KIFO CHA MARC VIVIEN FOE WA CAMEROON UWANJANI NCHINI UFARANSA
Mpira tayari umekwisha, Cameroon anaondoka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Colombia, ni nusu fainali ya Kombe la mabara pale dimba la Stade de Gerland Lyon Kaskazini mwa Ufaransa, wanaenda vyumbani wakishangilia kwa nguvu zote
Ghafla Nahodha Rigobert Song anaingia vyumbani huku akilia na kuwaambia kuwa Marc Vivien Foe hatunae tena, ghafla wachezaji walichanganyikiwa, alitoka nje winger Winfried Schafer mpaka chumba cha matibabu, alipofika alikutana na mwili wa Foe ukiwa bado na jezi ya Cameroon
Schafer alimuona Mama mzazi wa Foe na mkewe Marie Louise wakiwa pembeni ya Marc, Simba amelala mezani hakuamini macho yake, alimtazama Daktari Xavier Richaud, nae kwa ishara alimwambia Simba wetu amepumzika rasmi, hatoamka tena
Wakati kilio kimetawala sana, Kiungo mmoja Eric Djemba Djemba ndie alipata bahati ya kuongea na Foe kwa mara ya mwisho, wakati wapo kwenye basi kuelekea uwanjani, Foe alimwambia Djemba kuwa "Kama kuna mtu anabidi afe kwa ajili ya Cameroon basi afe ila timu lazima ifike fainali"
Djemba Djemba anatuambia kuwa Foe aliwaahidi Mkewe na watoto wake kuwa lazma washinde ile mechi kwa ajili yao, Djemba alimtazama sana Foe na kumpiga begani na kumwambia "lazima tutashinda Marco sisi ni Cameroon" hakuna kati yao aliejua kifuatacho, ni kama ambavyo Ruge aliaga offisini na kuwaambia atarejea
Wakati mchezo unapigwa pale Stade de Gerland, Foe alishapazoea kwakuwa ni mchezaji wa Lyon, alikuwa anacheza kwa jihad kubwa kwa ajili ya familia yake, ilitimu dakika ya 71, Foe kona inaenda kupigwa walishambulia Cameroon, kisha Foe akawa anakimbia kurudi kati
Foe alimwambia Djemba Djemba, "Eric nimechoka sana Mdogo wangu", Djemba alimwambia basi subiri mpira utoke nitamwambia Kocha ukapumzike Kaka, vumilia kidogo tu tukiupat mpira nitawaambia wautoe nje" lakini dakika chache baadae alimuona Marc kaenda hewani anawania mpira na Mario Yepes
Wakati anafika katikati ya dimba, ndipo anaanguka chini, kila mtu akimuita Marc kwa nguvu, Madaktari walikimbia kwa kasi sana mpaka eneo la tukio kujaribu kuokoa maisha ya Marc
Lakini baada ya Madaktari kumtoa uwanjani wachezaji waliamini kuwa atapona, hiyo ndio ilikuwa tafakuri ya mwisho ya Eric Djemba Djemba, muda mchache kabla ya mechi na dakika kadhaa baada ya mechi na kifo cha Kaka yake wa mpira Marc Vivien Foe
Wachezaji wa Cameroon wanautazama mwili wa Foe mezani hawaamini, jasiri na imara kama Rigobert Song analia hana raha, jezi ya Marc imelowa jasho lake la dakika 73 uwanjani, Song aliwageukia wenzake na kuwaambia nifuateni Mimi, kwa unyonge wakawa wanamfata
Song alianza kutoa tamko kwa wachezaji wake kama Captain "Sikilizeni, tupo mbali sana na nyumbani, tumekuja hapa kulipigania Taifa, lakini kafa Ndugu yetu vitani, hatuna nguvu ya kupambana, tuondokeni turudi nyumbani kumzika Ndugu yetu" ni kauli iliyoambatana na machungu makubwa
Song alipokea simu ya Nahodha wa zamani Stephen Tataw alieipeleke Cameroon robo fainali 1990 na kumpongeza kwa uamuzi huo kwakuwa akili zao hazipo tayari kucheza fainali ile ya Kombe la mabara dhidi ya Ufaransa, ikalazimu Rais wa FIFA Sepp Blatter kuwasihi sana wacheze ila waligoma kabisa, walikuwa tayari hata kufungiwa
Lakini kauli moja ya Mke wa Marehemu Marie Louise, alifika kambini na kuwaomba wachezaji wacheze kwa ajili ya Foe kwakuwa aliahidi familia yake kuleta kombe, kwahiyo Song na wenzake waende kuitimiza ahadi ya Ndugu yao, hii iliwapa nguvu ya ajabu sana ikichangiwa na uwepo wa watoto wa Foe
Song alizitazama nyuso za vijana wake Samuel Etoo Fils, Jeremy Njitap, Carlos Kameni,Pius Ndiefu na Modeste M'bami, akaitazama timu nzima na kuwaambia "twendeni tukafe kwa ajili ya Cameron" kisha wakaagiza picha ya Marc iwepo uwanjani siku ya fainali
June 29, 2003 pale Stade de France, St Denis Ufaransa ndipo fainali inapigwa, watu wengi kutoka Cameroon walihudhuria, akiwemo nguli wa muziki Manu Dibango na Legend Rodger Miller, Nahodha wa Cameroon na Marcel Desailly wa Ufaransa walibeba picha ya Marc Vivien Foe kuelekea uwanjani
Sahau kuhusu matokeo ya 1-0 aliyofungwa Cameroon ila lile bango limeandikwa, "A LION NEVER DIE, HE SLEEPS" wanaamini Simba hafi bali analala ipo siku ataamka tu💔 Pumzika FOE


Comments
Post a Comment