Ushuhuda wa Kusikitisha Wafichua Hatari ya Zebaki kwa Wachimbaji Wadogo Kahama



Na Napaul Kayanda, Kahama


Mhandisi Teostine Mwasha, Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Kuendeleza Uchimbaji Mdogo Tanzania, ameanza kampeni maalum ya kuelimisha jamii kuhusu athari mbaya za zebaki, kemikali inayotumika katika ukamataji wa dhahabu. Taasisi hiyo inalenga kuboresha mazingira ya kazi katika sekta ya uchimbaji mdogo kwa kuhakikisha wachimbaji wadogo wanatumia zebaki kwa njia salama ili kupunguza madhara yake.

Kwa sasa, Mhandisi Mwasha na timu yake wanahamasisha matumizi sahihi ya zebaki, kwa kuwa kemikali hii inaweza kusababisha madhara makubwa kwa afya ya binadamu, hususan kwa wale wanaoishi karibu na maeneo ya uchimbaji. Ameeleza kuwa serikali ya Tanzania imelidhia Mkataba wa Minamata unaolenga kupunguza madhara ya zebaki kwa asilimia 30 ifikapo mwaka 2030.

Akizungumza kuhusu jitihada zao, Mhandisi Mwasha amesema kwamba wao kama taasisi wanahusika moja kwa moja katika kuielimisha jamii, hususan wachimbaji wadogo na familia zinazozunguka migodi. Amefafanua kuwa zebaki inaweza kusababisha madhara kama misuli kutetemeka, maluelue, na kwa wanawake wajawazito, hali hii inaweza kupelekea mimba kuharibika.

Katika ushuhuda wa kusikitisha, Mhandisi Mwasha alieleza







kilichomhamasisha kuendeleza elimu hii: "Nilipokuwa Uganda, nilikutana na mama aliyekuwa akitumia zebaki wakati akiwa mjamzito. Alitueleza jinsi alivyoathirika, na tulipomwomba alete mtoto wake, niliona kwa macho yangu jinsi shingo ya mtoto ilivyoathirika. Hii ilinifanya nitambue ukubwa wa tatizo na umuhimu wa kutoa elimu hii."

Kwa sasa, elimu inayopewa kipaumbele ni kuwafundisha wachimbaji wadogo na jamii kwa ujumla jinsi ya kujikinga na madhara ya zebaki kwa kutumia vifaa vya kujikinga kama glovu na gambuti, na kuhakikisha wanapochoma dhahabu wanavaa vifaa kinga sahihi. Hii itasaidia kupunguza madhara mpaka suluhisho mbadala litakapopatikana.

Mhandisi Mwasha anatoa wito kwa wachimbaji wadogo kuacha mazoea ya kutumia zebaki kiholela na kuzingatia maelekezo ya kiafya. Anawaomba pia wazazi, walimu, na wahudumu wa afya walioko karibu na maeneo ya uchimbaji wa dhahabu kuchukua tahadhari stahiki ili kuwalinda watoto na jamii dhidi ya hatari zinazotokana na zebaki.

"Wachimbaji wadogo waache mazoea, zebaki ni hatari sana. Tusiwasubiri watu wafe ndipo tuchukue hatua. Sisi tulioona madhara yake tunapaswa kuwa mabalozi wa kuhamasisha mapambano dhidi ya kemikali hii hatari," alisisitiza Mhandisi Mwasha.

Comments

Popular posts from this blog

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?

UNAMKUMBUKA AMINA CHIFUPA WA MPAKANJIAA.

KADA MGEJA AHUDHURIA MAZIKO YA MAMA MZAZI WA MWANDISHI MWANDAMIZI WA HABARI KAHAMA