UONGO FITNA ZAMPONZA MBUNGE MPINA ATAKUWA NJE YA BUNGE KWA VIKAO 15

Spika Dkt. Tulia Ackson na  Katibu wa Bunge  Nenelwa Mwihambi wakibadilishana mawazo wakati taarifa maalum ya bunge kuhusu Mbunge Mpina ikisomwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge Ally Juma Makoa.


 

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

 


 

BUNGE LA TANZANIA

 

 

 

TAARIFA YA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA

   MADARAKA YA BUNGE KUHUSU:-

 

1.      MAONI YA KAMATI KUHUSU USHAHIDI WA MHE. LUHAGA JOELSON MPINA (MB) KUTHIBITISHA TUHUMA DHIDI YA WAZIRI WA KILIMO, MHE. HUSSEIN MOHAMED BASHE (MB) KUSEMA

          UONGO BUNGENI NA KULIPOTOSHA BUNGE

 

             NA

 

2.   TUHUMA DHIDI YA MHE. LUHAGA JOELSON MPINA (MB)

         KUDHARAU MAMLAKA YA SPIKA, BUNGE NA

            MWENENDO WA SHUGHULI ZA BUNGE

 

 

 

 

OFISI YA BUNGE,

DODOMA.

 

JUNI, 2024

TAARIFA YA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA

 MADARAKA YA BUNGE KUHUSU:-

 

1.                 MAONI YA KAMATI KUHUSU USHAHIDI WA MHE. LUHAGA JOELSON MPINA (MB) KUTHIBITISHA TUHUMA DHIDI YA WAZIRI WA KILIMO, MHE. HUSSEIN MOHAMED BASHE (MB) KUSEMA UONGO BUNGENI NA KULIPOTOSHA BUNGE

 

NA

 

2.    TUHUMA DHIDI YA MHE. LUHAGA JOELSON MPINA KUDHARAU MAMLAKA YA SPIKA, BUNGE NA MWENENDO WA SHUGHULI ZA BUNGE

 

1.0          UTANGULIZI

1.1          Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Fasili ya 4(2) na (3) ya Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Februari, 2023 naomba kuwasilisha Mbele ya Bunge lako Tukufu taarifa ya Kamati kuhusu:

a)       Maoni ya Kamati kuhusu ushahidi wa Mhe. Luhaga Joelson Mpina kuthibitisha Tuhuma dhidi ya Mhe. Hussein Mohamed Bashe kusema uongo Bungeni na kulipotosha Bunge.

b)       Uchunguzi wa Kamati kuhusu tuhuma dhidi ya Mhe. Luhaga Joelson Mpina kudharau Mamlaka ya Spika na Mwenendo wa Shughuli za Bunge.

 

1.2          Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kukushukuru wewe binafsi kwa weledi, busara na hekima unazozitumia katika kuliongoza Bunge letu kwa ufanisi mkubwa. Aidha, napenda kumshukuru Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wenyeviti wote wa Bunge letu kwa Miongozo na maelekezo wanayoipa Kamati yangu katika kutekeleza majukumu yake.

 

1.3          Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 18 Juni, 2024 kwa mamlaka uliyonayo chini ya Kanuni ya 84(2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Februari 2023 na Fasili ya 4(1) (a) na (b) ya Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Februari, 2023, ulielekeza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kutoa maoni na kutoa ushauri kuhusu masuala yaliyotajwa hapo juu. Hadidu za rejea zilieleza:-

 

a)       Kutafakari jambo lililofanywa na Mhe. Luhaga Joelson Mpina na kutoa maoni na mapendekezo ya nini kifanywe na Bunge;

 

 

b)       Kufanyia kazi ushahidi uliowasilishwa (kwa Mhe. Spika) na kutoa maoni iwapo ushahidi huo unathibitisha tuhuma kwamba Waziri wa Kilimo amesema uongo Bungeni na nini kifanywe na Bunge; na

c)       Kuwasilisha Taarifa kwa Spika Jumatatu tarehe 24 Juni, 2024.

 

2.0          CHIMBUKO LA SHAURI

2.1          Mheshimiwa Spika, tarehe 4 Juni, 2024 katika Kikao cha 40 cha Mkutano wa Kumi na Tano wa Bunge wakati wa mjadala wa Hoja ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025, Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Mohamed Bashe, (Mb) pamoja na mambo mengine, alichangia kuhusu upungufu wa sukari nchini (gap sugar) kwamba, kampuni na viwanda vya sukari nchini, vilivyopewa dhamana na Serikali ya kuhakikisha kunakuwa na sukari ya kutosha nchini, vimeshindwa kutekeleza wajibu huo kwa kushindwa kuagiza na kusambaza sukari kutoka nje ya nchi kama ilivyotakiwa. 

 

2.2          Mheshimiwa Spika, Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Mohamed Bashe alieleza kuwa, hali hiyo imesababisha kuendelea kuwepo kwa tatizo la uhaba wa sukari nchini. Aidha, Waziri wa Kilimo

 

Mhe. Hussein Mohamed Bashe alieleza kuwa jambo hilo lilichangia bei ya sukari nchini kupanda hadi kufikia shilingi 10,000/= kwa kilo moja. Miezi michache iliyopita Mhe. Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Mohamed Bashe alieleza kuwa kutokana na hali hiyo Serikali imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha sukari ya kutosha inakuwepo nchini. Miongoni mwa hatua hizo ni kuipa idhini Wakala wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuingiza sukari nchini, kutoa vibali kwa makampuni ili kuagiza sukari na kusamehe kodi na ushuru kwa sukari itakayoagizwa nje ya nchi na makampuni na viwanda vya sukari. Maelezo hayo yapo kwenye Kumbukumbu Rasmi za Bunge za tarehe 04 Juni, 2024 zinazomnukuu Mhe. Hussein Bashe (Mb) akisema ifuatavyo:-

 

Mheshimiwa Spika, mwezi Januari na Februari nchi hii sukari ilifika shilingi 10,000, makampuni na viwanda hivi tunavyoviita tuvilinde vilipewa vibali vya kuingiza sukari, havikuingiza sukari….mwaka jana nchi hii ilikuwa ina gap sugar ya tani 60,000 tulimpa Kagera Sugar, tulimpa Mtibwa, tulimpa Bagamoyo, tulimpa TPC, hakuna aliyeingiza hata kilo moja, mlitaka nikae naangalia? Tulitumia nini? Tumeenda kubadili Kanuni za National Food Reserve Agency kuruhusu NFRA kuwa na mandate ya kuingiza sukari (makofi). Mimi niingie on record na nitatoa takwimu kwa nini tumetoa vibali kupitia NFRA vya tani 400,000, numbers don’t lie….

 

 

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe elimu ndogo, gap sugar huwa tunaitoa kwa ajili ya window ya mwezi Machi, Aprili na Mei, miezi mitatu. Kutokana na mvua za El-Nino, baada ya TMA kutoa utabiri wa hali ya hewa, tuliyapatia makampuni na viwanda walete tani 50,000, mpaka mwezi Februari walikuwa hawajaleta hata kilo moja ya sukari na walipoingiza walifungia kwenye ma-godown yao……mwaka jana tulivyowapa vibali vya kuingiza na mpango mkakati ukiongozwa na TSPA, Tanzania Sugar Association ambaye Mwenyekiti wa Taasisi hii ni owner wa Mtibwa na Kagera Sugar…tumekaa Disemba, hakuna kilo moja iliyoingia, Januari, hakuna kilo moja iliyoingia. 

 

Mwishoni mwa Januari wameingiza tani 250 wakati wakifahamu sugar na buffer stock ya mwaka wa nyuma wa uzalishaji hawakuingiza hata kilo moja, kwa hiyo taifa lilikuwa halina sukari…tumewapa bei elekezi … shilingi 2300 na 2500. Waliwauzia distributors kwa shilingi 2800 na 3000 na sukari waliyoingiza bandarini tuliyowapa VAT exemption, hata wao tumewapa VAT exemption. Wameingiza bandarini wanaenda kuiuza mfuko wa kilo 50 x- Dar es Salaam shilingi 150,000 mpaka 160,000 mlaji wa Nzega ale kwa shilingi ngapi?”

 

2.3          Mheshimiwa Spika, wakati Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Mohamed Bashe akizungumza, Mhe. Luhaga Joelson Mpina, (Mb) alipata nafasi ya kutoa Taarifa kuhusu mchango huo. Taarifa ya Mhe. Luhaga Joelson Mpina ilieleza kuwa, Waziri wa

 

Kilimo Mhe. Hussein Mohamed Bashe alikuwa analidanganya na kulipotosha Bunge kwa sababu, maelezo hayo hayana ukweli wowote na alikiuka Sheria katika zoezi la kutoa vibali vya kuagiza sukari na kwa kusamehe kodi ya Serikali. Kwa mujibu wa Kumbukumbu Rasmi za Bunge za tarehe 4 Juni, 2024 Mhe. Luhaga Mpina (Mb) alinukuliwa akisema ifuatavyo:-

 

 Mheshimiwa Spika, kwa kuwa zipo taarifa za wazi kwamba Waziri hata hao waliosema kwamba aliwapa kibali cha kuagiza sukari, hakutangaza tender yoyote na haijulikani aliwapataje, lakini nyaraka zote zipo, na kuwa kuagiza sukari zaidi ya gap sugar ni makosa kisheria. Na kwa kuwa pia kuwaruhusu watu ambao hawaruhusiwi kwa mujibu wa Sheria tuliyonayo sasa hivi ya sukari ni makosa kisheria….Uagizaji wa gap sugar huwa unakuwa established na ile Timu ya Bodi ya Sukari ambayo inafanya na inawajulisha na wadau.

 

Sasa Waziri anasema kwamba ametoa Kibali cha tani 410,000 kama gap sugar…mpaka sasa hivi taarifa zilizopo katika hiyo tani 410,000 zimeshaingia tani 220,000…huu ni mwezi wa sita…gap sugar ambayo imekuwa established na hiyo Timu ya ushauri ya Bodi ya Sukari ni tani 120,000 siyo tani 410,000 na nchi yetu haijawahi kuwa na importation ya namna hiyo hata kama uzalishaji huo anaousema yeye.”

 

2.4          Mheshimiwa Spika, baada ya Taarifa hiyo ya Mhe. Luhaga Joelson Mpina (Mb) ulitoa ufafanuzi kuhusu masharti ya Kanuni ya 70 (1) (2) na (3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Februari, 2023. Inayosimamia suala la Mbunge ‘Kutosema Uongo Bungeni’. Kanuni inamtaka Mbunge yeyote anayetoa tuhuma kwamba Mbunge mwingine anasema uongo Bungeni, hutakiwa kuwasilisha ushahidi ili kuthibitisha uongo huo. Hivyo, kwa kutumia Kanuni hiyo, ulielekeza Mhe. Luhaga Joelson Mpina awasilishe ushahidi kuthibitisha tuhuma kwamba Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Mohamed Bashe amelidanganya Bunge tarehe 14 Juni, 2024.

 

2.5          Mheshimiwa Spika, Tarehe 14 Juni, 2024 Mhe. Luhaga Joelson Mpina aliwasilisha Ofisi ya Bunge barua yenye nyaraka za ushahidi kama ulivyoelekeza. Hata hivyo, kabla Bunge halijachukua hatua yeyote ya kujiridhisha kuhusu ushahidi huo, Mhe. Luhaga Joelson Mpina aliitisha Mkutano wa Waandishi wa Habari ambao aliutumia kueleza na kufafanua maudhui ya ushahidi aliouwasilisha kwa Spika.

 

2.6          Mheshimiwa Spika, Kwa mamlaka uliyonayo chini ya Kanuni ya 4 ya Nyongeza ya Nane na Kanuni ya 84 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, ulielekeza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya

 

2.7          Bunge itoe maoni kuhusu ushahidi uliowasilishwa na Mhe. Luhaga Joelson Mpina na kufanya uchunguzi wa kitendo cha Mhe. Luhaga Joelson Mpina kuitisha Mkutano wa vyombo vya habari na kuzungumzia ushahidi aliouwasilisha kwa Spika. Aidha, ulielekeza Kamati kutoa mapendekezo kwa Bunge kuhusu hatua za kuchukua. Kamati ilielekezwa kukamilisha Taarifa ya Kamati ifikapo Jumatatu tarehe 24 Juni, 2024

 

3.0          UCHUNGUZI WA KAMATI

 

MAONI YA KAMATI KUHUSU USHAHIDI WA MHE. LUHAGA JOELSON MPINA KUTHIBITISHA TUHUMA DHIDI YA MHE. HUSSEIN MOHAMED BASHE KUSEMA UONGO BUNGENI NA KULIPOTOSHA BUNGE

3.1          Mheshimiwa Spika, katika uchunguzi wa suala hili Kamati iliwaita mashahidi ambao ni Mhe. Luhaga Joelson Mpina na Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Mohamed Bashe. Mashahidi hao waliitwa kwa summons zilizowataka kufika kwenye Kamati kutoa Ushahidi na kuwasilisha nyaraka. Mashahidi walitii Wito wa Kamati na walitoa ushirikiano kwa kutoa ushahidi ulioisaidia Kamati kupata maoni kuhusu uchunguzi uliokuwa umefanywa na Kamati.

 

 

3.2          Mheshimiwa Spika, Kamati ilifanya uchunguzi wake kuhusu Taarifa iliyotolewa Bungeni kumlalamikia Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Mohamed Bashe kwamba alisema uongo Bungeni. Kamati imezingatia maelezo yaliyotolewa na Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Mohamed Bashe na yaliyotolewa na Mhe. Luhaga Joelson Mpina pamoja na vielelezo vyote walivyoviwasilisha mbele ya Kamati.

 

3.3    Mheshimiwa Spika, uchunguzi wa Kamati ulijikita katika Taarifa kuhusu uongo uliosemwa Bungeni tarehe 14 Juni, 2024 iliyotolewa na Mhe. Luhaga Joelson Mpina kuhusu maelezo yaliyotolewa na Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Mohamed Bashe kwa kufanya rejea ya Hansard.

 

3.4          Mheshimiwa Spika, baada ya uchambuzi wa hoja zote zilizowasilishwa na pande zote mbili uchambuzi na maoni ya Kamati ni kama ifuatavyo:-

 

a)       Mhe. Luhaga Joelson Mpina alisema kuwa Waziri alilidanganya Bunge kwa kusema mwaka jana nchi hii ilikuwa na gap ya tani 60,000 tulimpa Kagera Sugar, tulimpa Mtibwa, tulimpa Bagamoyo, tulimpa TPC, hakuna aliyeingiza hata kilo moja. Alidai kuwa Viwanda viliingiza sukari kwa mwaka huo. Waziri aliieleza Kamati kuwa ni

kweli Viwanda alivyovitaja havikuingiza hata kilo moja. Alifafanua kuwa walioingiza sukari ni kiwanda cha Kilombero na Kampuni nyingine ambayo si mzalishaji. Hivyo maelezo ya Waziri yalikuwa ya ukweli kama ambavyo alivyoeleza.

 

Aidha, Mhe. Luhaga Joelson Mpina alieleza kuwa Waziri alidanganya kwa kusema sugar gap kwa mwaka 2022/2023 ilikuwa tani 60,000. Alitoa ushahidi kuwa Bodi ya sukari ilieleza kuwa sugar gap ni tani 30,000. Waziri katika utetezi wake alileta ushahidi wa Muhtasari wa Kikao cha Waziri na Wadau wa Sukari cha tarehe 13 Februari, 2023 ambacho kiliidhinisha gap sugar ya tani 30,000 na buffer stock ya tani 30,000 hivyo kufanya jumla ya upungufu wa tani 60,000 za sukari. Kamati baada ya kupitia vielelezo hivyo imejiridhisha kuwa maelezo na vielelezo vya Mhe. Luhaga Joelson Mpina yalikuwa sahihi kwa upande wa sugar gap na maelezo ya Waziri hayakulipotosha Bunge kwakuwa aliongelea gap sugar pamoja na buffer stock.

 

b)       Mheshimiwa Spika, Mhe. Luhaga Joelson Mpina alimtuhumu Mhe. Waziri kuwa amelidanganya Bunge kwa kusema wamebadili kanuni za National Food Reserve Agency kuruhusu NFRA kuwa na mandate ya kuingiza sukari wakati hakuna Tangazo la Serikali (GN) iliyotangazwa kuipa NFRA mandate ya kuingiza sukari. Waziri aliieleza Kamati kuwa walitumia Sheria ya Usalama wa Chakula Sura ya 249 kukabiliana na uhaba wakati wa dharura kupitia NFRA. Alisema kuwa wameanza mchakato wa kubadilisha Sheria ili NFRA waruhusiwe kuagiza, kuhifadhi na kusambaza sukari hata kwa kipindi kisicho cha dharura na mchakato huo ulianza kwa kutoa Tangazo la Serikali Na. 225B la tarehe     01 Aprili, 2024.

 

c)       Mheshimiwa Spika, Kamati ilipitia kifungu cha 14 cha Sheria ya Tasnia ya Sukari kuhusu wanaoruhusiwa kuagiza sukari na kupitia kifungu cha 15 cha Sheria ya Usalama wa Chakula, 1991 na kubaini kuwa kwa wakati wa dharura kama iliyojitokeza Sheria ya Usalama wa Chakula inakuwa na nguvu zaidi kuliko Sheria ya Tasnia ya Sukari.

 

Kamati ilipata nafasi ya kujiridhisha kuhusu uwepo wa GN Na. 225B ya tarehe 1 Aprili, 2024 na kupitia Muswada wa Sheria ya Fedha iliona mapendekezo ya marekebisho yaliyoelezwa na Waziri. Kupitia Hansard na maelezo ya Waziri Kamati ilikuwa na maoni kuwa hakuna uongo

 

uliozungumzwa na kwamba hakuna ukiukwaji wa Sheria.

 

d)       Mheshimiwa Spika, Mhe. Luhaga Joelson Mpina alimtuhumu Waziri kwa kutoa vibali vya tani 410,000 kinyume na sugar gap iliyoidhinishwa ya tani 100,000. Waziri alieleza kuwa Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Sukari ilibaini upungufu ni tani 220,000 hadi Aprili, 2024. Hata hivyo, kutokana na tathmini iliyofanywa na Wizara ilibainika kuwa uzalishaji uliathirika kutokana na elnino na kutokana na uhaba uliokithiri kwa miezi ya Januari na Februari, 2024 nchi ilihitaji kuwa na uhakika wa sukari kwa ziada “buffer stock” hivyo kuidhinisha makisio ya gap sugar ya tani 410,000.

 

Waziri aliileza Kamati yetu kuwa vibali vilitolewa kwa tani 220,000 pekee na kwamba mpaka sasa zimeingia tani 180,000. Tani zilizosalia bado hazijatolewa vibali na kwamba wataendelea kufuatilia mwenendo wa uzalishaji na

 

upatikanaji wa sukari nchini kabla ya kuamua kutoa vibali vingine au kusitisha kabisa uagizaji kwa mwaka 2023/2024.

 

e)       Mheshimiwa Spika, Kamati imeridhika kuwa Kiwango cha tani 100,000 alichokisema Mhe. Luhaga Mpina ni makisio yaliyofanyika mwezi Disemba mwaka 2023. Kiwango hicho kilifanyiwa marejeo (review) mwezi Aprili, 2024 ambapo Kamati ilioneshwa Muhtasari wa kikao cha Kamati ya Ufundi kilichobainisha ongezeko la sugar gap kutoka tani 155,000 hadi tani 220,000. Kiwango cha tani 410,000 alizozisema Waziri zilijumuisha mahitaji yaliyokadiriwa mwezi Aprili na tathmini iliyofanyika baadaye iliyobaini kuwa hadi Mei, 2024 viwanda havikuwa vimeanza uzalishaji hivyo mahitaji pamoja na buffer stock kufikia Disemba, 2024 ni tani 410,000 hivyo kutoa Idhini ya tani hizo.

 

f)         Mheshimiwa Spika, Mhe. Luhaga Joelson Mpina alimtuhumu Waziri alidanganya aliposema Makampuni na viwanda vilivyopatiwa vibali vya kuingiza sukari tani 50,000 hayakuwa yameingiza sukari hata kilo moja Februari na walipoingiza walifungia kwenye magodown yao. Mhe waziri mbele ya kamati alieleza kuwa makampuni yote aliyoyataja yalikuwa hayajaingiza sukari isipokuwa Kilombero sugar

 

ambayo iliingia tarehe 29 Januari, 2024 na kwenda sokoni tarehe 5 Februari, 2024. Kamati imepitia vibali vilivyotolewa kwa makampuni na viwanda na kubaini kuwa Idhini ilitolewa kuanzia 29 Disemba, 2023 vibali vimetolewa tarehe 4 Januari, 2024. Kwa mazingira haya, isingewezekana kuingiza sukari mwezi kwa Disemba. Katika Hansard Mhe. Waziri ameleza wazi kuwa mwishoni mwa Januari, Kilombero sugar iliingiza tani 250.

 

g)       Mheshimiwa Spika, Mhe. Luhaga Joelson Mpina alimtuhumu Waziri kuwa hakuwaita wenye viwanda kukaa nao kuhusu suala la sukari. Waziri amesema kuwa hakutakataa kukutana na wazalishaji isipokuwa aliwapa masharti ya kutangaza mawakala kwa kila mkoa na kufungua maghala kila mkoa kabla ya kukutana. Baada ya Kamati kusikiliza ushahidi iliridhika kuwa Waziri hakukutana nao kwakuwa hawakuwa wametekeleza masharti aliyokuwa amewapa.

 

h)       Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina anamtuhumu Waziri wa Kilimo kwa kukiuka Sheria wakati wa kutoa vibali kwa makampuni ambayo si wazalishaji wa

 

sukari bila kutangaza zabuni. Waziri alieleza kwamba vibali vilitolewa wakati wa dharura baada ya kufanya utafiti na kujiridhisha kuhusu uwezo wa kampuni hizo. Aidha, alieleza kuwa katika mazingira ya dharura na kwa kuzingatia kuwa fedha zinazotumika sio za umma, hakukuwa na ulazima wa kutumia Sheria ya Ununuzi. Vilevile, Waziri aliwasilisha ushahidi wa leseni za biashara na nyaraka za usajili wa Kampuni hizo zinazowaruhusu kufanya biashara ya sukari. Kamati imejiridhisha kwamba utaratibu uliotumika ulitokana na hali ya dharura.

 

UCHUNGUZI WA KAMATI KUHUSU TUHUMA DHIDI YA MHE. LUHAGA JOELSON MPINA KUDHARAU MAMLAKA YA SPIKA NA MWENENDO WA SHUGHULI ZA BUNGE.

3.5    Mheshimiwa Spika, baada ya kamati kupokea Hadidu za Rejea kuhusu kufanya uchunguzi wa tuhuma dhidi ya Mhe. Luhaga Joelson Mpina, tarehe 18 Juni, 2024 ilikutana kujadili na hatimaye ikaamua Mhe. Luhaga Joelson Mpina apewe Wito wa kufika mbele ya Kamati ili aweze kujibu tuhuma zinazomkabili.

 

3.6    Mheshimiwa Spika, Wito huo ulimtaka Mhe. Luhaga Joelson Mpina atoe maelezo ya kwanini asichukuliwe hatua kwa kukiuka Kifungu cha 26(d) (e) na 34(1)(g) cha Sheria ya Kinga, Madaraka na Hadhi za Bunge Sura ya 296 pamoja Kanuni ya 84(1) (j) na (k) ambazo zinakataza kudharau Mamlaka ya Spika na mwenendo wa shughuli za Bunge. Tarehe 19 Juni, 2024 Mhe. Luhaga Joelson Mpina alikabidhiwa Hati ya wito huo na kufika mbele ya Kamati.

 

3.7          Mheshimiwa Spika, Katika kushughulikia suala hili, ili Kamati iweze kufanya uchunguzi wa kina wa tuhuma hizo, ilijielekeza kwenye hoja za uchunguzi (issues) zifuatazo:

(a)       Je, ni kweli kwamba Mhe. Luhaga Joelson Mpina (Mb) aliitisha Mkutano na vyombo vya habari na kuzungumza kuhusu maudhui ya ushahidi aliouwasilisha bungeni kabla Bunge halijaufanyia kazi na kukamilisha uchunguzi wake?

(b)       Endapo hoja (a) itathibitika, Je, kitendo cha Mhe. Luhaga Joelson Mpina kuzungumza na Waandishi wa Habari kuhusu ushahidi alioupeleka kwa Spika ni kudharau mamlaka ya Spika na mwenendo wa shughuli za Bunge?

(c)       Endapo hoja (a) na (b) ni kweli, Je, ni hatua gani za kisheria zinazopaswa kuchukuliwa dhidi yake?

 

3.8          Mheshimiwa Spika, Katika uchunguzi wake, Kamati ilirejea Sheria, Kanuni za Kudumu za Bunge, Taarifa Rasmi za Bunge na ushahidi wa picha za video za Mkutano wa Waandishi wa Habari na Mhe. Luhaga Mpina. Rejea hizo ni:

(i)              Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977;

(ii)            Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Februari, 2023

(iii)          Kumbukumbu Rasmi za Bunge za Tarehe 4 Juni, 2024, tarehe 18 Juni, 2024;

 

(iv)          Ushahidi uliowasilishwa na Mhe. Luhaga Joelson Mpina kwa Spika;

(v)           Mahojiano na nyaraka za ushahidi zilizowasilishwa na Mhe. Luhaga Joelson Mpina alipokuwa mbele ya Kamati;

(vi)          Video ya tarehe 4 Juni, 2024 iliyoonesha majadiliano ya Bunge kuhusu mchango wa Waziri wa Kilimo Mhe. Hussen Mohamed Bashe; na

(vii)        Video inayomuonesha Mhe. Luhaga Joelson Mpina akiongea na Mkutano wa Waandishi wa Habari aliouitisha.

 

3.9          Mheshimiwa Spika, katika kujibu hoja ya kwamba Je, ni kweli kwamba Mhe. Luhaga Joelson Mpina (Mb) aliitisha Mkutano na vyombo vya habari na kuzungumza kuhusu maudhui ya ushahidi aliouwasilisha Bungeni kabla Bunge halijaufanyia kazi na kukamilisha uchunguzi wake? Kamati ilianza kuchunguza Shauri hili kwa kuangalia picha za video za Mkutano wa Waandishi wa Habari ulioitishwa na Mhe. Luhaga Mpina (Mb) tarehe 14 Juni, 2024. Sehemu ya maelezo ambayo Kamati iliyaona na kuyasikia kutoka kwenye video hiyo yalieleza kuwa:

 

“…kufuatia maagizo ya kiti nalazimika kuandaa maelezo na kuwasilisha kwa mheshimiwa Spika leo tarehe 14 Juni,2024 nikiwasilisha ushahidi wa vielelezo vya kuthibitisha uongo wa Waziri Bashe aliousema bungeni tarehe 4 Juni, 2024….Gap sugar iliyoidhinishwa kwa msimu wa mwaka 2022/2023 ni tani 30,000 sio 60,000 kama alivyosema Waziri wa Kilimo. Rejea barua ya Bodi ya Sukari Tanzania yenye Kumb. Ref.No.SBT/DGO/26-38 ya tarehe       29 Machi, 2023 iliyoandikwa na Mkurugenzi wa Bodi ya Sukari, Prof. Bengesi kwenda kwa Katibu Mtendaji wa TCS SADC…

Maelezo ya Waziri kwamba, uzalishaji ukashindikana katika nchi yetu kuanzia Oktoba, Novemba, Disemba, Januari, Februari na Machi…maelezo hayo ni uongo…taarifa ya TSPA inaonyesha uzalishaji wa Sukari mwaka 2023/2024 ambapo uzalishaji ulifikia tani 394,829 (Kiambatishwa No.6)….

 

Waziri hakusema ukweli, kwani hajawaita wazalishaji wa sukari ili akae nao kujadili changamoto zinazowakabili badala yake ni wazalishaji wa sukari waliomba kuonana na Waziri kupitia barua yenye Kumb. Na. TSPA/SI-Gen/27/01/2024 ya tarehe 14 Februari, 2024 iliyoandikwa na Katibu Mtendaji wa TSPA, Deo Lyato kwenda kwa Waziri wa Kilimo (Kiambatisho Na.9) …..waziri wa kilimo aliwajibu wazalishaji wa sukari nchini kwamba atakutana nao pale tu wazalishaji sukari watakapokuwa wamekamilisha kutekeleza masharti waliyopewa ya kujenga maghala kila mkoa……rejea barua yenye Kumb. Na. SBT/DGO/01/33-33 ya tarehe 20 Machi, 2024

 

3.10     Mheshimiwa Spika, Baada ya kuangalia video na kuchambua nyaraka zilizowasilishwa na Mhe. Luhaga Joelson Mpina kwa Spika, Kamati ilimuita Mhe. Luhaga Joelson Mpina ili aweze kutoa utetezi wake.

 

3.11     Mheshimiwa Spika, Mara baada ya Mhe. Luhaga Joelson Mpina kufika mbele ya Kamati alitoa maelezo kuwa Kamati haina mamlaka ya kusikiliza shauri kwa kuwa vifungu vilivyotajwa katika Hati ya Wito ambavyo ni 26(d)(e) na 34(1)(g) pamoja na Kanuni ya 84(1)(j) na (k) vinatofautiana na kifungu kilichotajwa katika Taarifa ya Spika ya tarehe 18 Juni, 2024 ambacho ni kifungu cha 29(d) na (e).  Kwa maoni yake, Mhe. Mbunge alieleza kuwa kifungu hicho ndicho Spika alikusudia kitumike kumshitaki.

 

3.12     Mheshimiwa Spika, Katika kupata jibu la hoja hii, Kamati ilirejea Sheria, Hansard na nakala halisi ya Taarifa ya Spika na kujiridhisha kuwa vifungu vilivyotumika katika Hati ya Wito aliyopewa Mhe. Luhaga Joelson Mpina ni sahihi na ndivyo vinavyoipa Mamlaka Kamati kufanya uchunguzi wake. Vifungu vilivyotajwa katika Hati ya Wito ni Kifungu cha 26(d)(e) na 34(1)(g) cha Sheria ya Kinga, Madaraka na Hadhi ya Bunge pamoja na Kanuni ya 84(1)(j) na (k) ambavyo ni vifungu vinavyoeleza makosa anayotuhumiwa kuyafanya. Kifungu cha 26 kinaeleza:-

 

“26. any person who-

(d)   shows disrespect in speech or manner towards the Speaker; or

(e)     does any other act of intentional disrespect to or with reference to the proceedings of the Assembly or of a Committee of the Assembly or to any person presiding at such proceedings, commits an offence.”

 

Kifungu cha 34 kinaeleza: -

“34.-(1) Any person who-

(g)     publishes, save by the general or special leave of the Assembly, any paper, report or other document prepared expressly for submission to the Assembly before the same has been laid on the table of the Assembly;

 

Commits an offence and on conviction is liable to a fine not exceeding five hundred thousand shillings or to imprisonment for a term not exceeding three years or to both.”

 

Vifungu tajwa vinazuia vitendo vya dharau kwa Spika na Mwenendo wa Shughuli za Bunge. Baada ya kuchambua vifungu hivyo Kamati iliona kuwa hoja ya kwamba Kamati haina mamlaka ya kusikiliza shauri dhidi yake ni hoja isiyo na nguvu kisheria. Kwa hali hiyo, Kamati ilifikia uamuzi kuwa inayo mamlaka ya kufanya uchunguzi wa shauri linalomkabili Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina.

 

3.14  Mheshimiwa Spika, Baada ya kujiridhisha kuhusu mamlaka ya Kamati, Kamati ilimtaka Mhe. Luhaga Joelson Mpina kutoa maelezo kuhusu tuhuma zinazomkabili. Katika maelezo yake, Mhe. Luhaga Joelson Mpina alikiri kuwa aliitisha Mkutano wa Waandishi wa Habari kueleza umma kwamba ametekeleza maelezo ya Spika kwa kupeleka ushahidi kwa Spika ili kuthibitisha tuhuma dhidi ya Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Mohamed Bashe kusema uongo Bungeni.

 

3.15  Mheshimiwa Spika, Kamati ilipomuhoji ni kwanini alivieleza vyombo vya habari ushahidi aliouwasilisha kwa Spika, Mhe. Luhaga Joelson Mpina aliieleza Kamati kuwa alichokiwasilisha kwa vyombo vya habari ni maelezo yake binafsi na siyo vielelezo vya ushahidi alivyopeleka kwa Spika ambavyo, kwa maoni yake, ndiyo ushahidi. Katika kufafanua jambo hilo, Mhe. Luhaga Joelson Mpina alieleza kwamba anayo haki kama Mbunge kuwafahamisha wananchi kuhusu namna alivyotekeleza maelekezo ya Spika hivyo hakufanya kosa lolote.

 

Mhe. Luhaga Joelson Mpina aliendelea kueleza kwamba, Kanuni ya 70 kuhusu kuthibitisha tuhuma za uongo Bungeni haina masharti yanayomzuia Mbunge anayethibitisha tuhuma kuzungumza na vyombo vya habari. Mhe. Luhaga Joelson

 

Mpina alitoa mfano wa Wabunge wengine wanaothibitisha tuhuma za uongo ndani ya Bunge ambao katika kufanya hivyo wanaoneshwa na vyombo vya habari ha hakuna Kanuni inayovunjwa.

 

3.16  Mheshimiwa Spika, hakuna ubishi kuwa maelezo ya Mhe. Luhaga Joelson Mpina mbele ya vyombo vya habari ndiyo ushahidi aliouwasilisha kwa Spika. Utetezi wake kwamba maelezo yake, hayakuwa siyo ushahidi bali vielelezo alivyoambatisha kwenye maelezo yake hauna msingi kwa kuwa maelezo na viambatisho vyake vyote ni ushahidi ambao unatakiwa kufanyia kazi na Spika kwa mujibu wa Kanuni. Kitendo cha kuitisha Mkutano wa Waandishi wa Habari muda mfupi baada ya kuwasilisha Taarifa ya Spika Bungeni Kamati iliona kuwa hakikuwa na nia njema na hakioneshi heshima kwa mamlaka ya Spika. Aidha, utetezi kwamba Kifungu cha 70 hakizuii Mbunge anayetuhumu kuzungumza na vyombo vya habari haukubaliki, Vilevile, kitendo alichokifanya ni tofauti na Wabunge wanaokuwa Bungeni na kupigwa picha wakichangia, hii ni kwa sababu upo utofauti wa kimazingira.

 

3.17  Mheshimiwa Spika, Kanuni ya 70(4) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Februari, 2023 inaweka masharti yanayomtaka

 

Mbunge aliyetoa tuhuma kwamba Mbunge mwingine amesema uongo kuthibitisha tuhuma hizo. Maelezo ya Shahidi kwamba ushahidi ni vielelezo hayana uzito kwa sababu nyaraka zinazopelekwa kwa Spika, ikiwemo maudhui ya nyaraka alizowasilisha ndiyo ushahidi wenyewe na haukupaswa kuzungumzwa popote baada ya kufikishwa kwa Spika.

 

3.18  Mheshimiwa Spika, barua ya Mhe. Luhaga Joelson Mpina iliyowasilishwa kwa Spika yenye Kumb. Na. MB/KSS/2024/55 ya tarehe 14 Juni, 2024 iliambatishwa maelezo na vielelezo (viambatisho) mbalimbali. Mhe. Luhaga Joelson Mpina aliziita nyaraka hizo kuwa ni ushahidi kama inavyoonekana katika kichwa cha habari cha barua yake ambacho kinasomeka:

 

“Yah: Kuwasilisha Ushahidi kuhusu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Mohamed Bashe (Mb) kusema uongo Bungeni”.

 

Kwa hali hiyo, maelezo na viambatisho ni kitu kimoja kama barua yake inavyoonesha na huo ndiyo ushahidi aliouwasilisha kwa Spika. Katika hatua hiyo, kwa kuwa ushahidi huo ulikuwa mikononi mwa Spika, Mhe. Luhaga Joelson Mpina hakuruhusiwa kuuzungumzia.

 

3.19  Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo Kamati imejiridhisha kuwa Mhe. Luhaga Joelson Mpina alizungumza na vyombo vya habari kuhusu ushahidi aliouwasilisha kwa Mhe. Spika kabla ushahidi huo haujafanyiwa kazi na Spika au Bunge kama inavyoelekezwa na Kanuni za Bunge.

 

3.20  Mheshimiwa Spika, shahidi aliendelea kujitetea kuwa Kifungu cha 26(d)(e) na 34(1)(g) pamoja na Kanuni ya 84(1)(j) na (k) ya Kanuni za Kudumu havihusiani na maelezo aliyoyatoa kwenye Mkutano na vyombo vya habari kwa kuwa vifungu hivyi havina mawasiliano ya moja kwa moja kati ya Mbunge na Spika. Shahidi aliendelea kufafanua kuwa, maelezo yake kwa wanahabari yalilenga kuwapa taarifa wananchi kuhusu kazi anazozifanya na kuwafahamisha kuwa ametekeleza maelekezo ya Spika ya kuwasilisha ushahidi.

 

3.21  Mheshimiwa Spika. Kamati inaona kuwa, maelezo hayo ya Mhe. Luhaga Joelson Mpina hayana uzito wowote bali ni uthibitisho kuwa aliongea na vyombo vya habari kuhusu ushahidi alioupeleka kwa Spika.

 

3.22  Mheshimiwa Spika, Mbunge au mtu mwingine yeyote anao wajibu wa kuheshimu mamlaka, hadhi na heshima ya Spika, na

mwenendo wa Shughuli za Bunge. Mbunge kama sehemu ya Bunge na kiongozi wa umma analo jukumu kubwa zaidi la kuhakikisha kuwa, kila afanyalo na kila analolisema linaakisi heshima na hadhi ambayo Bunge linastahili. Kwa hali hiyo, Mbunge kwa nafasi yake kama kiongozi wa umma, hatakiwi kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu jambo lililowasilishwa kwa Spika ambalo linasubiri kufanyiwa kazi na Bunge.

 

4.0    MAONI YA KAMATI

4.1    Mheshimiwa Spika, Baada ya kujibu hoja (a) Kamati ilijielekeza katika hoja, Je, kitendo cha Mhe. Luhaga Joelson Mpina kuzungumza na Waandishi wa Habari kuhusu ushahidi alioupeleka kwa Spika ni kudharau mamlaka ya Spika na mwenendo wa shughuli za Bunge?

 

4.2    Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 26 (d) cha Sheria ya Kinga, Madaraka na Hadhi ya Bunge, Sura 296 (The Parliamentary Immunities, Powers and Privileges Act, CAP 296) kinakataza vitendo vya kumkosea heshima Spika kwa maneno au vitendo. Halikadhalika, Kifungu cha 26 (e) cha Sheria hiyo kinazuia vitendo vya dharau kwa mwenendo wa shughuli za Bunge.

 

4.3    Mheshimiwa Spika, Kitendo cha Mhe. Luhaga Joelson Mpina kwenda kuzungumza kwenye vyombo vya habari kuhusu maudhui ya ushahidi wa nyaraka alizowasilisha kwa Spika muda mfupi baada ya kufikisha ushahidi huo Bungeni ni kitendo cha ukosefu wa nidhamu kwa kutoheshimu mamlaka ya Spika na mwenendo wa shughuli za Bunge. Hivyo, haikubaliki Mbunge kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu jambo alilopeleka kwa Spika ili lifanyiwe kazi.

 

Kitendo hicho cha Mbunge ni dharau kwa mamlaka ya Spika, na kuingilia mwenendo wa Bunge. Kwa kufanya hivyo, Mhe. Luhaga Joelson Mpina ameshusha hadhi na heshima ya Bunge na kulidharaulisha mbele ya jamii hivyo kukiuka masharti ya kifungu cha 26(d) na (e) cha Sheria ya Kinga, Madaraka na Hadhi ya Bunge, Sura 296 (The Parliamentary Immunities, Powers and Privileges Act, CAP 296). Vilevile, kitendo hicho ni Utovu mkubwa wa nidhamu kwa mujibu wa Kanuni ya 84(1) (j) na (k) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Februari, 2023.

 

4.4    Mheshimiwa Spika, vilevile kifungu cha 34 (1) (g) cha Sheria ya Kinga, Madaraka na Hadhi ya Bunge, Sura 296 (The Parliamentary Immunities, Powers and Privileges Act, CAP 296) kinazuia, kuchapisha kwa Umma taarifa zilizoandaliwa mahususi

 

kwa ajili ya kuwasilishwa Bungeni, na kabla taarifa hizo kuwekwa Mezani. Kitendo cha Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina kuitisha Mkutano wa Waandishi wa Habari na kutoa ufafanuzi wa ushahidi alioupeleka kwa Spika ni kukiuka Kifungu cha 34 (1) (g) vya Sheria ya Kinga, Madaraka na Hadhi ya Bunge, Sura 296 kinachokataza kusambaza kwa umma, Taarifa zinazofanyiwa kazi na Bunge pasipo kupata kibali cha Bunge.

4.5    Mheshimiwa Spika, Ushahidi uliopo wa kitendo kilichofanywa na Mhe. Luhaga Joelson Mpina, masharti ya Sheria na Kanuni za Bunge, Kamati imemkuta na hatia Mhe. Luhaga Joelson Mpina (Mb) kwa kosa la kudharau Mamlaka ya Spika na mwenendo wa shughuli za Bunge. Kitendo hicho kinakatazwa na ni kinyume na Kifungu cha 26(d) na (e) na 34 (1) (g) cha Sheria ya Kinga, Madaraka na Hadhi ya Bunge, Sura 296 (The Parliamentary Immunities, Powers and Privileges Act, CAP 296). Aidha, kitendo hicho ni Utovu wa nidhamu / Utovu Mkubwa wa Nidhamu kwa mujibu wa Kanuni ya 84(1) (j) na (k) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Februari, 2023.

 

4.6    Mheshimiwa Spika, baada ya kujibu hoja hizo mbili za awali, Kamati ilijielekeza kwenye Hoja ya mwisho kwamba, Je, ni hatua gani za kisheria zinazopaswa kuchukuliwa dhidi yake?

 

4.7    Mheshimiwa Spika, Katika kujibu hoja hii, Kamati ilizingatia Sheria na Kanuni pamoja na, kutafakari kwa kina kuhusu ushahidi uliotolewa na Mhe. Luhaga Joelson Mpina (Mb) kuhusu suala hili. Aidha, Kamati ilizingatia maelezo yake kwamba yeye ni Mbunge wa muda mrefu chini ya viongozi wengi wa Bunge, kutowahii kufikishwa mbele ya Kamati ya Maadili na kuwa yeye ni mtiifu kwa viongozi naS za Bunge.

 

4.8    Mheshimiwa Spika, kabla ya kufikia uamuzi, Kamati ilitafakari utetezi wake na ilizingatia aina ya kosa lililofanyika, namna kosa hilo lilivyofanyika lakini pia athari ya kitendo hicho kuhusu heshima na hadhi ya Bunge na uongozi wa Bunge. Vilevile Kamati ilitilia maanani sifa na uzoefu anaopaswa kuwa nao Mbunge katika kupima matendo yake na athari zinazoweza kujitokeza kupitia kauli na vitendo vyake pamoja na wajibu wake katika kuheshimu Sheria na Kanuni za Bunge. Katika hili, Kamati iliona kuwa, Mhe. Luhaga Joelson Mpina akiwa Mbunge wa kipindi kirefu anapaswa kuonesha taswira njema ya uzingatiaji wa Maadili, Sheria na Kanuni za Bunge ili awe mfano bora kwa Wabunge wengine. Hivyo, kitendo cha kutoheshimu Mamlaka ya Spika ni jambo linaloshusha heshima ya Bunge.

 

4.9    Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 33 cha Sheria ya Kinga, Madaraka na Hadhi ya Bunge, Sura ya 296 kinatoa mamlaka kwa Bunge kupitia Azimio kutoa adhabu kwa mtu ambaye amekiuka masharti ya kifungu cha 26 au Sheria yoyote kuhusu kudharau mamlaka ya Bunge. Adhabu iliyotamkwa na Sheria ni ya kumsimamisha Mbunge kuhudhuria Vikao vya Bunge kwa namna itakavyoamuliwa kwa mujibu wa Sheria.

 

Kifungu hicho kinaeleza, nanukuu:-

33-(1) Where any Member commits any contempt of the Assembly whether specified in section 26 or otherwise, the Assembly may, by resolution, either direct the Speaker to reprimand such Member or suspend him from the service of the Assembly for such period as it may determine.

 

Provided that, such period shall not extend beyond the last day of the the session next following that which the resolution was passed or of the session in which the resolution is passed as the Assembly may so determine”.

 

4.10  Mheshimiwa Spika, Kanuni ya 84(3) ya Kanuni za kudumu za Bunge zinaweka adhabu kwa vitendo alivyovifanya Mhe. Luhaga Joelson Mpina kama ifuatavyo:-

a)       Ikiwa kosa ni la kwanza, Mbunge kutohudhuria Vikao vya Bunge visivyopungua kumi na visivyozidi kumi na tano;

b)      Ikiwa ni kosa lake la pili au zaidi Mbunge kutohudhuria vikao vya Bunge visivyopungua kumi na tano au visivyozidi ishirini; na

c)       Kanuni ya 84(4) inaweka masharti kwa Bunge kuzingatia ushauri mwingine wowote utakaotolewa na Kamati kuhusu adhabu anayostahili kupewa Mbunge aliyekiuka masharti ya Kanuni hii.

 

4.11  Mheshimiwa Spika, huo ndio ulikuwa uchunguzi wa Kamati kuhusu Shauri la kuwasilisha nyaraka za ushahidi kwa Spika na wakati huo huo kwenda kuzungumza kwenye vyombo vya habari kuhusu maudhui ya ushahidi huo kabla haujafanyiwa kazi na Spika na Bunge kwa mujibu wa Kanuni.

 

4.12  Mheshimiwa Spika, Kamati imejiridhisha kuwa, kitendo alichofanya Mhe. Luhaga Joelson Mpina ni utovu mkubwa wa nidhamu kwa Bunge kwa sababu ya kudharau Mamlaka ya Spika, kuingilia mwenendo wa shughuli za Bunge na vilevile ni kitendo kinachofedhehesha, kushusha hadhi na heshima ya Bunge.

 

Hivyo, Kamati inaliomba Bunge litafakari shauri hili linalomhusu Mhe. Luhaga Joelson Mpina (Mb), ushahidi uliopo, Sheria na Kanuni na kuuzingatia wakati wa kupitisha Azimio la kutoa adhabu anayostahili kwa kosa alilotenda.

 

5.0    HITIMISHO

5.1    Mheshimiwa Spika, mwisho, napenda kukushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi hii kuwasilisha maoni ya Kamati kwa niaba ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na napenda nitumie nafasi hii kukupongeza kwa dhati kwa jinsi unavyoliongoza Bunge hili ambalo ni chombo cha uwakilishi wa Wananchi kuisimamia na kuishauri Serikali ili kuhakikisha kuwa ustawi wa wananchi ndio kipaumbele cha kwanza.

 

5.2    Mheshimiwa Spika, kipekee, nawashukuru Wajumbe wote wa Kamati, kwa kazi nzuri ya kujadili na kuchambua kwa umakini mkubwa shauri la utovu wa nidhamu kwa Bunge na Spika, kudharau Mamlaka ya Spika, kuingilia mwenendo wa Bunge na kushusha hadhi na heshima ya Bunge. Wajumbe hawa

walifanya kazi hii na walizingatia misingi ya haki, bila kumwonea au kumpendelea mtu yeyote. Kwa heshima naomba niwatambue kwa majina kama ifuatavyo: -

 

1.                           Mhe. Dkt. Thea Medard Ntara (Mb) – Makamu Mwenyekiti

2.                           Mhe. Aloyce John Kamamba (Mb)

3.                           Mhe. Amour Khamis Mbarouk (Mb)

4.                           Mhe. Cecilia Daniel Paresso (Mb)

5.                           Mhe. Christopher Olonyokie Ole Sendeka (Mb)

6.                           Mhe. Deodatus Philip Mwanyika (Mb)

7.                           Mhe. Eng. Isack Aloyce Kamwelwe (Mb)

8.                           Mhe. Flatei Gregory Massay (Mb)

9.                           Mhe. Francis Kumba Ndulane (Mb)

10.                       Mhe. Khadija Shaaban Taya (Mb)

11.                       Mhe. Haji Amour Haji (Mb)

12.                       Mhe. Hawa Subira Mwaifunga (Mb)

13.                       Mhe. Janejelly James Ntate (Mb)

14.                       Mhe. Joseph Michael Mkundi (Mb)

15.                       Mhe. Khalifa Mohamed Issa (Mb)

16.                       Mhe. Maimuna Salum Mtanda (Mb)

17.                       Mhe. Mwantatu Mbarak Khamis (Mb)

18.                       Mhe. Prof. Patrick Alois Ndakidemi (Mb)

 

5.3    Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru kwa dhati Katibu wa Bunge, Ndugu Nenelwa J. Mwihambi, ndc kwa kuisaidia Kamati kutekeleza majukumu yake. Kipekee, nawashukuru Ndugu Pius T. Mboya, Mkurugenzi Idara ya Huduma za Sheria, Ndugu Agnes Ivor Ndumbati ndc Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Huduma za Sheria, Ndugu Maria Mdulugu (Katibu wa Kamati), Ndugu Ludovick Ringia, Ndugu Thuwaiba Jumbe Sekretarieti na Ndugu Mainda Shaban kwa kuratibu vyema kazi za Kamati na kuhakikisha kuwa Taarifa hii inakamilika kwa wakati.

5.4    Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, sasa naomba Bunge lako Tukufu, likubali kujadili na kupokea maoni na mapendekezo ya Kamati ili baada ya mjadala liazimie kuchukua hatua stahiki kwa kadiri litakavyoona inafaa.

 

 

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.

 

 

 

            Mhe. Ally Juma Makoa (Mb)

MWENYEKITI

KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE

 

24 Juni, 2024


Mpina akisikiliza majadiliano ya wabunge kaba hajatiwa kitanzini
Mpina akimpa taarifa mmoja wa wabunge waliokuwa wakimjadili









Mpina akitolewa Bungeni na Askari wa Bunge baada ya kupitishwa hukumu dhani yake

 

Comments

Popular posts from this blog

UNAMKUMBUKA AMINA CHIFUPA WA MPAKANJIAA.

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?

KADA MGEJA AHUDHURIA MAZIKO YA MAMA MZAZI WA MWANDISHI MWANDAMIZI WA HABARI KAHAMA