WARSHA YA MFUMO YA STAKABADHI ZA GHALA KWA MAKATIBU TAWALA WASAIDIZI WA MIKOA NA WARAJIS WASAIDIZI WA MIKOA
HOTUBA YA KATIBU MKUU WA WIZARA YA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA (DKT. HASHIL ABDALLAH) ALIYOITOA UZINDUZI WA MATUMIZI YA MFUMO WA STAKABADHI ZA GHALA KATIKA ZAO LA ILIKI PAMOJA NA MAFUNZO KWA MAKATIBU TAWALA WASAIDIZI (UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA) YALIYOFANYIKA KATIKA UKUMBI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA MVOMERO MOROGORO TAREHE 24 MACHI, 2023
-Ndugu, Katibu Tawala wa Mkoa,
- Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Mvomero,
-Ndugu, Mwenyekiti wa Halamashauri Mhe. Diwani.......
-Ndugu, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero,
-Ndugu, Waheshimiwa Madiwani wa Kata zote za Halmashauri ya Mvomero,
-Ndugu, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala
-Ndugu, Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji
- Ndugu, Warajis Wasaidizi wa Vya Vyama vya Ushirika
- Ndugu, Viongozi na wawakilishi wa Taasisi binafsi zinazofanya kazi na Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala,
- Ndugu wanachama, viongozi na watendaji wa Vyama vya Ushirika
-Ndugu Waratibu,
-Ndugu Wageni waalikwa;
-Ndugu Wanahabari,
-Mabibi na mabwana:
Nawasalimu kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ndugu washiriki, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ametujalia afya njema na kutuwezesha kushiriki katika uzinduzi wa mfumo stakabadhi za ghala katika zao la Iliki na mafunzo kwa Makatibu Tawala Wasaidizi na Warajis Wasaidizi wa Mikoa ambao ni wadau muhimu sana katika shughuli za Uwekezaji, Viwanda na Biashara katika Mikoa yao. Nawashukuruni nyote mlioweza kuandaa kuchangia na kushiriki katika uzinduzi na mafunzo haya. Aidha, ninawapongeza Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), Uongozi wa Mkoa wa Morogoro pamoja na Halamashauri ya Wilaya ya Mvomero kuratibu na kuandaa uzinduzi na mafunzo haya. Natambua kuwa suala la uratibu na maandalizi ya uzinduzi na mafunzo kama haya yanahitaji muda, rasilimali, kujitoa na kujituma, hongereni sana. Nimefurahishwa na kutiwa moyo sana kwa namna mlivyoshiriki kwa wingi katika shughuli hii na ni matumani yangu kuwa tumetambua umuhimu wa matumizi ya mfumo wa stakabadhi za ghala katika kuimarisha masoko ya bidhaa, kipato kwa wadau wa biashara ya mazao na taifa kwa ujumla. Matumizi ya Mfumo huu si mageni hapa Mvomero na Morogoro kwa ujumla kwani nimefahamishwa kuwa unatumika pia katika mauzo ya zao la Kakao katika Wilaya hii. Hivyo niwapongeze kwa hatua hii ya kuhakikisha kuwa mazao zaidi yanaingia katika mfumo huu ili kunufaika zaidi.
Ndugu washiriki, nampongeza sana Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini kwa kuwezesha Warajis wote wa Mikoa Kushiriki uzinduzi na mafunzo haya. Katika utambulisho nimesikia kuna uwakilishi wa wadau wote (Vyama vya Ushirika, Taasisi za Serikali na Binafsi, Wakulima, Watendaji wa Kata na Vijiji, Vyombo vya habari n.k.). Matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala yanahusisha taasisi nyingi za serikali na binafsi, wakulima, wanunuzi, watunza ghla na wadau wengine. Uwepo wenu hapa ni fursa kubwa kwani mtaweza kushuhudia uzinduzi huu pamoja na kuweka mikakati ya usimamizi kwa ajili ya uendelevu wa mfumo huu. Aidha, hapa kuna wa wawakilishi wa Taasisi za kifedha, tumieni fursa hii pia kuona namna ya kuwezesha wakulima kuongeza tija katika shughuli zao ikiwemo kuongeza thamani ya mazao yao na hata kusaidia ujenzi wa miundombinu ya kuhifadhi mazao hayo.
Ndugu washiriki, nimeelezwa kuwa mfumo wa stakabadhi za ghala ni mara ya kwanza kutumika katika zao la Iliki hapa nchini. Zao hili linapatikana katika Halamashauri hii lakini pia maeneo mengine katika mkoa huu. Mfumo huu unahitaji usimamizi thabiti ili kuweza kutekelezwa kwa ufanisi hasa kwa ushirikiano wa karibu baina ya wakulima, wanunuzi, watunza ghala na Serikali kwa ujumla, hivyo nitumie fursa hii kusisitiza kuwa asitokee mdau yeyote akahujumu utendaji kazi wa mfumo huu kwa kutokutimiza wajibu wake. Wakulima mhakikishe mnazingatia ubora wa mazao yanayokusanywa katika ghala kwa mujibu wa mwongozo sambamba na kutunza risiti na taarifa za mzigo. Vilevile, viongozi wa Vyama vya Ushirika muhakikishe mnatenda kazi kwa ueledi na kuzingatia sheria na Kanuni za Ushirika ili kuepuka ubadhirifu. Aidha, watumishi wote wa Serikali wanaohusika na mfumo huu wahakikishe wanashirikiana katika usimamizi ili asitokee mkulima aliyekosa malipo yake alkadharika mnunuzi kukosa mzigo aliokwisha ulipia.
Ndugu washiriki, Serikali kwa muda wote imekuwa ikiboresha mazingira ya ufanyaji biashara hasa kwa kuongeza wataalamu wanaohusika na usimamizi wa shughuli za uwekezaji, viwanda na biashara. Hivyo, uwepo wa Makatibu Tawala Wasaidizi katika Mamlaka za Mikoa mahsusi kwa usimamizi wa uwekezaji, viwanda na Biashara ni moja ya jitihada hizo. Naamini mnafahamu jukumu zito mlilokuwa nalo ili kuhakikisha sekta hizo zinaendelea na kutoa matokea tarajiwa kwa maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla. Mafunzo haya kuhusu utendaji kazi wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, Ushirika na Soko la Bidhaa ikawe chachu ya kuongeza ubunifu katika utendaji kazi wenu kwa kushauri Mamlaka za Mikoa yenu na Halmashauri zake juu ya usimamizi na uongezaji wa mapato.
Ndugu washiriki, nimearifiwa kuwa mafunzo haya kwa Makatibu Tawala Wasaidizi yatakuwa endelevu ili kuweza kubadilishana uzoefu katika utekelezaji wa matumizi ya Mfumo wa Stakabadi za Ghala katika maeneo yenu. Hivyo, nategemea ujuzi mtakaoupata mtauonesha kwa vitendo katika maeneo yenu ya kazi ili kuongeza ufanisi wa matumizi ya mfumo huu na pia kuongeza idadi ya bidhaa zitakazouzwa kwa kutumia mfumo huu.
Ndugu washiriki, katika kukabiliana na maendeleo ya kiuchumi, kijamii, kiteknolojia pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, utafiti ni muhimu sana kuendelea kufanyika katika sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na mifumo yetu ya masoko ili kuiboresha kuendana na mabadiliko ya mazingira.
Ndugu washiriki, ninawaelekeza Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala kwa kushirikiana na wadau wenza, kuendelea kutoa elimu ya matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ili umma upate uelewa na kufanya maamuzi juu ya namna ya kuendesha mfumo kutegemeana na zao husika. Utoaji wa elimu kwa umma utasaidia pia mfumo kutekelezwa kwa kutegemea mahitaji ya wazalishaji “Demand driven” badala ya kutekelezwa kwa kutozingatia mahitaji ya mzalishaji “Supply Driven”.
Ndugu washiriki, ni matarajio yangu kuwa kupitia uzinduzi wa matumizi ya mfumo uliofanyika katika zao la Iliki na mafunzo yatakayotolewa kwa pamoja vitasaidia kuimarisha utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi za ghala kwa vitendo na hivyo kuweza kujipima.
Ndugu washiriki, nikimalizia niwaombe tuendelee kuwahamasisha wakulima, viongozi na watendaji wa Vyama vya Ushirika pamoja na wadau wanaotekeleza mfumo wa Stakabadhi za Ghala kuendelea kushiriki katika shughuli kama hizi kwa ajili ya kuongeza uelewa na kuchangia katika kuibua maeneo yenye changamoto na kutafuta njia za utatuzi.ushirika. Aidha, matumizi ya mfumo katika mazao alkadharika mafunzo kwa watendaji wa mfumo yawe endelevu ili kuinua pato la mkulima na nchi kwa ujumla
Ndugu washiriki, sasa nitamke kuwa mafunzo ya kwanza ya Matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa yamefunguliwa rasmi na niwatakie mafunzo yenye mafanikio.
HOTUBA YA KATIBU MKUU WA WIZARA YA KILIMO (BW. GERALD MWELI) , KATIKA UZINDUZI WA MATUMIZI YA MFUMO WA STAKABADHI ZA GHALA KATIKA ZAO LA ILIKI PAMOJA NA MAFUNZO KWA MAKATIBU TAWALA WASAIDIZI (UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA) YANAYOFANYIKA KATIKA UKUMBI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA MVOMERO MOROGORO TAREHE 24 MACHI, 2023
Katibu Tawala wa Mkoa,
- Mhe.Judith Nguli, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero,
-Mhe. Yusuph Athuman Makunja, Mwenyekiti wa Halamashauri
-Dkt. Philipina Filipo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero,
Waheshimiwa Madiwani wa Kata zote za Halmashauri ya Mvomero,
-Ndugu Asangye Bangu, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala
- Mhandisi Benedict Ndomba, Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Serikali Mtandao
-Makatibu tawala Wasaidizi WA Mikoa mliopo hapa
- Ndugu, Warajis Wasaidizi wa Vya Vyama vya Ushirika kutoka Mikoa yote ha Tanzania Bara
- Ndugu, Viongozi na wawakilishi wa Taasisi za Umma na Taasisi binafsi zinazofanya kazi na Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala,
- Ndugu wanachama, viongozi na watendaji wa Vyama vya Ushirika
-Ndugu Waratibu,
-Ndugu Wageni waalikwa;
-Ndugu Wanahabari,
-Mabibi na mabwana:
Nawasalimu kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ndugu washiriki, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ametujalia afya njema na kutuwezesha kushiriki katika uzinduzi wa mfumo stakabadhi za ghala kwa njia ya kidijitali, kuzindua matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala katika zao la Iliki na pia mafunzo kwa Makatibu Tawala Wasaidizi na Warajis Wasaidizi wa Mikoa ambao ni wadau muhimu sana katika shughuli za Uwekezaji, Viwanda na Biashara katika Mikoa yao. Nawashukuruni nyote mlioweza kuandaa kuchangia na kushiriki katika uzinduzi na mafunzo haya. Aidha, ninawapongeza Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), Uongozi wa Mkoa wa Morogoro pamoja na Wilaya ya Mvomero kuratibu na kuandaa uzinduzi na mafunzo haya. Natambua kuwa suala la uratibu na maandalizi ya uzinduzi na mafunzo kama haya yanahitaji muda, rasilimali, kujitoa na kujituma, hongereni sana. Nimefurahishwa na kutiwa moyo sana kwa namna mlivyoshiriki kwa wingi katika shughuli hii na ni matumani yangu kuwa tumetambua umuhimu wa matumizi ya mfumo wa stakabadhi za ghala katika kuimarisha masoko ya bidhaa, kipato kwa wadau wa biashara ya mazao na Taifa kwa ujumla. Hivyo niwapongeze kwa hatua hii ya kuhakikisha kuwa tuna nia ya dhati ya kuwa na mifumo bora kwa maendeleo ya Taifa letu.
Ndugu washiriki, nampongeza sana Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini kwa kuwezesha Warajis wote wa Mikoa Kushiriki uzinduzi na mafunzo haya hii no kutokana na majukumu yao kwa kushirikiana na Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa. Pia nipongeze uwakilishi wa wadau wote (Vyama vya Ushirika, Taasisi za Serikali na Binafsi, Wakulima, Wanunuzi, Watendaji wa Kata na Vijiji, Vyombo vya habari n.k.). Uwepo wenu wote hapa ni fursa kubwa kwani naamini sasa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala unakwenda kutekelezwa si tu kwa mazao bali kwa bidhaa mbalimbali katika maeneo yenu ya kazi. Aidha, nina uhakika kuwa wakulima wa mazao mbalimbali katika mkoa huu wa Morogoro wamepata fursa ya kukutana na wadau mbalimbali hasa Taasisi za kifedha hivyo ni vyema kutengeneza mahusiano mazuri kwa ajili ya kuweza kunufaika na kuongeza tija ya uzalishaji na mnyororo mzima wa thamani.
Ndugu washiriki, Kipekee nitoe pongezi kwa uongozi mzima wa Mkoa wa Morogoro hasa ya Wilaya ya Mvomero kwa jitihada za kuhakikisha kuwa wakulima wananufaika na jasho lao kwa kutumia mifumo rasmi katika mauzo ya mazao yao. Nimeelezwa kuwa kwa sasa mazao ya Kakao na Iliki ndiyo mazao pekee yanayotumia mfumo wa Stakabadhi za Ghala katika Halmashauri hii, hivyo ningeomba mazao zaidi yaingizwe ktika mfumo huu ili manufaa zaidi yaweze kupatikana kwa mkoa na nchi kwa ujumla. Mfumo huu unahitaji usimamizi thabiti ili kuweza kutekelezwa kwa ufanisi hasa kwa ushirikiano wa karibu baina ya wakulima, wanunuzi, watunza ghala na Serikali kwa ujumla, hivyo nitumie fursa hii kusisitiza kuwa kila mdau atekeleze wajibu wake katika kuhakikisha uendelevu wa mfumo huu. Wakulima kupitia Vyama vyenu vya Ushirika, hakikisheni mnazingatia matakwa ya miongozo mbalimbali ili kulinda ubora wa mali na hatimaye kuleta bei zenye tija kwenu. Vilevile, viongozi wa Vyama vya Ushirika mnazuia ubadhirifu katika Vyama vyenu na hili linawezekana tu endapo mtatekeleza majukumu yenu kwa kuzingatia ueledi, sheria na Kanuni za Ushirika. Aidha, watumishi wote wa Serikali wanaohusika na mfumo huu wahakikishe wanashirikiana katika usimamizi ili asitokee mkulima aliyekosa malipo yake akaathirika na pia upande wa mnunuzi kukosa mzigo aliokwisha ulipia.
Ndugu washiriki, Sina shaka na mafunzo juu ya mifumo ya kijiditali yaliyotolewa kwa Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa pamoja na Warajis Wasaidizi wa Mikoa kutokana na kuwa nyie ni wadau muhimu katika maendeleo ya Uwekezaji, Biashara na Uwekezaji katika maeneo yenu. Hivyo, mafunzo haya ni juhudi za Serikali yetu chini ya Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kujenga ujuzi kwa wataalam wake. Naamini mtakuwa mabalozi wazuri kwa kuweka yote mliyojifunza katika matendo ili kuimarisha usimamizi na kuleta matokeo tarajiwa.
Ndugu washiriki, nasisitiza mafunzo haya yawe endelevu kutokana na mabadiliko ya mazingira hasa ya kiteknolojia katika ufanyaji biashara hivyo kuhitaji mabadilishano ya uzoefu kwa wadau. Hivyo, mtoke na maazimio kwa ajili ya mafunzo yajayo na kipimo kwa washiriki. Msiache kufanya tafiti mbalimbali ili kuweza kuboresha mifumo hii ya masoko kutegemea na mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.
Ndugu washiriki, ninawaelekeza Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala kwa kushirikiana na wadau wenza, kuendelea kutoa elimu ya matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ili umma upate uelewa na kufanya maamuzi juu ya namna ya kuendesha mfumo kutegemeana na zao husika. Utoaji wa elimu kwa umma utasaidia pia mfumo kutekelezwa kwa kutegemea mahitaji ya wazalishaji badala ya kutekelezwa kwa kutozingatia mahitaji ya mzalishaji.
Ndugu washiriki, ni matarajio yangu kuwa kupitia uzinduzi wa matumizi ya mfumo uliofanyika katika zao la Iliki na mafunzo yatakayotolewa kwa pamoja vitasaidia kuimarisha utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi za ghala kwa vitendo Marika maeneo mnakotoka
Ndugu washiriki, nikimalizia niwaombe tuendelee kuwahamasisha wakulima, viongozi na watendaji wa Vyama vya Ushirika pamoja na wadau wanaotekeleza mfumo wa Stakabadhi za Ghala kuendelea kushiriki katika shughuli kama hizi kwa ajili ya kuongeza uelewa na kuchangia katika kuibua maeneo yenye changamoto na kutafuta njia za utatuzi. Aidha, tuhamasishe wakulima kuzalisha mazao kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo ili kuogeza tija na ubora.
Ndugu washiriki, sasa nitamke kuwa mafunzo ya Matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa na Warajis Wasaidizi wa Mikoa yamefungwa rasmi na niwatakie utekelezaji mwema na safari njema mnaporudi katika maeneo yenu ya kazi.
Comments
Post a Comment