MKURUGENZI WA IDARA YA HABARI (MAELEZO) NA MSEMAJI MKUU WA SERIKALI ANENA NA WANAHABARI JIJINI DODOMA

YALIYOJIRI LEO JUNI 27, 2024 JIJINI DODOMA KWENYE MKUTANO WA MKURUGENZI WA IDARA YA HABARI (MAELEZO) NA MSEMAJI MKUU WA SERIKALI BW. THOBIAS MAKOBA NA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU MAAZIMIO YA MKUTANO WA WAZIRI MKUU NA JUMUIYA YA WAFANYABIASHARA NCHINI

# Kwa takribani siku nne sasa kumekuwa na majadiliano kwa ngazi mbalimbali kati ya serikali na viongozi wa jumuiya ya wafanyabiashara hapa nchini. Mazungumzo haya yalitokana na madai na hoja takribani 41 ambazo wafanyabiashara waliziwasilisha serikalini ikiwa ni sehemu ya kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini. Kutokana na hoja hizo, na baada ya vikao na mawaziri wa sekta husika, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia falsafa ya R 4 za Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hasa ile ya Reconciliation kwa maana ya maridhiano, Leo tarehe 27 Juni, 2024 amehitimisha mazungumzo hayo jiji Dodoma.

# Mheshimiwa Majaliwa, kwa niaba ya Serikali kwa pamoja na uongozi wa jumuiya ya wafanyabiashara nchini wameafikiana kusimamia maazimio 15 ambayo ndani yake serikali imetoa maagizo yafuatayo kwa taasisi husika.

MAAZIMIO YA MKUTANO WA WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHE. KASSIM MAJALIWA NA JUMUIYA YA WAFANYABIASHARA NCHINI

# Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeagizwa kusitisha mara moja zoezi la kamata kamata pamoja na kusitisha mazoezi mengine yote ya ufuatiliaji wa risisti za EFD katika maeneo yote nchini hadi mwezi Agosti, 2024. Aidha, pamoja kusitishwa huko wafanyabishara wanahimizwa kuelendelea kutoa risiti za mauzo.
 
# TRA imeagizwa kuweka mfumo mzuri utakaowezesha utoaji wa nyaraka muhimu za manunuzi wakati wa uingizaji wa bidhaa nchini kuanzia Julai, 2024. Aidha, utekelezaji wake utawekewa utaratibu mzuri kwa kushirikisha wadau wote muhimu.

# Serikali imeiagiza Mamlaka ya Bandari Tanzania kuongeza haraka Bandari Kavu (ICD) kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa mizigo kupitia utaratibu wa de-consolidation;

# TRA imeelekezwa kuongeza nguvu kwenye kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya kodi na maboresho ya kodi yanayofanyika ili kuwezesha kuongeza uelewa kwa wafanyabiashara kuhusu masuala ya kodi nchini. Aidha, Taasisi husika za Serikali pamoja na mabaraza ya biashara yashirikishwe kikamilifu katika ngazi zote.

# TRA pia inaelekezwa kubainisha na kusimamia vyema orodha ya bidhaa nane ambazo zitawekewa bei elekezi kama ilivyo katika bidhaa za magari yaliyotumika. Bidhaa hizo ni vitenge, mashati, nguo nyingine, vipodozi, vito vya thamani, nguo za ndani, leso na vesti.

# Serikali kwa ujumla itaendelea na zoezi la kuwapanga na kuwawekea mazingira rafiki wafanyabiashara wadogo ambao hawako kwenye maeneo rasmi ili kurahisha usimamizi, ufuatiliaji na urasimishaji wao wa biashara.

# Serikali itaendelea kufanya mapitio ya viwango vya kodi tulivyo navyo kwa sasa ili kuwawezesha wafanyabiashara kulipa kodi kwa amani na haki kulingana na thamani ya biashara zao.

# Katika kipindi cha muda mfupi na wa kati, Serikali itashughulikia changamoto zote za wafanyabaishara zilizowasilishwa Serikalini hususan zile ambazo hazihitaji mabadiliko ya sera au sheria.

# Katika maboresho zaidi, Serikali imeiagiza TRA ikamilishe maboresho ya mfumo wa TANCIS ambao utajumuisha moduli ya Auto valuation itakayoweka wazi na usawa katika ukokotoaji wa kodi kufikia Januari 2025.

# Wataalam wa TBS na TRA kwa pamoja wameelekezwa kukamilisha marekebisho ya mfumo wa TEHAMA ili mizigo inayoingia nchini kwa njia ya uchangiaji makasha iweze kugombolewa kwa namba ya usajili wa mlipakodi (TIN) ya mwenye mzigo badala ya TIN ya wakala bila ya kuwa na gharama za ziada kwa mlipakodi. Aidha, zoezi hili linatarajiwa kukamilika Julai, 2024.

# Serikali imeielekeza Wizara ya Fedha kuratibu zoezi la kufanya uchambuzi, tathmin na mapitio ya mfumo mzima wa utozaji na ukusanyaji pamoja na viwango vya Ushuru wa Huduma (Service Levy) pamoja na kushauri njia mbadala ya utozaji itakayo kuwa rafiki zaidi kwa wafanyabiashara ili kulinda mitaji na ukuaji wa biashara nchini.

# Kuhusu wafanyabiashara kutoka nje ya nchi, Serikali kupitia ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) na mamlaka zingine husika itaendelea kuimarisha ukaguzi wa vibali vya kazi kwa wageni  ili kuhakikisha kuwa wamiliki wa vibali hivyo wanafuata  masharti ya vibali hivyo kwa mujibu wa sheria za nchi. Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wanaokiuka sheria, kanuni, taratibu na masharti ya vibali vya ajira ikiwa ni pamoja na kuwafukuza nchini na waajiri husika kuchukuliwa hatua za kisheria.

# Serikali imeelekeza Mawaziri wanaohusika na Sekta ya Biashara kukutana na wafanyabiashara wote nchini kwa ajili ya kusikiliza changamoto za wafanyabiashara pamoja na kupokea maoni yatakayolenga kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini wakati wote.

# Serikali imeelekeza wataalamu wa forodha wakutane na Jumuiya ya Wafanyabishara nchini mara moja ili kujadiliana kuhusu taratibu za kiforodha hususani uthaminishaji na ugomboaji wa mizigo. Suala hili likamilike ifikapo tarehe 10 Julai, 2024.

# Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) itaendelea kuratibu suala la kutoa mrejesho kwa wafanyabiashara kila robo mwaka kuhusu utekelezaji wa mazimio baina ya wafanyabiashara na Serikali.

# Kutokana na maazimio haya na maagizo ya serikali, pande zote mbili zimekubaliana hali ya biashara kote nchini kuendelea kama kawaida ili kuwapa watanzania huduma wanazostahili. Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuboresha mazingira ya wafanyabiashara wote kama ambavyo Mheshimiwa Rais amekuwa akisisitiza katika uongozi wake.

Imeandaliwa na Idara ya Habari – (Maelezo)

Wanahabari wakimsikiliza kwa makini Mkurugenzi

 

Comments

Popular posts from this blog

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?

UNAMKUMBUKA AMINA CHIFUPA WA MPAKANJIAA.

KADA MGEJA AHUDHURIA MAZIKO YA MAMA MZAZI WA MWANDISHI MWANDAMIZI WA HABARI KAHAMA