MIGUNA MIGUNA NA SAKATA NA SERIKALI YA KENYA
Dk. Miguna pichani asimulia alivyojikuta Dubai
DUBAI, UAE
MWANASHERIA na mwanaharakati wa upinzani wa
Kenya, Miguna Miguna, ambaye kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Dubai amesimulia
namma alivyojikuta nchini hapa.
Dk. Miguna pia ameitaka jumuiya ya
kimataifa kuingilia arudi Kenya kwa vile anateseka.
“Niliamka
nikiwa hapa Dubai na bila kitu. Nahitaji jumuiya ya kimataifa na kila mtu
kuingilia kati suala hili,” Dk. Miguna alisikika
akimwagiza mmoja wa wanasheria wake kwa simu kuvijuza vyombo vya habari vya
kimataifa.
Mwanasheria huyo alisisitiza atapanda tu
ndege itakayoelekea Nairobi, si vinginevyo.
“Sitarajii kukubali kupanda chochote, kwa
sababu ni kinyume na matakwa yangu. Mimi ni mgonjwa na siwezi hata kutembea,
walichukua miwani yangu na walichukua kila kitu,” alisema akiwa hospitali.
Akisimulia jinsi alivyoamka asubuhi na
kushangaa kujikuta akiwa Dubai, Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE), Dk. Miguna
alisema:
“Mimi ni abiria niliye katika eneo la
kusubiria kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai, UAE.
Nimepitia vipimo vya msingi, ambavyo
vimethibitisha nililazimishwa kwa nguvu kupanda ndege chapa EK722 ya Shirika la
Ndege la Emirates kutoka Nairobi kuja Dubai, ambayo iliwasili asubuhi hii ya
leo (jana).
Karibu wahuni 50 wenye silaha wakiongozwa
na askari polisi aliyevalia kiraia wa Kisomali, ambaye aliwaongoza Jumatano kuvunja
kwa nguvu katika choo nilichokuwa nimeshikiliwa kinyume na sheria kwenye Uwanja
wa Ndege wa Jomo Kenyatta.
Bila kujitambulisha, waliniangusha chini kwa
nguvu, walinishikilia na kukaa juu yangu wakati kundi la wahuni wengine wanne
tofauti waliponichoma sindano yenye vimiminika visivyofahamika katika nyayo
zote mbili, mikono na pande zote za mbavu na mwili mzima ukapoteza mawasiliano.
Leo, saa 11:25 asubuhi (jana), baada ya Emirates
kutua na abiria kushushwa, nilipata fahamu na kumwuliza mtu aliyeketi kando
yangu, ambaye pia alionekana kuwa mmoja wa maofisa walionisindikiza, “tuko wapi?”
nilimuuliza, akanijibu kwamba tulikuwa Dubai.
Mara wanaume watatu waliovalia jaketi za njano
sare za Air Emirates walichomoza na kunifuata na kwa sauti ya jeuri walinitaka
nishuke kutoka kwenye ndege.
Yule anayechukiza zaidi alijitambulisha
mwenyewe kama “Njihia”, alidai kwamba lile fungu la karatasi aliloshikilia
mkononi zilikuwa ‘nyaraka’ zangu.
Nilimwambia sitoambatana naye kwenda popote;
kwamba sina hati yangu halali ya kusafiria ya Kenya na yeye ni mhalifu tu aliyeniteka,
aliyenilevya na kuniondoa kwa nguvu kutoka Kenya kinyume na matakwa yangu na
kukiuka amri mbalimbali za mahakama.
Niliwaambia wafanyakazi wa Air Emirates kuwa
kumsafirisha mtu asiye na fahamu na aliyechomwa sindano za kumlevya kama mimi
kutoka Kenya hadi Dubai bila kuwapo nyaraka zozote za kuhalalisha hilo ni kosa
la jinai.
Pamoja na jaribio lao la kutaka
kunilazimisha kwenda kituo cha polisi na Idara ya Uhamiaji Dubai, nilikataa na
kushinikiza nionane na daktari.
Baada ya mvutano mrefu, nilipewa ruhusa ya
kuonana na daktari ambaye amenifanyia vipimo vya msingi na kuthibitisha
simulizi yangu hii.
Vipimo zaidi hasa vya sumu vinahitaji niondoke
uwanja wa ndege, kitu ambacho naweza tu kukifanya nikiwa na hati yangu halali
ya kusafiria ya Kenya, nyaraka ambayo wahuni wameninyang’anya isivyo halali na
kuiharibu wakikiuka agizo la Jaji Kimaru.
Nina maumivu makali kushoto mwa kifua changu,
mkono wa kushoto, kiwiko cha kulia na mguuni.
Naamini hawa wahuni wamenichoma sindano na
vimiminika vya sumu.
Lakini pia, nimeweka wazi kwa mamlaka za Uhamiaji
za Muungano wa Falme za Kiarabu kwamba siwezi na kamwe sitaenda popote isipokuwa
tu Kenya.
Nimegoma kuondoka eneo la kimataifa la
uwanja wa ndege.
Lazima nirudi Kenya kama raia wa Kenya,
uraia wa kuzaliwa kama ilivyoelezwa na amri mbalimbali za mahakama.
Mheshimiwa Jaji Odunga alitoa amri Machi 28
(juzi) zikiwatia hatiani ya kutenda kosa Matiang’I, Kihalangwa na Boinett kwa
kosa la jinai la kuidharau amri halali na kuwataka wajitokeze kwa hukumu jana
saa nne kamili asubuhi.
Jaji Odunga pia aliagiza niachiliwe mara
moja bila masharti yoyote na nihudhurie mahakamani leo saa nne kamili (jana).
Hata hivyo, si Matiang'i (Fred, Waziri wa
Mambo ya Ndani), Kihalangwa (Gordon, Mkuu wa Idara ya Uhamiaji) wala Boinnet
(Joseph, Inspekta Jenerali wa Polisi) waliofika mahakamani jana.
Nilipanga kutoa taarifa ya athari nilizopata
wakati wa hukumu dhidi ya Matiang’i, Kihalangwa na Boinett chini ya Jaji Odunga.
Natumaini kupewa fursa hiyo hivi karibuni.
Mimi sina hatia. Uhalifu wangu pekee ni kumwapisha
Raila Odinga kuwa ‘Rais wa Watu’ Januari 30, 2018; Naongoza Vuguvugu la Taifa
la Mapinduzi (NRM) ili kuleta haki za uchaguzi na kuhitimisha utawala mbaya na usio
fanisi na tumedhamiria kuwaondoa madikteta kutoka nyadhifa wanazoshikilia
isivyo halali!
Wakati nikirudi Kenya, iwe leo (jana) au
kesho (leo), nawataka Wazalendo wa Kenya kubakia imara, kutoogopa chochote
linapokuja suala la wavunja sheria na utawala wa kiimla na usio halali wa Uhuru
Kenyatta na William Ruto.
Madikteta lazima waanguke, hakuna
kujisalimisha, hakuna kurudi nyuma,” alimaliza Dk. Miguna huku akijitambulisha
kama Jenerali wa NRM.
mwisho
Putin, Trump kukutana tena
MOSCOW, URUSI
RAIS wa Urusi, Vladimir Putin, yuko tayari kukutana na mwenzake wa Marekani,
Donald Trump, licha ya uamuzi wa Washington wa kuwatimua wanadiplomasia 60 wa
Urusi.
Msemaji wa Ikulu ya Urusi – Kremlin, Dmitry Peskov alisema: “Putin yuko
tayari na Urusi yenyewe iko tayari kuendeleza uhusiano wa pande mbili kwa
kulingana na uaminifu wa kila nchi, ikiwamo Marekani.”
Marekani na zaidi ya mataifa 20 yalitangaza kuwafukuza wanadiplomasia wa
Urusi katika kile kinachoonekana ni kushikamana na Uingereza kuhusu mzozo wa mahasimu
hao wa zamani wa vita baridi wa kumwekea sumu jasusi wa zamani wa nchi hizo.
Peskov amebainisha wanataraji mataifa yaliyoungana na Uingereza
kufikiria upya juu ya uamuzi wao.
“Tuna matumaini nchi zilizoonyesha mshikamano na Uingereza na kuchukua
uamuzi wa kufukuza wanadiplomasia wetu, zitatafakari iwapo tuhuma hizo ni za
kuaminika. Hazitoshi kuwa ushahidi kwamba Urusi ilihusika na matukio ya
Salisbury,” alisema Peskov.
Naye balozi wa Urusi nchini Australia, ameonya dunia inaweza kujikuta ikitumbukia
katika hali ya vita baridi ikiwa mataifa ya magharibi yataendelea na chuki
dhidi ya Moscow.
Uingereza tayari imewatimua wanadiplomasia 23 wa Urusi, ambayo nayo
ikalipa kisasi kufukuza idadi sawa na hiyo ya wanadiplomasia.
Uingereza inadai kwamba Urusi ilitumia silaha ya kemikali kumshambulia
jasusi wake wa zamani ambaye pia alikuwa jasusi wa Urusi, Sergei Skripal kusini mwa Uingereza mapema mwezi huu.
Mwisho
Comments
Post a Comment