NI KWELI WAGIRIKI WALIUPIGA JEKI MUZIKI WA KONGO HEBU FUATANA NA MIMI
Katika karne ya 20, hasa kati ya miaka ya 1940 hadi 1960, wafanyabiashara kadhaa kutoka Ugiriki walihamia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hasa jijini Kinshasa (zamani Leopoldville).
Wengi walijihusisha na biashara ya kawaida kama nguo na maduka, lakini wachache waliobahatika kutambua vipaji vya muziki waligeuka kuwa waanzilishi wa mapinduzi ya kisanaa.
Hawa Wagiriki walifungua studio na lebo muhimu za kurekodi ambazo ziliendeleza na kueneza muziki wa rumba ya Kongo.
Mwaka 1948, Nicolas Jéronimidis alianzisha lebo ya Ngoma, iliyomrekodi Wendo Kolosoy na wimbo maarufu “Marie-Louise” – moja ya nyimbo za kwanza za rumba.
Baadaye, ndugu wawili kutoka Macedonia Gabriel Moussa Benatar na Joseph Benatar, wakaanzisha Opika, ambayo ilimtoa Franco Luambo, aliyekuja kuwa gwiji wa muziki wa Afrika.
Makampuni mengine ya Kigiriki kama Olympia na Loningisa pia yalifuata, yote yakichochea ushindani na ubunifu mkubwa.
Wagiriki walitoa vifaa vya kurekodi, mitandao ya usambazaji na msaada wa kifedha – mambo ambayo wasanii wengi wa Kiafrika walikosa. Bila wao, rumba ya Kongo isingepaa hadi kuwa urithi wa kimataifa.
Mbali na Wendo na Franco, nyota wengine walionufaika walikuwa Joseph “Grand Kallé” Kabasele, aliyeanzisha African Jazz na kutoa wimbo “Indépendance Cha Cha”, na Docteur Nico Kasanda, fundi wa gitaa aliyevuma hadi Afrika nzima.
Wengine ni Tabu Ley Rochereau, alikuja kuwa a nyota mkubwa kupitia lebo hizo, Jean Bosco Mwenda, mtaalamu wa fingerstyle kutoka Katanga, na hata Manu Dibango wa Cameroon alipata msukumo mkubwa kutokana na muziki wa Kongo ulioandaliwa na Wagiriki.
Hivyo basi, kwa mchanganyiko wa miondoko ya nchi za Kilatini hasa Cuba, midundo ya ngoma za Kiafrika na ladha za Kimagharibi muziki wa rumba ulizaliwa kupitia usaidizi wa hawa Wagiriki.
Bila wao, huenda rumba isingefika nje ya Congo wala kutangazwa kuwa ni urithi wa dunia. Kwani ingawa mastaa wa rumba walikuwa Waafrika, mzizi wa mafanikio yao ulikuwa pia mikononi mwa Wagiriki waliowaamini, kuwasaidia na kuwapa jukwaa la dunia.
Comments
Post a Comment