani ya Chama cha Mapinduzi pamoja na Mipango ya Maendeleo ya Kitaifa, ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, kwa gharama nafuu na kwa wakati zikiwa zimesogezwa karibu na wananchi hususani waishio maeneo ya vijijini.

Katika Kipindi cha miaka minne, Mkoa wa Arusha umepiga hatua kubwa za kimaendeleo kwenye nyanja za kiuchumi na ustawi wa jamii huku wananchi wake wakinufaika kupitia miradi ya maendeleo iliyotekelezwa kwenye maeneo yao. Miradi ambayo imekamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi walliokuwa na kiu kubwa ya kupata huduma za kijamii mathalani huduma za afya, maji, umeme na barabara kwenye maaeneo yao.

Ndugu Waandishi wa Habari;

Katika Awamu ya Sita Mkoa wa Arusha umepokea na kukusanya fedha kiasi cha shilingi Trilioni 3.5, ambazo zimetumika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo kwenye sekta za:

ü Utawala Bora                              -               Bilioni 958.6

ü Afya                                          -               Bilioni   94.2

ü Elimu                                        -               Bilioni 267.0

ü Maji                                          -               Bilioni 686.9

ü Miundombinu ya Barabara           -               Bilioni 638.9

ü Nishati ya Umeme                       -                 Bilioni   99.2 

ü Mapato ya Ndani                         -                 Bilioni 240.9

ü TASAF                                                 -               Bilioni   61.6

ü Sekta Nyingine                                   -             Bilioni 465.39   

Aidha, kiwango cha ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo kimeongezeka pamoja na uibuaji na utekelezaji wa miradi katika maeneo yao umeongezeka na kufikia asilimia 84, pato la Mwananchi katika mkoa wetu waArusha limeongeka kutoka Shilingi milioni  3.2 mwaka 2020 hadi shilingi milioni 3.6 kwa mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 12.5.

Ndugu Waandishi wa Habari;

Mafaniko katika Sekta ya Utawala Bora, yamelenga katika huduma bora na wananchi kwa wakati. Jumla ya shilingi Bilioni 958.7 zilitolewa na kutumika kujenga majengo mapya na ya kisasa ya utawala katika Halmashauri za Monduli, Ngorongoro, Arusha Jiji (ujenzi unaendelea) na Ukumbi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na nyumba ya Mkuu wa Mkoa. Ujenzi wa majengo hayo umerahisisha shughuli za utoaji na upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.

Ndugu Waandishi wa Habari;

Mafaniko katika Sekta ya Afya, yamedhihirika katika kutekeleza Mpango Mkakati wa upatikanaji wa huduma bora za afya kwa kuzingatia afya ya msingi kuwafikia wananchi katika  maeneo yao kwa lengo la kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua. Serikali imetoa jumla ya shilingi Bilioni 94.2 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya kwa kujenga na kuboresha miundombinu ya afya, ununuzi wa dawa na vifaa tiba.

Kati ya fedha hizo Bilioni 57.07 zimetumika kuboresha miundombinu ya afya ikiwemo ujenzi, ukarabati na ukamilishaji wa majengo na shilingi Bilioni 26 zimetumika katika manunuzi ya dawa, vifaa tiba na vitenganishi.

Ndugu Waandishi wa Habari;

Juhudi hizo za Serikali ya Awamu ya Sita, zimewezesha kupatikana kwa mafanikio yafuatayo:

a)        Ongezeko la idadi ya vituo vipya vya kutolea huduma za afya 87, kutoka Vituo 249 hadi vituo 350, sawa na asilimia 71.14 .

§  Ujenzi wa Hospitali mpya 8 na kuufanya Mkoa kuwa na jumla ya Hospitali 21, zikiwa na majengo ya kutolea huduma za dharura (EMD).

§  Ujenzi wa Vituo vipya vya afya 8, na kuufanya mkoa kuwa na Vituo 66.

§  Ujenzi wa Zahanati mpya 38, na kuufanya Mkoa kuwa na jumla ya Zahanati 350.

 

b)        Huduma za kibingwa mpya 11 zimeanzishwa ikiwemo; upasuaji, pua, koo na masikio, mifupa, magonjwa ya figo, magonjwa ya ngozi, uchunguzi wa magonjwa ya saratani, magonjwa ya uzazi na mtoto, magonjwa ya afya ya kisayansi, magonjwa ya ndani, watoto, mfumo wa mkojo.

 

c)        Hali ya upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitengenishi imeongezeka kufikia asilimia 93 (2025) kutoka asilimia 65 (2021).

 

d)        Mashine za kisasa zimesimikwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mount Meru, ikiwemo: CT-Scan, ECHO, ECG na MAMOGRAPHY. Uwepo wa mashine hizi umepunguza rufaa za wagonjwa kwenda Hospitali za Rufaa nje ya Mkoa, kama KCMC (Kilimanjaro) na Muhimbili (Dar es Salaam).

 

Kwa sasa wagonjwa wa rufaa wanaotibiwa ndani ya Mkoa wameongezeka, mathalani wagonjwa 152,332 walitakiwa kwenda kutibiwa nje ya Mkoa wametibiwa katika Hospitali yetu ya Mount Meru.

 

e)        Jumla ya watumishi 1,403 wameajiriwa na kufanya idadi ya watumishi wa afya kufikia watumishi 3,542  sawa na ongezeko la asilimia 66.

 

f)         Nyumba 105 za watumishi wa sekta ya afya zimeongezeka na kufikia nyumba 423, sawa ongezeko la asilimia 33.

 

g)        Mkoa kwa sasa una magari 14 ya huduma za dharura (ambulance), magari tisa kwa ajili Timu za Uendeshaji Mkoa (RHMT) na Halmashauri (CHMT) kwa ajili ya shughuli za usimamizi wa huduma za afya yamenunuliwa, pamoja na ununuzi wa gari moja la huduma M-mkoba (Mobile Clinic).

 

Ndugu Waandishi wa Habari;

Uboreshaji wa huduma za afya umerahisisha upatikanaji wa huduma za afya katika maeneo mbalimbali ndani ya Mkoa wa Arusha na kuwezesha:

a)     Kupunguza vifo vya kinamama wajawazito kwa asilimia 78, kutoka vifo 50 (2021) hadi vifo 11 (2025).

b)    Vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua kutoka vifo 859 (2021) hadi 117 (2025), vikishuka kwa asilimia 86.4.

c)     Kuanzishwa kwa Mfumo wa Rufaa wa M-Mama, umechangia jumla ya akina mama wajawazito 1,332 kujifungulia kwenye Vituo vya kutolea huduma za afya.

Ndugu Waandishi wa Habari;

Mafaniko katika Sekta ya Elimu, yamechagizwa na utekelezaji wa Sera ya Elimu Bila Malipo ya mwaka 2015, ambapo Serikali imetoa kiasi cha shilingi Bilioni 267 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule na utekelezaji elimu bila malipo, kama ifuatavyo:

a)     Uboreshaji wa Miundombinu ya shule kwa gharama ya shilingi Bilioni 98.9 kwa:

§  Kujenga shule mpya 27 za sekondari na shule mpya saba za msingi.

§  Ujenzi wa vyumba vya madarasa 843.

§  Ujenzi wa mabweni 60 ya wavulana na wasichana.

§  Ujenzi wa Maabara 78 za kufundishia masomo ya sayansi.

§  Pamoja na ujenzi wa majengo ya Maktaba 26, majengo ya TEHAMA 26, majengo ya utawala 26, nyumba za walimu 27 na matundu ya vyoo 940.

§  Mkoa pia umepokea fedha shilingi Bilioni 1.6  kwa ajili ya ujenzi wa shule ya Amali katika Kata ya Makiba, kijiji cha Valeska wilaya ya Arumeru, ujenzi unaendelea.

b)    Mkoa umetekeleza programu ya Elimu Bila Malipo kwa gharama ya shilingi Bilioni 168.2, ambapo idadi ya wanafunzi walionufaika imeongezeka kutoka wanafunzi 390,910 (2021) hadi 430,511 (2025).

c)     Elimu ya Awali imeendelea kuboreka, idadi ya madarasa imeongezeka kutoka madarasa 802 (2021) hadi madarasa 853 (2025). Aidha, idadi ya walimu wa elimu ya awali wameongezeka kutoka walimu 1,459 (2021) hadi walimu 1,891 (2025).

d)    Mafanikio katika sekta ya elimu haijawacha mbali wanafunzi wenye Mahitaji Maalum. Wanafunzi wenye mahitaji maalum wameongezeka kutoka wanafunzi 1,545 (2021) hadi wanafunzi 2,835 (2025). Shule zinazotoa elimu hii zimeongezeka kutoka shule 38 (2021) hadi shule 149 (2025).

e)     Uwepo wa shule za Bweni zimewezesha watoto wa kike hasa kutoka jamii ya Kimasai kupata elimu. Mkoa unajivunia kuwa na shule mpya ya wasichana Longido Samia Girls, pamoja na shule ya Wasicha Arusha Girls ya mchepuo wa Sayansi.

Ndugu Waandishi wa Habari;

Sekta ya Maji katika Mkoa wa Arusha umepokea kiasi cha shilingi Bilioni 686.925 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji Mjini kupitia Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingiza Arusha (AUWSA) na Vijijini kupitia Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).

a)    Huduma za Maji Mjini - AUWSA

§  Mamlaka ya Maji (AUWSA) imepokea kiasi cha shilingi  Bilioni 568.425 kwa ajili ya miradi ya maji na usafi wa mazingira.

§  Kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya shilingi Bilioni 520 wa Jiji la Arusha umeongeza uzalishaji wa maji kufikia  Lita milioni 200 kwa siku kutoka Lita milioni 60 (2021).

§  Aidha, Serikali imetoa kiasi cha shilingi Bilioni 38 kwa ajili ya kuongeza mtandao wa maji wenye urefu wa kilomita 810 ukilenga kupanua upatikanaji wa huduma za maji katika Jiji la Arusha na Miji jirani ya Longido na Monduli.

§  Huduma ya upatikanaji wa maji safi katika Jiji la Arusha imefikia asilimia 99 (2025) ikilinganishwa na asilimia 54.4 (2021).

§  Muda wa upatikanaji wa maji safi na salama pia umeongezeka na kufikia saa 22 (2025) kwa siku kutoka saa 11 (2021).

§  Aidha, kiasi cha shilingi Bilioni 6.6 kimekamilisha mradi wa maji katika Mji wa Namanga Wilaya ya Longgido na umeanza kutoa huduma kwa wananchi wa Kata ya Namanga.

 

b)      Huduma za Maji Vijijini - RUWASA

Ndugu Waandishi wa Habari;

§  Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Mkoa wa Arusha unahudumia Wilaya Tano za Arumeru, Karatu, Longido, Monduli na Ngorongoro.

 

§  Kupitia Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mkoa wa Arusha umepokea shilingi Bilioni 118.5 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji Vijijini, ikilenga kuhakikisha upatikanaji wa huduma za maji safi na salama unafikia asilimia 85 ifikapo 2025.

 

§  Jumla ya miradi 72 imekamilika yenye thamani ya shilingi Bilioni 41.38 ikihudumia vijiji 47 vipya na kufikisha jumla ya vijiji 351 vyenye huduma ya maji katika Mkoa wa Arusha.

 

§  Ununuzi wa seti moja ya mitambo ya kuchimba visima kwa Mkoa wa Arushai umewezesha uchimbaji wa visima 96 katika Majimbo sita za Arumeru Mashariki, Arumeru Magharibi, Karatu, Longido, Monduli na Ngorongoro, pamoja na kujengwa bwawa moja la Lepurko Wilaya ya Monduli.

 

§  Uzalishaji wa maji umeongezeka na kufikia Lita milioni 58.4 (2025) kwa siku, kutoka wastani wa Lita milioni 42.8 (2021). 

 

§  Hali ya upatikanaji wa huduma ya maji vijijini imeongezeka na kufikia asilimia 77.3 kutoka asilimia 69.4 (2020), tukiwa na lengo la kufikia asilimia 85 ifikapo Desemba, 2025.

 

§  Idadi ya Watu Wanaopata huduma ya maji ni 1,168,102 sawa na 77% ya idadi ya watu waishio Vijijjini wapatao 1,511,611.

 

§  Aidha, jumla ya ajira rasmi 354 zimezalishwa kupitia Vyombo vya Watoa Huduuma Ngazi ya Jamii (CBWSOs) na ajira zisizo rasmi 540 kupitia ujenzi wa miradi ya maji.

 

 

 

Ndugu Waandishi wa Habari;

Katika Sekta ya Miundombinu ya Barabara, Mkoa wa Arusha umepokea kiasi cha shilingi Bilioni 635.8 kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara Mijini na Vijiji (TARURA) kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara na madaraja.

a)    Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS)

Mkoa wa Arusha umepokea kiasi cha shilingi Bilioni 575.7 kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS). Kiasi hicho cha fedha kimewezesha mtandao wa barabara za Mkoa wa Arusha kufikia Kilomita 1,493.12, kati ya barabara hizo Kilomita 479.88 ni za kiwango cha lami, sawa na asilimia 32.

§  Idadi ya Makalvati kutoka 870 hadi 1,650

§  Idadi ya madaraja kutoka 90 hadi 144

 

Hata hivyo Mkoa kupitia TANROADS, unaendelea na mikakati ya kukamilisha barabara zinazounganisha wilaya za Arusha na mikoa jirani kama vile barabara za Mto wa Mbu - Selela, Selela – Engaruka, Wasso – Loliondo yenye urefu wa Kilomita 10 na Engaruka – Engarasero yenye urefu wa Kilomita 24.

§  Mkataba wa kujenga jumla ya Kilomita 70, barabara ya Arusha - Kibaya - Kongwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 221.35 umesainiwa.

§  Mapitio ya usanifu sehemu ya barabara ya Tengeru - USA River yenye urefu wa Kilomita 11.3 pamoja na usanifu wa barabara ya njia nne kati ya Momela hadi KIA yenye urefu wa Kilomita 20.3 unaendelea.

§  Usanifu wa barabara ya Arusha  Kisongo yenye urefu wa Kilomita 9.1 kuwa njia nne umekamilika. Barabara hiyo inatarajia kutekelezwa katika bajeti ya mwaka 2025/2026.

§  Usanifu wa ujenzi wa barabara ya Longido hadi Siha yenye urefu wa Kilomita 53.1 umekamilika.

§  Ujenzi wa barabara ya Mianzini - Olemringaringa -Ngaramtoni Juu na Olemringaringa - Timbolo yenye urefu wa Kilometa 18 kwa gharama ya shilingi Bilioni 23.31.

 

b)   Wakala wa Barabara Mijini na Vijiji (TARURA)

Ndugu Waandishi wa Habari;

Mkoa wa Arusha umepokea kiasi cha shilingi Bilioni 63.3 kupitia Wakala wa Barabara Mijini na Vijiji (TARURA) kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara vijijini.

 

Kati ya fedha hizo kiasi cha shilingi  Bilioni 8.588 ni fedha za Mapato ya Ndani za Jiji la Arusha zilizotolewa kutekeleza ujenzi wa barabara za kiwango cha lami zenye urefu wa Kilomita 4.12, Mita 150 za barabara ya zege, pamoja na Kilomita 10.4 za barabara za changarawe. Aidha, Kilomita 1.56 za mitaro ya maji ya mvua zimejengwa na kusimika jumla ya taa 495 za barabarani ndani ya Jiji la Arusha.

     Mafanikio yaliyopatikana kupitia Wakala wa Barabara Mijini na Vijiji (TARURA)     ni pamoja na Ujenzi wa daraja la mawe la Jema katika Mto Mmbaga Wilaya ya Ngorongoro pamoja na ujenzi na ukarabati wa barabara za ndani ya wilaya kwa kiwango cha lami zenye urefu wa Kilomita 4.71.

Hata hivyo, Jiji la Arusha linatekeleza miradi ya uboreshaji wa barabara za Oljoro, Engo Sheratoni na Olasiti zenye jumla ya Kilomita 10.3 kwa kiwango cha lami kuunganisha kituo kipya cha mabasi cha Bondeni city kupitia programu ya Uendelezaji Miji Tanzania (TACTIC) kwa thamani ya shilingi bilioni 15.4 ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 61.

Ndugu Waandishi wa Habari;

Katika Sekta ya Nishati - TANESCO, Mkoa wa Arusha umepokea kiasi cha shilingi Bilioni 117.739, Kati ya fedha hizo shilingi Bilioni 39.693 kwa ajili ya TANESCO na shilingi Bilioni 78 kwa ajili ya Wakala wa Kusambaza Umeme Vijijini (REA) kwa ajili ya utekelezaji wa miundombinu ya Nishati ili kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia wananchi..

Mapokezi ya fedha hizo yameleta mafanikio yafuatayo:

§  Upatikanaji wa umeme kwa asilimia 100 kwenye vijiji vyote 368 vya Mkoa wa Arusha vikiwa na wateja 306,674 waliounganishwa na huduma ya umeme.

 

§  Ujenzi wa kituo cha kupozea umeme cha Lemugur (400kV), chenye uwezo wa Megawati 250 kimekamilika.

 

§  Visima vya maji 17 na migodi midogo 22 vimepatiwa huduma ya umeme.

 

§  Ujenzi wa laini ya umeme wa msongo wa Kilovolt 400 kuanzia Arusha hadi Namanga kwa lengo la kuunganisha grid ya Taifa ya kenya na Tanzania.

 

§  Kituo cha kupoza umeme kilichopo Njiro - Arusha Jiji kilichoongezewa transfoma yenye uwezo wa MVA 90 kutoka gridi ya Taifa na kufanya kituo kuwa na jumla ya uwezo wa MVA 210.

 

Ndugu Waandishi wa Habari;

Katika Sekta ya Killimo na ikiwa ni kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa, na kwa Mkoa wa Arusha asilimia 75 ya wakazi wake wanategemea shughuli za kilimo na ufugaji, Mkoa umepokea kiasi cha shilingi Bilioni 85.2 kwa ajili ya sekta ya kilimo na shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Mifugo.

 

 

Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na:

 

§  Ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika maeneo mbalimbali ikimo; Bonde la Eyasi unatekelezwa kwenye ukubwa wa eneo la Hekta 5,000 katika Kata za Mang’ola na Baray Wilaya ya Karatu kwa gharama ya shilingi Bilioni 38.434. Mradi unatarajiwa kunufaisha wakulima 3,000 wa vitunguu na mazao mengine utakapo kamilika.

§  Uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka na kufikia Tani 536,581 kutoka Tani 450,015 mwaka 2021 hadi  sawa na ongezeko la Tani 86,566 (19%).

§  Uzalishaji wa mahindi kwa ekari moja (Hekta) umeongezeka kutoka Hekta 124,054 hadi kufikia Hekta 135,540 sawa na ongezeka la Hekta 11,486 (9.3%).

§  Uzalishaji wa mahindi kwa ekari moja (Tani) umeongezeka kutoka Tani 264,383 hadi kufikia Tani 291,405 sawa na ongezeko la Tani 27,022 (10.2%).

§  Uzalishaji wa maharage kwa ekari moja (Tani) umeongezeka kutoka Tani 39,688 hadi kufikia Tani 40,976 sawa na ongezeko la Tani 1,288 (3.2%).

Ndugu Waandishi wa Habari;

Mkoa wa Arusha kupitia mkakati wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, umefanya yafuatayo:

§  Vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vilivyopewa mikopo isiyo na riba ya asilimia 10 vimeongezeka kutoka vikundi 721 (2021) hadi vikundi 1,380 mwaka 2025.

§  Makundi hayo yameendelea kunufaika na mikopo hiyo na kubadili hali zao za kiuchumi. Mathalani, kikundi cha vijana cha USA River kinachojishuhulisha na biashara ya bodaboda kilipokea kiasi cha shilingi Milioni 100 kutoka Halmashauri ya Meru na kununua gari aina ya Coster na kikundi cha wanawake wafugaji Halmashauri ya Arusha kilichokopeshwa shilingi Milioni 35 na kuanzisha mradi wa kutengeneza mikate (Bakery).  

§  Aidha, kiwango cha mikopo iliyotolewa kimeongezeka kutoka shilingi Bilioni 3.08 (2021) hadi shilingi Bilioni 13.55 mwaka 2025.

§  Aidha, Mkoa umepokea jumla ya shilingi Bilioni 57.22 kutoka kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF). Kati ya fedha hizo shilingi Bilioni 38.39 kwa ajili ya uhawilishaji wa fedha kwenye kaya masikini na shilingi Bilioni 18.82 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu.

§  Ukusanyaji Mapato ya Ndani Katika Halmashauri yameongezeka kutoka shilingi Bilioni 34.631 mwaka 2020/21 hadi shilingi Bilioni 110.116 mwaka 2024/25 kufikia mwezi Mei, 2025 sawa na ongezeko la asilimia 318.

§  Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kutoka Mapato ya ndani ya Halmashauri kimeendelea kuongezeka hadi kufikia shilingi Bilioni 40.475 mwaka 2024/25 kutoka kiasi cha shilingi Bilioni 16.376 mwaka 2020/21.

MAPOKEZI YA FEDHA KWENYE TAASISI NYINGINE  ZA SERIKALI (2021-2025)

Ndugu Waandishi wa Habari;

Mkoa wa Arusha umepokea jumla ya shilingi Bilioni 465.39 kupitia Taasisi za Serikali kama ifuatavyo:-  ikiwemo Vyuo vya Elimu shilingi

·       Shilingi Bilioni 26.92, zimetumika kuboresha miundombinu Katika Taasisi za Vyuo vya Elimu ikiwepo ujenzi mabweni, Majengo ya TEHAMA, majengo ya utawala,  majengo ya kufundishia katika Vyuo vya Patandi, Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA),  Chuo cha Uhasibu Arusha, Chuo Cha Ufundi Arusha na Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru.

Ndugu Waandishi wa Habari;

Kufuatia onhezekola watalii nchini, uliochagizwa na Filamu ya Royal Tour iliyochezwa na Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, Mkoa umepokea Kiasi cha shilingi Bilioni 103 kwa ajili ya uboreshaji wa Viwanja vya Ndege viwili,  Uwanja wa Ndege Arusha eneo la Kisongo na Uwanja wa Ndege ziwa Manyara, kiasi hicho cha fedha kimefanya maboresho ili kuvipa hadhi na kuonheza idadi abiria kufuatia idadi ya miruko, kiasi hicho cha fedha kimetumika :-

·       Kuboresha eneo la maegesho ya magari kiasi cha Shilingi milioni 640 na shilingi Bilioni 2.8 zimetumika kujenga Jengo la kisasa la abiria pamoja na kuongeza barabra za kurukia ndage. Ujenzi umekamilika na umeanza kutoa huduma kwa abiria,  Uwanja huu wa ndege ni wa pili kwa miruko ya ndage Tanzania na watatu kwa idadi ya abiria ikifuatia Kilimanjaro International Air port na Julias Nyerere International Air Port, hata hivyo Serikali imetoa shilingi bilioni 11 kwaajili ya kutengeneza mindombinu ya taa ndani za kuongozea ndege, kukamilika kwa matengenezo hayo utaanza kufanya kazi kwa saa 24 na kupokea ndege za kimataifa

·       Aidha Shilingi  Bilioni 88.539 zimetumika kuboresha Kiwanja cha Ndege Ziwa Manyara huku  Bilioni 5.93 zimetumika kulipa fidia kwa Waathirika 187, Mradi ambao utasaidia  kufikia malengo ya utalii katika ukanda wa Kaskazini ukiwemo Mkoa wa Arusha.

·       Kupitia Mamlaka ya Uhifadhi Ngorongoro Mkoa unatekeleza  Mradi wa ujenzi wa  Jengo la Makumbusho ya Jiolojia ya kisasa, (NGORONGORO - LENGAI UNESCO GLOBAL GEOPARK) linalojengwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Serikali ya China, kwa gharama ya shilingi Bilioni 25. Jengo hilo ni maktaba ya inayoonesha mandhari ya vituo vyote vinavyopatikana ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro Crater pamoja na Jamii zote zilizowahi kuishi ndani ya bonde hilo la Ngorongoro, lengo likiwa ni kulinda na kutangaza urithi wa Jiolojia na utamaduni ndani ya Hifadhi pamoja, kuongeza maudhui ya kielimu kupitia muundo wa makumbusho yenye taarifa za kisayansi, Kuboresha huduma kwa wageni pamoja na kuongeza muda wa kukaa wageni na kuchochea uchumi wa maeneo ndani ya Mkoa.

·       Serikali ya awamu ya sita imeendelea kuwekeza kwenye sekta ya michezo ikiwa na lengo la kuimarisha sekta ya utalii, Serikali imetoa shilingi Bilioni 298 kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Miguu wa SAMIA SULUHU AFCON ARUSHA,  ikiwa ni maandalizi ya mashindano ya AFCON mwaka 2027 yanayotarajia kufanyika nchini, ujenzi umefikia 44.2%

HITIMISHO

Ndugu Waandishi wa Habari;

Tunayo kila sababu ya kujivunia mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Daktari Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nikiwa Mtendaji Mkuu wa Serikali Mkoani Arusha, ninaahidi kuendelea kutekeleza kikamilifu shughuli za maendeleo zinazoendelea kutekelezwa.

 

Tunatoa shukrani za dhati kwa wadau mbalimbali wa maendeleo Mkoa wa Arusha, ikiwemo Serikali Kuu, Wilaya, Taasisi zote, Mamlaka za Serikali za Mitaa na ngazi zote za kiutawala kuanzia Tarafa, Kata, Mitaa, Vijiji na Vitongoji kwa ushirikiano uliowezesha mafanikio haya ya miaka mitano.

 






Wanahabari wakimsikiliza kwa makini Mkuu huyo wa mkoa














Mkuu huyo akipiga picha na wanahabari 




 

Comments

Popular posts from this blog

KADA MGEJA AHUDHURIA MAZIKO YA MAMA MZAZI WA MWANDISHI MWANDAMIZI WA HABARI KAHAMA

UNAMKUMBUKA AMINA CHIFUPA WA MPAKANJIAA.

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?