Barua ya Wazi kwa Mheshimiwa Rais

Mhandisi Manala Tabu Mbumba
  

Barua ya Wazi kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan
Kupitia Waziri wa Ujenzi na Wizara ya Uchukuzi

Mheshimiwa Rais,

YAH: OMBI LA UJENZI WA UWANJA WA NDEGE KATIKA MANISPAA YA KAHAMA

Kwa heshima na taadhima kubwa, naomba kuchukua nafasi hii kukushukuru na kukupongeza, Mheshimiwa Rais, kwa juhudi zako thabiti na za kipekee zinazolenga kuleta maendeleo kwa Watanzania wote. Katika moyo huo wa kuthamini maendeleo, ninakuandikia ombi hili muhimu nikiwa kama mwananchi mzalendo na mdau wa maendeleo ya Manispaa ya Kahama. Ombi langu kuu ni ujenzi wa uwanja wa ndege katika manispaa yetu, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kijamii kwa kiwango cha juu.

Manispaa ya Kahama, inayokadiriwa kuwa na wakazi wapatao milioni 1 kufuatia Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, imekuwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa uwanja wa ndege. Ukosefu huu unaleta vikwazo vya kiuchumi na kijamii, ambapo wakazi na wafanyabiashara wanakabiliwa na gharama kubwa za usafiri na muda mwingi wanapotumia viwanja vya ndege vya Shinyanga au Mwanza. Hali hii inakwaza juhudi za kuimarisha uchumi wa wananchi na kupunguza kasi ya maendeleo katika eneo hili lenye fursa kubwa za kiuchumi.

Kahama, ikiwa miongoni mwa wilaya zinazochangia kwa kiwango kikubwa katika Pato la Taifa kupitia sekta za madini, kilimo, na biashara, ina nafasi ya kipekee ya kufaidika na uwepo wa uwanja wa ndege. Uwanja huu utasaidia kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, na kuimarisha mapato ya serikali kupitia ada na kodi mbalimbali. Takwimu zinaonyesha kuwa uwekezaji katika miundombinu ya usafiri wa anga unachangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa, jambo ambalo linaweza kuleta mapinduzi makubwa kwa Kahama na nchi kwa ujumla.

Aidha, utekelezaji wa mradi huu utaleta ajira nyingi kwa wananchi wa Kahama, kuimarisha usafirishaji wa bidhaa za kilimo, madini, na biashara, na kuboresha maisha ya watu. Kwa kuwa Kahama ni kitovu cha vitega uchumi, uwekezaji huu utaongeza thamani ya mnyororo wa uchumi wa eneo hili na kuchangia maendeleo endelevu ya taifa.

Kwa kuzingatia changamoto zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa mradi huu, naomba pia kuwasilisha mapendekezo yafuatayo:

1. Kutathmini na kupanua uwanja wa ndege wa Buzwagi: Uwanja huu, ambao tayari ni mali ya serikali, unaweza kufanyiwa upanuzi ili kutosheleza mahitaji ya usafiri wa anga kwa wakazi wa Kahama na maeneo jirani.

2. Kupitia upya ratiba za ndege: Kuongeza idadi ya safari za ndege zinazotumia uwanja wa Buzwagi kwa wiki, ili kupunguza gharama za usafiri kwa wakazi wa Kahama wanaohitaji huduma za anga.

Mheshimiwa Rais, kwa dhati kabisa, naomba serikali yako sikivu ifanyie kazi ombi hili kwa haraka kwa ajili ya ustawi wa wananchi wa Kahama na maendeleo ya taifa kwa ujumla. Nakutakia kila la heri katika utekelezaji wa majukumu yako mazito kwa maslahi ya mapana ya Watanzania.

Wako katika ujenzi wa taifa,  
Mhandisi Manala Tabu Mbumba
Mdau wa Maendeleo, Kahama

Comments

Popular posts from this blog

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?

UNAMKUMBUKA AMINA CHIFUPA WA MPAKANJIAA.

KADA MGEJA AHUDHURIA MAZIKO YA MAMA MZAZI WA MWANDISHI MWANDAMIZI WA HABARI KAHAMA