UBUNGO NA LISHE YA WATOTO

Mradi wa kukuza lishe (SUN), wawanufaisha wanawake na watoto

 Na PATRICIA KIMELEMETA

MANISPAA ya Ubungo imetoa elimu ya lishe kwenye vituo 76 vya kulea Watoto (day care) vilivyopo kwenye Manispaa hiyo ili kuhakikisha kuwa watoto wanaosoma katika shule hizo wanapata lishe bora kwa ajili ya ukuaji wao.

Hatua hiyo imekuja kutokana na utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM) iliyozinduliwa Desemba 2021, itatekelezwa hadi Mwaka 2026, ambayo inahusu watoto kuanzia umri sifuri hadi miaka minane.

Katika Programu hiyo, Halmashauri zimetakiwa kushirikiana na Asasi za kiraia ili kutekeleza mpango huo na kuwafikia wananchi wengi zaidi Ili waweze kubadili mfumo wa maisha na kulea watoto wao kwa kuzingatia afua tano za Malezi na makuzi.

Afua hizo ni pamoja na lishe, afya, elimu, Malezi yenye mwitikio na ulinzi na Usalama kwa watoto kuanzia umri sifuri hadi miaka minane.

Akizungumza hivi karibuni, Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Manispaa hiyo, Bupe Mwansasu amesema kuwa, lengo la kutoa elimu hiyo ni kuwajengea uwezo walimu na walezi ili waweze kuwaa lishe bora, jambo ambalo litasaidia kukuza ubongo wa mtoto na kuondoa udumavu.

Amesema kuwa, kwenye vituo hivyo wameweza kuwajenga uwezo walimu na walezi hao ulaji unaofaa kwa watoto hao ili waweze kuzingatia, jambo ambalo litawafanya watoto kuwa na afya bora, kupenda kusoma kuondoa utoro.

" Tumeanza kutoa elimu kwenye vituo 76 vilivyopo kwenye manispaa yetu kwa kutoa elimu ya ulaji unaofaa kwa watoto wanaosoma vituoni hapo, lengo ni kuwajenga uwezo wazazi, walimu na walezi ili waweze kuzingatia ulaji unaofaa kwa watoto kuanzia umri sifuri hadi miaka minane.

" Mkakati wetu ni kufikia vituo vingi zaidi ili viweze kupata elimu hiyo, jambo ambalo litapunguza udumavu na watoto watakua na afya bora itakayosaidia kukuza ubongo wao, kusoma kwa bidii, kucheza na kufaulu, hali ambayo itapunguza udumavu," amesema Mwansasu.

Ameongeza kuwa, lakini pia wameweza kupima hali ya lishe kwa kushirikiana na wtalaam wa afya la watoto wenye umri wa miezi sita hadi miaka mitano wanaofika katika hospitali mbalimbali zilizopo kwenye wilaya hiyo kwa ajili ya kliniki.

"Wazazi wanapaswa kupewa elimu ya afya ya msingi pamoja na elimu ya kuondoa udumavu ilpi waweze kuwapa watoto wao chakula bora, jambo ambalo litawasaidia watoto kuwa na afya timilifu," amesema.

Amesema kuwa, katika kuhakikisha mpango huo unawafikia wengi zaidi, wameweza kutoa elimu kwa wahudumu 36 wa afya waliyopo kwenye manispaa hiyo.

Amesema kuwa, mkakati uliopo ni kuhakikisha kuwa, wanaendelea kutoa elimu ya lishe kwa wazazi na walezi wengi zaidi kuanzia ngazi ya jamii ili kuhakikiaha kuwa kila mmoja anazingatia ulaji unaofaa kwa mtoto, jambo ambalo litapunguza udumavu.

Programu jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM)  inalenga kuongeza kasi ya mafanikio yanayopatikana katika huduma kwa kuboresha ushirikiano wa kisekta katika utoaji wa huduma za Malezi jumuishi kwa watoto na kuongeza uratibu wa huduma na kuimarisha utekelezaji wa Sheria na sera zinazohusu masuala hayo ikiwa ni pamoja na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, sera ya afya ya mwaka 2007, sera ya maendeleo ya mtoto ya mwaka 2008, sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 ambazo zimelenga kushughulikia mahitaji yote ya mtoto kuanzia umri sifuri hadi miaka minane.

Comments

Popular posts from this blog

AJIRA MPYA 41,500 SERIKALINI ZATANGAZWA KATIBU MKUU UTUMISHI JUMA MKOMI

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?

WALIOPITA KURA ZA MAONI CCM HAWA HAPA