HOSPITALI YA MOUNT MERU YAPONGEZWA KWA UTOAJI WA HUDUMA BORA ZA AFYA


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Ally Mwalimu (Mb), ameridhishwa na hali ya utoaji na upatikanaji wa huduma za Afya, zinazotolewa kwenye hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru, na kuwapongeza Watumishi wote, kwa kutoa huduma bora kwa wagonjwa, wanaofika hospitalini hapo kupata huduma.

Mhe. Ummy, ametoa pongezi hizo, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua huduma za Afya, pamoja na kuzindua Maabara ya Patholojia inayohusika na upimaji wa magonjwa sugu ikiwemo Saratani hospitalini hapo.

Mhe. Waziri, amekiri kuridhishwa na hali ya utoaji huduma za afya pamoja na shughuli za kitabibu zinazoendelea kutolewa katika mazingira safi na rafiki, hali inayosababisha kupanda hadhi hali ya utoaji bora wa huduma za Afya za wagonjwa.

“Hospitali ya Mount Meru inafanya vizuri kati ya hospitali zote za Rufaa nchini, ninakupongeza Dkt. Alex na watumishi wote, niwasihi hospitali zote nchini kuiga mfano wa Hospitali ya Mount Meru, kuna vifaa vya kutosha, mazingira ni masafi, huduma zote zinapatikana na zinatolewa kwa wagonjwa muda wote kama vile hospitali ya ‘private'” Amesema Waziri Ummy.

Aidha, ametoa rai kwa hospitali zote za Serikali nchini kuiga mfano wa Hospitali ya Mount Meru kwa kutoa huduma bora za Afya kwa wananchi, kwa kuwa ndiyo malengo ya Serikali ua awamu ya sita, ya kila mwananchi ana haki ya kupata huduma bora katika hospitali za Serikali, ambazo kwa sasa zina vifaa vya kutosha na vya kisasa.

“Serikali imehakikisha uwepo wa ongezeko la vifaa tiba, upatikanaji wa vipimo muhimu vya maabara kwa 98 % na uwepo wa dawa muhimu za magonjwa mbalimbali, hivyo ni wajibu wenu watoa huduma za afya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma hizi na kufurahia matunda ya Serikali yao ya awamu ya sita”Amesema Mhe. Ummy.

Hata hivyo, hakusita kuupongeza Uongozi wa Mount Meru, kwa kufanikiwa kuongeza mapato ya Hospitali kutoka shilingi Milioni 6 kwa siku hadi Milioni 25 kwa siku, bila kupandisha gharama za matibabu, bali kwa kusimamia na kudhibiti upotevu wa mapato kupitia matumizi sahihi ya mifumo ya malipo ya huduma za afya. 

Ameongeza kuwa uboreshaji wa miundo mbinu na vifaa tiba katika hospitali hiyo, ni jambo la msingi sana, lililosababisha ongezeko la wagonjwa wanaokuja kutibiwa na kuacha kwenda hospitali zingine za binafsi pamoja na kupungua kwa malalamiko ya huduma, huku ukiweka mbele utoaji stahiki za watumishi pamoja na kuwapa fursa ya kuwaendeleza kimasomo.

Awali, uwepo wa maabara ya Patholojia alioizindua, itasaidia upatikanaji wa vipimo vya kuchakata vinyama ili kugundua uwepo wa magonjwa mbalimbali ikiwemo Saratani.

Mganga Mfawidhi Hosptali ya Mount Meru, Dkt. Alex Ernest, amesema kuwa, Maabara hiyo ya Patholojia imegharimu kiasi cha shilingi Milioni 380 na kufanya Mount Meru kuwa, hospitali ya kwanza ya Rufaa ya Mkoa kuwa na Maabara hiyo na hospitali ya 5 ya Serikali Nchi nzima.

Aidha Dkt. Alex, ameishukuru Serikali chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Afya kwa kuhakikisha fedha za dawa na uendeshaji wa hospitali zinafika kwa wakati hali inayorahisisha upatikaji vifaa tiba na dawa huku hospitali ikiendelea kuboresha utoaji huduma za Afya kwa kuongeza huduma bora.

Comments

Popular posts from this blog

UNAMKUMBUKA AMINA CHIFUPA WA MPAKANJIAA.

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?

KADA MGEJA AHUDHURIA MAZIKO YA MAMA MZAZI WA MWANDISHI MWANDAMIZI WA HABARI KAHAMA