Kigogo Escrow aruhusiwa kwenda kutibiwa
Amri hiyo imekuja baada ya Seth
kusimama mbele ya mahakama hiyo jana wakati shauri lake likiendelea na kudai kuwa
ana matatizo ya kiafya na kuomba apewe kibali ili aweze kutibiwa.
Kutokana na hali hiyo, Hakimu Mkazi
Mkuu, Huruma Shahidi, aliitaka Serikali kumpeleka hospitali ili aweze kupatiwa
matibabu kutokana na maradhi hayo.
Hakimu Shahidi aliahirisha shauri
hilo hadi Agosti 3, mwaka huu, kwa ajili ya kutajwa tena. Julai 14, mwaka huu,
upande wa utetezi, ukiongozwa na Wakili Alex Balomi, uliieleza mahakama hiyo kuwa
mteja wao anahitaji kupewa mtaalamu wa afya kwa sababu ana uvimbe tumboni kama
puto, pia anakosa usingizi.
Awali, washtakiwa hao walipandishwa
kizimbani na kusomewa mashtaka sita, yakiwamo kula njama, uhujumu uchumi, kujihusisha
na mtandao wa uhalifu, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za
udanganyifu na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 300.
Wakati kesi hiyo inaendelea, Julai
3, mwaka huu, vigogo hao walisomewa hati nyingine mpya ya mashtaka mengine sita
yanayofanana na yale ya awali, yakiwamo matano ya kutakatisha fedha na moja la
kuhamisha fedha.
Wanadaiwa kuwa, kati ya Oktoba 18,
2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam, walikula njama katika nchi za
Afrika Kusini, Kenya na India ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Katika shtaka la kujihusisha na
mtandao, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014,
jijini Dar es Salaam, wakiwa si watumishi wa umma na watumishi wa umma, walitekeleza mtandao huo wa uhalifu kwa lengo
la kujipatia faida.
Kwa upande wa Seth, anadaiwa
kuwa Oktoba 10, 2011, katika Mtaa wa
Ohio, Ilala, jijini Dar es Salaam, akiwa na nia ya ulaghai, alighushi fomu
namba 14 ya usajili wa kampuni na kuonesha yeye ni Mtanzania anayeishi kitalu
namba 887, Masaki, wakati akijua ni uongo.
Pia Sethi anadaiwa kughushi fomu
namba 14 ya usajili wa kampuni kwa Ofisa Msajili wa Kampuni, Seka Kasera, kwa
njia ya kuonyesha kwamba yeye ni Mtanzania na mkazi wa Mtaa wa Mrikau.

Comments
Post a Comment