DODOMA NDIO MKOA WENYE MADINI MENGI NCHINI------KAIMU MHANDISI GST
Kaimu Mtendaji Mkuu wa GST, Notka Banteze
JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MADINI
TAASISI YA JIOLOJIA NA UTAFITI WA
MADINI TANZANIA (GST)
MAFANIKIO YA GST KATIKA KIPINDI CHA MIAKA MINNE YA SERIKALI YA AWAMU YA SITA (2021 – 2025)
MACHI, 2025
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania…
Awali ya yote napenda kumshukuru mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema aliyetusazia afya njema, pumzi na uhai na kutuwezesha kukutana mahali hapa siku ya leo. Taarifa yangu itakuwa na vipenge vikuu vinne ambavyo ni:
Utangulizi (Dhima na Dira); Mafanikio ya GST katika kipindi cha miaka minne cha Serikali ya Awamu ya Sita, Mwelekeo wa GST kwa mwaka 2025/2026 na Hitimisho.
1. UTANGULIZI
Ndugu wanahabari na watanzania wote kwa ujumla;
Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ni Taasisi iliyo chini ya Wizara ya Madini na ilianzishwa kupitia Sheria ya Madini Sura Na. 123 kifungu cha 27A ambapo imekasimiwa kutekeleza majukumu 15.
Taasisi hii imetokana na iliyokuwa Wakala wa Jiolojia Tanzania ulioanzishwa mwaka 2005 chini ya iliyojulikana kama Wizara ya Nishati na Madini. Wakala huu ulitokana na Idara ya Jiolojia ilioanzishwa na Serikali ya Uingereza mwaka 1925. Jukumu la msingi la GST tangu kuanzishwa kwake limeendelea kuwa ni kufanya tafiti za jiosayansi (geology, geochemistry na geophysics) ili kubaini aina za miamba na rasilimali madini zinazopatikana nchini kwa lengo la kuchochea uwekezaji hasa katika Sekta ya Madini na Sekta nyingine fungamanishi. Kutokana na tafiti hizo zinazofanywa na GST, zimewezesha kuchangia sehemu kubwa ya mnyororo wa uchumi kwa kupelekea migodi mingi (midogo, ya kati na mikubwa) kuanzishwa.
Aidha, ukiacha jukumu hilo la utafiti wa madini nchini, GST ina maabara ya kisasa inayotoa huduma za uchunguzi wa madini kwenye sampuli za miamba, udongo, maji na mimea. Ni maabara kubwa na ya kipekee ya Serikali na inaendeshwa kwa kuzingatia miongozo ya kimataifa (accreditated laboratory). Pia, GST ina jukumu la kuratibu majanga asili ya jiolojia na kushauri namna bora ya kupunguza au kuondoa athari zake. Majanga hayo ni pamoja na matetemeko ya ardhi, kububujika kwa tope, milipuko ya volkano na maporomoko ya udongo/mawe.
Kuwa kituo mahiri katika kutoa takwimu, taarifa na huduma za jiosayansi kulingana na mahitaji ya wateja kwa maendeleo ya Taifa.
Kutoa takwimu/taarifa na huduma za jiosayansi zenye ubora wa hali ya juu na kwa gharama nafuu kwa Serikali na wadau mbalimbali ili kuwezesha kufanya maamuzi sahihi katika matumizi endelevu ya rasilimali madini; uratibu wa majanga asili ya jiolojia na hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa na ustawi wa jamii.
2. MAFANIKIO YA GST KATIKA KIPINDI CHA MIAKA MINNE CHA SERIKALI YA AWAMU WA SITA.
Ndugu wanahabari na watanzania wote kwa ujumla, Katika kipindi cha miaka minne (2021 – 2025) cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, GST imeshuhudia mafanikio makubwa ambayo ni pamoja na:-
i) Kuongezeka kwa Makusanyo ya ndani kutoka wastani wa shilingi 1,251,428,472.91 mwaka 2021 hadi shilingi 2,394,211,348 mwaka 2023/2024, sawa na ongezeko la asilimia 91.32. Ongezeko hili limepatikana kupitia mageuzi na maboresho mbalimbali ya kiutendaji yaliyofanyika katika kipindi husika ambayo yaliongeza ubora wa huduma zitolewazo na GST;
ii) Kuongezeka kwa idadi ya sampuli zinazochunguzwa kutoka wastani wa sampuli 19,184 mwaka 2021 hadi sampuli 25,793 mwaka 2023/2024 sawa na ongezeko la asilimia 34.45. Ongezeko hili limetokana na maboresho makubwa ya maabara yaliyofanyika hasa katika ununuzi wa vifaa na mashine za kisasa za uchunguzi wa sampuli;
iii) Kuongezeka kwa bajeti ya Taasisi kutoka wastani wa shilingi bilioni 10 mwaka 2021/2022 hadi bilioni 110 mwaka 2024/2025 sawa na ongezeko la asilimia 1,000 kwa ajili ya kukamilisha majukumu mbalimbali ya Taasisi ikiwemo miradi ya maendeleo.
iv) GST ilikamilisha ugani wa jiolojia kwa lengo la kubaini miamba na madini yanayopatikana kwenye QDS 278 na 290 zilizopo Hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Nyerere na Pori la Akiba la Selous – katika sehemu ya Mikoa wa Lindi na Ruvuma); QDS mbili (2) mpya ambazo ni QDS 203 na 204) katika sehemu ya Mkoa wa Pwani na sehemu ndogo ya Mkoa wa Dar es salaam. Matokeo ya awali ya utafiti yanaonesha uwepo wa mchanga wa ujenzi, madini ya dhahabu na urani kwenye QDS 278 na 290; na uwepo wa madini ya kaolin, chokaa, udongo mfinyanzi, silica sand, madini tembo (heavy mineral sands) na metali adimu (rare earth elements) kwenye QDS 203 na 204; (note, QDS ni quarter degree sheet eneo lenye ukubwa wa kilometer 54 kwa 54)
Matumizi ya madini adimu
v) Kukamilisha ugani wa jiolojia na jiokemia kwa lengo la kubainisha mikondo ya madini kwa QDS 125 (iliyopo katika sehemu ya Wilaya za Kiteto, Chemba na Chamwino) na QDS 126 (iliyopo katika sehemu ya Wilayani ya Kiteto). Ugani huo ulibaini uwepo wa madini ya chokaa;
vi) GST kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilikamilisha utafiti na uchoraji wa ramani ya jiolojia ya visiwa vya Zanzibar (Unguja na Pemba); ikumbukwe kuwa visiwa vya Zanzibar havijawai kufanyiwa utafiti huo wa jiolojia. Matokeo ya utafiti huo yamebaini uwepo wa miamba ya chokaa yenye ubora wa kutengeneza saruji, madini tembo (heavy mineral sands), madini ya silica, strontium, vyanzo vya maji ardhi, maeneo yenye vivutio vya utalii wa jiolojia na maeneo hatarishi kwa majanga ya asili ya jiolojia.
Uchukuaji wa sampuli za mchanga wa bahari kwa ajili ya kuchunguzi madini tembo (heavy minerals sands) katika Kisiwa cha Unguja na Pemba
vii) Kuhuisha ramani ya jiolojia ya Wilaya ya Mahenge na kuibua maeneo mapya yenye madini ya kinywe (graphite), vito, dhahabu na marble baada ya kufanya utafiti maalumu mwezi Oktoba mwaka 2022 wa jiolojia katika Wilaya hiyo;
viii) Kukamilika kwa utafiti na uhakiki wa taarifa za uwepo wa madini katika mikoa ya Arusha, Manyara, Lindi, Mtwara na Kilimanjaro. Kukamilika kwa utafiti huo kulisaidia kuboresha ramani za uwepo wa madini katika mikoa hiyo, kanzidata ya madini na Kitabu cha Madini Yapatikanayo nchini Tanzania;
ix) Utafiti wa madini ya viwandani ulikamilika na jumla ya madini viwanda 44 yalibainishwa na miongoni mwao yakiwemo madini viwanda ambayo ni mkakati kidunia (critical minerals) kama vile kinywe;
x) Utafiti wa madini ya helium katika mikoa ya Arusha, Manyara, Dodoma, Singida na Shinyanga ambapo kiwango cha helium kilibainika kwenye chemchem za majimoto zinazofaa kwa hatua ya utafiti wa kina katika maeneo ya Ziwa Natron na ziwa Eyasi- Arusha, Masware-Babati, maeneo ya Kondoa, Tarkwa na Gonga – Dodoma na Ibadakuli-Shinyanga.
Upimaji wa gesi ya helium katika eneo ya Ziwa Eyasi-Karatu
xi) Kukamilisha mapitio ya vitabu viwili (2) ambavyo ni Kitabu cha Madini yapatikanayo nchini Tanzania toleo la tano na Kitabu cha Madini Viwanda toleo la pili. Vitabu hivyo vimechapishwa na kusambazwa kwa wadau. Vitabu hivyo vinataarifa mpya juu ya maeneo yenye madini nchini na hivyo inatarajiwa kuchochea uwekezaji katika Sekta ya Madini;
Kitabu cha Madini yapatikanayo Tanzania
xii) GST ilikamilisha utafiti maalumu wa jiolojia, jiofizikia na jiokemia uliofanyika kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo Wilayani Biharamulo Mkoa wa Kagera na kubaini uwepo wa madini ya kaolini;
xiii) GST ilikamilisha utoaji wa mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini 2,733 kuhusu uchukuaji wa sampuli wakilishi na utambuzi wa jiolojia ya maeneo yenye uwepo wa madini. Mafunzo yalifanyika katika mikoa ya Lindi, Morogoro, Geita na Mwanza;
xiv) Kupata ithibati za njia nyingine mbili za uchunguzi wa sampuli za madini na kufikisha jumla ya njia tatu zenye Ithibati. Njia hizo ni uchunguzi wa sampuli za dhahabu kwa njia ya kemikali (Aqua Regia) na upimaji wa kiwango cha majivu katika makaa ya mawe kwa njia ya tofauti ya uzito (gravimetric). Kupatikana kwa ithibati hizo kumekuwa na manufaa mengi kwa Taifa ikiwemo; kupanua wigo wa majibu ya uchunguzi unaofanywa na maabara ya GST mpaka kutambulika kimataifa; kuongezeka kwa idadi ya sampuli zinazoletwa katika maabara ya GST kwa ajili ya uchunguzi, kuongezeka kwa makusanyo yanayotokana na huduma za maabara.
Aidha, baaada ya ukaguzi uliofanyika mwezi machi, 2025 kupitia chombo kinachotoa Ithibati (SADCAS), maabara ya GST imeendelea kukidhi vigezo vya kuendelea kubaki na ithibati kwa kipindi kingine cha miaka mitano mpaka Oktoba, 2029.
xv) Taasisi imefanikiwa kupata kibali cha ajira na kukamilisha taratibu zote za ajira na kuwezesha watumishi 24 katika kada mbalimbali kuajiriwa na kuripoti kazini. Aidha, katika bajeti ya 2024/2025 Taasisi imepata kibali cha kuajiri watumishi wengine 34, taratibu za ajira zinaendelea katika mamlaka ya ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira.
xvi) Maboresho ya mazingira ya kazi na vitendea kazi yamefanyika kwa kiwango kikubwa. Vitendea kazi na vifaa vya kisasa vilivyonunuliwa katika kipindi husika ni pamoja na:-
a) Mashine za mionzi za XRD na XRF kwa ajili ya uchunguzi wa sampuli za miamba na udongo;
b) tanuru kubwa la kisasa la uchunguzi wa sampuli za dhahabu lenye uwezo wa kuchunguza sampuli 50 kwa mkupuo kwa muda wa saa moja ikilinganishwa na uwezo wa sampuli 16 kwa mkupuo kwa muda wa saa moja kwa tanuru lililokuwepo;
c) vifaa vipya ambavyo ni Abem Terrameter LS2 (1), Abem Terraloc Pro 2 (1), GDD IP Receivers (3), Electromagnetic machine Promis 10 (1), Hanna Multiparameter (2), Dipper T (2). Upatikanaji wa vifaa hivi utaiwezesha Taasisi kuwa na timu za ufanyaji tafiti kati ya tatu mpaka tano kutegemeana na mahitaji ya wateja ukilinganisha na timu moja hapo awali. Pia, kwa uwepo wa vifaa hivyo, Taasisi itaweza kufanya tafiti za madini ya kinywe (graphite), shaba (copper) na nickel kwa ufanisi mkubwa pamoja na tafiti za maji na upimaji wa ubora wa maji na kina chake tofauti na awali ambapo Taasisi haikuwa na uwezo huo.
xvii) GST iliongeza mashirikiano na Taasisi za ndani na nje ya nchi kwa lengo la kubadilishana uzoefu na teknolojia katika masuala ya utafiti wa madini. Taasisi ambazo GST inashirikiana na imeingia MoU nazo ni pamoja na Vyuo Vikuu vya Dodoma na Dar es Salaam, Shirika la Taifa la Madini (STAMICO), Taasisi za Jiolojia za Korea Kusini, Urusi, Finland na Burundi.
3. Mwelekeo wa GST kwa mwaka 2025/2026
i) Kufanya utafiti wa kina wa jiofizikia kwa kutumia ndege ili kuongeza eneo la nchi lililofanyiwa utafiti huo kutoka asilimia 16 ya sasa hadi asilimia 34. (utafiti huo unatarajiwa kufanyika katika eneo lenye ukubwa wa asilimia 18 ya eneo lote la nchi yetu); Lengo la Serikali ni kufika asilimia 50 ifikapo mwaka 2030. Utafiti huo ukikamilika utakuwa na manufaa mengi kwa nchi yetu katika sekta za madini, kilimo, maji, mazingira, mipango miji na sekta ya ujenzi;
Mgawanyo wa maeneo yanayopendekezwa kufanyiwa utafiti wa jiofizikia
Kabla ya maandalizi haya, tukumbuke kwamba nchi yetu imefanyiwa utafiti wa jiofizikia kwa njia ya kurusha ndage katika viwango hivi:
Low resolution (ground clearance ya 200 - 250m line spacing ya 1km) kwa asilimia 100%
High resolution (ground clearance ya 40 - 60m line spacing ya 200m) kwa asilimia 16%
ii) Kuendelea kuboresha huduma na utendaji kazi wa GST kwa kuwaendeleza watumishi zaidi kupitia mafunzo, kununua vifaa vya kisasa vya kufanya uchunguzi wa sampuli za madini kupitia maabara na vya kufanya tafiti za madini ikiwemo helkopta. Kukamilika kwa ununuzi wa Helikopta hiyo kutaongeza kasi ya tafiti za jiofizikia ambazo ni muhimu kujua tabia za miamba na rasimali nyingine zinazopatina chini ya tabaka la juu la ardhi ikiwemo madini na maji;
iii) Kujenga maabara ya kisasa (state of art labaoratory) katika mkoa wa Dodoma kwa ajili kuimarisha uchunguzi wa sampuli za madini nchini ili kuchochea shughuli za utafiti nchini na hivyo kuhamasisha ukuaji wa Sekta ya Madini. Maabara husika itakuwa na vifaa vya kisasa na itaweza kufanya uchunguzi wa sampuli za madini nyingi zaidi ikiwemo zinazojumuisha madini ya kimkakati na madini muhimu;
Maabara ya kisasa ya uchunguzi wa sampuli mbalimbali
iv) Kusogeza huduma karibu zaidi na wachimbaji wa madini ikiwemo wachimbaji wadogo wa madini. Katika eneo hili Serikali imepanga kuanza ujenzi wa majengo ya kisasa ya ofisi na maabara katika Mikoa ya Mbeya na Geita. Ujezi wa maabara hizo ukikamilika utasaidia kuharakisha shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini katika maeneo tajwa na kuwasaidia wachimbaji wadogo kuongeza tija na vipato vyao katika kazi zao kwani watachimba kwa uhakika na sio kubahatisha tena;
Ofisi na Maabara ya GST Mkoani Geita
Ofisi na Maabara ya GST Wilayani Chunya
v) Kukamilisha ujenzi wa mfumo wa usimamizi wa Kanzidata ya taifa ya taarifa za madini. Kukamilika kwa mfumo huo utarahisisha usambazaji wa taarifa hizo kwa wadau na hivyo kuchochea uwekezaji katika Sekta ya Madini.
4. HITIMISHO
Katika kipindi cha miaka minne (2021 – 2025) ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, GST imeshuhudia mageuzi na maboresho makubwa katika utoaji wa huduma zake na utendaji kazi wake kwa ujumla. Mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali pamoja na utayari wa viongozi wetu kuona GST inaimarika zaidi kwa ukuaji endelevu wa Sekta ya Madini.
Kwa niaba ya Bodi, Menejimenti na watumishi wa GST naomba kuchukua fursa hii kumshukuru tena Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuiwezesha GST kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi na kupata mafanikio hayo makubwa. Pia, nimshukuru sana Mhe. Antony Peter Mavunde (Mb) Waziri wa Madini na Mhe.Dkt. Stephen Lemomo Kiruswa (Mb) Naibu Waziri wa Madini kwa maelekezo na ushirikiano wao mkubwa wanaoipatia Menejimenti ya GST. Aidha, kipekee namshukuru Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mha. Yahya Samamba, kwa ushauri na ushirikiano mkubwa kwa Taasisi ambao umeiwezesha kutekeleza majukumu yake kwa mafanikio makubwa.
Baada ya kusema hayo machache naomba kuwasilisha.
Notka Banteze
KAIMU MTENDAJI MKUU WA GST
Comments
Post a Comment