TAARIFA YA MWAKA YA SHUGHULI ZA KAMATI KWA KIPINDI CHA JANUARI, 2022 HADI JANUARI, 2023
1
SEHEMU YA KWANZA
1.0 UTANGULIZI
1.1 Maelezo ya Jumla
Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Kamati ya Kudumu ya Bunge
2
1.2 Muundo wa Taarifa
Mheshimiwa Spika, kanuni ya 142 ya kanuni za Kudumu za
Bunge, Toleo la Juni, 2020, imeweka masharti kuhusu Muundo wa
Taarifa ya Kamati. Kwa kuzingatia masharti hayo, naomba
kutambulisha muundo wa Taarifa kwa kutaja sehemu kuu kama
ifuatavyo: -
(i) Sehemu ya kwanza ni utangulizi inaotoa maelezo ya jumla,
ikiwemo msingi wa shughuli za Kamati, njia na mbinu
zilizotumika pamoja na orodha ya shughuli zilizotekelezwa;
(ii) Sehemu ya pili inafafanua shughuli zilizotekelezwa na
uchambuzi kwa yaliyojitokeza wakati wa utekelezaji. Aidha,
sehemu hii inabainisha mafanikio na changamoto
zilizojitokeza;
(iii) Sehemu ya tatu inatoa maoni ya jumla na mapendekezo ili
kuliwezesha Bunge kuamua; na
(iv) Sehemu ya nne inahitimisha na kutoa hoja kwa hatua ya
Bunge lako tukufu kujadili na kufanya uamuzi.
1.3 Msingi wa Shughuli zilizotekelezwa na Kamati
Mheshimiwa Spika, Msingi wa shughuli zilizotekelezwa na
Kamati kwa kipindi cha mwaka mmoja unatokana na masharti ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kanuni za Bunge
Toleo la Juni, 2020. Katiba ambayo ni mwongozo mkuu wa
uendeshaji wa Nchi, imebainisha lengo kuu la Serikali na kuonesha
madaraka na jukumu la Bunge. Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo
la Juni, 2020, zimeweka utaratibu wa utekelezaji bora wa
madaraka ya Bunge unaowezesha kufuatilia shughuli za umma ili
kufanikisha lengo kuu la Serikali.
3
Mheshimiwa Spika, Ibara ya 8 (1) (b) ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inatambulisha lengo kuu
la Serikali la kuwezesha ustawi wa wananchi. Aidha, Ibara ya 96
ya Katiba inalipa Bunge uwezo wa kuunda Kamati za namna
mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji bora wa madaraka yake.
Vilevile, Ibara ya 63(2) ya Katiba imeipa madaraka ya kuisimamia
na kuishauri Serikali kwa niaba ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kifungu cha 6(8) cha
Nyongeza ya nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Juni,
2020, Jukumu la Kamati ya Miundombinu ni kuisimamia Wizara ya
Ujenzi na Uchukuzi pamoja na Wizara ya Habari, Mawasiliano na
Teknolojia ya Habari.
Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 7 (1) cha Nyongeza ya Nane ya
Kanuni za Bunge, kimebainisha majukumu ya Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Miundombinu kama ifuatavyo: -
(i) Kushughulikia bajeti za Wizara inazozisimamia;
(ii) Kushughulikia miswada ya sheria na mikataba
inayopendekezwa kuridhiwa na Bunge iliyo chini ya Wizara
inazozisimamia;
(iii) Kushughulikia Taarifa za utendaji za kila mwaka za Wizara
inazozisimamia; na
(iv) Kufuatilia utekelezaji unaofanywa na Wizara hizo.
Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, katika kipindi cha Januari
2022 hadi Februari, 2023, Kamati ilitekeleza shughuli zifuatazo: -
4
(i) Kujadili taarifa za utekelezaji wa bajeti za Wizara na utendaji
wa taasisI inazozisimamia kwa kipindi cha nusu mwaka (Julai
– Desemba, 2022) kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa
Bajeti;
(ii) Kutembelea na Kukagua miradi ya maendeleo chini ya Wizara
inazozisimamia iliyotengewa fedha kwa mwaka wa fedha
2021/2022; na
(iii) Kuchambua taarifa za utekelezaji wa bajeti ya mwaka
2021/2022 na makadirio ya bajeti ya mwaka 2022/2023 za
Wizara inazozisimamia.
1.4 Njia iliyotumika
Mheshimiwa Spika, Kanuni ya 142 ya Kanuni za Kudumu za
Bunge Toleo la Juni, 2020, imeweka masharti yanayotaka taarifa
ya Kamati inayoingia Bungeni ibainishe njia au mbinu iliyotumia.
Kwa msingi huo, naomba kulijulisha Bunge kuwa Kamati ilitumia
njia na mbinu zifuatazo: -
(i) Kujadili masuala ya sekta na kuibua ajenda za kuweka
kwenye ratiba ili kuwasilisha kwa Spika kwa ajili ya
kuidhinishwa;
(ii) Kufanya uchambuzi wa taarifa zilizowasilishwa na kutathimini
mambo yaliyoripotiwa kwa kuoanisha na mtazamo wa
wananchi kuhusu ustawi wao;
(iii) Kudadavua maudhui ya taarifa zote zilizowasilishwa ili kupata
utoshelevu wa maudhui kwa kulinganisha na mahitaji ya
uelewa wa Kamati kuhusu jambo linahusika;
(iv) Kutembelea baadhi ya maeneo na kuona hali halisi kwa lengo
la kulinganisha yaliyoripotiwa na hali halisi uwandani; na
5
(v) Kujumuisha mambo yanayobainika kwenye vikao wakati wa
majadiliano na mahojiano ili kuorodhesha mambo makuu ya
kutolewa maoni na ushauri.
Mheshimiwa Spika, naomba kulihakikishia Bunge lako tukufu
kuwa njia na mbinu hizo ziliisaidia Kamati kupata matokeo
yanayoripotiwa katika taarifa hii. Aidha, uthabiti wa maudhui ya
taarifa hii umetokana na njia na mbinu hizo. Naliomba Bunge lako
tukufu liipokee na kuijadili taarifa hii kwa kuzingatia ufanisi wa njia
na mbinu zilizotumika.
6
SEHEMU YA PILI
2.0 SHUGHULI ZILIZOTEKELEZWA NA UCHAMBUZI WA
MATOKEO
2.1 Ufafanuzi wa Jumla
Mheshimiwa Spika, katika kufuatilia sekta hizo Kamati ilitekeleza
shughuli zifuatazo: -
2.1.1 Ufuatiliaji wa Maazimio ya Bunge katika taarifa ya
Mwaka 2021/ 2022
i) Sekta ya Uchukuzi
a. Mamlaka ya Bandari Tanzania
Mifumo ya TEHAMA inayotumiwa na Mamlaka ya Bandari
Tanzania iboreshwe ili kuimarisha ulinzi wa mizigo pamoja
na miundombinu ya Bandari.
b. Vyuo vilivyo chini ya Sekta ya uchukuzi
Serikali iviwezeshe kifedha vyuo hivyo, pamoja na
kuimarisha miundombinu yake kwa kutumia mpango
kabambe wa kuendeleza vyuo.
c. Ujenzi wa Reli ya kisasa
Serikali ione umuhimu wa kipande cha Reli cha Tabora –
Kigoma katika kukuza uchumi wa Taifa letu.
d. Ujenzi Reli uzingatie hali ya jiografia ya maeneo
Ujenzi wa Reli nchini unapofanyika, tahadhari kubwa
ichukuliwe ili kuepusha uharibifu wa mazingira na
miundombinu ya reli.
7
e. Ununuzi wa vichwa na mabehewa ya Treni
Upungufu wa vichwa 45 vya treni pamoja na mabehewa
imekuwa ni changamoto inayoathiri ufanisi na mchango wa
sekta kwenye maendeleo ya ustawi wa uchumi wetu.
Mheshimiwa Spika, Utekelezaji wa Mapendekezo Sekta
ya Uchukuzi ni kama ifuatavyo: -
a) Katika sekta hii kuna baadhi ya mapendekezo
yaliyotolewa na Bunge yamefanyiwa kazi kwa asilimia
ndogo na mengine yanaendelea kutekelezwa, Hivyo
basi, hakuna mapendekezo yaliyotekezwa kwa asilimia
mia moja.
b) Mapendekezo ya Bunge yanayoendelea kufanyiwa kazi
ni kama yafuatayo: -
(i) Uboreshaji wa Mifumo ya TEHAMA inayotumiwa
na Mamlaka ya Bandari Tanzania
Mheshimiwa Spika, Awamu ya kwanza ya mfumo huo
umekamilika. Mawakala wa forodha wapatao 877
wamesajiliwa na wanatumia mfumo. Aidha, Uboreshwaji na
mafunzo ya mfumo huo kwa awamu ya kwanza, upande wa
Zanzibar umeanza na unategemea kukamilika mwishoni
mwa mwezi Machi 2023. Mfumo wa pamoja wa Kieletroniki
wa uondoshwaji wa shehena Bandarini (Tanzania Electronic
Single Window System - TeSWs) unategemewa kukamilika
mwezi Juni, 2023.
8
(ii) Kuwezeshwa kifedha na kuimarisha
miundombinu ya Vyuo vilivyo chini ya Sekta ya
Uchukuzi
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuongeza fedha
kwa vyuo vya DMI na NIT kama ifuatavyo: -
Kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Chuo cha DMI
kilitengewa Shilingi bilioni 2.48 ikilinganishwa na
mwaka 2022/2023 ambapo Chuo hicho kimetengewa
Shilingi bilioni 3.90 sawa na ongezeko la asilimia 57.
Aidha, Serikali kupitia Mamlaka ya Bandari (TPA)
itanunua kifaa cha kufundishia manahodha na wahandisi
wa Meli (simulator), tayari Shilingi bilioni 3.6
zimetengwa katika mwaka huu wa fedha kwa ajili hiyo.
Chuo cha NIT kilitengewa jumla ya Shilingi bilioni 35.66
katika mwaka 2021/2022 ikilinganishwa na Shilingi
bilioni 39.05 katika mwaka 2022/2023, sawa na
ongezeko la asilimia 9.5. Aidha, katika mwaka wa fedha
2021/2022, Chuo cha NIT kilitengewa bajeti ya jumla
Shilingi bilioni 9.53 kwa ajili ya ununuzi wa Ndege mbili
(2) za injini moja (1) za kufundishia marubani.
(iii)Ujenzi wa Reli ya Kisasa kipande cha Tabora -
Kigoma kipewe kipaumbele
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TRC imesaini
mkataba na Kampuni ya CCECC na CRCC kutoka China
mnamo tarehe 20 Desemba, 2022 kwa ajili ya Ujenzi wa
Reli ya Kisasa ya SGR kwa Kipande cha Tabora –
9
Kigoma (Km 506). Mkataba huo utatekelezwa kwa
muda wa miezi 42.
(iv)Ujenzi wa Reli uzingatie hali ya jiografia ya
maeneo
Mheshimiwa Spika, Serikali imeeleza kuwa itaendelea
kufanya upembuzi yakinifu kabla ya kuanza kutekeleza
miradi yote mikubwa ikiwa ni pamoja na miradi ya SGR,
uboreshaji wa Bandari na ujenzi wa Meli.
(v)Ununuzi wa vichwa na mabehewa ya Treni
Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa vitendea kazi vya
Miter Gauge Railway (MGR) Ununuzi wa Mabehewa 22
wenye mkataba wa dola 14,964,852.34, manunuzi ya
vipuri vya ukarabati wa mabehewa 600 ya mizigo yenye
thamani ya shilingi 2,135,620,191.97 na mabehewa 37
ya abiria kwa Dola za Marekani 3,655,099.76.
Hadi kufikia Januari, 2023, Serikali imepata mkopo kutoka
Exim Bank ya Korea wenye jumla ya Dola za Marekani
milioni 346.73 kwa ajili ya ununuzi wa vitendea kazi
(vichwa vya treni na mabehewa).
Mheshimiwa Spika, katika sekta hii ya ujenzi Kamati
imeridhika na kasi ya utekelezaji wa Mapendekezo
yaliyotolewa na Bunge kwani kamati ilifuatilia na kubaini
hakuna mapendekezo ambayo hayajafanyiwa kazi kabisa.
10
ii) Sekta ya Ujenzi
a. Ujenzi wa viwanja vya ndege
Serikali ione umuhimu wa kuiachia Mamlaka ya Viwanja wa
Ndege Tanzania (TAA) kazi ya Ujenzi na Usimamizi wa
Viwanja vya Ndege.
b. Ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya mabasi
yaendayo haraka Dar es Salaam (BRT)
Serikali ione namna ya kutatua changamoto ya mradi huu ili
ulete matokeo yaliyokusudiwa.
c. Vyuo vilivyopo Sekta ya Ujenzi
Serikali iandae mikakati ya kuboresha miundombinu, vifaa
vya kufundishia na mazingira ya kujifunza katika vyuo hivyo
na kuviongezea bajeti.
d. Nyumba za Magomeni Kota
TBA waongezewe fedha za kwa ajili ya kuendeleza
uwekezaji kwenye eneo lililo wazi la Magomeni kota.
Mheshimiwa Spika, Utekelezaji wa Mapendekezo
katika sekta ya ujenzi ni kama ifuatavyo: -
a) Kamati imebaini kuwa yapo mapendekezo ya Bunge
yaliyofanyiwa kazi na mengine yapo kwenye hatua
mbalimbali za utekelezaji. Hivyo hakuna mapendekezo
yaliyofanyiwa kazi kikamilifu;
b) Mapendekezo ya Bunge yanayoendelea kufanyiwa kazi ni
kama ifuatavyo: -
11
(i) Kuhusu Ujenzi wa viwanja vya ndege kuachiwa
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA)
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi iliunda
Timu ya Wataalam kutoka Wizara mbalimbali kwa ajili ya
kupitia na kubaini iwapo kama kuna muingiliano wa
majukumu kati ya TAA na TANROADS ikiwa ni utekelezaji
wa maelekezo ya Katibu Mkuu Kiongozi yaliyotokana na
taarifa ya CAG. Timu ilikamilisha na ilitoa ushauri kuwa,
kuna haja ya majukumu ya ujenzi wa viwanja vya ndege
kurudishwa TAA kutoka TANROADS.
(ii) Kuhusu ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya
mabasi yaendayo haraka Dar es Salaam (BRT) ili
kuleta matokeo yaliyokusudiwa
Mheshimiwa Spika, TANROADS inaendelea kushirikiana
na wadau wengine zikiwepo taasisi za Serikali kama DART ili
kufanya pembuzi yakinifu zinazozingatia mazingira halisi na
hatimaye utekelezaji wa miradi yenye manufaa.
(iii) Kuhusu Vyuo vilivyopo Sekta ya Ujenzi
Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka 2022/2023
imeongezeka kwa asilimia 10 ambapo ukarabati na ujenzi
wa majengo mapya umetengewa jumla ya Shilingi bilioni 6.
Usanifu kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Taasisi ya
Ujenzi (ICoT) Morogoro pamoja na tawi la Mbeya
umekamilika. Ukarabati wa majengo katika kampasi ya
12
Mbeya, unatekelezwa na Wakala wa Majengo Tanzania
(TBA). Ujenzi umefikia asilimia 47.5.
(iv) Nyumba za Magomeni Kota
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa jambo hili bado
unaendelea kwani Serikali imeendelea na mchakato wa
kurekebisha kanuni zinazoendesha TBA ili kuruhusu
uwekezaji shirikishi.
c) Mheshimiwa Spika, katika sekta hii ya Ujenzi, Kamati
imeridhika na kasi ya utekelezaji wa Mapendekezo
yaliyotolewa na Bunge kwani kamati ilifuatilia na kubaini
kuwa, hakuna mapendekezo ambayo hayajafanyiwa kazi
kabisa. Kamati inatoa pongezi kwa Serikali kwa kuona
umuhimu wa kutatua changamoto.
iii) Sekta ya Mawasiliano
a. Uhalifu wa kimtandao
TCRA ishirikiane na Jeshi la Polisi kukabiliana na tatizo hilo.
b. Kupungua kwa miamala ya simu
Serikali iisimamie TCRA kukutana na wadau na watoa
huduma ili kutatua changamoto hizo.
c. Udhibiti hafifu wa huduma za usafirishaji wa
mizigo, vipeto na vifurushi nchini
Serikali ije na Kanuni zitakazosimamia kumbukumbu za
kielektroniki za usafirishaji wa mizigo, vifurushi na vipeto;
na kuisimamia TCRA ambaye ni mtoa leseni ili kuondoa
tatizo hilo.
13
d. Changamoto za shughuli za Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)
Serikali itenge fedha zaidi kadiri inavyowezekana kwa ajili
ya Mfuko huu (UCSAF); pamoja na kuisimamia Kampuni ya
Mawasiliano Tanzania (TTCL) kukamilisha miradi ya ujenzi
wa minara.
e. Madeni makubwa kwa Shirika la Posta Tanzania
(TPC)
Serikali ilisaidie Shirika la Posta liweze kulipwa madeni yake
mapema; na isimamie na kuitaka TCRA kulilipa fedha
Shirika hilo ikiwa ni kamisheni kutokana na mapato
wanayopata ya ada ya leseni ya wasafirishaji wa mizigo.
f. Changamoto ya madeni ya TTCL na uendeshaji
wa Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa
Serikali isimamie Kampuni ya Mawasiliano ya Simu (TTCL) ili
iweze kulipwa madeni yake, kukamilisha Kanuni za
uendeshaji wa Mkongo wa Taifa, kutoa fedha kwa TTCL na
kufanya marekebisho ya sheria ya manunuzi ili kuruhusu
TTCL iweze kununua vifaa vilivyotumika kutoka makampuni
mengine.
a) Mheshimiwa Spika, mapendekezo yaliyotolewa na
Bunge yanaendelea na utekelezaji, hivyo basi, hakuna
mapendekezo yaliyotekezwa kikamilifu; na
b) Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Bunge
yanayoendelea kufanyiwa kazi ni kama ifuatavyo: -
14
(i) Kuhusu Uhalifu wa kimtandao
Mheshimiwa Spika, Serikali imechukua hatua
mbalimbali katika kukabiliana na uhalifu wa kimtandao
na inaendelea kuchukua hatua.
(a) Serikali imeanzisha timu maalum inayojumuisha
wataalam kutoka vyombo vya Ulinzi na Usalama,
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka - DPP na TCRA;
(b) Serikali inahamasisha zoezi la uhakiki wa laini za
simu (namba) na kuwa laini zote ambazo
hazitahakikiwa mpaka ifikapo tarehe 13 Februari,
2023 zitafungiwa;
(c) Kesi 42 zipo katika upelelezi, ambapo kesi 6
upelelezi umekamilika (zinaenda mahakamani hivi
karibuni) na kesi 36 upelelezi unaendelea. TCRA pia
ilichukua hatua za kukabiliana na uhalifu wa
kimtandao kwa kusimamisha usajili kwa mawakalahuru kwenye maeneo yanayoripotiwa kuwa na idadi
kubwa ya matukio ya wizi wa kimtandao.
(ii) Kupungua kwa miamala ya simu
Mheshimiwa Spika, TCRA imeendelea kufuatilia kwa
ukaribu mienendo ya miamala ya fedha inayopita katika
mitandao ya simu. Kwa kipindi cha Julai hadi Disemba
2022, idadi ya miamala ya fedha ilipanda kutoka
349,952,830 kwa mwezi Julai, 2022 hadi kufikia
miamala 410,741,783,982 kwa mwezi Disemba, 2022.
Pia idadi ya watumiaji wa Mobile Money iliongezeka toka
15
38,407,233 mwezi Julai mpaka 40,953,496 kwa mwezi
Disemba.
(iii) Udhibiti hafifu wa huduma za usafirishaji wa
mizigo, vipeto na vifurushi nchini;
Mheshimiwa Spika, Hatua zimechukuliwa kwa kuanza
kupitia Kanuni za Usafirishaji wa Mizigo, Vifurushi na
Vipeto kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili
kuongeza umadhubuti wa mfumo wa udhibiti.
Aidha, usajili wa watoa huduma hizo unaendelea ukiwa
na lengo la kupata taarifa za watoa huduma wote katika
Sekta ya Posta.
(iv) Madeni makubwa kwa Shirika la Posta
Tanzania
Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na
Shirika la Posta imewasilisha Wizara ya Fedha na
Mipango andiko la kuomba kufutiwa deni la muda mrefu
la kodi kiasi cha Shilingi Billioni 26.8 Hii itakuwa njia
ya kuisaidia Posta katika kukusanya madeni, Wizara kwa
kushirikiana na Shirika la Posta imeandika barua kwenda
taasisi za umma zenye madeni kuwataka kulipa madeni
hayo.
(v) Changamoto za shughuli za Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote - UCSAF
Mheshimiwa Spika, Serikali imetenga jumla ya Dola
za Marekani milioni 30 kupitia fedha za mradi wa
Tanzania ya Kidigitali ambazo ni mkopo kutoka Benki ya
16
Dunia ili kutekeleza miradi ya kufikisha huduma za
mawasiliano vijijini. Fedha hizo zitawezesha ujenzi wa
minara mipya takribani 380 na kuongeza nguvu ya
minara 488.
(vi) Changamoto ya madeni ya TTCL na
uendeshaji wa Mkongo wa Mawasiliano wa
Taifa
Mheshimiwa Spika, Wizara imewasilisha madeni hayo
Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya kufanyiwa
uhakiki na mara utakapomilika malipo yatafanyika.
Wizara imekamilisha taratibu za kukabidhi majukumu ya
usimamizi, uendeshaji na uendelezaji wa Mkongo wa
Taifa wa Mawasiliano kwa TTCL na taratibu za
kuwasilisha Waraka wa Baraza la Mawaziri kuwezesha
TTCL kumiliki Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano
zinaendelea.
c) Mheshimiwa Spika, Kamati ilielezwa kuwa hakuna
Mapendekezo ya Bunge ambayo hayajatekelezwa
kabisa. Kamati inaendelea kusisitiza kuwa mapendekezo
ya Bunge yafanyiwe kazi kikamilifu ili kupunguza
changamoto zilizopo.
2.1.2 Uchambuzi wa Bajeti za Wizara na Ukaguzi wa
Miradi ya Maendeleo
Mheshimiwa Spika, Kamati ilibaini mambo yafuatayo katika
Sekta ya ujenzi: -
17
(i) Kulijitokeza suala la fedha zinazotolewa kulipa madeni ya miradi
ya nyuma badala ya utekelezaji wa miradi mipya. Kamati
ilishauri kwamba katika maombi ya fedha, Serikali itofautishe
fedha itakayotumika kulipa madeni na ya utekelezaji wa miradi
mipya; na
(ii)Changamoto ya kuwa na miradi mingi kuliko uhalisia wa fedha.
Kamati inaona ni vyema Serikali ikaweka mkakati wa kutekeleza
miradi michache kwa ufanisi kuliko miradi mingi isiyotekelezeka
Pamoja na kuwa ilitengewa bajeti.
2.1.3 Ziara za ufuatiliaji wa Miradi ya Maendeleo
Mheshimiwa Spika, tarehe 13 – 20 Machi, 2021, Kamati
ilizingatia masharti ya Kanuni ya 117 (1) ya Kanuni za Bunge na
kutembelea miradi inayotekelezwa na Wizara zilizo chini yake.
Kamati ilitembelea mikoa mitatu ambayo ni Simiyu, Mwanza na
Kagera na kukagua miradi ya Ujenzi wa Reli ya Kisasa – kipande
cha Isaka - Mwanza (Lot 1V), Ujenzi na ukarabati wa Meli kwenye
Maziwa Makuu, Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, Ujenzi na
ukarabati wa Vivuko, Maegesho na Utekelezaji wa mradi wa
Postikodi na Anwani za Makazi, Ujenzi wa Miundombinu ya Viwanja
vya Ndege, Ununuzi wa Rada, vifaa na ujenzi wa miundombinu ya
hali ya hewa na Mradi wa Ujenzi wa barabara na Madaraja.
Mheshimiwa Spika, Katika ziara hiyo, Kamati ilibaini mafanikio
na changamoto ambazo ziliwasilishwa kwenye taarifa yake. Ni rai
ya kamati kuwa zitapatiwa ufumbuzi wa haraka.
18
2.1.4 Uchambuzi wa Taarifa za Utendaji
Mheshimiwa Spika, naomba kulijulisha Bunge lako tukufu kuwa
utaratibu wa kupokea na kujadili taarifa za kutoka Serikalini
unaiwezesha Kamati kulisaidia Bunge kutekeleza majukumu yake
ya kuisimamia Serikali kwa mujibu wa Ibara ya 63 (2) ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
2.1.5 Uchambuzi wa Mswada na Maazimio
Mheshimiwa Spika, Kamati ilipata fursa ya kuwasilisha taarifa
yake bungeni kuhusu Muswada wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi ambao
ulipitishwa na Bunge na kusainiwa kuwa sheria rasmi na
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 27
Novemba, 2022.
2.2 Uchambuzi wa Matokeo
Mheshimiwa Spika, Kamati ilitoa taarifa ya ziara kwa miradi
mbalimbali iliyokagua na kutembelea kupitia taarifa ya Kamati
inayohusu utekelezaji wa bajeti ya Wizara hizo kwa mwaka wa
fedha wa 2022/2023.
Mheshimiwa Spika, Aidha, ziara hizo zilifanyika kwa Lengo la
kuhakiki shughuli za umma zilizotekelezwa katika sekta
zinazosimamiwa na Kamati kwa kuzingatia matarajio ya wananchi.
2.2.1 Mafanikio na Changamoto
Mheshimiwa Spika, naomba kulijulisha Bunge, matokeo ya
uhakiki yanayoonesha mafanikio na changamoto kwa kila sekta
kama ifuatavyo: -
19
a. Sekta ya Uchukuzi
Mheshimiwa Spika, Kamati ilihakiki mchango wa sekta hii na
kubaini mafanikio mbalimbali katika sekta hii. Serikali itaendelea
kuimarisha na kuboresha miundombinu na huduma za reli, bandari,
viwanja vya ndege, kununua ndege, meli za abiria na mizigo na
kuboresha utabiri wa hali ya hewa nchini, Kama ilivyoeleza katika
Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2020-2025, Ibara 59 (a) – (j).
Mheshimiwa Spika, Katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025
imeeleza kuwa Serikali kupitia Wizara mbalimbali imeweka mkakati
mpya uitwao “Tekeleza sasa kwa matokeo makubwa”. Serikali
imeeleza nia ya kuimarisha miundombinu ya usafiri hususan
uboreshaji wa bandari ya Dar es Salaam pamoja na reli ya kati.
Mheshimiwa Spika, Kamati ilibaini changamoto mbalimbali katika
sekta ya usafiri na usafirishaji majini na usafiri wa Reli, mfano kuna
uhaba wa wataalam wenye ujuzi na uzoefu, kuchelewa kulipwa
fedha za ujenzi wa miradi hali inayozorotesha maendeleo ya sekta,
uchumi wa nchi na wananchi.
Mheshimiwa Spika, Kamati inatoa msisitizo kuwa changamoto
hizo zifanyiwe kazi kikamilifu kwa ustawi wa wananchi.
b. Sekta ya Ujenzi
Mheshimiwa Spika, Kuna miradi mbalimbali ambayo Kamati
ilipata nafasi ya kuitembelea katika kipindi cha mwezi Julai, 2022 –
Mpaka Januari 2023 kama ifuatavyo: -
20
(i) Mradi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha zege
wa Itoni-Ludewa-Manda - Lusitu-Mawengi (Km 50.0)
Mheshimiwa Spika, katika ziara hiyo, Kamati ilijulishwa
mafanikio mbalimbali ya mradi huo kama ifuatavyo: -
a) Ushirikishwaji wa wazawa katika mradi kwani umeajiri
wafanyakazi 690 ambapo wazawa 650 sawa na asilimia
94;
b) Mkandarasi ameleta wataalam mahiri na wenye uzoefu; na
c) Mkandarasi ameongeza muda wa kufanya kazi hadi usiku
na ameandaa mpango kazi mpya unaolenga kumaliza kazi
kwa wakati;
Mheshimiwa Spika, Kamati ilijulishwa changamoto
zinazoukabili mradi huo kuwa ni pamoja na: -
a) Fedha kutotolewa kwa wakati hali inayosababisha
Kuongezeka kwa gharama za mradi kutokana na
kuongezwa kwa muda kutoka miezi 28 - hadi miezi 69;
b) Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mawengi ambao ardhi yao
imetwaliwa ili kupisha ujenzi wa mradi bado hawajalipwa
fidia;
c) Mvua nyingi zimeathiri utekelezaji wa mradi pia kuna
uhalibifu wa mazingira kwenye chanzo cha maji kutokana
na ukataji wa mlima;
d) Maporomoko ya udongo kwenye maeneo yenye kina kirefu
cha kuchimba kwa ajili ya kupitisha barabara; na
e) Uhaba wa malighafi mfano saruji kutoka kwenye viwanda
vya TWIGA na DANGOTE.
21
Mheshimiwa Spika, Serikali iimarishe usafiri wa maji katika
Ziwa Nyasa ili kusafirisha madini yanayochimbwa Mkoani
Njombe na kusaidia wananchi wanaoishi pembezoni mwa ziwa
kunufaika na fursa za kiuchumi.
(ii) Ujenzi wa nyumba 3500 za watumishi wa umma
katika eneo la Nzuguni – Jijini Dodoma
Mheshimiwa Spika, mradi huo ukikamilika utakuwa na manufaa
mbalimbali kama ifuatavyo: -
a) Mradi umewezesha wataalam wa ndani ya Wakala wa
Majengo kujipatia uzoefu zaidi kwenye ubunifu na usanifu
wa majengo;
b) Wakazi wa Dodoma zaidi ya 100 wamenufaika na ajira
rasmi na zisizo rasmi kama mafundi ujenzi, vibarua na
mama lishe;
c) Mradi umenufaisha viwanda kwani vifaa vyote vya ujenzi
vinavyotumiwa kwenye mradi vinatoka kwenye viwanda
hivyo;
d) Awamu ya kwanza ya mradi una thamani ya shilingi bilioni
14, fedha hizo zimetolewa zote kwa asilimia 100;
e) Utekelezaji wa mradi huu umepunguza uhalifu katika eneo
la Nzuguni kwani kabla ya mradi eneo hilo lilikuwa maficho
ya wahalifu;
f) Mradi utapunguza changamoto ya uhaba wa nyumba kwa
watumishi wa umma waliopo Dodoma; na
g) Mradi utaongeza mapato ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, changamoto zinazoukabili mradi huu
kuwa ni pamoja na: -
22
a) Ukosefu wa barabara ya kufika eneo la mradi na uhaba
mkubwa wa maji;
b) Kupanda kwa gharama vifaa vya ujenzi hali inayopelekea
kuongezeka kwa gharama za utekelezaji wa mradi; na
c) TBA wanadai fedha nyingi kutoka kwa wapangaji pamoja na
kutolipwa fedha za ujenzi wa miradi mbalimbali ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, chimbuko la mradi huo ni utekelezaji wa
maamuzi ya Serikali ya kuhamishia Makao Makuu Jijini
Dodoma na hivyo kuongezeka kwa mahitaji ya nyumba za
makazi kwa watumishi wa Umma.
c. Sekta ya Mawasiliano
Mheshimiwa Spika, Kamati imebaini mafanikio mbalimbali
yaliyopatikana katika sekta hii, mfano kuandaliwa kwa mkakati wa
miaka mitano (2021-2025) wa kuharakisha utekelezaji na matumizi
ya Mfumo wa Anwani za makazi na postikodi, kuongeza kwa pato
la Taifa na kuongeza matumizi ya TEHAMA nchini.
Mheshimiwa Spika, Changamoto katika sekta hii zinaweza
kusababisha malengo yaliyoelezwa kwenye Ilani ya Chama cha
Mapinduzi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020-2025
yasitimie endapo kama hazitapatiwa ufumbuzi wa haraka.
Kuchelewa kukamilika kwa mikataba na taratibu za manunuzi ya
vifaa kwa ajili ya miradi mbalimbali, baadhi ya wakandarasi
kutokuwa na uwezo wa kutekeleza miradi kwa kiwango
kinachotakiwa, na miradi kutokamilika kwa wakati ni moja ya
vikwazo vinavyoikabili Sekta hii.
23
Mheshimiwa Spika, Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa ajili ya
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020-2025 ibara ya 61 (a) –(o) inaeleza
kuwa Sekta hii imejikita zaidi katika kuimarisha ubora wa
mawasiliano nchini na kuhakikisha wigo wa mawasiliano
unaongezeka na kuwafikia wananchi wote.
Aidha, Dira ya maendeleo ya Taifa 2020, imeeleza kuwa ukuzaji wa
Teknolojia ya upashanaji Habari na Mawasiliano ni muhimu katika
kuleta mageuzi ya kijamii na kiuchumi.
2.3 Majumuisho ya Sehemu ya Pili
Mheshimiwa Spika, uimarishaji wa miundombinu katika sekta ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ni uwekezaji muhimu hivyo basi,
Serikali inatakiwa kuwa mstari wa mbele katika suala hili ili kujenga
mtandao mzuri utaowezesha kuleta maendeleo mijini na vijijini
katika kuimarisha ustawi wa wananchi na kuweka mazingira ya
kukua kwa uchumi na maisha bora kwa kila Mtanzania kama Ilani
ya Chama cha Mapinduzi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2020 -2025 na Dira ya maendeleo ya Taifa 2025 inavyoeleza.
Mheshimiwa Spika, Kamati inatoa rai kuwa changamoto zilizopo
katika sekta hizo zikapatiwa ufumbuzi wa haraka ili kufikia
malengo.
24
SEHEMU YA TATU
3.0 MAONI NA MAPENDEKEZO
3.1 Maoni ya jumla
Mheshimiwa Spika, Wananchi wanayo matumaini makubwa
yanayopaswa kutimizwa katika sekta zinazosimamiwa na Kamati hii
kwani bado juhudi za Serikali zinahitajika katika kuboresha na
kutatua changamoto.
Kamati inatoa maoni yafuatayo: -
1. Upungufu wa watumishi na vitendea kazi imekuwa ni
changamoto kubwa kwa baadhi ya taasisi na hivyo kuathiri
utendaji kazi wa Taasisi hizo. Ni maoni ya Kamati kuwa Serikali
iajiri watumishi wa kutosha;
2. Yafanyike marekebisho ya sheria ya Reli kuruhusu sekta binafsi
kuwekeza katika kutoa huduma za reli;
3. Ucheleweshwaji wa malipo ya kodi ya pango kwa nyumba za
TBA ambako kunasababisha Wakala kushindwa kutimiza
malengo yake kutafutiwe ufumbuzi wa haraka;
4. Serikali iongeze bajeti ili kukabiliana na Ufinyu wa bajeti kwa
taasisi zilizo katika Wizara kunakopelekea kukwamisha
utekelezaji wa majukumu na miradi mbalimbali mfano
TANROADS na Roadfund;
5. Kutokuwa na kanuni za uendeshaji kwa TBA, ni jambo
linalopelekea TBA kushindwa kuendesha miradi kwa kushirikisha
sekta binafsi, ni maoni ya kamati kuwa Serikali irekebishe kanuni
hizo;
25
6. Serikali isimamie utekelezaji wa ulipwaji wa fidia kwa Wananchi
waliopisha utekelezaji na miradi ya maendeleo;
7. Kuchelewa kutekeleza kwa baadhi ya miradi au kasi ndogo ya
utekelezaji kunachangia miradi mingi kutokamilka kwa wakati.
Mathalani, ujenzi wa minara, mradi wa reli ya kisasa kipande
cha Dar es Salaam – Morogoro hali hii inakwamisha kufikia
lengo lililokusudiwa. Ni maoni ya Kamati kuwa Serikali
iwasimamie Wakandarasi ili wamalize miradi katika muda
unaopangwa;
8. Serikali iendelee kusimamia ukamilishwaji wa mikataba na
taratibu za manunuzi ya vifaa ili miradi iweze kutekelezwa kwa
wakati;
9. Serikali isimamie Wakandarasi wanaotekeleza miradi Miradi chini
ya kiwango;
10. Serikali iwasimamie Wasafirishaji binafsi wa mizigo na vifurushi
ili waweze kutoa kamisheni au wawe Mawakala wa Posta; na
11. Ajira za TBC zitoe fursa kwa watu wenye vipaji kuliko kuangalia
sifa za vyeti.
26
3.2 Mapendekezo
Mheshimiwa Spika, Napenda kuchukua nafasi hii kuipongeza
Serikali kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Sekta za
Ujenzi, Uchukuzi, Habari na Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari.
Taarifa hii imeeleza shughuli zilizotekelezwa na Kamati pamoja na
kubainisha mafanikio na changamoto kama ilivyobainika wakati wa
utekelezaji wa shughuli za Kamati, Utekelezaji wa Maazimio ya
Bunge katika Taarifa ya Mwaka 2021/ 2022. Aidha, Taarifa
imeonesha jinsi Katiba, Dira ya Taifa 2025, na Ilani ya Chama cha
Mapinduzi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020-2025
vinavyoelekeza kuhusu Sekta zinazosimamiwa na Kamati hii.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo zipo changamoto
zilizobainika na ambazo utatuzi wake utasaidia kuwezesha huduma
bora, kukua kwa uchumi, maisha bora ya wananchi na maendeleo
ya Taifa letu. Kwa sababu hiyo, naomba kutoa mapendekezo ya
utatuzi wa changamoto kwa kila sekta kama ifuatavyo: -
3.2.1 Sekta ya Uchukuzi
a) Uhaba wa Watumishi na Vitendea Kazi
KWA KUWA, Uhaba wa watumishi na vitendea kazi katika
sekta za usafiri wa anga, reli, hali ya hewa na usafiri kwa njia
ya maji hali inayosababisha maendeleo ya sekta hii yasifikie
malengo yaliyokusudiwa,
NA KWA KUWA, changamoto hizo zinasababisha sekta ya
uchukuzi kutotoa mchango unaokusudiwa kwa pato la Taifa.
27
KWA HIYO BASI, Bunge linashauri kwamba, Serikali iajiri
watumishi wa kutosha na wenye uzoefu, ili kukidhi mahitaji
yaliyopo.
b) Marekebisho ya sheria ya Reli ili kuruhusu uwekezaji
KWA KUWA, umuhimu wa sekta ya reli kufanya
marekebisho ya sheria ni mkubwa ili kuruhusu sekta binafsi
kuwekeza katika kutoa huduma za reli nchini;
NA KWA KUWA, changamoto hiyo inasababisha wawekezaji
kutoka sekta binafsi kushindwa kuwekeza katika reli hivyo
kuchelewesha na kurudisha nyuma ukuaji wa uchumi wa nchi,
KWA HIYO BASI, Bunge linashauri kwamba, Serikali
iharakishe mchakato wa marekebisho ya sheria ya Reli iliiweze
kuruhusu sekta binafsi kufanya uwekezaji.
3.2.2 Sekta ya Ujenzi
a) Changamoto ya Wapangaji wa nyumba za TBA kutolipa
kodi kwa wakati
KWA KUWA, imeonekana kuna changamoto ya ulipaji wa kodi
kwa wapangaji wa TBA na kusababisha shirika kupata hasara
na kushindwa kutekeleza miradi mingine;
NA KWA KUWA, changamoto hiyo inasababisha TBA
kushindwa kukusanya fedha ili iweze kujiendesha kibiashara,
KWA HIYO BASI, Bunge linashauri kwamba; TBA ifuatilie
wadaiwa sugu, iwachukulie hatua za kisheria bila kumuonea
mtu aibu, aidha ipeleke taarifa ya wadaiwa kwa msajili wa
Hazina.
28
b) TBA Kuchelewa kulipwa fedha za ujenzi wa miradi kwa
wakati
KWA KUWA, kuna changamoto ya TBA kuchelewa kulipwa
fedha za ujenzi wa miradi kwa wakati hali inayosababisha miradi
kutofikia malengo;
NA KWA KUWA, changamoto hizo zinaweza kuchelewesha
miradi kutokamilika kwa wakati kama ilivyokusudiwa,
KWA HIYO BASI, Bunge linashauri kwamba; Serikali itoe
fedha kwa TBA ili waweze kutekeleza majukumu yake kwa
ufanisi.
c) Changamoto ya Kanuni zinazoendesha TBA kutoruhusu
uwekezaji mkubwa
KWA KUWA imeonekana kuna mapungufu kwa TBA kutokuwa na
kanuni zinazoruhusu kushirikisha sekta binafsi katika utekelezaji wa
miradi yake kunakosababisha ishindwe kufikia malengo yake;
NA KWA KUWA, kutorekebisha kanuni hizo kunakosesha wakala
kufanya uwekezaji mkubwa;
KWA HIYO BASI, Bunge linashauri kwamba; TBA ifanye
mchakato wa kurekebisha Kanuni zake kwa haraka ili iweze
kushirikiana na Sekta binafsi katika kutekeleza miradi.
d) Changamoto ya kuchelewa kulipwa fidia Ujenzi wa
barabara ya Itoni – Ludewa - Manda - Lusitu-Mawengi
KWA KUWA, kuna changamoto ya kuchelewa kulipwa fidia kwa
wananchi wanaopitiwa na mradi, kunasababisha mradi huo
kutofikia malengo kama yalivyoainishwa katika Ilani ya Chama cha
29
Mapinduzi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020-2025 Ibara
ya 55 (c) (I),
NA KWA KUWA, changamoto hizo zinaweza kuchelewesha mradi
na kuongeza gharama jambo ambalo linaongeza mzigo wa madeni
kwa Serikali,
KWA HIYO BASI, Bunge linashauri kwamba;
(i) Serikali iwalipe fidia Wananchi wa kijiji cha Mawengi ambao
ardhi yao imetwaliwa kwa ajili ya kutekeleza mradi; na
(ii) Serikali iongeze fedha kwa TANROADS ili iweze kutekeleza
miradi hii ambayo ni muhimu katika ukuaji wa uchumi wa
nchi na ustawi wa wananchi.
e) Miradi kutokamilika kwa wakati
KWA KUWA, Miradi kutokamilika kwa wakati
kunakosababishwa na kutotolewa fedha kwa wakati hivyo,
kupelekea ongezeko la gharama,
NA KWA KUWA, changamoto hiyo inapelekea sekta ya
ujenzi kutotoa mchango unaokusudiwa kwa pato la nchi na
wananchi kwa wake,
KWA HIYO BASI, Bunge linashauri kwamba, Serikali ilipe
Wakandarasi kwa wakati ili waweze kukamilisha miradi ndani ya
muda uliowekwa na kuepuka kupanda kwa gharama za ujenzi
pamoja na riba.
f) Kuongezeka kwa gharama za miradi
KWA KUWA, kuna changamoto ya kuongezeka kwa gharama
za miradi kunakosababishwa na kuongezeka kwa bei za vifaa
30
wakati wa utekelezaji kusababisha kupanda kwa gharama za
mradi na kunarudisha nyuma maendeleo katika miradi;
NA KWA KUWA, changamoto hiyo inapelekea kupanda kwa
gharama za mradi na kutokamilika kwa wakati,
KWA HIYO BASI, Bunge linashauri kwamba, Serikali isimamie
mikataba ya TANROADS wanayoingia ili kusiwe na mabadiliko ya
gharama wakati wa kutekeleza miradi.
3.2.3 Sekta ya Mawasiliano
a) Kuchelewa kukamilika kwa mikataba na taratibu za
manunuzi
KWA KUWA, kuchelewa kukamilika kwa mikataba na taratibu
za manunuzi ya vifaa kwa ajili ya miradi mbalimbali,
kunasababisha sekta kutofikia malengo stahiki,
NA KWA KUWA, Changamoto hizo zinaweza kuchelewesha
miradi katika sekta hii kutokukamilika kwa wakati na
kuongezeka kwa gharama za miradi jambo ambalo linaongeza
mzigo wa madeni kwa Serikali,
KWA HIYO BASI, Bunge linashauri kwamba, Serikali ikamilishe
kwa wakati mikataba na taratibu za manunuzi ya vifaa kwa ajili
ya miradi mbalimbali.
b) Changamoto ya Miradi kutekelezwa chini ya kiwango
KWA KUWA, kuna baadhi ya Wakandarasi kutokuwa na uwezo
wa kutekeleza miradi kwa kiwango kinachotakiwa katika ujenzi
wa minara na miradi mingine kunapelekea serikali kupata
hasara;
31
NA KWA KUWA, Changamoto hiyo inaweza kusababisha miradi
katika sekta hii kutokukamilika kwa wakati na kuongezeka kwa
gharama za miradi jambo ambalo linaongeza mzigo wa madeni
kwa Serikali,
KWA HIYO BASI, Bunge linashauri kwamba, Serikali isimamie
kwa ukaribu Wakandarasi ambao hawana uwezo wa kutekeleza
miradi kwa kiwango kinachotakiwa.
c) Upotevu wa Mapato ya Serikali unaotokana na Shirika la
Posta
KWA KUWA, Serikali kupitia shirika la POSTA inakosa mapato
yanayotokana na usafirishaji wa mizigo, vipeto na vifurushi
vinavyosafirishwa na Makampuni binafsi ya usafirishaji;
NA KWA KUWA, makampuni hayo hayatoi Kamisheni yeyote
kwa Serikali, hali inayosababisha Serikali kukosa mapato;
KWA HIYO BASI, Bunge linashauri kwamba, Serikali iandae
mkakati wa kupata kamisheni kutoka kwa wasafirishaji binafsi
au kuwatumia makampuni binafsi kama Mawakala wa
kusafirisha mizigo.
d) TBC iajiri Wasanii wenye Vipaji
KWA KUWA, TBC kuna watangazaji au wasanii wenye vipaji
vizuri lakini hawana sifa za kupata ajira kwa mujibu wa taratibu
za Serikali, na hali hiyo inasababisha shirika linashindwa kufanya
ushindani na makampuni binafsi ya utangazaji ambayo
yanazingatia vipaji;
NA KWA KUWA, changamoto hiyo inasababisha kupunguza
mvuto kwa wananchi ambao huvutiwa na vipaji hivyo,
32
KWA HIYO BASI, Bunge linashauri kwamba, Serikali iruhusu
shirika la Utangazaji Tanzania - TBC kutoa ajira kwa watu wenye
vipaji kulingana na matakwa ya soko.
3.3 Majumuisho Sehemu ya Tatu
Mheshimiwa Spika, katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa
ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020-2025 Ibara ya 55 (a) - (c)
inaelezea kwamba” Serikali kuendeleza shughuli za ujenzi wa
Miundombinu mbalimbali ili kuifanya sekta ya ujenzi ifikie malengo
yake ya kuwezesha wananchi kuendelea na uzalishaji kwa ajili ya
kuongeza kipato”.
Kwa Sekta ya uchukuzi, Kamati inaendelea kusisitiza kuwa
maboresho yaendelee kufanyika katika eneo la bandari, reli,
viwanja vya ndege na meli vinahitajika ili kuweza kuboresha
usafirishaji wa mizigo, bidhaa na abiria.
Mheshimiwa Spika, Katika Sekta ya Mawasiliano kamati inatoa
maoni kuwa, Serikali iendelee na maboresho ili kuwezesha huduma
za mawasiliano kupatikana kwa asilimia 94 ifikapo 2025 kama
inavyoelezwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa ajili ya
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020-2025 Ibara ya 60 (d).
33
SEHEMU YA NNE
4.0 HITIMISHO NA HOJA
4.1 Maelezo ya Kuhitimisha
Mheshimiwa Spika, naomba kuhitimisha Taarifa hii kwa
kuthamini utaratibu uliowekwa na Bunge wa kuzitaka Kamati za
Kudumu za Bunge kuripoti shughuli zake kwa kipindi cha mwaka.
Utaratibu huu unaliweka Bunge katika nafasi ya kutambua hali
ilivyo katika sekta mbalimbali. Kwa kuwa Taarifa hizo zinatolewa
katika Mkutano wa Mwisho kabla ya mkutano wa bajeti, ushauri wa
Bunge kwa serikali unaweza kufanyiwa kazi kwa mwaka wa fedha
unaofuata.
Mheshimiwa Spika, kwa maelezo hayo, napenda kukushukuru
tena kwa kunipa nafasi hii adhimu ili niweze kuwasilisha Taarifa hii
mbele ya Bunge lako Tukufu. Naamini maelezo na ufafanuzi
nilioutoa, utaliwezesha Bunge kujadili inavyostahili na kutoa
ushauri kwa Serikali ili kuboresha shughuli na kuongeza tija katika
sekta zinazosimamiwa na Kamati hii.
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Miundombinu, naomba kumshukuru kwa dhati Mhe. Prof.
Makame Mnyaa Mbarawa (Mb), Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi
akishirikiana na Manaibu Mawaziri Mhe. Eng. Msongwe Geofrey
Kasekenya (Mb) (Ujenzi), na Mhe. Atupele Fredy Mwakibete (Mb)
(Uchukuzi) kwa ushirikiano mzuri wanaoutoa kwa Kamati. Vile vile,
namshukuru Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb) Waziri wa Habari,
Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Eng. Kundo Andrea
34
Mathew (Mb), Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya
Habari kwa kuipa Kamati ushirikiano stahiki.
Mheshimiwa Spika, nawashukuru pia Makatibu Wakuu, Naibu
Makatibu Wakuu na Watendaji wote wa Wizara ya Ujenzi na
Uchukuzi, na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya
Habari kwa kuwawezesha Mawaziri na Naibu Mawaziri kutoa
ushirikiano kwa Kamati.
Mwisho lakini si kwa umuhimu, namshukuru Ndg. Athumani
Hussein Mkurugenzi wa Idara ya Kamati, Ndg. Gerald Magili,
Mkurugenzi Msaidizi na Makatibu wa Kamati Ndg. Janeth Malangu
na Ndg. Victory Mrema, pamoja na Ndg. Grace Samweli, Msaidizi
wa Kamati kwa Shughuli za uratibu na kufanikisha kazi za Kamati
kama ilivyostahili.
Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa nawashukuru Wajumbe wa
Kamati hii kwa kujituma wakilenga kutoa ushauri unaofaa kwa
Bunge. Kufanya hivyo kutaiwezesha Serikali kuboresha maeneo
mbalimbali na kuendelea kukidhi matarajio ya wananchi kwa
Serikali yao. Kwa kutambua mchango wao, naomba kuwataja kwa
majina kama ifuatavyo: -
35
1. Mhe. Moshi Seleman Kakoso, Mb - Mwenyekiti
2. Mhe. Anne Kilango Malecela, Mb - Makamu Mwenyekiti
3. Mhe. Zuberi Mohamed Kuchauka, Mb - Mjumbe
4. Mhe. Abbas Ali Hassan Mwinyi, Mb - “
5. Mhe. Miraji Jumanne Mtaturu, Mb - “
6. Mhe. Sofia Hebron Mwakagenda, Mb - “
7. Mhe. Ahmed Mabkhut Shabiby, Mb - “
8. Mhe. Aeshi Khalfan Hilaly, Mb - “
9. Mhe. Abdulazizi Mohamed Abood Mb - “
10. Mhe. Eng.Mwanaisha N. Ulenge, Mb - “
11. Mhe. Mohamed Maulid Ali, Mb - “
12. Mhe. Innocent Edward Kalogeris, Mb - “
13. Mhe. Mbarouk Juma Khatibu, Mb - “
14. Mhe. Amina Ally Mzee, Mb - “
15. Mhe. Rose Vicent Busiga, Mb - “
16. Mhe. Ally Anyigulile Jumbe Mlaghila, Mb - “
17. Mhe. Fredric Edward Lowassa, Mb - “
18. Mhe. Stella Simon Fiyao, Mb - “
19. Mhe. Innocent Sebba Bilakwate, Mb - “
20. Mhe. Ghati Zephania Chomete, Mb - “
21. Mhe. Ahmed Yahya Abdulwakil, Mb - “
22. Mhe. Bahati Khamis Kombo, Mb - “
23. Mhe. Angelina Adam Malembeka, Mb - “
24. Mhe. Ahmed Ally Salum, Mb - “
4.2 Hoja
Mheshimiwa Spika, baada yakusema hayo, naliomba Bunge lako
tukufu lipokee na kuijadili Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati
36
ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kwa kipindi cha Januari,
2022 hadi Februari, 2023, ili hatimaye kupitisha mapendekezo ya
Kamati yawe ushauri wa Bunge kwa Serikali.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
Moshi Selemani Kakoso, Mb
MWENYEKITI
KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MIUNDOMBINU
31 Januari, 2023
Comments
Post a Comment