Maafisa Habari Kupewa Mbinu za Kisasa Utangazaji Shughuli za Serikali
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa akiwasilisha mada juu ya umuhimu wa mawasiliano ya kimkakati kwa Maafisa habari wa Serikali katika Kikao kazi cha 20 cha Maafisa habari hao kinachoendelea katika Ukumbi wa Hoteli ya Amaan, Zanzibar leo tarehe 4 Aprili 2025
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amesema mada mbalimbali zitakazojadiliwa katika Kikao kazi cha 20 cha Maafisa Habari, Uhusiano, Mawasiliano na Itifaki wa Serikali, zitawaongezea uelewa na mbinu za kisasa za kutangaza shughuli za serikali pamoja na namna bora ya kukabiliana na upotoshaji unaofanywa kwa makusudi na baadhi ya watu.
Mhe. Prof. Kabudi ameyasema hayo Aprili 3, 2025 wakati wa ufunguzi wa Kikao kazi cha 20 cha Maafisa Habari, Mawasiliano, Uhusiano na Itifaki kilichofunguliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla katika ukumbi wa New Amaan Hotel Zanzibar.
Prof. Kabudi amemshukuru Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuridhia Kikao kazi hicho cha 20 cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Serikali kufanyika Zanzibar akieleza kuwa ni fursa kubwa kwa Maafisa hao kukutana na wenzao wa Zanzibar kwa lengo la kujadiliana, kujifunza na kubadilishana uzoefu ili kuwafikishia wananchi habari sahihi za utekelezaji wa shughuli za Serikali.
"Katika Kikao kazi hiki, kutakuwa na mada mbalimbali zitakazowasilishwa na kujadiliwa kwa kina kwa lengo la kuwaongezea Maafisa Habari uelewa na mbinu za kisasa za kutangaza shughuli za utekelezaji wa Serikali lakini pia mbinu na namna bora ya kukabiliana na majanga pamoja na upotoshaji wa taarifa unaofanywa kwa makusudi na watu wasiokuwa na nia njema na Serikali yetu", amesema Prof. Kabudi.
Amezitaja baadhi ya mada zitakazowasilishwa katika kikao kazi hicho kuwa ni Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani: Uzoefu wa Vyombo vya Habari na Utangazaji katika kufanikisha chaguzi zilizopita; Wajibu wa Jeshi la Polisi katika kufanikisha Uchaguzi Mkuu na kuhakikisha usalama wa wananchi na waandishi wa habari watakaoshiriki kwenye kuandika habari za uchaguzi pamoja na Mwongozo wa Vyombo vya Habari na Waandishi wakati wa Uchaguzi.
Mada nyingine ni Wajibu wa Maafisa Habari kutoa taarifa za maendeleo kupitia vyombo vya habari; Fursa zilizopo Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) katika kutangaza habari za Maendeleo; Matumizi ya Takwimu katika Uandishi wa Habari za Uchaguzi na Afya ya Moyo na namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukizwa.
Mawasiliano ya Kimkakati ndani ya Serikali; Wajibu wa Vitengo vya Mawasiliano Serikalini katika kutangaza miradi ya maendeleo inyotekelezwa na Serikali; Matumizi ya teknolojia inayoibukia kama Akili Unde na “Big Data” katika kufikisha taarifa kwa Umma na kukabiliana na upotoshaji na matumizi ya mitandao ya kijamii katika mawasiliano ya Serikali.
Fauka ya hayo, Mhe. Prof. Kabudi amesema washiriki wa kikao kazi hicho watapata fursa ya kwenda kushiriki matendo ya kurejesha kwa jamii kwa kupanda miti 2000 katika msitu wa Muyuni-Jambiani uliopo Mkoa wa Kusini Unguja lengo likiwa ni kuunga mkono juhudi zinazoendelea kufanywa na Serikali katika kuhifadhi mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Comments
Post a Comment